Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi juu ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

TUME ya Mabadiliko ya Katiba mpya Tanzania, tayari imejipanga kupokea maoni ya wananchi kuhusu masuala yoyote yanayohusu nchi hiyo pamoja na hoja za kuvunja Muungano, ama venginevyo. Akizungumza katika uzinduzi wa Shughuli za Tume jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alisema Katiba mpya ni lazima kujadili mambo yaliomo kwenye Katiba ya sasa likiwemo suala la Muungano.

Jaji Warioba, alisema wanatarajia ikifika mwishoni mwa mwaka huu, kumaliza kazi ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi na mapema mwakani wataanza kazi ya kukuandika mapendekezo ya Rasimu ya Katiba Mpya.

Alisema kazi yao ni kupokea maoni ya wananchi na kama watataka marekebisho kuhusu aina ya muundo wa Muungano, mipaka ya nchi na kadhalika, ni jumla ya mambo TISA ya msingi yaliyomo katika Sheria:

“Kwa kufuata sheria tunapokea maoni ya kila aina ikiwa ni pamoja na suala la Muungano, hata ikiwa wapo wanaotaka uvunjwe nasi tutayachambua,” alisema na kufafanua:

“Ninawahakikishia wananchi kuwa Tume hii itafanya kazi kwa uwazi na maoni yote yatakayosikilizwa yatafanyiwa kazi ipasavyo,” alisema Jaji Warioba.

Alisema wanalazimika kutumia busara ya kutosha kusikiliza maoni ya wananchi, na wasipofanya hivyo watakwama katika kura za maoni, baada ya kutoka katika Bunge Maalumu la Katiba.

Jaji Warioba alisema Tume itaanza safari za kwenda Mikoani hivi karibuni, na imejigawa makundi saba ambapo kila kundi moja litafanya safari mara nne za kwenda Mikoani kuanzia sasa hadi mwisho wa mwaka huu.

Alisema kwa wastani kila kundi litafanyakazi kwa mwezi mmoja kila Mkoa isipokuwa Mikoa midogo ambako Tume itatumia muda mfupi.Tume itaanza kusikiliza maoni ya wananchi kwa Mikoa ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga:

“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kwa uwazi bila hofu na kwa utulivu, wawe wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza maoni ya wengine hata kama hawakubaliani nayo,” alisema Jaji Warioba.

Alisema lengo la Tume ni kuhakikisha Watanzania wote wanatoa maoni, kwa kuzingatia ukubwa na mazingira ya nchi, hawataweza kuonana na kila mtu ingawa wanataka wapate maoni ya watu wote kwa njia mbalimbali:

“Pia kutakuwa na mfumo wa kupokea maoni ya raia wote Watanzania wa ndani na nje ya nchi kwa kutumia simu, barua pepe, mitandao ya kijamii ya Facebook, twitter, blogu pamoja na njia ya Posta,” alisema jaji Warioba.

Alisema katika mikutano ya hadhara ya wananchi, maoni yao yatakuwa ya kiandikwa na kurekodiwa kwa video, ili kuwa rahisi kuchambuliwa, na baadae kutunzwa katika Maktaba za Taifa kwa matumizi ya baadae.

Mwenyekiti huyo, amesema wametayarisha nakala 500,000 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, nakala 10,000 za Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na nakala 500,000 za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012.

Jaji Warioba alisema wanafahamu nyaraka hizo hazitoshi na hata kama zikipatikana kwa wingi, ni vigumu wananchi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi. Pia zimetayarisha nyaraka zinazosomeka kwa urahisi na kueleweka:

“Nyaraka hizo ni Katiba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Lugha Nyepesi, Hadidu za Rejea, Programu ya Elimu kwa Umma na Utekelezaji wa Kazi za Tume ambazo tayari wameanza kuzisambaza,” alisema Jaji Warioba.

One thought on “Tume kupokea maoni yote hata ya kuuvunja Muungano”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.