Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume.

Na Ahmed Rajab

ULE mjadala mkubwa — na mkali— unaovuma na kuchaga Visiwani Zanzibar kuhusu mustakbali wa Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar umefichua jambo moja lenye kuwagusa na kuwaunganisha Wazanzibari wengi.  Nalo ni dai la kutaka pafanywe mageuzi ya kimsingi katika mahusiano baina ya hizo nchi mbili zilizo katika Muungano wa Tanzania. Wanapoulizwa kwa nini wanasisitiza mahusiano hayo yageuzwe wanatoa kila aina ya sababu.  Baadhi yao wanazieleza sababu hizo kwa makini wakizijenga juu ya misingi ya hoja za kimantiki.  Wengine  wanajibu kwa jazba.

Shutuma wanazozitoa ni nzito.  Kuna wanaosema kuwa miaka 48 ya Muungano haikuinufaisha kitu Zanzibar.  Kuna wanaosema kuwa Muungano umeifanya Zanzibar itoweke kwenye ramani ya dunia.  Kuna wasemao kuwa Muungano umeifanya Zanzibar idhurike kisiasa, kiuchumi na kijamii ikilinganishwa na visiwa vingine kama vile Mauritius na Seychelles.

Kuna wanaoutupia Muungano lawama zote za dhiki za kiuchumi na shida za kijamii zilizoisibu Zanzibar kwa muda wa takriban nusu karne.  Wanasahau kwamba katika kipindi chote hicho pamekuwako na utawala mbovu Visiwani na kwamba matatizo mengine ni ya kujitakia wenyewe.

Kadhalika, kwa vile Zanzibar imepoteza mamlaka muhimu ya kidola kwa kuungana na Tanganyika kuna wanaokereka na utata uliopo kuhusu hadhi ya Zanzibar: iwapo ni nchi ama si nchi ndani ya Muungano.  Wanalalama kwamba Zanzibar haina uwezo wala uhuru wa kujiamulia yenyewe njia gani ya kiuchumi na kijamii ya kuifuata ili iweze kujigomboa kutokana na shida ilizo nazo.  Wananung’unika kwamba kwa muda wa miaka 48 serikali ya Muungano haikuyatumia vyema madaraka iliyoyatwaa kutoka Zanzibar kupigana na umasikini, magonjwa na ujinga.

Bara pia kuna watu wenye mtizamo sawa na ule wa Wazanzibari wenye kutaka mageuzi ya kimsingi yafanywe katika mahusiano ya Tanganyika na Zanzibar.  Baadhi yao nao pia wana jazba na wanasema kwamba Zanzibar imekuwa mzigo wa Bara na kwamba potelea mbali iachwe itokomee.  Wanasema kwamba Wazanzibari hawana kheri na waachiwe wajionee wenyewe kitachowafika watapouua Muungano.

Visiwani Zanzibar hakuna mgogoro kuhusu nini uwe mustakbali wa visiwa hivyo.  Inavyoelekea ni kwamba wengi wa wananchi wa huko wanaiunga mkono ile wanayoiita Ajenda ya Zanzibar yenye lengo la kuirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili ya kidola na kubadili mfumo wa mahusiano kati ya Zanzibar na Tanganyika.

Huenda ikawa Wazanzibari wanatofautiana juu ya mbinu za kulifikia lengo hilo lakini si juu ya mkakati wenyewe kwani hata wale wasio na imani na mchakato wa sasa wa kuiandika upya katiba ya Tanzania nao pia wanakubali kwamba mustakbali wa Zanzibar unapaswa uwe wa uhuru na utaoirejeshea Zanzibar mamlaka yake kamili ya kujitawala.

Huo muundo mpya wa ushirikiano wa baadaye wanaoutaka baina ya Zanzibar na Tanganyika ni tofauti kabisa kinadharia na kiutendaji na ile dhana ya kuuimarisha Muungano ambayo huenda ikawa na maana ya kuwa na serikali moja katika taifa moja.

Dhana hiyo si ngeni.   Viongozi kadhaa wa Tanzania wamekwishawahi kuipigia debe.   Mmojawao ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye mnamo mwaka 1995 katika hafla yake ya kuyaacha madaraka alisema wakati umefika wa kuwa na Muungano wa serikali moja.   Miaka kadhaa baadaye alipoulizwa iwapo Zanzibar ni nchi au si nchi alisema hajui.

Hamna shaka yoyote kwamba ukiibuka Muungano wa aina hiyo anaoutaka Mwinyi wa kuwa na serikali moja nchini Tanzania basi itabidi pasiwepo Serikali ya Zanzibar na pingine visiwa vya Unguja na Pemba vitakuwa mikoa au tarafa za Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.  Nakumbuka Dk Mohamed Gharib Bilal alipokuwa waziri kiongozi wa Zanzibar aliwahi kusema kwamba hilo halitotokea hata miaka 100.

Kwa upande mwingine,  kuna watu Bara wanaoamini ya kuwa muundo bora wa Muungano ni wa kuwa na ‘Dola moja, serikali mbili.’  Katika muundo huo Zanzibar itakuwa huru kuyashughulikia mambo yake yote yasiyo ya Muungano.  Hivyo, kwa kiwango kikubwa Muungano utabaki kama ulivyo isipokuwa tu utafanyiwa marekebisho ya hapa na pale ya kuzibaziba viraka na kuondosha zile zinazoitwa ‘kero’ za Muungano .

Halafu kuna wanasiasa na wasomi wa Bara wanaohisi kwamba lazima pawepo na ‘nipe, nikupe’ na hivyo pande mbili za Muungano zisikilizane na zikubaliane kuwa na Muungano wenye muundo wa shirikisho wenye serikali tatu.  Muundo huo utahakikisha kwamba Muungano unaendelea kuwapo.  Wenye kutoa rai hiyo wanashikilia kwamba muundo huo wa shirikisho uwe miongoni mwa mapendekezo yatayozingatiwa na Tume ya Katiba.

Mapendekezo yote hayo ya kikatiba yana ila moja: yanazinyima Zanzibar na Tanganyika na hivyo watu wa nchi mbili hizo za kindugu haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe na kuwa na uhuru wa kujipangia mambo yao bila ya kuingiliwa na wageni; yaani bila ya Watanganyika kuyaingilia mambo ya ndani ya Zanzibar na bila ya Wazanzibari kuyaingilia mambo ya ndani ya Tanganyika.

Kwa hivi sasa Zanzibar na Tanganyika haziwezi kuwa na hata vyama  vyao vya kisiasa visivyo na sifa au sura ya kimuungano.  Wazanzibari kadhalika wanapinga nguvu za walio wengi kuwaamulia wasio wengi na wanaiona hali hii kuwa ndilo tatizo kubwa ambalo lazima litafutiwe ufumbuzi ili maslahi na mahusiano ya baadaye ya nchi hizo mbili yasihasirike.

Hadi sasa nimekuwa nikiuzungumzia muundo wa Muungano uliojengwa juu ya mfumo wa kikatiba.  Lakini mfumo huo una madosari mengi na haufai kwa mahusiano ya nchi mbili zilizo huru na zilizo na usawa machoni mwa sheria ya kimataifa na mwenendo wake ambao hauruhusu kuwako kwa ile dhana ya ‘ukaka’ kwani nchi zote, ziwe kubwa au ndogo, zinaangaliwa sawasawa kisheria na jumuiya ya kimataifa ilimradi ziwe huru na ziwe na mamlaka kamili ya kidola.

Ndiyo maana  kuna Wazanzibari wengi wa itikadi zote za kisiasa, wa vyama tofauti vya kisiasa na hata wasio wanachama wa chama chochote wanaopinga kabisa aina yoyote ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Wanachotaka wao ni kurejeshwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baada ya kura ya maoni itayowauliza Wazanzibari iwapo wanautaka au hawautaki Muungano. Watu wenye fikra hiyo wanahisi kwamba huu mchakato wa sasa wa katiba unastahiki ufanywe baada ya hiyo kura ya maoni.

Kinyume nao ninavyohisi ni kuwa wengi wa Wazanzibari hawauoni mchakato huo wa katiba kuwa hauna maana.  Wanavyoona wao ni kuwa mchakato huo ni fursa nzuri waliyoipata ya kulitanzua tatizo liliopo.

Wanakumbusha kwamba kinyume na mambo yalivyokuwa zamani safari hii wananchi wenyewe wanashiriki katika mchakato wa katiba utaomalizika kwa kupigwa kura mbili za maoni — moja Bara na nyingine itapigwa Zanzibar. Wanaamini kwamba matokeo yake yatakuwa kupatikana mfumo mpya wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili zilizoungana kikatiba tangu Aprili 1964.

Baada ya kuukataa muundo wa Muungano wa Katiba, wanatoa hii dhana ya mfumo ulio tofauti kabisa yaani mfumo wa Muungano wa Mkataba.  Wengi Visiwani hivi sasa wanaiunga mkono dhana hii ambayo pengine ndio yenye suluhisho bora na mujarab kwa Muungano.

Mahusiano yatayojengwa kwa Mkataba yatairejeshea Tanganyika na pia Zanzibar mamlaka yao kamili ya kidola na yatawezesha kuwapo na utaratibu wa ushirikiano kati ya nchi mbili zilizo sawa na zilizo huru na zenye mamlaka kamili ya kidola.

Mkataba utaoongoza mahusiano hayo utaweka wazi ni mambo gani nchi hizo zitashirikiana na namna ushirikiano wao wa baadaye utavyokuwa.

Pale nchi iliyo na mamlaka yake kamili inapoandikiana mkataba wa kuwa na ushirikiano au muungano na nchi nyingine inakuwa haiyapotezi mamlaka yake au uhuru wake.  Hali hiyo ni kinyume na Muungano wa kikatiba uliopo sasa ambao umeifanya Zanzibar iyahaulishe kwenye Serikali ya Muungano mamlaka na madaraka yake ya kimsingi.

Zanzibar imezitoa mhanga nguvu zake za kidola wakati mwenzake Tanganyika haikulazimika kujitosa na kutoa mhanga kama huo kwa vile utawala wa Tanganyika unaendeshwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Jambo jingine lenye kuvutia panapokuwako ushirikiano au muungano wa Mkataba ni kwamba kila nchi iliyotia saini mkataba wa muungano inakuwa na nguvu ya ‘turufu’.  Hivyo hata katika mambo yaliyokubaliwa kuingizwa katika ushirikiano nchi inayohusika inaweza kuitumia nguvu yake ya turufu na ikaomba hifadhi ya watu wake endapo inahisi kwamba inahatarishwa na sera za huo muungano katika utekelezaji wa mahusiano na ushirikiano wa nchi hizo.

Muungano wa aina hiyo, yaani wa Mkataba, utairejeshea Serikali ya Umoja wa Kitaifa mamlaka na  madaraka muhimu ambayo Zanzibar haikuwa nayo kwa muda wa miaka 48.  Yakitumiwa vyema madaraka hayo yataiwezesha Zanzibar kutekeleza sera zitazoirejeshea Zanzibar adhama na fahari iliyokuwa nayo zamani na kuifanya ishiriki kikamilifu katika shughuli za kanda ya Afrika ya Mashariki na ya Kati na hata kupindukia mipaka ya kanda hii.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.