Na Jabir Idrissa, MwanaHALISI la 13 Juni 2012

Ukweli kwamba Zanzibar ni nchi yenye athari na alama ya Uislamu umeipatia maadui wengi kwenye vyombo vya habari na serikali zilizo kinyume na imani hiyo.

NINAHOFU kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejipanga. Naona imefikwa; imo katika mtihani, tena mgumu. Uongozi wa juu na matawi yake – wizara, idara zinazojitegemea na mashirika yake – lazima wafikiri upya namna nzuri ya kuwatumikia wananchi. Imewasilisha bajeti yake Baraza la Wawakilishi. Sawa, hili ni moja ya mahitaji muhimu ya kikatiba ambayo serikali inatakiwa kuyatekeleza.

Tatizo ni kwamba akili za wananchi hazipo kabisa huko. Kwa kiwango kikubwa, wananchi wanaotakiwa kufuatilia mjadala wa bajeti mpya, akili zao zipo kwengine.

Kila ninavyopima, nabaini kwa kipindi chote hiki, wamezielekeza kwenye Muungano na ndio suala linalowasumbua zaidi kwa sasa.

Wazanzibari wanataka kujua hatima ya nchi yao. Wanataka kujua kwani wakitoa maoni itakapokuja Tume ya Mabadiliko ya Katiba, watanufaika kwa lipi. Wanajiuliza ni nini hasa maana ya wao kutakiwa kutoa maoni yao kwa tume hii?

Wala si uongo kwamba Muungano ndio suala linalochukua nafasi kubwa zaidi katika akili za wananchi wa Unguja na Pemba. Si bajeti ya serikali kamwe.

Wanasema zimewasilishwa bajeti ngapi za serikali tangu siasa za mageuzi ziliporudishwa nchini mwaka 1992. Jibu muafaka, ni “nyingi tu.” Na bado hali zao zipo palepale na hata kuzidi kuwa ngumu kimaisha.

Nina wasiwasi kuwa bajeti ya safari hii inayoanza kujadiliwa, haitakuwa na mvuto kama ilivyozoeleka miaka mingi. Naona kama itapita na kupitishwa ilivyo bila ya wananchi kuihoji itabadilisha nini.

Ni kama vile wameshapima haitakuwa na maana yoyote maishani mwao. Sasa wanasema wazi kuwa mbele ya minyonyoro ambayo serikali yao ya umoja (SUK) imefungwa na Serikali ya Muungano, hawatarajii jambo la manufaa.

Wanajua mkutano wa Baraza la Wawakilishi umeanza kwa kuwasilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano, Na. 8 ya mwaka 2011, lakini wanajua pia kuwa baraza lao halitabadilisha chochote katika sheria hiyo. Ukweli huu wanaujua.

Wao wanabaki na hofu yao kuu kwamba nini maana ya yote hayo wakati wanachokihitaji kufahamishwa hawasikii viongozi wao wakikizungumza?

Si wao wanataka kwanza fursa ya kupiga kura ya maoni ili kueleza msimamo wao kama wanautaka Muungano? Sasa mbona viongozi wao wanaowapenda kupitia SUK, wanalipuuza hili; badala yake unawasikia tu wakisema, “ndugu wananchi kuweni watulivu, subirini tume ije mtoe maoni yenu?”

Wazanzibari wengi kwa muda huu wameelekeza macho na masikio yao kwa suala la Muungano – uhusiano wa kisiasa uliojengwa kupitia kuunganishwa kwa dola mbili zilizo huru ikiwemo ya kwao ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Mjadala kuhusu hatima yao na Muungano umepamba moto nchi nzima, licha ya kasheshe zinazotokea, ikiwemo vurugu zilizokumba mitaa ya mji wao wiki mbili zilizopita.

Popote upitapo mjini Zanzibar, na miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete, kisiwani Pemba, utasikia simulizi za utawala na vyombo vyake kuchochea vurugu zile. Wanasema wamezoea kufitinishwa.

Kwamba kwao, imekuwa ni kawaida, kulazimika kukabiliana na visa vilivyopandikizwa na vyombo vya dola na mawakala wao kwa lengo la kuzubaisha wananchi, wageni na pengine, ulimwengu mzima. Walishavisahau lakini watawala wao bado.

Wanakumbuka vyombo hivyo vilivyojiingiza katika kupanga visa mara tu baada ya mfumo wa vyama vingi kurudishwa nchini; ili kuzua kitahanani na hatimaye askari wapate nafasi ya kuhilikisha wananchi wema.

Dola inapozua tafrani kwa makusudi, wananchi wataamua kujihami, wakivamiwa watajitetea, wakijitetea wataumizwa maana hawana silaha isipokuwa mawe na nguvu za miili. Kushindana na askari wenye bunduki si jambo rahisi na matokeo yake mara nyingi ni raia kuumia na kuumizwa.

Basi baada ya watu kusahau kupigwa mijeledi baada ya askari kulipua makanisa, baa na matawi ya CCM, pamoja na visima vya maji ya kunywa wanavyotumia kumwagiwa vinyesi na madarasani vivyo, wamezinduliwa kumbe bado vyaweza kuendelea.

Hakika wanashangaa kuwa wapangaji wamerudia mipango yao ya kiharamia ndani ya mshikamano imara uliopo katika jamii. Tena hakuna msuguano wa kisiasa wala wa kidini. Watu bukheri khamsa ishirini na shughuli zao.

Wanajiuliza vyereje leo nchi ambayo watu wake haijatokea hata mara kupigana kwa sababu ya tofauti ya dini zao, warukiane, kuvamiana na kuchomeana makanisa?

Isitoshe, wanasikitika hata msikiti uliomaliza kujengwa upya juzi tu, wa mtaa wa Nyerere, nao umepigwa bomu na polisi. Hatua ya mwisho ni sheikh Mussa Juma aliyekamatwa na polisi.

Haiyumkini, wanasema, Wazanzibari ambao ni mchanganyiko wa Wakristo na Waislamu wahasimiane ilhali wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani kwa karne nyingi. Wanawaza lazima kumeingia kidudumtu.

Naam. Katika historia ya karne kwa karne Zanzibar, hakujawahi kudhihirika hasama kati ya Waislamu na Wakristo. Hakuna tukio la kutolewa mfano kuthibitisha uhasama kati ya jamii za dini hizi mbili kuu Zanzibar.

Hebu kidogo niwapitishe kwenye historia ya enzi ya maisha ya uhusiano mzuri kati ya Wazanzibari wa jamii hizi.

Profesa Abdul Sharif, mwanahistoria mtukuka wa Zanzibar, amekuja na andishi mahsusi la kuonyesha namna watu wa dini hizi walivyoshikana na kushikamana tangu enzi za himaya ya Sultan visiwani Zanzibar.

Profesa huyu ambaye katika kipindi cha kuelekea kuundwa kwa tume ya mabadiliko ya katiba amejishirikisha kikamilifu, pamoja na wenzake, kusaidia kuwapa wananchi elimu kuhusiana na Muungano, anasema historia ya muingiliano wa watu wa dini hizi umeanza zaidi ya miaka 170 nyuma.

Uhusiano huo umedumu na kudumu mpaka ilipofika mwaka 1987. Anabainisha jambo la ziada hapa kwamba tena Zanzibar mtengamano wa dini umeimarika licha ya kuwa karibu asilimia 100 ya watu wake ni Waislamu. Wapo pia watu wa dini ya Hindu na mapagani.

Alama muhimu inayochukuliwa kama kielelezo cha maisha mfungamano hayo ya watu wa dini mchanganyiko ni stempu iliyochapishwa baada ya Zanzibar kupata uhuru 10 Disemba 1963. Hii ilichorwa na mwalimu maarufu wa somo la sanaa, Mwalimu Abdalla Farhan. Stempu hiyo ilikuwa na picha ya makanisa ya Katoliki na Anglikana, msikiti wa Sunni na Shia, pamoja na hekalu la Wahindu.

Historia hiyo ilianzia mwaka 1840 pale Mmishonari wa Kijerumani, Dk. Johanne Krapf, alipozuru Zanzibar na kuomba ruhusa ya kujenga kanisa kwenye mji wa Mombasa, nchini Kenya, ambao kwa wakati huo, ulikuwa ni sehemu ya himaya ya Zanzibar.

Ushahidi wa Wamishonari wenyewe unaonesha Sultani wa Kiislamu aliyekuwa mtawala wa dola ya Zanzibar, Seyyid Said bin Sultan, alimwandikia gavana wake aliyekuwa kiongozi mwakilishi wa Mombasa, akisema:

“Namleta kwako Dk. Krapf. Ni mtumishi wa Mungu ambaye anataka kueneza neno la Mungu. Fanya kila uwezalo umsaidie kufanikisha kazi yake.”

Profesa Sharif anasema siyo kwamba sultani alitenda hivyo kwa vile alikuwa mtawala mwenye uvumilivu wa aina ya kipekee, bali ni kwasababu ilikuwa ni desturi ya uvumilivu wa kidini katika eneo la mwambao wa Bahari ya Hindi tangu wakoloni hawajaingia.

Leo ni ajabu kutokea watu wakataka kulazimisha Waislamu na Wakristo wapigane na kuharibiana mali. Fitna tupu. Allah awaangamize wafitini – Amin.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.