Nafikiria wengi tumeyasikia maneno ya Mheshimiwa Mansour Yusuf Himid, mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki na waziri mwandimizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nataka kwanza kumpongeza kaka yetu Mansour kwa ujasiri wake na mapenzi yake kwa Zanzibar na kwa Tanzania kiujumla.

Mansoor Yussuf Himid
Mansoor Yussuf Himid

Mheshimiwa Mansour amegusia suala muhimu katika mustakabali wa Muungano wetu, na ametuonyesha kwamba CCM ipo tayari kusikiliza maoni ya Wazanzibari juu ya mfumo gani wanaoutaka wa Muungano wa Tanzania. Ameeleza kinagaubaga kwamba muungano unawezekana kuendelea katika mfumo mpya wa mkataba baina ya nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar kama vile muungano wa nchi za Ulaya.

Na Foum Kimara
Na Foum Kimara

Mheshimiwa Mansour hakumalizia hapo tu, bali amechambuwa kwamba katika dunia ya sasa ya utandawazi ni muhimu kujuwa kwamba muungano wa nchi mbili unawezekana ukaimarika zaidi bila ya nchi moja kupoteza utambulisho, uraia wala asli yake.

Akamalizia kwa kusema kwamba Zanzibar inaweza kufarajika zaidi katika mfumo mpya wa maelewano mazuri zaidi na Tanganyika katika mfumo wa kimkataba, huku baadhi ya sekta za serikali zikibakia ndani ya uongozi wa serikali husika na baadhi kubakia katika mikono muungano.

Aligusia pia kuhusu kiti cha Zanzibar kwenye Umoja wa Mataifa, kwamba tunaweza kurejesha kiti chetu bila ya kuvunja Muungano wa udugu baina yetu na Tanganyika katika mfumo huo mpya.

Kikwete, Seif na Karume wanastahiki sifa

Serikali ya Mheshimwa Dr. Jakaya Kikwete imejitahidi sana kuondosha zile kadhia za kukandamiza wananchi, na binafsi nampongeza Rais Kikwete kwa kuwa muwazi na mpenda demokrasia ya kweli. Wale wengi waliomsikiliza katika hotuba yake ya mwanzo tangu kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, watakumbuka kwamba alisisitiza kulisimamia suala la Zanzibar na kuhakikisha migogoro yote baina ya wanasiasa inamalizika na hata migogoro ya Muungano.

Rais Jakaya Kikwete

Tuanze na kuangalia namna gani hakuingilia muundo wa katiba mpya ya Zanzibar na namna gani amewaachia Wazanzibari kuamua nini wanachokitaka katika muundo wa serikali mpya. Haya maneno ya CHADEMA kwamba Rais Kikwete ni dhaifu, ni kwa sababu ya mtazamo na msimamo wake juu ya Tanzania mpya yenye uhuru zaidi na Zanzibar mpya yenye nafasi inayoridhiwa na wananchi katika masuala ya muungano.

Wazanzibari tuwashukuru sana Dr. Amani Karume kwa kuweka msingi madhubuti wa serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na Maalim Seif kwa jitihada zao katika kuondosha dosari zilizodumu kwa takriban miaka 20.

Kukubali kuondowa tafauti zao za kisiasa na kukaa pamoja kushirikiana pole pole kuendeleza gurudumu la maendeleo ya nchi kumepelekea nchi kurejea katika hali ya utulivu na amani ambayo yapaswa kudumishwa.
Rais Shein na Makamo wake, Maalim Seif, ndio kikatiba na kidemokraisia waliopewa dhamana na asilimia 98 ya wananchi kuliongoza taifa hili la Zanzibar kwa kile wananchokiamini kuwa ndicho chenye maslahi mazuri zaidi kwa nchi.

Masuala ya uongozi hayataki wakuu wa nchi kufuata mada zinazopendwa sana tu na watu, bali ni kile wanachokiamini kuwa na  maslahi kwa wananchi na taifa kwa jumla. Wananchi walio wengi ndio waliowapa haki ya mwisho ya maamuzi yao bila ya upinzani.

Anayekufa kwa sukari, hana haja ya kupewa sumu

Kama kuna watu baina yetu wanaoamini kwamba serikali haipo sawa katika masuala fulani, kwa mfano ya kura ya maoni, basi njia iliyo madhubuti ya kupinga maamuzi ya serikali ni kwa kutumia haki yao ya kidemokrasia katika uchaguzi unaofuata kwa kuenda kinyume na masharti ya wapiga kura wao.

Amani Karume (kushoto), Maalim Seif (kulia) mashujaa wa Zanzibar.

Masuala ya kura ya maoni yanaweza kukubalika au kukataliwa na serikali bila ya serikali kuwajibika, kwa sababu ya ile idhini  ya kura walizoshinda katika uchaguzi mkuu.

Mifano ipo tele katika nchi zilizojengwa katika misingi ya demokrasia kuliko Tanzania, mfano Uingereza ambako wananchi wengi kwa miaka wamekuwa wakililia kura ya maoni ya kuitoa katika Umoja wa Ulaya huku serikali zote tokea ya Labour na hadi sasa ya Conservative na LibDems kuwa wawazi kwamba hawako tayari kuwapa wananchi haki yao hiyo kwa sababu kubwa kwamba hilo halikuwa katika manifesto ya chama kabla ya uchaguzi na wananchi walijuwa hilo mapema na still wakawachagua.
Maombi yangu kwa sasa kwa jamii ya Wazanzibari kukaa chini na kutafakari njia mpya za kuimeguwa Zanzibar katika mfumo wa sasa potofu wa Muungano kwa kutoa masharti mapya ya namna gani muungano uendeshwe na kwa mfumo wa aina gani.

Kama lengo kuirejesha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, basi katika mfumo wa mkataba tunaweza kuirejesha serikali iliyohuru na kutambulika kama nchi kamili huku tukifaidika na muungano mpya uliojengwa kwa misingi ya usawa na umoja wa kimaendeleo. Tukumbuke Wazanzibari kwamba umoja wetu ndio msingi wa maendeleo makubwa ya visiwa hivi.

Tuangalie ugumu wa kura ya maoni katika mifano ifuatayo: kwanza, katika daftari la wapiga kura, wanaostahili kupiga kura ya maoni ni watu wasiozidi laki sita kwa Zanzibar yote. Takwimu kutoka Bara zinaonyesha kwamba Dar es Salaam peke yake kuna Wazanzibari 350,000. Je, Tanzania nzima?

Dhana kubwa inayowahofisha viongozi wa serikali juu ya kura ya maoni ni kwamba jee ikiwa 30% ya Wazanzibari wanaoishi Zanzibar wataukubali muungano wa sasa au wa serikali moja wakiungwa mkono na Wazanzibari laki tatu na nusu kutoka Bara, kweli kutakuwa na Zanzibar huru? Au kukiwa na matokeo ya kati na kati bila ya majibu sahihi itakuwaje?

Tukumbuke kwamba asilimia karibu 40 ya Wazanzibari waliyapinga Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya 2010. Sasa ikiwa watajumuika na Wazanzibari waishio Bara itakuwaje?
Kwa upande wa upinzani, mazingatio yao makubwa yalilenga katika Tume ya Uchaguzi ambayo imekuwa ikiilalamikia kwa miaka zaidi ya ishirini kuwa haitendi haki, wakitathmini kwamba matokeo pia yakitangazwa kinyume na matarajio yao itakuwa na athari gani kwa Zanzibar mpya?

Muungano wa Mkataba ndio suluhisho

Suluhisho kubwa lililowafikiwa kwa wote ni kuwaachia wananchi kutoa maoni ya mfumo upi wanautaka na serikali kulinda maamuzi ya wananchi hao na ndio maana kura ya maoni ya kuwepo au kutokuwepo kwa Muungano imekuwa ngumu kupitishwa na wanasiasa wengi wa visiwani kwa hofu hiyo.

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume.

Katika mfumo mpya wa mkataba, Zanzibar itaweza kurejesha mamlaka yake iliyoyapoteza tokea kuunganika na Tanganyika na Zanzibar, huku Muungano ukilenga masuala ya kiserikali yasiyoingilia uhuru wa kitaifa au maamuzi ya maslahi ya taifa la Wazanzibari.

Ndio tukasema katika mfumo huu wa mkataba kila Mzanzibari ni mshindi, kwa wapenda muungano (wale asilimia 40 Zanzibar na Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara) hawatakuwa na ile khofu ya kupoteza mali zao walizozichuma kwa jasho lao. Wale wanaopendezewa kurejea kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwanza, basi pia kiu yao itakuwa imepatiwa ufumbuzi, kwani muungano wa kimkataba hauondoshi utaifa wa nchi zilizoungana.

Na mwisho wasioutaka Muungano kabisa watakuwa na haki ya kuukataa kata kata katika kura ya maoni kwa yale yaliyopendekezwa kuwamo katika muungano au katika chaguzi zijazo.
Wazanzibari tusahau tafauti zetu na tuachane na masuala ya wapi asili zetu zimetokea. Tukae pamoja kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuirejesha Zanzibar katika ramani ya kimataifa.

Kubakia kwa muungano kunawezekana bila ya kupoteza utaifa wetu. Tutapokaa tukabishana na kupigana miongoni mwetu, basi ni sawa na vita vya panzi faida kwa kunguru.

Hivi tutathmini kwamba kura ya maoni ndio njia pekee ya kuirejesha Zanzibar katika mamlaka ya uhuru pekee? Ikiwa njia hii imeweza kutumiwa kuwagonganisha Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe, jee ni hekima kushikilia msimamo huo huku tukijuwa inaweza kuwagawa Wazanzibari katika makundi yatayoimega Zanzibar kidogo kidogo?

Kama ipo njia mbadala, kwa nini tusitumie kuleta msimamo mmoja wa Wazanzibari wote? Hebu tukae chini tufikiri kwani kura ya maoni hazijapigwa tokea mwaka 1995 mpaka 2000 na jee matokeo hayajulikani? Tafauti gani ya miaka ya nyuma na sasa wakati mfumo ndio ule ule?

Tufikiri namna gani Scotland imeweka mikakati ya kushinda kura ya maoni yao: kwanza, imepangwa kupigwa katika mwaka 2014 kwa sababu ndio historia ya Scotland ya kujitenga inapokuwa muhimu. Jengine ni kuhakikisha hata wale wenye miaka 16 wanapiga kura kwa sababu wanajuwa vijana wengi ndio wanaunga mkono kujitenga kwao.

Kwa sisi Wazanzibari, nini mkakati wetu katika kura ya maoni? Je, haitakuja kututia shimoni zaidi ikiwa Tume itaamua kutangaza matokeo yasiyo sahihi? Au tuseme haya masuala ninayoyauliza ni ndoto zaidi kuliko ukweli ulivyo?

Kama wametupa hadidu rejea katika kujadili katiba mpya wakisistiza kujadili kuvunja Muungano ni kosa la jinai, basi kwa nini tushindane nao kimaguvu wakati nafasi na sisi tunayo ya kuwapa hadidu rejea zetu ya namna gani mfumo mpya wa Muungano tunaoutaka? Hivi sote tukisema tunataka muungano wa kimkataba wenye lengo la kuirejesha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, hatutafaidika na Umoja wetu? Akushindae kwa matonge mshinde kwa kutoelea.

4 thoughts on “Muungano wa mkataba ndio dira yetu”

 1. Binafsi nimefarijika na kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusiana na Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba kuwa watakusanya maoni pia kuhusiana na matakwa ya wananchi ya muundo wa muungano wanaoutaka. Kimsingi Neno TANZANIA limejengwa kwa mizizi miwili mikuu yaani TAN = Tanganyika na ZAN = Zanzibar. Hizi ni nchi mbili huru zenye historia zao tofauti ambazo kila moja inastahiki kuhakikisha kuwa zinabakia kwa faida ya vizazi vijavyo. Hivyo basi muundo wa Muungano unaofaa unapashwa kuwa ni ule utakaojali hitaji hili la msingi. Pia maadamu masuala mengi hayapo kwenye Makubaliano ya Muungano wa sasa, ni wazi kwamba kila nchi inayo haki ya kuyashughulikia masuala hayo bila kuingiliwa na serikali ya Muungano.

  Kwa bahati mbaya muundo wa sasa unamitazamo miwili ambayo inaendelea kuzalisha matatizo na manung’uniko kila kukicha. Mitazamo yenyewe ni hii:
  a). Kwa Mzanzibari, upo mtazamo kuwa Serikali ya Tanganyika ndiyo iliyojivika wadhifa wa kuwa serikali ya Muungano. Hivyo wanaona kuwa Tanganyika haiwatendei haki kwa kuwanyima haki zao za msingi chini ya mwavuli wa Muungano.

  b). Kwa Mtanganyika, upo mtazamo kuwa tofauti na ilivyo kwa upande wa Zanzibar, Serikali ya Muungano imehodhi maamuzi hata kwa masuala yasiyo ya Muungano ya upande wa Tanganyika na kuwahusisha Wazanzibari katika kuyafanyia maamuzi katika ngazi mbali mbali mfano Bungeni na katika wizara na idara mbalimbali za Serikali ya Muungano ambapo Wazanzibari pia huuhusishwa katika utumishi. Mfano mzuri ni katika Bunge la Muungano ambalo hushughulikia bajeti za Wizara za Muungano na Zisizo kuwa za Muungano; Rais wa Muungano anapokuwa Mzanzibari huteua viongozi katika ngazi za Mikoa na Wilaya ambazo siyo masuala ya Muungano.

  Kutokana na masuala hayo hapo juu, wazo la Waziri Mansour Yusuf Himid, Mwakilishi wa Kiembesamaki na Waziri wa SMZ, kuwa inafaa kuutafakari upya muundo wa muungano na kufanya maamuzi ya mfumo mpya wa mkataba baina ya nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar kama vile muungano wa nchi za Ulaya linapashwa kuungwa mkono na wote wanaozitakia mema nchi zetu za Tanganyika na Zanzibar katika kuelekea kufanya maamuzi muhimu ya mstakabali wa muungano. Kipindi muafaka ni hiki ili tuwe na aina bora zaidi ya Muungano kabla ya mwaka 2015.

  Kwa hili hakuna sababu ya kuwa na baadhi ya watanzania ndani ya vyama vyao au katika nyadhifa mbalimbali kuwa kikwazo kwa kuwa hili ni jambo la kheri kwa mustakabali wa taifa na lenye faida kwa vizazi vijavyo. Hakuna sababu ya mtanzania yeyote kupoteza maisha au kusumbuliwa mahakamani kwa namna yoyote maana inavyozidi kucheleweshwa itakuwa ni njia ya kuwalazimisha kuingia katika harakati za kudai haki yao hii ya msingi hali ambayo haitakuwa ya kistaarabu.

 2. Haloo Moderator, Comment hii iache. Badala yake iliyoboreshwa zaidi iliyopo hapa chini ndiyo uifanyie Moderation.
  Wasalaam.
  By. Wambura Sambayeti.

 3. Ahsante. Tumwombe Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ashushe Baraka zinazohitajika katika kipindi hiki cha mchakato wa maamuzi kuhusiana na mstakabali wa Muungano na taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.