Na Ahmed Rajab, Raia Mwema, Julai 4, 2012.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.

WA KALE walisema: “Kila upepo una tanga lake.” Na upepo tulio nao leo ni upepo wa kidemokrasia. Alhamdulillahi, leo Watanzania wanaishi katika mazingira ya kidemokrasia ingawa demokrasia yenyewe ni changa na ina mapungufu kadha wa kadha.

Hata hivyo, Wazanzibari na wenzao wa Bara wanaweza kujifaragua kidogo kwa vile wana uhuru wa kukusanyika na wa kusema, wana uhuru wa kutoa maoni yao bila ya hofu ya kuingiliwa na vyombo vya dola.

Sisemi kwamba hivyo vyombo vya dola havijaribu kuuingilia uhuru huo; vinajaribu lakini vinashindwa kwa sababu ya haya mazingira ya kidemokrasi yaliyopo. Hii leo Tanzania haina tena mfumo wa kuwa na chama kimoja kilichojipa uhalali wa kuwa chama pekee cha kisiasa na chenye kiongozi mwenye mamlaka na uwezo unaomfanya awe na amri juu ya mzingo mzima wa kisiasa nchini.

Katika enzi zilizopita kiongozi aina hiyo kwa kutumia njia za halali au za dhulma, alikuwa na tabia ya kulitaka Taifa zima lifuate amri zake, wananchi waitikie ‘amin’ kwa kila alichokisema. Bila ya shaka kiongozi wa sampuli hiyo hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo peke yake. Akifanya hivyo kwa kushirikiana na vibaraka wake pamoja na taasisi za usalama ambazo zilikuwa na kazi ya kuwaziba mdomo wananchi na kuwafanya wasithubutu kutamka hata ‘kwi’ dhidi ya matendo yake kiongozi.

Kinyume na mambo yalivyo sasa siku hizo kulikuwako pia sheria za kimabavu zilizowafanya watawala watende matendo ya kinguvu na kijeuri. Wakati huohuo sheria hizo zikiziminya haki za wananchi. Hiyo ndiyo hali iliyokuwako Zanzibar wakati nchi hiyo ilipokuwa inaendeshwa katika mfumo wa chama kimoja cha kisiasa tangu mwaka 1964 hadi 1995. Hali hiyo ilikuwapo pia Bara.

Katiba ya Zanzibar, katika vifungu vyake vinavyohusika na haki za kimsingi za binadamu, inampa nguvu mwananchi ya kutokubaliana na maamuzi ya kisera ya wale wenye kushika hatamu za utawala wa nchi. Nao huwa ni watu wanaochaguliwa na wananchi wawawakilishe kwa muda maalumu hadi utapofanywa uchaguzi mwingine.

Wakati huo wa uchaguzi ndipo wananchi wanapokuwa tena na uwezo wa ama kuwachagua kwa mara nyingine au kuwatupilia mbali. Aghalabu, wananchi hufanya chaguo lao kwa kuyazingatia matendo ya hao viongozi na huyapima iwapo yalilingana au hayakulingana na matakwa yao.

Visiwani Zanzibar kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hakujasababisha kuvunjwa kwa vyama vya CCM wala CUF, ambavyo ndivyo vyama vikuu vya kisiasa nchini humo. Kilichojiri ni kwamba vyama hivyo vimeunda serikali ya pamoja, inayoviwezesha vitawale kwa ubia.

Lakini vyama hivyo vinakuwa pamoja na vinashirikiana katika utawala kwa muda tu. Utapowadia uchaguzi mkuu vyama hivyo vitachuana tena. Kila chama kitatoa ilani yake na kueleza sera zake. Wananchi ndio wataoamua kwa kura zao chama kipi kiwe na haki ya kutawala.

Katika mfumo wa kidemokrasia pale chama cha kisiasa kinapochaguliwa kutawala huwa kinapewa mamlaka ya kulitawala taifa zima. Chama hicho huwa kina dhamana ya kuangalia maslahi ya wananchi wote — ya wapigaji kura, ya wale waliowachagua, ya wale waliowapinga na kutowapa kura zao katika uchaguzi na hata ya wale wasiokwenda kupiga kura. Vivyo hivyo kwa rais. Hivyo, serikali na rais wake huwa wanatarajiwa kuwa na utawala bora na kuheshimu sheria.

Kwa kawaida katika mfumo wa aina hiyo, viongozi wa serikali hujizuia kuwa na sera za kuwatisha wananchi au za kuzikandamiza haki zao za kimsingi kama zile za kuwa na uhuru wa kukusanyika au wa kutoa maoni wayatakayo — haki ambazo zimo katika katiba ya Muungano na ya Zanzibar. Kutokana na hayo serikali haiwezi kuyatumia majeshi ya usalama kuwanyima wananchi haki zao za kimsingi.

Ni muhimu kuzigusia kanuni hizi japokuwa kwa muhtasari hasa tukiizingatia hali ya mambo ilivyo Visiwani. Ni muhimu kwa sababu sasa Zanzibar imejikuta katika njia panda ikigubikwa na wingu la mjadala unaoendelea kuhusu mustakbali wake na wa vizazi vijavyo vya Wazanzibari ambavyo lazima viepushwe visifikwe na nuksi na maafa yatayotokana na makosa yaliyofanywa na kizazi cha sasa.

Hakuna atayekataa kwamba Zanzibar ya leo ni Zanzibar ya amani, utulivu, umoja na suluhu. Wazanzibari hawajapatapo kuungana namna hivi wakiwa na hamu na lengo moja la kuhakikisha kwamba serikali yao inarejeshewa mamlaka yake yote ya utawala yaliyohamishiwa katika serikali ya Muungano ili iweze kujipangia maendeleo yake.

Ni wazi kwamba zoezi la sasa la mchakato wa kutunga Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania linawapa fursa viongozi wote wa Zanzibar pamoja na Wazanzibari wote kwa jumla kushiriki katika mjadala uliokwishaanza.

Ni jambo jema na la kutia moyo kuona kwamba mjadala huo umewawezesha wengi watoe maoni yao. Kila mmojawao ametamka lake. Miongoni mwao ni Rais wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mawaziri wa Zanzibar pamoja na umati mkubwa wa Wazanzibari waliotoa maoni yao ama binafsi au kwa niaba ya vyama au taasisi zao.

Katika nadhari yangu nionavyo ni kwamba baadhi ya viongozi wamekwishaanza kuyafichua makucha yao na kucheza karata zao wakiwa na lengo la kuwatisha wananchi ili waweze kuwateka kifikra. Si jambo baya wala si dhambi kutaka kumteka mtu kifikra. Hii ni moja ya changamoto za mfumo wa kidemokrasia. Ubaya unakuja pale panapotumiwa vitisho kutimiza lengo hilo.

Kuna mambo mawili mengineyo yanayojidhihirisha pale kiongozi anapotumia vitisho. Kwanza, kwa kutumia vitisho anakuwa anauanika udhaifu wa msimamo wake. Pili, anaonyesha kwamba hajiamini. Kama si dhaifu na anajiamini basi huwa hana haja ya kutumia nguvu au kitisho cha kutumia nguvu kuutetea msimamo wake au kuupinga ule wenye kupingana na wake.

La kusikitisha ni kuwa hivi vitisho vinavyotumiwa na baadhi ya viongozi huko Zanzibar ni moja ya mbinu zao za kuudhoofisha uzalendo Wakizanzibari na kupunguza kasi za mjadala unaoendelea.

Ni muhimu kwamba mjadala huo uendelee kuwa huru na wazi. Kadhalika, ni muhimu kwamba matokeo ya mjadala huo yawe ni kutimizwa kwa matakwa ya wengi wa Wazanzibari wenye kusema kila uchao kwamba hawaridhiki na hadhi yao na ya nchi yao katika mfumo wa sasa wa Muungano na Tanganyika. Huu ni ukweli usiofichika tena na ni ukweli ambao kwa muda mrefu umekuwa ukidhulumiwa.

Itakuwa dhambi kubwa endapo kiongozi yeyote atatumia madaraka yake kuwatisha wananchi ili wasiweze kuwa na uhuru wa kutoa maoni yao. Kadhalika, ni dhambi kwa kiongozi yeyote kuwarushia vumbi wananchi kwa nia ya kuwaziba macho ili wasiweze kupambanua baina ya haki na kisichokuwa cha haki.

Kisichokuwa cha haki si kingine ila dhulma tupu. Na ni dhambi kubwa kukubali dhulma na maonevu yanayofanywa na viumbe wengine. Historia daima itakuwa ikimlaani kiongozi sampuli hiyo mwenye kuipalilia dhulma. Historia haitosita hapo bali itawalaani wote wale wenye kunyamaza kimya, wenye kuwaachia viongozi kama hao waendelee kucheza ngoma zao.

Sitokuwa ninafichua siri nisemapo kwamba wengi wa Wazanzibari hawana imani na katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Hawana imani si na vifungu vyake tu bali hata na haja ya kuwako kwa katiba yenyewe. Wala si siri tena kwamba Visiwani Zanzibar watu wataingiwa na ghadhabu na watapiga makelele endapo mchakato huu wa katiba utahitimishwa kwa pendekezo la kuwa na aina ya mfumo wa utawala utaoushabihi mfumo uliopo sasa wa Muungano wa Katiba.

Bahati iliyoje kwamba hii leo Wazanzibari wanazitambua vilivyo haki zao na hakuna kundi lolote miongoni mwao, au hata jumuiya yoyote huko Zanzibar, yenye nia ya kuichafua hali iliyopo ya amani, utulivu na umoja. Hali hiyo imeyafanya mashindano ya kisiasa kati ya vyama vikuu Visiwani humo yawe ni mashindano ya amani na ya kiungwana.

Hali hiyo pia imewafanya Wazanzibari wawe na fikra moja kuhusu Muungano bila ya kuijali misimamo rasmi ya vyama vyao. Ndiyo maana ikawa si siri kwamba lau itapigwa kura ya maoni ya kuwataka Wazanzibari waseme kama wanautaka au hawautaki Muungano kama hivi ulivyo wengi wao wataukataa. Kwa hali hizo na ikiwa inazikubali kanuni za kidemokrasia basi serikali ya Zanzibar inakuwa haina budi ila iyatetee matakwa ya Wazanzibari. Lazima iwe na ujasiri wa haki kuiita haki. Kutenda kinyume na hivyo itakuwa ni kuwafanyia khiyana Wazanzibari na kuwadhulumu wanapotetea haki yao.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.