Panajengwa picha. Hapana, kwa hakika panategwa mtego. Tukinasa kwenye mtego huu, Zanzibar itakuwa imeshindwa kwa mara nyengine tena ndani ya historia yake ya nusu karne iliyopita, na tutalazimika kusubiri miaka mingine 50 ijayo kujikwamua na mkwamo tutakaokwama.

Picha inayojengwa ni kwamba Zanzibar inaelekea kwenye utaratibu wa kukusanya maoni ya kuandika katika mpya ya Muungano ikiwa imegawanyika katika makundi matatu.

Kundi la kwanza ni la Wazanzibari wanaotaka Muungano huu uvunjwe haraka iwezekanavyo. Katika fremu ya picha hii, munaingizwa halaiki ya Wazanzibari chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho. Kaulimbiu ni “Tuwachiwe Tupumuwe!“ Njia ya kufikia kwenye upumzi huo wa kupumuwa, ni kuitishwa kwa kura ya maoni kuwauliza Wazanzibari ikiwa wanataka Muungano ama la.

Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu wakiongoza wananchi kwenye maandamano ya kutaka mamlaka ya Zanzibar yaheshimiwe.
Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu wakiongoza wananchi kwenye maandamano ya kutaka mamlaka ya Zanzibar yaheshimiwe.

Kwa sababu za ufuasi wa kwenye mikutano ya hadhara na uchangiaji kwenye mitandao ya kijamii, kundi hili linaonekana kuamini kuwa, kwanza, hilo la kuitishwa kura ya maoni linawezekana kwa sababu Katiba ya Zanzibar inacho kifungu kinachoruhusu na, pili, kupigwa kura ya “Hapana kwa Muungano“ kunawezekana kwa kuwa Wazanzibari wengi hawautaki Muungano na, tatu, Tanganyika itakuwa haina tena hiyari ila kuiwachia Zanzibar kwenda kwa kuwa huo utakuwa ni uamuzi wa Wazanzibari walio wengi.

Kundi la pili ni la Wazanzibari ambao wanataka mabadiliko makubwa ya kimsingi kwenye Muungano na wakati aina mpya ya Muungano ikizaliwa. Katika fremu ya picha hii, munaingizwa uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na sehemu ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao wana msimamo wa Uzanzibari Kwanza linapokuja suala la nchi, na chama baadaye.

Kwa hakika, CUF tayari imo kwenye hatua za mwisho za kubadilisha sera yake ya Muungano, kutoka ile ya muundo wa serikali tatu hadi ya Muungano wa Mkataba unaofanana na wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki au wa Umoja wa Ulaya. Kundi hili linaamini kwamba njia ya kufika huko ni kupitia utaratibu wa kisiasa, kwa kuanza na hatua za kushiriki kwenye uundaji wa Katiba Mpya, hadi kufikia utoaji wa maamuzi mazito kwa Wazanzibari.

Kundi la tatu ni Wazanzibari wanaotaka hali ya sasa ibakie kama ilivyo, na ikiwezekana isogee mbele zaidi – yaani ikiwa sasa tuna muundo wa Muungano wa serikali mbili, ni bora kumalizia kabisa na kuwa na wa Serikali Moja. Kama ilivyokuwa kwenye Kura ya Maoni ya Julai 31, 2010 juu ya uundwaji wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kundi hili haliwezi kujitokeza wazi kusema maoni yake, lakini likipata nafasi ya kuonesha msimamo wake, linafanya na litafanya hivyo. Kama ambavyo asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura wa Zanzibar walikataa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ndivyo pia itakavyopiga kura ya kuendelea na serikali mbili na hata ikibidi kuwa na moja, kama kura ya maoni itapigwa leo.

Kwa sababu moja ama nyengine, kundi hili la tatu lina mashiko yake kwenye siasa za kihafidhina. Lina nguvu zake kutokea upande wa pili Muungano. Lina uhalali wake katika mgawanyiko wa Zanzibar – kwa misingi ya asili, visiwa, rangi na makabila. Si tatizo kwamba waliomo kwenye kundi hili ni Wazanzibari nao. Tatizo ni kwamba wana nguvu zinazoweza kuwafanikishia azma yao kwa kutumia mikono iliyo nyuma yao.

Katika picha hii inayojengwa, kundi la tatu ndilo linalofaidika nayo. Tayari hivi sasa, watu wa kundi la kwanza wamefanywa wajiamini kwamba wao peke yao ndio Wazanzibari halisi na wazalendo wa kupigiwa mfano. Wanawaona wa kundi la pili kuwa wasaliti na wanaopenda madaraka, ambao wamesahau ahadi zao baada ya kuingia kwenye serikali. Wakipunguza kidogo tafsiri yao kwao, wanasema kwamba walioko serikalini wanatumia njia za kuzunguka kufikia suluhisho ambalo lina njia ya mkato kabisa – nguvu ambayo Zanzibar imepewa kwenye Mabadiliko ya 10 ya Katiba.

Wa kundi la pili nao wanaamini kwamba wa kundi la kwanza ni “Kuukia“: ule mti unaoota na kuimarika juu ya mti mwingine, halafu ukauuwa huo mti uliourukia kabla ya wenyewe nao kufa, kwa sababu unakuwa hauna pa kupatia chakula chake. Hii ni kwa sababu ufuasi ulio nyuma ya Uamsho hivi sasa, kwa kiasi kikubwa, unachimbukia kwenye maeneo ambayo CUF na CCM yenye msimamo wa Uzanzibari Kwanza inaungwa mkono. Kiwango kile kile cha ufuasi wa mikutano ya CUF kuelekea uchaguzi wa 2010, ndicho kinachomiminika kwenye mihadhara ya Uamsho.

Siku itakapokuwa dhahiri kwamba hakuna namna ya Zanzibar kukwamuka kupitia njia ya mkato; na sasa Uamsho ikataka kuugeuza umma kurudi kwenye ajenda ya mabadiliko kwa kutumia njia za siasa, Wazanzibari ambao waliwaamini watajikuta hawana pa kushika. Sababu ni kuwa, wanaweza wasiwaamini tena Uamsho wala wasiweze tena kurudi kwenye mtazamo wa CUF na CCM yenye msimamo wa Uzanzibari Kwanza.

Kundi la tatu, ndilo linalofaidika hapo. Vyombo vya habari, ambavyo vingi vyao ni mikono nyuma ya minyororo iliyoifunga Zanzibar, vinafanya usahihi wa picha ya mgawanyiko wa Zanzibar ionekane kwa uwazi zaidi kuliko uhalisia wake. Hamasa za vijana zinapochanganyika na haraka ya kufikia suluhisho, inasababisha makosa mengi na makubwa ambayo hayataweza kusahihishika kirahisi ndani ya miaka 50 ijayo.

Ushauri wangu: Makundi mawili ya mwanzo niliyoyataja, la Uamsho na CUF/CCM Msimamo, yanapigania kitu kimoja. Yanatafautiana njia za kukifikia kitu hicho. Ni kosa kubwa kwa CUF/CCM Msimamo kuichukulia Uamsho kama kitisho. Ni dhambi kwa Uamsho kuwachukulia CUF/CCM Msimamo kama kikwazo. Wawili hawa wana mengi ya kuwaunganisha kuliko kuwatenganisha. Ni suala la kuusawazisha mkakati wao na kuweka vigezo vya pamoja vya kupambana. Baada ya yote, Zanzibar ni ya wote hao. Uamsho, CCM, CUF ni majina tu. Dhamira ndio ya kuzingatiwa hapa.

Ikiwa hili halikufanyika, kundi la tatu ambalo lenyewe ni sehemu ya picha iliyojengwa na kujengeka, lina fursa kubwa zaidi ya kushinda. Na wakishinda wao, itakuwa imeshindwa Zanzibar.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.