Mzee Hassan Nassor Moyo, muasisi wa CCM na Muungano.

Na Ahmed Raajab

ALEXANDER Pope, mshairi Wakiingereza wa karne ya 18, aliwahi kuandika kuwa “wapumbavu hukimbilia kule malaika wanakohofia kukukanyaga”.

Niliyakumbuka matamshi hayo Jumapili wiki hii, baada ya futari hapa kwetu Zanzibar ambako siku hizi hali za hewa — ya kimaumbile na ya kisiasa — ni za kuridhisha. Watu wanaifunga Ramadhani bila ya kuteswa na joto lililoshtadi.

Kadhalika, utulivu uliopo na mshikamano wa wananchi wa itikadi tofauti za kisiasa unazidi kuashiria matumaini mema kuhusu mustakbali wa Visiwa hivi. Hali ya hewa imepoa na hali ya kisiasa pia kama wasemavyo vijana siku hizi ‘iko poa.’

Nilipokuwa nikiyakumbuka hayo aliyoyaandika mshairi Pope nilikuwa nikitafakari kuhusu njama za wanasiasa duniani kote wenye kujaribu kujijenga ili wajipatie ulwa. Siku mbili hizi tumewashuhudia wanasiasa aina hiyo wakiibuka hapa Zanzibar.

Wanasiasa wa sampuli hiyo huwa hawajali wanapita wapi ili wafike waendako. Hata ikiwa njia inayowakabili imejaa makaa ya moto wao watakhiyari wayakanyage hayo makaa ya moto.

Wanasiasa wana sababu zao zinazowafanya wautapie ulwa hata ikiwa nyayo zao zitateketea. Wengi wao wanauona ulwa kuwa ni njia ya mkato wanayoweza kuitumia kufikia malengo mengi na kujipatia mengi.

Usifikiri kwamba ninawachukia wanasiasa, la hasha. Kuna ninaowapenda na wako ninaowapenda sana. Huwapenda sana pale wanapokuwa na misimamo ya kizalendo au wanapowatetea walio wanyonge. Au panapotokea miujiza kama pale wanaposema: “Nchi yangu kwanza, potelea mbali mengine.” Katika historia mara kwa mara tunawaona wanasiasa wa aina hiyo wakichomoza katika jamii, ingawa kwa nadra kwani miujiza haitokei kila siku.

Kwa jumla, katika hali za kawaida huwa siwaamini wanasiasa. Na siwaamini kwa sababu wanasiasa si watu wa kuaminika. Na siko peke yangu. Kama husadiki fanya utafiti katika jamii zilizotofauti barani Afrika na kwingineko na nina hakika utapata matokeo yanayofanana. Utaona kuwa wanasiasa wanawekwa safu ya mbele ya watu wasioaminika katika jamii — jamii hiyo iwe yenye demokrasia iliyopevuka au yenye demokrasia iliyochanga, yenye kwenda tata kama yetu.

Kote huko aghalabu wanasiasa huwa hawaamini wala hawaaminiki. Wanaonekana kuwa ni watu waongo, makidhab, wazandiki, wanafiki na wenye kuyatetea maslahi yao tu. Hawajali iwapo yao yanawaendea iwe kwa njia za kifisadi au za ulaghai.

Wengine huwa tayari hata kuziuza nchi zao ilimradi yao yawe yanawaendea vizuri na wanayapata matlaba wayatakayo. Hao ndio walio hatari kushinda wote. Na hao tumekuwa tukiwasikia siku mbili hizi wakijaribu kuzipaza sauti zao hapa Zanzibar.

Moja ya hila zenye kukirihisha walizonazo wanasiasa ni ile ya kutumia vitisho dhidi ya wenzao wenye kuwashinda kwa hoja. Mara tu wanapotanabahi kuwa wanashindwa kwa hoja huanza kutumia kila aina ya vitisho ili kuwatia hofu mahasimu wao wa kisiasa.

Mbinu hiyo iliwapa ushindi wanasiasa wa aina hiyo nchini mwetu katika enzi iliyopita ya utawala wa kimabavu pale wanasiasa wakorofi walipoweza kufanya watakavyo na pasiwe kitu. Lakini si leo. Mazingira ya kisiasa yamebadilika.

Wananchi kadhalika wamebadilika. Waliokuwa wamelala sasa wameamka. Na waliokuwa wameamka tangu zamani sasa wamezidi kuamka. Siku hizi wananchi si tu kwamba wanazitambua haki zao kama zinavyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano lakini wanajua pia namna ya kuzitumia taasisi zilizopo ili kuzitetea hizo haki zao. Kweli baadhi ya taasisi hizo si madhubuti sana lakini angalau zipo na wananchi wanathubutu kuzitumia. Zama za kukubali kuonewa zimekwisha.

Hila nyingine ya wanasiasa ni ile kujifanya kwamba wao, na wao tu, ndio wenye kujua kila kitu. Kinyume na wasomi ambao mara nyingi huona muhali kujisifu hata ikiwa wanatambulika kwa weledi wa fani zao, wanasiasa kwa upande wao hawachelewi kujigamba kuwa wamebobea katika fani mbalimbali hata zile wasizozilalia wala kuziamkia. Kwa mfano, hujifanya kuwa wao ndio mastadi wa kiuchumi au wa uhusiano wa kijamii. Mara nyingi hujifanya kuwa ni wao na wao peke yao, wenye kuyatambua matakwa ya wananchi na nini kilicho na maslahi nao.

Tofauti hii kubwa kati ya wanasiasa na wasomi aliiona zamani Plato, yule mwanafalsafa Wakiyunani ambaye kwenye kitabu chake ‘Jamhuri’ ameieleza vyema dhana yake ya kwamba dola bora ni ile yenye kutawaliwa na wasomi. Ndipo ilipoanza kupigiwa mbiu ile dhana ya ‘mwanafalsafa mfalme,’ yaani mtawala aliye msomi. Kuna sababu nyingi zinazotufanya tuwaegemee wasomi.

Kwa ufupi, wasomi hutwambia mambo tunayohitaji kuyajua. Wanatueleza kwa mfano jinsi maumbile na jamii zinavyopaswa kuwiana na kufanya kazi, wanatukumbusha yaliyotokea zama za kale, wanatuonyesha namna ya kuzichambua dhana, na pia wanatufahamisha jinsi ya kuzithamini sanaa na fasihi ili zitustareheshe.

Wasomi pia hutuwezesha tuwe tunaongea — au kwa kutumia lugha ya leo ya mitaani tuwe ‘tunabonga’ — na magwiji wa kale. Si lazima kwamba maongezi hayo yawe yanatuwezesha kuchota kutoka chemchemi ya hekima endelevu. Itatosha iwapo wasomi wetu watatufanya tuwe na tabia ya kusoma vitabu au kama si vitabu basi angalau tuwe na hamu na uwezo wa kusoma makala mbalimbali katika majarida ya maana kuhusu sayansi, utamaduni na fani nyingine.

Hiyo ndiyo dhima na jukumu la wasomi. Wakilitekeleza jukumu hilo watatusaidia kutupa mazingira ya kisomi. Tukiwa na mazingira kama hayo sidhani kwamba kutakuwa na ulazima wawanasiasa wazuri wawe wasomi. Naamini itatosha ikiwa wanasiasa wetu watakuwa na uzoefu wa kujadili mambo kisomi. Kwa ufupi, ikiwa wataishi maisha ya kisomi.

Wanachokihitaji zaidi wanasiasa na viongozi wetu ni kuwa na uwezo wa kufanya mambo kiakili; yaani kwa kutumia hekima na busara. Hawahitaji nadharia za kumeremeta. Wanachohitaji ni kuweza kuwa na msimamo unaokwenda sambamba na matakwa ya wananchi wengi. Hivyo ndivyo demokrasia halisi inavyopasa iwe.

Wasichohitaji ni kuwa na sera zilizopitwa na wakati na zisizokumbatiwa na idadi kubwa ya wananchi. Haijuzu kwa viongozi wa kisiasa kuzing’ang’ania sera ambazo wananchi wanazikataa. Wala haijuzu wanasiasa hao kuipuuza historia na kutokubali kujifunza kutokana na yaliyopita katika jamii.

Nimezunguka sana kwa makusudi kwa sababu naona kuna umuhimu mkubwa wa kuyazingatia yote haya wakati wa huu mchakato wa sasa wa kulitafutia taifa la Tanzania Katiba mpya. Huku kwetu mchakato huo umetawaliwa na mjadala mkali kuhusu Muungano.

Linalotia moyo na lililo jipya ni kuwa mjadala huu tangu uanzwe umekuwa ukiongozwa na wananchi wa kawaida. Mpaka sasa wao ndio walio safu ya mbele kueleza hisia na matakwa ya wananchi wenzao. Kwa hili wamewapiku viongozi wao wa kisiasa. Ile hali ya kale ya wananchi kuburuzwa kimawazo na viongozi wao wa kisiasa sasa haipo tena. Jingine la kutia moyo ni kwamba viongozi nao wameueleza msimamo wao ambao hauna hitilafu na ule wa wananchi.

Ushahidi uliopo kutokana na maoni yaliyotolewa hadi sasa ni kuwa wengi wanataka muundo wa Muungano tulio nao ubadilishwe. Wapo vile vile wachache wenye kutaka muundo wa sasa uendelee. Katika demokrasia watu wana haki ya kuwa na mawazo wayatakayo. Wana haki pia hata ya kulindwa na taasisi za dola ili wawe na uhuru wa kutoa maoni yao na kuyatetea maoni hayo kwa hoja.

Wasichopaswa kuwa nacho ni haki ya kuwatisha au kuwabughudhi wengine wenye maoni yanayopingana na yao. Wala hawana haki ya kuipotosha historia au ya kuwaita wenzao “mafisadi” kwa kuwa tu wana mawazo yanayotafautiana na yao. Au kuzitaja nasaba za wenye maoni tafauti na yao. Tusiyasahau maneno ya wahenga ya kuwa mtafuta nyingi nasaba hufikwa na mwingi msiba.

Mijadala kama hii iliwahi kuibuka China zama za Mwenyekiti Mao na ndipo alipotoa yale matamshi yake maarufu alipoagiza wananchi waachiwe watoe maoni yao kwa uhuru. Mao alisema: “Acheni fikra mia zikinzane na maua mia yachanuwe.” Alitambua kwamba kuzizima fikra zisizowapendeza baadhi ya wakuu na kuyazuia mageuzi ni kwenda kinyume cha mkondo wa kihistoria.

Jamii inayokataa mageuzi pale mageuzi yanapohitajika ni jamii iliyoganda isiyoweza tena kuendelea. Jamii inayoweza kuendelea ni ile yenye kuruhusu mageuzi na inayowapa wananchi fursa ya kuweza kutoa maoni yao kwa uhuru na yenye kufuata utaratibu wa kuwaridhia walio wengi. ‘Wengi wape’ ni kanuni muhimu ya mfumo wa kidemokrasia.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.