Mansour Yusuf Himid
Na Rasmi

Tokea lianze vuguvugu la Wazanzibari kudai haki zao za msingi katika nchi yao, kumejitokeza vidudu watu ambao wengine wana majina eti ya kuitwa ‘viongozi’, wanaoendesha kampeni chafu za kuwabeza, kuwatisha na kuwakashifu viongozi na wazee wetu ambao wameonyesha nia ya kutetea maslahi ya nchi yao.

Kampeni hizi ambazo zinaendeshwa na watu wanaojulikana kwa ukorofi wao, na ukosefu wa kutokujua tafsiri halisi ya uhuru wa mtu kuwa na mawazo katika siasa za Zanzibar, zinaendeshwa hasa na kundi linalotumiwa na viongozi wa Tanzania bara linalojulikana kama UV- CCM, wakisaidiwa na viongozi wasiopendelea kuona mabadiliko Zanzibar (Wahafidhina) wa mifano ya Shamsi Nahodha.

Katika kundi hili pia muna viongozi wastaafu waliochoka wa mifano ya Ali Ameir, ambao bila ya hofu wala kisisi wameona watoke katika mapango na kuanza kuanika siasa za fitna na vitisho ili kuwavunja moyo Wazanzibari na viongozi wenye mawazo tofauti na yao juu ya muundo wa muungano.

Viongozi hawa licha ya uzoefu wao “wanasiasa wakongwe” lakini kwa sababu ya nia zao mbaya kwa Wazanzibari wameona kipindi hichi ambacho kunaanza kuonekena matumaini ya Zanzibar kuwa huru kuelekea kwenye nuru ya maendeleo waamshe munkari na kuanza kushutumu, kutisha na kutia fitna kuwaelekezea viongozi wote wa CCM – Zanzibar wanaodai mabadiliko.

Miongoni mwa viongozi vipenzi vya Wazanzibari ambao wamekuwa sasa hivi wanapikiwa kila aina ya ‘nyungu’ ni Mh Mansour Yussuf Himidi kutokana na msimamo wake usiotikisika katika kudai mamlaka kamili ya Zanzibar ndani ya muungano, na Raisi mstaafu aliyesimamia maridhiano hadi kufikia kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, Mh Amani Abeid Karume.

Viongozi hawa wawili wamekua ni mwiba kwa maadui wa Zanzibar hata kufikia hadi ya kuambiwa warudishe kadi zao za CCM, kulikoni!? Kisa ni kudai Zanzibar irejeshewe haki zake wakati wakiwa ndani ya chama cha Mapinduzi, na sera ya chama hicho hairuhusu mtu kudai haki hiyo akiwa ndani ya chama – bila ya kuipeleka hoja Dodoma, ikiwa watakataa kufanya hivyo basi warudishe kadi!

Mansouri anaambiwa amefanya kituko kikubwa kudai muungano wa mkataba wakati sera ya CCM ni Serikali mbili, Je hii maana yake ni kwamba mwanachama wa CCM hana haki ya uhuru wa mawazo yake, hata ikiwa jambo hilo linaonyesha udhaifu katika itikadi?

Anaambiwa akiwa ana mawazo yoyote asiyaseme “barabarani”, kwa dharau kabisa Bwana Nape Nauye anamuelekeza kama ana wazo la kufikiri alipeleke kikaoni ‘Dodoma’ likajadiliwe. Nina uhakika Baraza la Wawakilishi ambamo Mh Mansouri amekua akitoa matamko ya kuupinga muundo huu wa ‘muungano’ kwake yeye Nape ni Barabarani.

Wengine, akina Mzee Ali Ameir wamemgeukia Mzee wetu Hassan Nassor Moyo na kumdharau aonekane hana hanani katika siasa za Zanzibar- na anachokifanya kutetea maslahi ya nchi sio haki yake. Hivi ni lini watu kama hawa wanaojiita Wazanzibari walikabidhiwa haki ya kuwasemea nini Wazanzibari wanakitaka katika muungano, ikiwa hata huyo muasisi wenyewe wa huu muungano Mzee Abeid Amani Karume aliupinga katika namna tofauti na ushahidi tele upo!?

Je haki ya kuwa na hoja mbadala ni yao peke yao tu kwa lile wanalolitaka wao japokuwa Wazanzibari hawalitaki?

Sisi Wazanzibari jibu letu la kuwapa hawa ni kuwapenda zaidi na kuwalinda na njama zao mbaya viongozi na wazee wetu hawa ambao nia na madhumuni yao ni kuona tunaishi tukiwa taifa huru lenye maamuzi kamili katika mambo yake ya ki nchi. Tuwageuzie kibao maadui wote wa Zanzibar kwa kuzidisha ari ya mfano katika kuwasapoti viongozi wetu hawa wanaotishiwa ili wafunge midomo yao katika utetezi wa haki zetu.

Tuwaambie maadui wote wasiotupendelea mema kwamba harakati hizi zitaendelea na hazitosimama ndani ya Baraza la Wawakilishi, nje na nchi za nje pia hadi pale Zanzibar itapopata haki zake zote, na hili halina mjadala.

Tuwaambie pia na waandishi wao wanaowatumilia kuandika habari za kizushi, mfano wa Mwinyi Sadalla kwamba azidishe kuandika kwani ni uhuru wake, na sisi tunaendelea kuwatandikia mazulia mekundu (red carpets) na kuwamwagia maua viongozi wetu hawa kila wanamopita, kwani hawa ni mashujaa halisi wa Zanzibar, na Zanzibar itawakumbuka si leo tu wakiwa hai; bali historia itawawekea kumbukumbu katika nyoyo zetu na vizazi vyetu vijavyo.

Viongozi na wazee wetu wote muliojitolea kudai haki, endeleeni kututandikia njia njema ya kupita, na sisi Wazanzibari tuko pamoja na nyinyi. Historia itawakumbuka kwa wema muliowafanyia Wazanzibari; munamopita tutamwaga maua kwa furaha.

Zanzibar Kwanza

One thought on “Kila wakiwachukia, sisi tuwamwagie maua”

  1. ukale umepita ni lazima tukubali na usipokuwa pamoja na haya wewe si kamili kwanza jiangalie wewe mwenyewe ndivyo ulivyozaliwa kama ni la basi kila kitu kinabadilika kama ulivyobadilika wewe mabadiliko ni lazima yajana si ya leo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.