Baraza la Mawaziri la mwanzo la baada ya uhuru wa Zanzibar.

Ni vyema kwanza ichukuliwe tahadhari kwamba uzalendo wa mtu kwa pahala alipo si kabila, rangi wala aina ya ngozi. Uzalendo pia haupimwi kwa kigezo cha ni nani aliyetangulia kufika pahala hapo kuliko wenzake, bali uzalendo ni pale mtu alipozaliwa kwa kuwa wazazi wake aliwakuta hapo, au ni pale mtu anapopenda, alipopachagua na kuamua kuwa kwao kwa kuhamia, kukaa, kufia na kuzikwa.

Kama uzalendo ni kufika mwanzo, basi kamwe Wamarekani wasingejisifia uzalendo wao wa Kimarekani, kwani Wamarekani wa leo wanaofanya idadi kubwa ya wazalendo wa Kimarekani ni wahamizi waliotokea Siberia na kuingia Alaska kiasi cha miaka 20 hadi 40 kabla ya Kristo (B.C), wakiwakuta huko Wahindi Wekundu (Red Indians) wakiwa tayari wameshafanya masikani yao kwa miaka mingi. Lakini hata hivyo Mmarekani anabaki kuwa Mmarekani tu, iwe anatokana na kizazi cha Wahindi Wekundu, awe ni mhamizi kutokea Siberia, au awe ni kizazi cha Waafrika Weusi waliohamia huko wakati wa bishara ya utumwa.
Wazanzibari na Uarabu
Baadhi ya wanahistoria wanadai wahamizi wa mwanzo walikuwa ni wageni kutoka bara la Asia waliokwenda huko kwa sababu za kibiashara. Inadaiwa watu hao walikuwa na asili za Yemen na Oman na walikuwa ni wafuasi wa dini ya Kiislamu katika madhehebu ya Sunni.

Hii ilitokana na kutanda kwa utawala wa Yemen wa wakati huo ambapo hata Oman ilikuwa ni sehemu ya Yemen. Baada ya kuhamia kwao huko mwambaoni watu hao walimtambua mfalme wa Yemen kuwa ndie mtawala wao. Maneno haya yanathibitishwa na mwandishi wa kitabu maarufu na muhimu kinachoelezea safari ya udadisi na biashara katika mwambao wa Bahari ya Hindi, The Periplus of Erythrean Sea, kitabu ambacho mwandishi mwenyewe Wilfred H. Schoff, mfanyabiashara wa karne ya kwanza ndiye aliefanya safari hiyo, safari ambayo ilimfikisha hadi katika mwambao wa Afrika Mashariki.

Wahamizi hao wa mwanzo katika mwambao walikuwa wakifanya biashara na wagiriki na warumi na baadae baada ya kuanguka kwa ufalme wa warumi, soko la bidhaa za biashara lilihamia China na India. Bidhaa kubwa kutoka Afrika Mashariki zilikuwa ni meno ya ndovu. Bidhaa zilizokuwa zikiletwa Afrika Mashariki zilikuwa ni silaha, vifaa vya chuma na vitu vya urembo.

Hoja hii inadai mahusiano ya mapema sana kati ya mwambao wa Afrika ya Mashariki na Waarabu. Wilfred Schoff anasema katika kitabu chake, The Periplus of Erythrean Sea , kuwa ameukuta mwambao wote wa Afrika Mashariki wakati huo ukiwa umeshahamiwa na watu wa asili ya Kiarabu tu, na wanamtambua mfalme wa Yemen kuwa ndiye mtawala wao.

Schoff anasema kuwa watu aliowakuta wote ni wa asili za watu wasiokuwa Waafrika, na hakukuwa na hata alama ya mtu mweusi kwa wakati huo. Kwa hakika Periplus, inayozungumzia mwambao wa Afrika ya Mashariki na kuja chini kusini mpaka Zanzibar, haikuwataja kabisa watu weusi.

Pia hoja hii inategemea sana maandishi yatokanayo na Jiografia ya Ptolemy (mwanagiografia na mnujumu maarufu wa Alexandria). Jiografia ya Ptolemy inawazungumzia (wabantu) na kuwepo kwao mwambaoni, lakini ni kusini kabisa ya eneo hilo ndiko wanakotokea, ambako bila shaka ni kusini ya kiasi cha Msumbiji ya sasa, ukija kwa juu kaskazini zaidi ya eneo hilo (la Afrika Mashariki), watu waliokuwepo ni Wasomali na Waethiopia watupu (Oliver na Fage 1962: 98).

Pia madai ya hoja hii yameegemezwa na wakati wa Ibn Batuta, msafiri na mwandishi mashuhuri. Katika maandishi yake, Ibn Batuta anadai alipoutembelea mwambao wa Afrika Mashariki katika karne ya 14 alishangazwa sana alipowaona Waswahili kuwa ni watu waliokuwa na nyumba zao nzuri, waliokuwa wakijuwa kuvaa na kula kama walivyokuwa Wazungu wa wakati huo.
Kwa mujibu wa hoja hizo, basi Waarabu walikuwepo katika mwambao wa Afrika ya Mashariki na Zanzibar kwa zaidi ya miaka 2000 nyuma. Msikiti wa Kizimkazi, ni katika mabaki ya kihistoria yaliyo na umri mkubwa zaidi Zanzibar. Msikiti huo unakisiwa kuwepo hapo si chini ya miaka 900. Msikiti huu unaakisi ustaarabu wa Waarabu au Wapashia (Wairani) ambao walikuwa wameshafanya masikani yao Zanzibar karne nyingi huko nyuma. Kwenye ukuta wa mihrab wa msikiti huu pameandikwa hivi kwa Kipashia: “hii ni amri ya Kiongozi Mtukufu Sheikh Assayid Abu Imran Musa bin Alhassan bin Muhammad, Mungu ampe maisha marefu na awaangamize maadui wake.”
Kuhusu maneno hayo ya Kipashia katika mihraab kwa mujibu wa hoja hii ni kwamba Waarabu hawa walipitia Pashia na kukaa muda mrefu kiasi cha kwamba utamaduni wao wa asili wa Kiarabu uliathiriwa na ule wa Kishirazi. Ndio maana maandishi ya kwenye mihraab yanaonekana kuwa ni ya mchanganyiko wa lugha mbili (maneno yameandikwa kwa lugha ya Kipashia lakini nambari zimeandikwa kwa Kiarabu). Staili ya ujenzi wa msikiti huo pia haitofauiani na zile za misikiti mingine iliyojengwa na Waarabu.

Wazanzibari na Ubantu
Wanahistoria wanaounga mkono Uarabu kama ndio athari ya mwanzo ya ustaarabu katika mwambao wa Afrika ya Mashariki, pia hawakuacha kuwazungumzia Wabantu, ujio wao na uhusiano wao na mwambao huo. Wabantu ni jamii za Waafrika weusi wanaozungumza lugha za kikabila za Kiafrika ambao wana asili zao kutokea Afrika ya Kati Kusini.

Wanahistoria hawa wanakana kuwepo kwa tarehe rasmi ya uhakika ambapo Wabantu walihamia mara ya kwanza Zanzibar, lakini wao wanadai kwamba mpaka mwishoni mwa mwaka wa 700 kabla ya Kristo (B.C ) kwa yakini sio Zanzibar tu, bali Afrika Mashariki yote kiujumla ilikuwa imeshavumbuliwa na kuhamiwa na watu wasio na asili ya Kiafrika. Wanasisitiza kwamba ni vigumu kukisia ni karne ngapi nyuma hasa Wabantu walifika katika mwambao wa Afrika ya Mashariki na hatimaye wakafika Unguja na Pemba, lakini wanachoweza kusema ni kwamba walifika huko baada ya mwambao kwisha kuvumbuliwa tayari na watu wa asili zisizokuwa za Kiafrika.

Mwambao wa Afrika Mashariki, kwa mujibu wa wanahistoria hawa, ulikuwa unafahamika na wenyeji wa Arabuni katika karne ya 8 kabla ya Kristo. Kumbukumbu zao zinadai pia kwamba taifa la Kiarabu la Ausan ambalo lilisambaratika mwaka wa 700 Kabla ya Kristo, lilifanya biashara na na bila shaka lilimiliki sehemu ya mwambao (Gray 1962: 10-11).
Utafiti wao unadai kwamba katika nyakati za karne ya 16, ndani ya ukoloni wa Kireno ndipo hasa mababu na mabibi wa Wazanzibari wa asili za Kibantu walipoanza kuingia katika visiwa vya Zanzibar, zaidi kwa kupitia biashara ya utumwa. Kutokea hapo sasa uingiaji wa Wabantu kutoka Mrima kuingia Zanzibar ukawa ni wa kawaida na kwa wingi. Hata baharia, mpelelezi wa kireno, Vasco Dagama, aliekuwa akifanya upelelezi sehemu mbalimbali kwa lengo la kuweka ukoloni, mwishoni mwa karne ya 10 alifika katika pwani ya Afrika ya mashariki na anakiri aliwakuta huko watu wa mwambao kuwa ni wale watu wenye ustaarabu wa jahazi tu, na akasisitiza kuwa watu hao walikuwa wanauwelewa vyema ustaarabu wa ubaharia wa jahazi kama alivyokuwa akiujua yeye (Issa 1999).
Madai yao zaidi ni kwamba mara baada ya kuhamia Wabantu wakitokea Mrima, walioana na wenyeji wale walioitwa Wahadimu, Wapemba, na Watumbatu na kupatikana watoto machotara. Machotara hawa ndio wale waitwao Waswahili. Wakijaribu kutoa uthibitisho wao wanadai hata Mwinyi Mkuu wa Dunga anaonekana naye alihemkwa na mabibi wa Kibantu na kuzaa watoto machotara. Ipo picha maarufu sana kwa kumbukumbu za kihistoria, inamuonyesha Mwinyi Mkuu wa Dunga (ambae bado anatambuliwa kama Mshirazi), yeye amekozea maumbile ya Kiarabu, akiwa na mtoto wake ambae ni chotara, ameshapoteza ule Uarabu wa baba yake na amekozea zaidi Ubantu wa mama yake.
Hata hivyo, Ipo mijadala mirefu miongoni mwa wanahistoria na wanasiasa wanaodai kwamba wenyeji wa mwanzo wa Zanzibar walikuwa Wabantu kutokea bara hususan Tanganyika. Miongoni mwa wanahistoria hao ni Matokke na Mrina. Katika hoja hii panadaiwa kwamba wavuvi kutoka Bara walifika na kuhamia sehemu mbali mbali za visiwani na matokeo yake sehemu hizi zikakuwa na kufanyika vijiji.

Kutokana na upokeaji wa wageni zaidi, vijiji navyo vikakuwa zaidi na watu wakaendelea kuzaliana. Kwa ari ya kutaka kuyamudu mazingira yao, watu hawa waliweza kujipatia maarifa, ujuzi na uwezo wa kujenga vibanda vidogo vidogo na kuimarisha vitendea kazi vyao. Sambamba na hoja hiyo, yapo pia madai kwamba wahamizi wa mwanzo wa Zanzibar waliingia sehemu ya kKsini Unguja wakitokea katika sehemu nyegine za mwambao wa Afrika ya Mashariki. Baadhi ya masimulizi ya watu wa Muyuni yanadai watu wa mwanzo wa Muyuni walikuwa ni Wagunya. Wagunya hawa walitokea katika mwambao wa Kenya ambao pia inasemekana walihamia na maeneo ya Bwejuu. Halikadhalika baadhi ya watu wa Paje na Jambiani inaaminika walitokea Pate na Rufiji ambapo hapo mwanzoni walikuwa ni wavuvi wa dago.

Wazanzibari na Ushirazi
Kuna utata mwingi kuhusiana na historia ya Washirazi na kuwepo kwao katika Zanzibar na Afrika ya Mashariki. Mengi yameandikwa na kusemwa kuhusiana na Washirazi. Wako wanaosema Washirazi na ujio wao sio kitu cha ukweli bali ni hadithi za kubuni. Kwa mujibu wa wanahistoria hawa, neno ’Ushirazi’ lilizushwa na kuungwa mkono na wakoloni ili kukidhi matakwa ya kurahisisha utawala kwa misingi ya ukabila. Miongoni mwa hoja wanazozitoa wanahistoria hawa akiwemo S. J. Kirkman ni vile kukosekana kwa athari za maingiliano ya kimila za Kishirazi na Waswahili pamoja na kukosekana kwa matumizi ya lugha ya Kipashia katika utamaduni wa Kiswahili. Hata hivyo mwanahistoria B. Kurmm amegundua athari ya maneno 78 ya Kipashia katika lugha ya Kiswahili.
Pia mwanahistoria T. Spear anawaelezea Washirazi kama sio kabila la watu bali ni kundi la watu wa tabaka la wafanyabiashara na matajiri. Bila shaka kundi hilo linatokana na maingiliano kati ya wenyeji wa sehemu za Afrika Mashariki na wageni. Kwa mujibu wa Spear, kwa hivyo, neno Shirazi linahusiana na tabaka la matajiri au watawala. Akifafanua, Spear anasema Washirazi sio Wapashia bali ni Waafrika au ni wafanyabiashara wenye asili ya Kiarabu. Makabila ya watawala (mamwinyi) wa watu hao walioitwa Washirazi yanatoa uthibitisho wa hoja ya Spear. Makabila ya mamwinyi wa Washirazi ni kamavile Al-alawi, Al-Bajuni, Al-Addibawy, Al-Bahasany, Al-Ahdali, Al-Attasi n.k, ambayo bila shaka ni makabila ya Waarabu na sio Waajemi (Issa 1999).
Pamoja na hoja hizo zinazoukataa Ushirazi, pia upo ushahidi wa kuthibitisha kuwepo kwa Ushirazi. Moja ni matumizi ya kalenda kama zile wanazotumia Washirazi. Sio Zanzibar tu bali hata maeneo mengine ya Afrika Mashariki, mpaka leo kuna watu wanaofuata kalenda zao za kinujumu mbali ya zile za Kiislamu. Kwa mfano Nairuzi, yaani Siku ya Mwaka au Mwaka Kogwa. Siku hiyo ya mwanzo wa mwaka wa Kishirazi hufuatana na tarehe 21 Machi ambapo urefu wa mchana na usiku hulingana.

Sherehe za mwaka kogwa Unguja husherehekewa kwa kukoga baharinikamanjia ya kujitoharisha mwili, kuzima moto wa wa zamani na kuwasha moto mpya kwa kutumia fimbo mambo ambayo yanalingana mno na sherehe za kishirazi. Msikiti wa Kizimkazi unaokisiwa kuwa na miaka 900 tangu kujengwa kwake na maneno ya lugha ya Kipashia katika mihraab yake unaakisi ujio wa washirazi mapemasanakatika visiwa hivi.

Uchambuzi wa takwimu za kuzaliwa zilizofanywa kuanzia mwaka 1953 hadi 1963 ambapo Wazanzibari walitakiwa kuwaandikisha watoto wao kwa makabila yao halisi zinaonyesha wenyeji wa visiwani walijitambulisha miongoni mwa makabila matatu. Makabila yenyewe ni Wahadimu, Watumbatu na Washirazi. Makabila ya Wapemba na Waswahili ambayo yalitumika kabla ya hapo hayakutambuliwa tena kama makabila. Thuluthi moja ya wenyeji wa Unguja na takriban nusu ya Wapemba walijitambulisha kama Washirazi.

Ushirazi ulionekana, kwa hivyo, kushamiri zaidi na kuota mizizi katika kisiwa cha Pemba. Katika kipindi cha karne ya 8 hadi ya 15 ndipo Washirazi wanapodhaniwa kuwa waliwasili. Washirazi ndio waliokuwa wafanya biashara wakubwa katika pwani nzima ya Afrika Mashariki na visiwa vyake vya Unguja, Pemba na Mafia katika kipindi hicho jambo ambalo lilisababisha kukua sana kwa miji hiyo.

Wahadimu, Wapemba na Watumbatu ndio hasa historia inaowaita Washirazi wa Unguja na Pemba. Wahadimu walikuwepo katika maeneo ya kaskazini ya kisiwa cha Unguja na walikuwa wakiishi kwa wingi katika maeneo ya Nungwi, Kijini, Muyuni, Pwani Mchangani, Chwaka, Bwejuu, Makunduchi, Kizimkazi na Uzi. Mji mkuu, au mji muhimu wa Wahadimu ulikuwa ni Dunga. Watumbatu walikuwa wakiishi katika maeneo ya kisiwa cha Tumbatu. Pia Watumbatu walionekana kuishi maeneo kama vile Donge, Bumbwini na Mwanda (Ingrams 1962).
Wapemba (Wadiba) ambao ndio wenyeji wa kisiwa cha Pemba pia wananasibishwa na Washirazi. Hata hivyo, Wadiba pia wananasibishwa na Waarabu. Kwa mujibu wa wanahistoria hawa, Wadiba ni watu walio na asili zao kutokea katika mji wa Diba. Diba ni mji ulioko baina ya Oman na Sharjah. Inasemekana kuwa uko mji mwengine unaoitwa Diba maeneo ya Bara Hindi, lakini hiyo sio Diba ya asili.

Kwa kutilia nguvu hoja yao hiyo ni mitindo yao ya misikiti na majengo waliojenga huko Pemba katika masikani yao katika miji kama vile Pujini na Kengeja ni sawa na ile ya Diba ya Uarabuni. Ushahidi wa mabaki ya majengo ya kale na vihame vya Mkamandume ndio wanaotumia kuyakinisha madai yao haya. Wanahistora hawa hawakanushi Ushirazi bali wanadai kwamba mji wa Shirazi ulikuwa ni kituo chao walichopitia na kuishi hapo wakitokea Bara Arabu kabla ya safari yao ya kuja katika mwambao wa Afrika ya Mashariki na visiwa vya Zanzibar.
Watu hawa, yaani Watumbatu, Wahadimu na Wapemba mwanzoni kabisa baada ya uhamiaji wao, walikuwa wakiishi kwa mifumo ya tawala za kienyeji za umwinyi mkuu. Waliishi katika tawala zao za kienyeji zinazojitegemea. Watumbatu walikuwa na Mwinyi Mkuu wao, Wahadimu walikuwa na Mwinyi Mkuu wao na Wapemba walikuwa na Mwinyi Mkuu wao. Mwinyi Mkuu wa mwanzo wa Dunga, Hassan bin Abdallah, anadhaniwa kutawala katika karne ya 13 na Mwinyi Mkuu wa mwisho, Ahmed Bin Muhammed, ambaye alikuwa mashuhuri zaidi na ambaye ndie aliyejenga kasri iliyopo Dunga, anadhaniwa kutawala kuanzia mwaka 1728 hadi 1865. Mwinyi Mkuu wa Wapemba anayekumbukwa zaidi na historia ni Mkamandume. Baadhi ya wakati tawala hizi zilikuwa na masikizano na baadhi ya wakati zilikuwa na migogoro ya hapa na pale.
Totauti kidogo na kisiwa cha Unguja ambacho kilikuwa chini ya tawala zaidi ya moja za kienyeji, Pemba yote kwa upande wake ilikuwa chini ya Mwinyi Mkuu mmoja tu wa Kishirazi. Taifa la kisiwa cha Pemba liliasisiwa mwaka 1550 chini ya utawala wa Mwinyi Mkuu. Hichi ndio kipindi peke yake katika historia ambapo Pembailijitegemea yenyewe kiutawala. Mmoja wa mamwinyi hao anayekumbukwa zaidi na historia ni Mwinyi Mkuu wa Pujini, mtawala wa Washirazi. Huyu alikuwa akiitwa Mohammed bin Abdulrahman Al-Addibawy na kujulikana kwa jina la umaarufu la “Mkamandume”.

Kimakosa jina hili lilifahamika na kuelezwa vibaya na baadhi ya walioandika historia au pia inawezekana waliandika kwa makusudi kwa malengo yao binafsi. Wapotoshaji hawa wa historia wameandika kwamba aliitwa mkamandume kwa kuwa mtawala huyu akiwafanyia vibaya wanaume wenzake kwa kuwavuta uume wao kama anavyokamwa ng’ombe maziwa.

Huu ni upotoshaji wa historia na dharau kwa wahenga hawa wa Wapemba. Vikongwe wengi wa kipemba wanakataa kabisa kupokea ngano hizo kutoka kwa mababu na mabibi zao. Kauli nzito ni kwamba neno “mkama” linatoka kwenye neno la Kiarabu “maqaam” kwa maana ya nafasi ya cheo. Kwa Mswahili wa kawida atakubaliana na mimi kwamba neno “Mkamandume” halina jengo la Kiswahili kizuri (fasaha) bali neno “Makamo wa madume” ambalo ndio asili yake lina jingo la Kiswahili kizuri ambalo bila shaka ndio neno la awali na maana halisi iliyokusudiwa kwa mtawala huyu. Kwa hivyo, neno Mkamandume lilikuwa na maana ya kuwa huyu bwana alikuwa juu zaidi kwa cheo na utukufu kuliko watu wote waliokuwa chini ya utawala wake. Kwa kiingereza ni kwamba alikuwa “above men’ na sio “milker of men.”

Kutoka mtandao wa kijamii wa Facebook.

One thought on “Wazalendo wa Kizanzibari na nasaba zao”

  1. Hatuko tayari kuacha Uzalendo wa nchi yetu kwa ajili ya kujiunga na umoja wa Afrika usiokuwa na mwelekeo kuwepo!
    Nchi yetu ni ndogo haihimili muungano na mataifa yaliyotuzidi kwa idadi ya watu zaidi ya mara 40!
    Tunataka viongozi wachukuwe hadhari kwa kuweka utaratibu utakaoweza kulinda maslaha ya zanzibar wala sio Afrika!
    Haiwezekani nchi ndogo kama hii kuachiwa watu kuingia kiholela na kuathiri utamaduni na uwiyano wa watu wa asili.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.