Mansour Yusuf Himid, Waziri wa SMZ

Waziri asiye na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mansour Yussuf Himid, amependekeza kuwepo na Muungano wa mkataba kati ya Tanzania bara na Zanzibar. Mansour alitoa matamshi hayo wakati akichangia hoja kwenye semina ya mjadala wa mchakato wa ukusanyaji maaoni ya uundwaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muugano Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.

Alisema ipo haja ya kuwa na Muungano wa mkataba ili kuondokana na malalamiko mengi ambayo yanalalamikiwa katika Muungano wa sasa.

Katika maelezo yake, Mansoor alisema bado ataendelea kuwa muumini wa mfumo wa serikali mbili chini ya mkataba na si kama ilivyo sasa ili kuipa fursa zaidi Zanzibar kujijenga na kujitegemea kiuchumi.

Alisema si dhambi Zanzibar na Tanganyika chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zote zikawa na viti viwili katika Umoja wa Mataifa (UN).

Alieleza kuwa kuna baadhi ya viongozi kwa malengo yao binafsi wanajaribu kuwajengea hofu wenzao na kuwazuia kutoa maoni yao kwa upana kama raia huru kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Aliongeza kuwa hajawahi hata mara moja kukataa Muungano, ila mara zote amekuwa akihimiza mabadiliko ya kimfumo katika Muungano huo na kwamba anaamini kuwa kufanya hivyo si uadui wala usaliti.

“Hata NEC ya CCM ilipoanzisha mchakato wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kulienezwa hofu kila mahali, nashukuru tumefanikiwa kuunda GNU, sasa imesimama na kusomga mbele, kila mmoja anaona fahari, faida na tija ya jambo hilo,” alisema.

Hata hivyo, kauli ya Mansoour ya kutaka Muungano wa mkataba na suala zima la kila upande kuwa na kiti UN, inamaanisha kwamba Zanzibar inapaswa kuwa huru.

Alisema awali suala la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lilipoibuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kulikuwa na mtazamo hasi kwa baadhi ya wanasiasa waliokuwa wakiamini kuwa kuundwa kwa GNU kungetoa mwanya wa kuwarejesha watawala waliopinduliwa Januari 12,mwaka 1964 na kulipizana visasi.

“Hata wenzetu wa CUF kabla ya GNU, walikuwa wakipinga kila kitu kizuri cha SMZ, baada ya kushirikishwa serikalini hata yale waliyokuwa wakiyapinga wakati ule, sasa wanayaunga mkono, kuyasimamia na kuyashangilia,” alisema Waziri Mansoor.

Akizungumzia umuhimu wa dhana ya Muungano alisema hapendi uvunjike na kwamba mara zote amekuwa akitaka hoja na haja ya Muungano huo kufanyiwa marekebisho ya msingi na kuwa chini ya mkataba.

Waziri huyo wa SMZ ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki kwa tiketi ya CCM, aliongeza kuwa ikiwa maoni yake yatachukuliwa na chama chake kuwa ametenda dhambi, atakuwa tayari kukabiliana na adhabu yoyote atakayopewa.

“Niko tayari kuadhibiwa kwa kutoa maoni ninayoyaamini kama ni ya kujenga, nafikiri nimetumia haki yangu ya Kikatiba na kiraia, nataka Zanzibar iwe na nyenzo zake za kiuchumi kwa maendeleo ya watu wake, sijali na wala sitawasikiliza wanaoeneza maneno ya uzushi,” aliongeza Waziri Mansoor.

Alisema kila Mzanzibari anayo haki ya kutoa maoni yake bila mtu mwingine kuzuia utashi wake huku akisisitiza kuwa hiyo ndiyo demokrasia anayoijua yeye ndani ya chama chake.

Hata hivyo, aliipongeza CCM kuwa ina mwelekeo, viongozi wake wana uwezo wa kuvumiliana na kupima mabadiliko ya nyakati.

“Ninakiheshimu sana chama changu, ninakipenda, ndicho kilichonilea, bado ni imara sana, kuna watu wanataka kukichafua, kufika kwetu hapa ni kutokana na utashi wa viongozi wake kuwa na dira na uvumilivu,” alisema.

TUME YA WARIOBA YATUPIWA LAWAMA

Tume ya kukusanya maoni ya Katiba inayoongozwa na ya Jaji Joseph Warioba, imetupiwa lawama kwa kushindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya viongozi wa CCM wanaowatisha wanachama wasitoe maoni ambayo yanatofautiana na msimamo wa chama hicho.

Waziri wa Miundombinu na Mwasiliano wa Zanzibar, Rashid Seif Suleiman, alisema tume hiyo ina kila sababu za kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu wanachofanya ni kosa chini ya Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema kitendo hicho kinapora uhuru wa wananchi kutoa maoni juu ya aina ya mfumo wa Muungano wanaoutaka.

Seif alikuwa anachangia mada juu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa katika semina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Aboubakar Khamis Bakary, mjini hapa.

“Nadhani Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakataza mtu au taasisi kumzuia mtu mwingine kutoa maoni yake au kumlazimisha aseme anavyotaka yeye, sasa hawa viongozi wa CCM wanaotaka kuwanyang’anya kadi wawakilishi wao wanakiuka sheria hii,” alisema Waziri Seif.

Alisema ataendelea kuishangaa Tume ikiwa itaendelea kushindwa kukemea au kuwachukulia hatua wale wote wanaotoa vitisho dhidi ya watu wenye mitazamo tofauti na ya CCM katika Katiba mpya.

Seif alisema kila mtu yuko huru kutoa maoni yake mbele ya tume hiyo na kwamba si haki kwa mtu au chama chochote cha siasa kuwakataza wanachama wake kutoa maoni yanayogusa mitazamo yao binafsi tofauti na ya vyama vyao.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Zanzibar, Asha Bakar Makame, aliwataka viongozi wenzake ndani ya CCM kutowatisha wanachama wenye maoni tofauti na chama hicho katika suala la mabadiliko ya Katiba.

Asha alisema ni jambo la kushangaza katika ukuaji wa demokrasia wanapojitokeza watu kuwazuia wengine kuwa na mawazo huru kwenye mchakato wa kupata Katiba mpya.

“Jamani tusitishane, kama CCM kila mtu ni CCM hapa hakuna mtu asiyenijua msimamo wangu kuhusu Chama, ninakipenda na nitakitetea, lakini si vizuri kuanza kutishana kwa kuambiana huyu hivi huyu vile, haifai jamani,” alisema.

Asha alikumbusha kwamba wakati wa kutafuta maridhiano ya kisiasa Zanzibar, wapo wana-CCM na viongozi waliopinga suala hilo, lakini hakuna mtu aliyeadhibiwa kwa kuvuliwa uanachama na kuwataka viongozi kuwavumilia wanachama na wafuasi wengine wa CCM katika suala zima la maoni tofauti kuhusu Muungano.

Mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, alisema Rais Kikwete, hajazuia kutoa maoni tofauti na msimamo wa CCM juu ya suala hilo na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo na kuwa wavumilivu.

Hamza aliongeza kwamba CCM bado ni bora, hivyo kisiogope mageuzi kama ilivyotokea wakati wa mageuzi kutoka demokrasia ya chama kimoja kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

CHANZO: NIPASHE

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.