Umma wa Kizanzibari ukiwasikiliza viongozi wa Jumuiya ya Uamsho katika Msikiti wa Mbuyuni.

Na Ahmed Raajab, Raia Mwema 6 Juni 2012

UKILALA unaamka. Kama huamki na bado una uhai basi unaamshwa. Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiko) ya huko Zanzibar inasema kwamba imejitweka jukumu la kuwaamsha Wazanzibari kuhusu mengi — ya dini na dunia.

Miongoni mwa hayo ni Muungano wa Tanzania ulioziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili mwaka 1964. Kwa ufupi, Jumuiya ya Uamsho inaupinga Muungano. Hamna shaka yoyote kwamba kwa hilo ina wafuasi wengi sana Visiwani.

Jumuiya hiyo imekuwa ikiandaa mihadhara ya kuwapa elimu ya kiraia waumini wa dini ya Kiislamu kuhusu masuala ya katiba likiwamo suala la Muungano na uhalali wake.

Tukumbuke kwamba wanao uhuru wa kufanya hivyo na wakati huohuo tusiyasahau maneno ambayo Mwalimu Julius Nyerere alimwambia mwandishi Colin Legum wa gazeti la Obsever la Uingereza mwaka 1965 kwamba hatowapiga mabomu Wazanzibari wamridhie endapo watakataa kuendelea na Muungano.

Mihadhara hiyo ya Uamsho inapendwa na huhudhuriwa na watu mia kadhaa kama si elfu kadhaa kila inapofanywa. Japokuwa inapendwa hivyo imekuwa ikiwakera baadhi ya walio na madaraka Zanzibar na wasiofurahishwa na Maridhiano yaliyopo Visiwani. Wanachokitaka waheshimiwa hao ni kuzuka kwa fujo zitazoweza kuisambaratisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hata kuzusha hali zitazopelekea kusimamishwa kwa mchakato wa katiba.

Mkakati wao ni rahisi kuuelewa: chochea fujo kwa kuwatumia vijana, watomeze wenye jazba washambulie makanisa, wahusishe viongozi wa Uamsho na mtandao wa kigaidi wa al-Qa’eda, wahusishe viongozi wa CUF na Uamsho na harakati zao.

Wanatumai kwamba kwa kufanya hivyo wataweza kuwafanya wakuu wa serikali ya Tanzania na wakubwa wa dunia hii waiangalie Zanzibar kwa jicho jingine. Wanachotaka hasa, na kwa hili wana wenzao Bara, ni kuzizima harakati za kuujadli Muungano.

Fujo zilizoanzia Jumamosi ya tarehe 26 Mei zilichochewa na polisi kwa kutotumia hekima walipomtia nguvuni Sheikh Mussa Issa. Wafuasi wake wakamiminika, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo mbele ya kituo cha polisi alikoshikwa na wakadai aachiwe huru.

Polisi nao wakapambana na umati huo kwa kuwarushia mabomu ya kutoa machozi. Ndipo palipozuka kikundi cha watu na kwenda kutia moto kanisa na kuvunja mabaa. Baadhi ya waliovunja hizo baa wakipiga takbir (Allahu Akbar) na huku wakinywa pombe. Haiyumkiniki kwamba hawa walikuwa wafuasi wa dhati wa Uamsho.

Inafaa tuangalie jinsi matukio hayo yalivyokuzwa kupita kiasi na vyombo vya habari na kuwapelekea watu waamini kwamba ‘Zanzibar yateketea’ na si pahala pa watalii, Wakristo au Wabara.

Bahati nzuri hakuna ubalozi wowote wa kigeni uliotoa taarifa kuwaonya wananchi wao wasiizuru Zanzibar; na wala hakuna mtalii yoyote au Mkristo kutoka Bara aliyedhuriwa. Kwa hakika tunapaswa kuwapongeza waandamanaji pamoja na majeshi ya usalama kwa kutofanya mambo ambayo yangelizidi kuifanya hali iwe mbaya.

Zamani polisi wakizoea kutumia nguvu kupita kiasi na waliwahi kuwaua waandamanaji wasiokuwa na silaha kama ilivyotokea Pemba mapema mwa mwaka 2001 pale watu kadhaa wasio na silaha walipouawa na vikosi vya usalama walipokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010. Wao wakishikilia kwamba chama cha CUF ndicho kilichoshinda kwenye uchaguzi huo. Hayo yamepita.

Tukiyaangazia ya leo inasikitisha kwamba miongoni mwa waathirika wa matukio ya siku ile ya machafuko ni kanisa moja lililotiwa moto. Hiki ni kitendo kiovu, cha kishenzi na chenye kwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu.

Ni kosa la jinai kuchoma moto mahala popote pa ibada. Pia ni kosa kubwa kujaribu kukilaumu chama chochote au jumuiya yoyote kuwa ndio iliyohusika na uchomaji moto huo.

Zanzibar ina umaarufu kwa mchanganyiko wake wa watu wa makabila, rangi na dini tofauti. Pia inasifika kwa jinsi Waislamu wake — ambao ndio wengi nchini humo — wanavyoingiliana na Wakristo wake ambao ni wachache sana. Kwa muda wa zaidi ya karne Wakristo hao wamekuwa na uhuru kamili wa kuabudu na wamekuwa wakipata hifadhi.

Juu ya kuwa Zanzibar inatafahari kuwa ni nchi ya Kiislamu, hatukuwahi kusikia katika historia au kushuhudia kwamba Wakristo wa Zanzibar wanabughudhiwa kwa sababu ya imani yao.

Kwa hakika, katikati mwa karne ya 19 na baadaye pale wamisionari Wakikristo wa kizungu walipokuwa wakitafuta njia za usalama za kupenya na kuingia katika eneo la Maziwa Makuu na sehemu za bara za Afrika ya Mashariki misafara yao yote ilianzia Zanzibar.

Masultani wa wakati huo waliwapa hao mamisionari wakizungu risala za kuwajulisha na machifu wa bara. Isitoshe masultani waliwapa hifadhi wamisionari huko Zanzibar. Hakuna mtu yoyote aliyethubutu kuwagusa hao wamisionari.

Kadhalika masultani walikuwa wakiwapa wamisionari watu wa kuwaongoza katika misafara yao ya kueneza Ukristo katika kanda ya Afrika ya Mashariki. Kama ilivyokuwa kwa mengi katika zama zile Ukristo nao pia ulianzia Zanzibar. Ndio maana makanisa makongwe kabisa katika Afrika ya Mashariki yako Zanzibar. Hata ile ardhi iliyojengewa makanisa ya Kianglikana na Kikatoliki katika Mji Mkongwe huko Unguja ilitolewa bure na sultani wa Zanzibar na kugaiwa madhehebu hayo mawili ya Kikristo.

Haielekei kwamba uvumilivu huo utatoweka. Hautotoweka kwa sababu uvumilivu huo umejengeka katika utamaduni Wakizanzibari na utamaduni huo ni wenye kuufuata Uislamu kama unavyotakiwa kufuatwa bila ya kuufanya uwe mgumu.

Utamaduni huo si tu kwamba unavumilia dini nyingine bali pia unaheshimu tofauti za kidini na za kitamaduni zilizo katika jamii. Na wala tofauti hizo hazitumiwi vibaya kwa minajili ya kisiasa.
Ndipo tunapokuwa hatuna budi ila kukubaliana na Rais Jakaya Kikwete aliposema kwamba kuuvunja Muungano hakuwezi kupatikana kwa kuchoma moto makanisa.

Kwa sasa jambo la busara ni kusubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi kuhusu kadhia ya uchomaji moto kanisa. Tunatumai kwamba wahalifu waliochukua hatua hiyo watafikishwa mahakamani. Hatua yao si ya kijinga tu bali inaweza kuleta hasara kwa mengi.

Tusighafilike tukasahau kwamba hii leo wananchi wa Zanzibar wana uhuru wa kusema na wa kukusanyika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na sheria za nchi hiyo pamoja na zile za serikali ya Muungano zinazosema kwamba Tanzania — na hivyo Zanzibar — ni nchi za kidemokrasia.

Kadhalika, ni muhimu kukumbuka kwamba suala la Muungano ni suala lenye kuzusha hamasa na jazba kubwa kila linapojadiliwa na huvutia makundi ya watu bila ya kujali nani au jumuiya gani inalijadili suala hilo.

Jambo moja linalojitokeza katika mijadala yote hiyo na bahati nzuri hili si siri tena kwani Wazanzibari wamekwishauvua woga wao ni kwamba wengi wao, ingawa hawataki Muungano uvunjike, hawaitaki hali iliyopo sasa ya Muungano wa Katiba wenye kuifanya serikali yake iwe na nguvu na madaraka makubwa mno.
Wengi wao wangependelea badala yake pawepo na Muungano kama ule Muungano wa Ulaya. Kwa ufupi, wanataka Muungano wa nchi mbili zilizo huru zenye kutendeana wema na kushirikiana.

Kwa sasa Wazanzibari wanavuta subra wakingojea fursa ya kutoa maoni yao katika shehia zao juu ya mustakbali wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Kadhalika wanatambua kwamba baada ya hapo watapata fursa nyingine ya kutoa maoni yao kwenye kura ya maoni watapoulizwa iwapo wanaikubali au hawaikubali katiba mpya itayotungwa baada ya mchakato wa kutoa maoni.

Hiyo itakuwa ni fursa wasiowahi kuipata na itawawezesha kuigeuza hiyo kura ya maoni kuhusu katiba iwe kura juu ya Muungano.

Uamsho una msimamo wenye kuupinga Muungano. Sasa tujiulize iwapo Uamsho unaweza kuupata muradi wake wakati huu wa sasa katika mchakato wa kuipitia tena katiba.

Tusisahau kuwa jumuiya za kidini na zisizo za kidini zote zinaruhusiwa kutoa maoni yao juu ya suala la Muungano na hatima yake. Ruhusa hiyo ipo ilimradi pasiwe na sera ya kupambana na vyombo vya dola.

Kwa Zanzibar mpambano huo hauhitajiki kwa vile viongozi wa kisiasa wa itikadi tofauti mara nyingi wametoa matamshi wakieleza wazi msimamo wao kuhusu Muungano. Hata Rais Dk. Ali Mohamed Shein alinukuliwa hivi karibuni akisema kwamba anashiriki kikamilifu katika zoezi la kuipitia katiba akishirikiana na Rais Kikwete.

Tena kuna wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakieleza jinsi wasivyoridhishwa na Muungano. Hata kabla ya Uamsho kuanza harakati zake wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa wakiyatetea maslahi ya Zanzibar kama pale masuala ya mafuta na gesi asilia yalipofikishwa mbele ya Baraza.

Ingawa Uamsho bado haujatoa taarifa rasmi kuhusu sera zake, na ukifanya hivyo utajigeuza na kuwa chama cha kisiasa, viongozi wake hata hivyo, wamekuwa wakitoa mwito kutaka irejeshwe ile iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa kupitia kura ya maoni itayowauliza wananchi iwapo wanautaka au hawautaki Muungano.

Ni wazi kuwa viongozi wa Uamsho wanauona huu mchakato wa sasa kuhusu katiba kuwa usio na maana.
Juu ya hayo bado viongozi hao hawakuonyesha njia inayoweza kutumiwa kutimiza lengo la kuirejeshea Zanzibar uhuru wake. Wala hawakuonyesha vipi hiyo kura ya maoni itapigwa na iwapo wataweza kutimiza lengo lao kwa kutumia njia za kidini na mikusanyiko ya kidini bila ya kuwahusisha viongozi wa Zanzibar na wa Muungano.

One thought on “Kuchoma makanisa si kuvunja Muungano”

  1. Kama Watanganyika na Wazanzibari wangelikua na uhuru wa kueleza kero zao kuhusu Muungano na mambo mengine yanayohusu mustakbali wao tangu awali, pengine tusingelikua na hali tuliyonayo leo hii. Muungano kati ya mataifa yetu mawili, hauna tofauti na wa mataifa mengine.

    Mathlan, serikal ya Uingereza ‘haimshughulikii’ Bwana Alex Salmond, wa Scottish National Party (SNP), kwa kuwa na ajenda ya Scotland kujitoa katika Muungano wa falme hiyo. Kadhalika, raia wa Quebec hawapati misukasuko kwa kuwa hujadili mara kwa mara kujitoa kwenye taifa la Canada. Muungano hauwezi kulindwa kwa kumkamata Sheikh Mussa Issa, kama ambavyo hauwezi kuvunjika kwa kulichoma kanisa.

    Inaonyesha tatizo siyo watu wa mataifa haya mawili wanaojadili hatma ya Muungano, bali matumizi mabaya ya madaraka ya kisiasa na nguvu za dola katika jitihada za kuuzima mjadala wenyewe. Ninadhani ni kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar (na hizo, nguvu ziwazo) kujua wananchi wanafikiri nini hasa juu ya suala hili kuliko kutojua.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.