Hoja ya Wazanzibari ni mamlaka kamili ya nchi yao na kisha ndio Muungano wa Mkataba na Tanganyika.

Na Khalid Gwiji

Muungano wa Katiba uliopo umekuwa ndio chanzo cha migogoro yote ya muungano huu. Watanzania wote ni mashahidi wa jinsi mfumo wa aina hii ulivyoshindwa kuweka utulivu na maridhiano katika mahusiano ya nchi zetu mbili. Zaidi ya yote umeshapitwa na wakati na hauwezi kuhimili mageuzi ya kikanda na kimataifa yanayotokea.

Mbali na kero zilizoshinda za humu humu ndani, lakini tuchukulie mfano mdogo wa kuwepo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushiriki wa Tanzania. Zanzibar haimo kama mwanachama katika Jumuiya hii bali iliyomo ni Tanzania. Kati ya mambo 18 yanayoshughulikiwa na Jumuiya hii, ni mambo 4 tu ambayo ni ya muungano na ambayo Tanzania ina mamlaka ya kisheria kuiwakilisha Zanzibar. Kwa yaliyobakia 14 Tanzania kuiwakilisha Zanzibar ni kwenda kinyume na Katiba.

Hata suala la Zanzibar kujiunga na OIC lilikwamishwa kutokana na mfumo wa muundo huu na Tanzania ikadai ingejiunga kwa vile ndio yenye mamlaka. Takriban inakaribia miaka 20 tokea kutolewa kwa ahadi hio lakini wananchi hawajaelezwa maombi yalikwama wapi.

Hata hivyo, hili la OIC ni utashi wa kisiasa au kidini tu ndio uliokwamisha; lakini mfumo huu wa Muungano wa Kikatiba unasutwa hata na maumbile ya mataifa haya yaliyoungana. Kwa mfano upo umoja wa visiwa vya Bahari ya Hindi ambao Zanzibar kama kisiwa wanastahiki kujiunga, lakini Zanzizibar ambayo ni kisiwa inaambiwa haina mamlaka; na hio Tanzania yenye mamlaka haiwezi kujiunga kwa vile sio kisiwa – hii imepelekea Zanzibar kukosa haki zake mbali mbali za kimaendeleo.

Njia pekee kwa sasa ambayo itakata mzizi wa fitina ni kuwa na Mashirikiano ya Mkataba na si ya Kikatiba. Haya ni mashirikiano mema ambapo kila nchi inajitegemea na inabaki na serikali yake, na uendeshaji wa mambo yake, utaifa wake n.k, na huingia katika mashirikiano kwa njia ya Mkataba (Treaty) juu ya mambo maalum yaliyo wazi na kwa utaratibu wanaokubaliana hizo pande mbili au zaidi zinazoshirikiana.

Mifano ya aina hii ni kama EAC (Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi) na Europena Union ulio na nchi wanachama 27. Uzuri wa muundo huu ni kuwa unatoa fursa kwa nchi zilizoshirikiana kuweza kuuagalia kila inapobidi ule mkataba wao bila vikwazo vya Kikatiba na hivyo kusukuma mbele maslahi yao bila kumezana, kubebana au kuoneana.

Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Kwanza – JWZK!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.