Baraza la Wawakilishi la Zanzibar

Na Khalid Gwiji

 

Tujipe somo la upishi wa kuoka keki hapa. Weka unga kwenye chungio. Uchunge vizuri. Unga laini na mzuri utapenya chini na ule mbaya utakaa juu. Niko sahihi? Lakini sisi tunakula keki, kwa hakika. Hii ni methali. Keki katika muktadha wa hapa ni Zanzibar iliyo na mamlaka kamili kitaifa na kimataifa.  Chungio ni uchaguzi. Unga mzuri ni wawakilishi makini wanaojua kuwa ile ni amana inayoambatana na jukumu la kuwatumikia wananchi. Matapitapi ni wawakilishi wanaotawaliwa na utashi wa ubinafsi na usaliti, vigeugeu.

Kwa ajili hiyo, tunahitaji Wawakilishi wanaoelewa kuwa Zanzibar inayo haki kujiamulia mambo yake yenyewe na kujitegemea. Hakuna anaepaswa wala alie na uwezo wa kuiamulia Zanzibar. Tunahitaji Wawakilishi wanaoelewa kuwa Wazanzbari wanahitaji kujitawala na kwamba Zanzibar ijifungue kabisa kutokana na pingu za Muungano.

Nikisema hivyo, sina maana ya kufuta uwezekano wa ushirikiano baina ya Zanzibar na Tanganyika, au Rwanda, Kenya, Burundi, Uganda au nchi za visiwa nk; mradi tu ushirika huo uwe katika misingi ya Mkataba na sio Katiba ambao utakubaliwa baada ya majadiliano na msingi wa usawa, uwazi kwa wote wanaoshiriki.

Tunahitaji Wawakilishi wanaojua kuwa sisi wananchi hatukubali hata kidogo hali ya umaskini na kukosekana kwa maendeleo ya kielimu na kiuchumi kama ilivyo sasa.

Tunahitai Wawakilishi watakaoziunga mkono juhudi zetu za kuirudishia Zanzibar mamlaka yake ndani na nje na kwamba juhudi hizo ni za taifa zima zinazojumuisha haki za Wazanzibari WOTE; na kwamba Wazanzibari WOTE watapata fursa sawa na heshima ya kibinaadamu.

Tunahitaji Wawakilishi wanaotambua kuwa kila Mzanzibari anayo haki kamili ya uhuru katika mambo ya uchumi na siasa. Lazima Wawakilishi watambue kuwa wana wajibu wa kutimiza mahitaji ya Wazanzibari. Wao si zaidi ya ‘watumishi’ wetu; na lazima iwe hivyo; na watumishi hawawezi kuwa na haki zinazozidi mabwana zao. Wana kazi nyingi zaidi na majukumu mengi zaidi. Na mabwana wa Wawakilishi ni wananchi; na lazima iwe hivyo.

Wawakilishi lazima wawe wazalendo wenye kuwa tayari kujitolea kwa ajili ya kudai mamlaka ya Zanzibar, na kazi zao ni lazima ziwe na shabaha ya kuihudumia Zanzibar na Wazanzbari WOTE kwa ujumla wao. Wanapaswa wawe wakweli, maana nchi huhudumiwa katika ukweli. Wanalazimika wasimame katika ukweli kama wanavyouona, bila ya kujali yatakayowatokea wao binafsi.

Zanzibar inahitaji ukweli kutoka Baraza lake la Wawakilishi. Tunapambana na matatizo mapya, tunahitaji ujuzi wote unaoweza kupatikana katika kuyatatua. Vile vile, Baraza la Wawakilishi lazima liwe chombo kinachotumikia taifa; lijitolee kuhakikisha na kutafuta maendeleo ya Zanzibar na ya Wazanzibari. Lazima liwe ni chombo kinachotoa huduma ya kizalendo, na kwa sababu hiyo, itakuwa ni huduma ya kweli na ya moyo.

Mafano wa juu wa keki ni kuwa uchaguzi utakapofika, hatutadaiwa kupiga kura ya ahsante kwa kazi za siku zilizopita au kwa wasaliti na vibaraka; tutaombwa kupiga kura kwa mtu tutakaemchagua atakaeweza kututumikia katika siku zijazo. Kazi ya siku zilizopita ni kipimo kimoja tu cha uwezo wa mtu kututumikia; siyo ‘hirizi’ ya uwezo wa siku za mbele.

Jamhuri ya Watu wa Zanzibar – KWANZA !

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.