Na Juma Mohammed, MAELEZO Zanzibar

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Zanzibar haikuwahi kutawaliwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, akimshangaa Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu kudai Zanzibar imejitangazia uhuru, kauli hiyo sio sahihi. “Mimi nimepata kusoma na kuangalia hiyo hotuba ya Mhe Tundu Lisu, lakini pia nimeona majibu ambayo yalitolewa na Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha (Waziri wa Ulinzi) aliyesema maeelzo ya Mbunge Lissu yamejaa hadaa na upotoshaji naungana naye.” Aliliambia Baraza Mwanasheria Mkuu.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Othman alisema marekebisho 10 katika katiba ya Zanzibar yalifanywa baada ya hoja nyingi zisizojibika katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyokuwa ikieleza Zanzibar ni sehemu ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika kuna mambo yalikuwa hayana majibu kama hili la Zanzibar kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano,watu walikuwa wakijiuliza ni kama nini Mkoa? Shehia? Kata? au Kijiji?, haya hayakuwa na jibu katika Katiba ya muungano…kwa sababu hiyo ndipo Wazanzibari wakafanya marekebisho sioni kama ni tatizo” Alisema Mwanasheria Mkuu.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika marekebisho ya 10 ya mwaka 2010, sehemu ya kwanza inatamka kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Sasa kuja kwa haya yametuonesha kwamba kuna wenzetu kumbe wana fikra kwamba Zanzibar iliwahi kutawaliwa, Maana mtu anaposema marekebisho ya 10 ya Zanzibar yamjitangazia uhuru maana yake ana fikra na huyu ni mwanasheria mtu kafika mpaka kuwa Mbunge anayeaminika na chama chake, lakini anasema kwa kufanya hivyo Zanzibar imejitangazia kuwa huru kwani tuliwahi kutawaliwa Aliuliza Mwanasheria Mkuu.

Akisoma hotuba ya kambi ya upinzani Bungeni katika bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano), Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Tundu Lissu alisema Katiba ya Zanzibar inakiuka makubaliano ya Muungano kwa kujitangazia nchi huru kupitia marekebisho ya 10 katiba.

Othman alisema maridhiano ya kisiasa yamefanya Wazanzibari kupitia Baraza la Wawakilishi kufanya marekebisho ya kumi ya katiba ambayo yamefafanua kuwa Zanzibar ni nchi na ndivyo ilivyo kwa sababu haikuwahi kutawaliwa kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wanavyofikiria.

“Marekebisho ya 10 ilichofanya ni kusema kwamba ikiwa mtu hatambui, maana ilikuwa imeshaonesha dalili kwamba kuna wengine hawatambui hilo tena wakubwa. Sasa marekebisho ya 10 yalipokuja ni kufafanua tu, kama kuna mtu hatambui sisi wenyewe tunajitambua” alisema Mwasheria Mkuu katika Baraza.

Akitoa mfano wa muundo wa Muungano wa Taifa la Uswis,Othman alisema Muungano huo ni miongoni mwa muungano uliodumu kwa miaka mingi kutokana na misingi imara iliyowekwa na wananchi wake.

Alisema muungano ambao umedumu na unasifiwa ni Swiss federation kwa sababu umeanza tokea mwaka 1292 na umekwenda kwa mafahamiano hadi mwaka 1874 wakatunga katiba ambayo wameifanyia mapitio upya mwaka 1999 na nchi hiyo ina Serikali 26, lugha nne rasmi na ndio muungano amabo umedumu na nchi ambayo ni imetulia duniani.

“Mheshimiwa Naibu Spika nitumie fursa hii hapa hapa niseme wakati tupo katika mchakato wa maoni ya katiba nadhani ni wakati mzuri kuiweka sawa ile misingi ya muugano kama Uswis”

“Wakati mwengine napata wasiwasi naseme hii khofu yangu niiseme hapa kwamba tunaanza kubishana kuhusiana na watunza nyumba wawe wangapi, waendeshaji nyumba wawe wangapi, wawili, watatu, wanane au watano?. Lakini tatizo letu la msingi mimi nadhani ni nyumba yenyewe iweje. Kama tunaamua kuishi, maana mfumo wa sasa hivi mmoja anaishi nyumba kubwa na mwengine mabandani huko uwani huo sio utaratibu tunao”alisema Mwanasheria Mkuu.

One thought on ““Zanzibar haikuwahi kutawaliwa baada ya 1964””

  1. Mh Othman nakupongeza kumbe nawe umeona kua katika jumba hili la Muungzno sisi wazanzibar tunaishi mabandani tu katika nyumba tuliyoshiriki kuijenga.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.