Wazanzibari wakihudhuria moja ya mikutano ya Jumuiya ya Uamsho kudai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Na Masoud Sanani

VIJANA na wananchi wenye umri mkubwa (vikongwe) wa Mkoa wa Kusini Pemba wengi wao wameonyesha kuwa hawataki Muungano uliopo sasa nchini Tanzania.

Wakitoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayochukua maoni kutoka wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba, vijana wengi na vikongwe wamekuwa wakieleza kuwa hawataki Muungano.

Hata wale ambao wanataka mfumo mwingine wa Muungano, wanasema huu wa sasa haufai, bali wanapendekeza kuwe na Muungano wanaouita wa mkataba.

Wale ambao waliulizwa na wajumbe wa Tume ya Katiba Muungano wa mkataba una maana gani, wengi walieleza kuwa baada ya Zanzibar kuwa na Serikali yake yenye mamlaka kamili na Tanganyika nayo kuwa na Serikali yake, Serikali hizo mbili zitatoa wajumbe watakaounda Serikali ya Muungano ambayo wanaeleza kuwa ni ndogo.

Vijana na vikongwe ambao hawataki Muungano wanasema kwamba hauna faida yoyote kwa Zanzibar na umekuwa ukiwadhulumu haki zao, na unapendelea zaidi upande wa Tanzania Bara.

Mambo makubwa ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi walio wengi ni ajira katika Jeshi na Polisi na mgawanyo wa mabalozi wa Tanzania nje ya nchi na hata wafanyakazi wa balozi hizo kuwa zina Wazanzibari wachache mno.

Pia wanaeleza kuwa wakuu wa vyombo vya ulinzi, Jeshi na Polisi hawajawahi kutoka Zanzibar, pia Gavana wa Benki Kuu na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wananchi hao pia walieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tananzania kila wakati anatoka Tanzania Bara na mwananchi mmoja akadai kuwa hata aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi hakuwa Mzanzibari halisi.

Maimuna Said Rashid (42) ambaye ni mtumishi wa Serikali mkazi wa Ngambwa alieleza kuwa kuna haja ya kuwepo dola huru kwa Tanganyika na Zanzibar, kwani “Watanganyika walivaa koti la Muungano kwa maslahi yao.”

Tathmini inaonesha kuwa vijana wengi wanaotoa maoni yao wenye umri kati ya miaka 18 hadi miaka 40 na wazee wenye umri kuanzia miaka 70 na kuendelea hawataki Muungano.

Wengine wanaotoa maoni yao wanaeleza kwamba hawataki Muungano hata kuusikia huku wengine wakieleza kuwa ubaki urafiki na udugu lakini kila mmoja awe na chungu chake ila waombane chumvi.

Baadhi walipendekeza Muungano uwepo kati ya Zanzibar na Tanganyika lakini uwe kama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi za Ulaya badala ya mfumo huu wa sasa.

Wananchi wengine walieleza kuwa waliotaka Muungano wamefariki dunia, Mwalimu Julius Nyerere na Abedi Amani Karume kwa hiyo sasa ni muhimu kwa watoto kurithi mali ili kila mmoja awe na yake na sio kuendelea na hali hii ya kaka (Tanzania Bara) kumdhulumu mdogo (Zanzibar).

Haji Suleiman Omari (85) mkulima wa Matale alisema Muungano hautaki kwa vile “umetufanya Wazanzibari kama vigogo vilivyotiwa moto, hatuna raha hata moja, tuacheni tupumue.”

Bakari Waziri Bakari (80) mkulima wa Chonga alisema hautaki Muungano kwani hauna faida hata moja na hataki kuhojiwa kwanini ana msimamo huo.

Hafidh Mohammed Salum (54) mfanyabiahara wa Ngambwa alitaka dola huru Zanzibar na Tanganyika na kusema kwamba urafiki unatakiwa usihie sokoni sio nyumbani.

Fatma Abdallah Said (21), Nasor Soud Kheri (33), Juma Amour Ali (43), Aziza Waziri Bakari (35) Raya Othmani Juma (40), Ziada Rashid Salum (32), Maryam Mohammed Suleiman na Rehema Said Abdallah (39) ni baaadhi ya vina walioukataa Muungano wakieleza kuwa hauna faida.

Kuanzia Jumatano Julai 25 mbali na wajumbe wa Tume ya Katiba waliopo katika Mkoa wa Kusini Pemba aliongezeka Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na siku chache kabla aliongezeka mjumbe wa Tume, Dk Salim Ahmed Salim.

Wajumbe waliopo Mkoa wa Kusini Pemba wanaongozwa na Mohammed Yusuf Mshamba akiwa na Dk Sengondo Mvungi, Kibibi Mwinyi Hassan na Richard Lyimo. Wajumbe hao pia ndio waliochukua maoni ya wananchi kutoka Mkoa wa Kusini Unguja.

Jaji Warioba ambaye alikuwepo katika Shehia ya Ndagoni iliyopo Wilaya ya Chakechake, aliwaongoza wajumbe kuwahoji wananchi hasa wale ambao walikuwa hawataki mfumo wa sasa wa Muungano uendelee.

Tofauti na siku za nyuma ambapo wananchi walikuwa wakiulizwa na wajumbe pale ambapo walikuwa hawakuelewa wanachotaka kueleza, hali ilibadilika na kuhojiwa hata pale ambapo wananchotaka kinaeleweka vizuri.

Hali hiyo, ilileta kero kwa wananchi na mmoja kabla ya kutoa maoni yake, Mohammed Mmanga Hamad (50), aliuliza “mmekuja hapa kuchukua maoni au mmekuja kufanya mjadala na wananchi. Naomba nijue hilo kwanza kabla sijatoa maoni yangu.”

Hali ya namna hiyo imekuwa inapunguza idadi ya wananchi wanaopata fursa ya kutoa maoni kwani katika Shehia ya Ndagoni walitoa maoni wananchi 76 tu wakati siku moja kabla katika shule ya Chanjamjawiri walitoa maoni zaidi ya watu 130.

Imeonesha kuwa wananchi wengi wa Zanzibar wanatoa maoni yao juu ya suala la Muungano na baadhi hugusia Jeshi, Polisi na mabalozi kutokana na mambo hayo kuwa ndiyo yanayohusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Mambo mengi yanayohusu maisha yao ya kila siku si mambo ya Muungano na kwa vile walielezwa kuwa wanachangia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaona hayafai kuzunguzwa katika mikutano hiyo.

Jaji Warioba aliwaleza wananchi kuwa alikuwa Tanga ambako walimu walieleza matatizo ya elimu na watu wengine waliotoa maoni walichangia juu ya afya, kilimo na mambo mengine yanayowahusu, lakini alisahau kwa Mzanzibari mambo hayo si ya Muungano na ni tofauti na mkazi wa Tanga.

Katika elimu baadhi ya wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamikia Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa maelezo kuwa linawafelisha wanafunzi kutoka Zanzibar .
Wazanzibar Wazanzibar wengi walichagia kusema kuwa matatizo mingi na ulalamishi na utata mwingi umekuja pole ilipo jifanya Tanganyika kuvaa Koti la Tanzania na baadae kuwa Tanganyika ndio Tanzania.

Wazanzibar wengi walipendelea mfumo wa kimkataba ili kuifufua Tanganyika na mambo yake yasio ya Muungano ili kuondokana na kujificha katika kichaka cha Tanzania.

Chanzo Mwananchi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.