Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, akikagua gwaride la vikosi vya Jeshi la Tanzania.

Mwaka 2009, wakati wa kuadhimisha miaka 45 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho Zanzibar, iliandaa kongamano la Wazanzibari kujadili hatima ya nchi yao ndani ya Muungano huo. Nilialikwa kama mmoja wa watoa mada, na nilizungumzia Siasa za Muungano na hatima ya uchumi wa Zanzibar. Sehemu ya mwisho, yaani hitimisho la mada, ilisema hivi:

“…..Wazanzibari na Watanganyika wana malezi tafauti kuhusiana na sura ya Muungano. Ambapo Watanganyika wanauangalia huu kuwa ni Muungano wa Serikali Moja, Wazanzibari wanauangalia kuwa ni wa shirikisho la Serikali Tatu. Hata hivyo, si serikali moja wala tatu zilizoandikwa popote katika sheria kuu zinazoongoza sehemu hizi mbili, isipokuwa tabia, matendo na maono ya watu yanasomeka hivyo. Ndiyo maana, si rahisi kwa Mtanganyika kumkuta anajiita kwa jina hilo, maana kwa wengi wao Tanganyika imeshapotea, lakini kila mara utamkuta Mzanzibari akijiita na akijinasibisha kwa Uzanzibari wake.

 
“Huu ni uamuzi wa kimapinduzi kwa pande zote mbili za Muungano. Kwa Tanganyika ni wa kimapinduzi kwa kuwa umeweza kupindua fikra za karibuni vichwa milioni 37 na kuvifanya viamini kitu kimoja. Kwa Zanzibar ni wa kimapinduzi kwa kuwa vichwa milioni moja tu, ambavyo vinafanya chini ya asilimia 3 tu ya Watanzania wote na vinakaa chini ya asilimia moja tu ya ardhi yote ya Tanzania, vimeweza kuhimili kubakia na hisia za kutokuridhika kwa takribani nusu karne ya Muungano huu….

 
Zanzibar inauona ukweli kuwa Muungano huu, katika hali uliyo, ni tatizo kwake na, sasa, ingelitaka kuuona kuwa ni sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo. Huko hakuwezekani ila kwa Mapinduzi; na hayo si mapinduzi ya mapanga na marungu, wala bunduki na mizinga, bali ya fikra na mkakati, ambayo yanatakiwa yapitie hatua tano zifuatazo:

 
i. Hatua ya matayarisho kwa ajili ya mapinduzi
ii. Hatua ya kuporomoka kwa mfumo mkongwe
iii. Hatua ya kuharibika kwa mahusiano makongwe
iv. Hatua ya kujenga mahusiano mapya
v. Hatua ya kuuimarisha mfumo mpya

 
Ama kwa kujijua au kutojijua, tayari tumeshapita kipindi cha kwanza cha matayarisho kwa ajili ya mapinduzi, ambacho kilitawaliwa na woga wa wananchi na mateso ya watawala. Kilikuwa ni kipindi ambacho, ingawa palikuwa na kiwango kikubwa cha kutokuridhika na jinsi Muungano huu unavyoikandamiza Zanzibar, si Wazanzibari wengi waliokuwa na uthubutu wa kukusema kutokuridhika huko. Bali hata wale wachache waliothubutu, walisemea vibuyuni ambako ama walichokisema kilimalizwa huko huko au wenyewe walimalizwa kwa njia zao za kumalizana.

 
Sasa tulipo, kwa maoni yangu, ni katika hatua ya pili ya mapinduzi, ambapo mfumo mkongwe wa Muungano usio na maslahi kwa Zanzibar unaelekea kuporomoka. Kawaida kipindi hichi ni matokeo ya kupotea kwa uongozi (leadership vacuum) ndani ya kundi la watawala, ambapo mgawanyiko wa makundi humfanya kila mmoja kutenda vyake. Mara nyingi hatua hii haifikiwi mpaka ajitokeze kiongozi anayejiona kuwa mwanamageuzi kutaka kuunusuru mfumo mkongwe; na akafeli. Turgot na Necker walijaribu kuunusuru ufalme wa Ufaransa kabla ya mwaka 1798 na Stolpyin akafanya jaribio kama hilo nchini Urusi kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini wote walishindwa.

 
Huwa ni wakati ambapo, kutokana na mtikisiko wake, mfumo mkongwe huwa kama tayari umeshakufa kitambo, lakini kwa kuwa watu wanaothubutu kuyathibitisha mauti yake hawajatokea, basi huendelea kuwepo tu ukiendea upepo na kudura ya Mungu. Nabii Suleiman (A.S) alifariki siku nyingi, lakini watumishi wake wakaendelea kutumika wakidhani bosi wao amekaa kitini akiwasimamia, hadi mchwa alipokuja kuila fimbo yake. Kuna watu waliojuwa kuwa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Ufaransa imeshakufa tangu mwaka 1934, lakini maziko yake yalikuja kufanywa mwaka 1940.

 
Wazo ninalojaribu kuliwasilisha kwenu hapa ni kwamba, kuna siku yale yale matakwa ya Wazanzibari, kama yalivyoelezwa kupitia Ripoti za Tume za Jaji Nyalali na Jaji Kisanga, ndiyo yatakayoiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Katiba hizi zilizopo sasa; na viashiria vya utabiri huo vimeanza kujengeka sasa.

 
Changamoto iliyo mbele yetu kwa sasa ni ukweli kwamba hatua za tatu, nne na tano zinakuja kwa kasi na, yumkini, hatuna matayarisho mazuri kuzikabili. Kwa mfano, hatua ya tatu, ambayo ni ya kuharibika kwa mahusiano makongwe, kwa mintarafu ya kuharibika kwa muundo wa sasa wa Muungano, ina matatizo yake. Mojawapo ni kwamba, wenye maslahi na mahusiano haya hivi sasa, watajitahidi kutumia nguvu zao za ziada kuzuia yasiharibike. Na ingawa, kutokana na matakwa ya kiwakati hawataweza kufanya hivyo, lakini kama ilivyo kawaida ya mti mkubwa unapoanguka, husababisha maafa kwa pale unapong’okea (panaweza kuchimbika shimo kubwa) na kule unakoangukia (unaweza kuelemea nyumba au wapita njia na kuwajeruhi kama si kuwatoa roho zao).

 
Wakati mahusiano makongwe baina ya Syria na Lebanon yalipoharibika, kwa mfano, ni Lebanon ndiyo iliyoonekana kulipia gharama za kipindi hiki kwa wale wanaharakati wake walio mstari wa mbele katika kusaidia maharibiko hayo, kukabiliwa na vitendo vya kigaidi vinavyoaminika kusimamiwa na kuongozwa na Syria ndani ya ardhi ya Lebanon, yakiwemo mauaji ya Waziri Mkuu Rafiq Hariri.

 
Lakini mara tu kipindi hiki kinapoanza, hutanguliwa haraka sana na kipindi cha ujenzi wa mahusiano mapya. Huu ni mfano wa ujenzi wa nyumba mpya juu ya kongwe, ambapo mwenye nyumba huendelea kujenga nyumba mpya, huku yeye akiwemo ndani. Huvunja kiambaza kimoja kwanza na kusimamisha kipya mahala pa kilichovunjwa, kabla hajakwenda katika kiambaza chengine.

 

 

Ingawa huweza kuchukua muda mrefu kwa nyumba kukamilika, kutegemea na uwezo wa kifedha, kiufundi na mazingira ya ujenzi; lakini ni staili ya ujenzi ambayo ina faida moja kubwa: hakuna wakati ambapo mwenye nyumba analazimika kulala nje, hata kama katika kipindi cha ujenzi huwa hakai katika makaazi mazuri sana.

 
Hapo ndipo, kwa maoni yangu, nchi hii inapoelekea. Muungano huu utaingia kwenye kuvunjika na kuundika kwa wakati mmoja, yaani tunakwenda katika kipindi ambacho hatutasema kuwa hatuna Muungano moja kwa moja, lakini pia hatutakuwa na Muungano huu.

 
Mwisho tutaingia kwenye kuimarisha mahusiano mapya tutakayoyajenga; maana ukweli ni kwamba Zanzibar na Tanganyika, bali pamoja na mataifa mengine ya karibuni, yataendelea kuwa katika mahusiano dumu daima. Lakini tafauti na sasa, mahusiano yajayo kwa sababu ya mapinduzi haya, yatakuwa na sura nyengine na matakwa mengine.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.