Na Jabir Idrissa, MwanaHALISI, 4 Julai 2012

Waziri wa Uwezeshaji wa Zanzibar na Mwakilishi wa Makunduchi, Haroun Ali Suleiman.

KAULI aliyoitoa Dk. Ali Mohamed Shein kuhusu Muungano haimsumbui mtu yeyote; si Unguja wa Pemba – Zanzibar. Anaposema Muungano hautavunjika, hakuna anayemsumbua. Anaposema yeye ndiye rais, hivyo hakuna atakayeuvunja Muungano, hakuna anayesumbuka.

Rais anaalikwa kufungua mkutano wa jumuiya ya wastaafu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema atautetea Muungano; na hakuna atakayemlaghai wala kumchezea katika uongozi wake. Waliomnukuu, wanasema Dk. Shein amesema yeye kama rais, hatomuogopa mtu wala kusita kuchukulia hatua wale watakaokwenda kinyume na matakwa ya katiba.

Hili moja ni dhahiri – Dk. Ali Mohamed Shein ndiye rais Zanzibar , na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyorekebishwa mwaka 2010; inamuongezea wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Katika maelezo ya Dk. Shein kwa wastaafu, kuna maneno yanasumbua kidogo labda tu kama umma utaambiwa kuna mtu amehoji mamlaka ya rais.

Anaposema “sitomuogopa mtu yeyote” wengine wanauliza kwani kuna mtu anamtisha rais? Anayemtisha rais anastahili kuchukuliwa hatua haraka ya kushitakiwa. Kwa mantiki ya sheria, kumtisha rais ni kutishia mamlaka ya wananchi waliompa dhamana ya kuongoza nchi yao.

Hili watu wangetarajia kuliona linafanyika haraka. Nataka kuamini hakuna mtu aliyemtisha rais. Kama yupo ni wajibu wa rais kusema “nimetishwa.” Akishasema, ni jukumu la wasaidizi wake kuchukua hatua kulingana na sheria. Kama rais ametishwa, au ametishiwa, huo ni uhalifu. Mhalifu anapaswa kudhibitiwa.

Inapotokea uhalifu umetendeka, ni muhimu vyombo vya dola vikachukua hatua haraka, pasina kusita. Hakuna kuchelewa maana uhalifu huo waweza kudhuhuru mamlaka hii na hivyo kuchochea wananchi kukasirika kwa kuona kiongozi wao anadharauliwa.

Sasa inapotokea uhalifu umetendeka dhidi ya mamlaka ya rais, kasi ya ushughulikiaji wake yapasa iwe kubwa zaidi. Rais si ndiyo alama ya nchi yetu? Sasa tunazubaa nini kumshika anayemhalifu? Labda nimkumbushe rais. Katiba hiyohiyo, Ibara ya 9(2)(a) inazungumzia mamlaka waliyonayo wananchi wa Zanzibar : Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa serikali kufuatana na katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.

Sehemu (b) ya ibara inaelekeza uhakikisho wa usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la serikali. Katika hali hii, baada ya rais kutaka kuyahisi mamlaka aliyopewa na katiba ya nchi, basi ni vema pia akatambua na mamlaka waliyonayo wananchi anaowaongoza kupitia katiba hiyohiyo.

Kutambua mamlaka ya wananchi kuna maana kubwa kiutawala na kiuongozi. Ni suala la kustawisha misingi ya utawala bora na kuilea pia. Kiongozi anayelea misingi ya utawala bora ni yule anayezungumza na wananchi kwa lugha fasaha siyo ya kupinda na kufumba.

Makamu wa Kwanza wa Rais, msaidizi mmoja wapo wa Dk. Shein, Maalim Seif Shariff Hamad, amezungumza na wananchi kuhusu suala muhimu linalojadiliwa sana Zanzibar – Muungano. Anasema, “Hakuna mwananchi atakayeadhibiwa kwa kutoa maoni yake kuhusu mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , iwapo atayatoa kwa utaratibu uliowekwa.

“…Njia pekee ya kuondoa kero za Muungano ni kwa wananchi kujitokeza kutoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni, na maoni yao yatazingatiwa, kuheshimiwa na kufanyiwa kazi kwa kadri watakavyoyatoa.”

Hizi ni lugha mbili tofauti kama mbingu na ardhi. Moja inaelekeza wananchi kutambua wajibu wao katika kile kilichopo mbele yao , huku nyingine ikiwa inayowatisha, inawatia hofu. Kwanini Dk. Shein anawaelekeza watu wamtambue kuwa ana hasira? Majibu yaweza kuwa tofauti kutegemea na yale mtu anayoyasikia au kuyajua kumhusu rais.

Watu waamini pengine rais wao anatishwa? Au anashinikizwa kutaka kile asichokipenda? Au anabanwa na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – asikilize na kutii maelekezo ambayo kwa uoni wake, ni tofauti na dhamira yake au ni tofauti na anavyoona wananchi wanafikiri?

Hebu Dk. Shein aangalie hili. Wakati akitafakari namna Wazanzibari watakavyotoa maoni yao kwa Tume ya Jaji Warioba kuhusu msimamo wao na Muungano, waziri wake, tena wa CCM, ametajwa kuwa ameandika barua moja, kuichapa nakala nyingi na kuigawa kwa wananchi ili hayo ndiyo yawe maoni yao kwa tume hiyo.

Sasa waziri huyu ametajwa hadharani na baadhi ya waliofika kwenye mkutano wa kwanza wa tume hiyo jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, walizionyesha barua hizi na kuzikabidhi kwa tume kama ushahidi.

Barua hiyo inaelekeza maoni yawe serikali mbili. Pengine kungekuwa na barua inayoelekeza wananchi kutoa maoni ya kuwepo kwa muungano wa serikali tatu, ingekuwa kashfa kubwa. Kwa kuwa mtenda hilo ni kiongozi katika CCM, natabiri haitakuwa chochote.

Jimbo la Makunduchi linalowakilishwa na Haroun Ali Suleiman, waziri wa uwezeshaji wananchi, linajulikana kuwa na wafuasi wengi wa CCM ingawa katika miaka ya karibuni limeshuhudia vuguvugu zito la vijana kupenda siasa za mageuzi.

Makunduchi pia ni nyumbani kwa viongozi wengi waandamizi serikalini na katika CCM, akiwemo Waziri wa Ulinzi wa Muungano, Shamsi Vuai Nahodha, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.

Mbinu ya waziri kuandaa barua inaonyesha dhamira ya kulaghai wananchi hasa wale wenye mawazo tofauti na yanayoaminiwa na kiongozi huyo na chama chake, CCM.. Hiyo ni mbinu chafu ya kuwasilisha msimamo. Hakika huko ni kutisha wananchi, kuchezea uhuru wao unaotajwa na Katiba ya Zanzibar ; wa kujieleza na kutoa mawazo yao kwa masuala yanayohusu uendeshaji wa nchi yao.

Mbinu hii yaweza kuchochea vurugu kwa sababu ni kinyume na ahadi ya Jaji Warioba kwamba wananchi wapo huru kutoa maoni yao tume itakapofika kwenye maeneo yao. Pale Dk. Salim Ahmed Salim, mwanadiplomasia mahiri kitaifa na kimataifa, na mjumbe wa Tume, aliposema “tumewasikia wanaopinga Muungano sasa tuwasikie na wanaoutaka,” hakuwa na maana waziri au mawaziri na mtu yeyote yule kuandaa barua au waraka wa kuelekeza watu cha kusema.

Hebu wakubwa wafanye kama huu ni wakati wa mtihani, baada ya mtahiniwa kufanyiwa mazoezi wakati wa maandalizi, aachiwe huru kufanya kwa akili yake anapoingia kwenye chumba cha mtihani chenye ulinzi.

Nilidhani rais Dk. Shein angeshitukia wakubwa hawa wanaolazimisha watu wanayoyaamini wao, japo si lazima yawe ndiyo maoni ya wananchi husika.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.