• Utengenezaji wa michezo ya kuigiza ya redio nchini Tanzania

Kwa mara ya pili kituo cha utangazaji cha kimataifa cha Ujerumani, Deutsche Welle (DW), kinatayarisha vipindi vya kuburudisha na kuelimisha kwa michezo ya kuigiza kwa ajili ya vijana chipukizi nchini Tanzania. Utengenezaji wa vipindi hivyo utaanza Jumatano tarehe 2 Mei hadi Juni 2, wakishiriki wachezaji wa kuigiza wenye vipaji.

Kituo cha Kimataifa cha Utangazaji cha Ujerumani, Deutsche Welle.

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Bibi Andrea Schmidt anasema: “ ’Learning by Ear-Noa bongo! Jenga maisha yako!’ sio kipindi cha kawaida cha redio. Badala yake tunatoa mfululizo wa michezo ya redio inayojikita kwenye vijana wa Kiafrika na changamoto zao za kila siku. Hadithi zao zinachangamsha, zinavuta hisia na wakati mwengine zinachekesha sana – lakini kamwe hazichokeshi.”

Ni vipindi vya mchanganyiko wa ripoti za kina, michezo ya kuigiza ya redio na hadithi kupitia makala ambazo zitawapa wasikilizaji vijana fursa ya kuelimika kupitia burudani. Masuala ya afya, mazingira, ushiriki katika mambo ya kisiasa, ni miongoni mwa mada kadhaa zinazoangaziwa.

Mwaka huu tunarudi tena jijini Dar es Salaam na tuna furaha ya kuungana na waigizaji chipukizi katika sanaa ya maigizo, tukiwa na mada kuu nane: Haki za Binaadamu, Uhamiaji ulimwenguni, Changamoto za Akina Mama Vijana wanaowasomesha watoto wao peke yao, Mapambano dhidi ya Ufisadi, Unyanyasaji wa Kijinsia, Namna ya Kuepuka Madeni, Changamoto kwa Watu Wenye Matatizo ya Akili na Kuondoa Dharau dhidi ya Jamii za Wachache. Vipindi hivi vinawalenga wasichana na wavulana kuanzia miaka 12 hadi 20.

Vipindi hivi vimetayarishwa na waandishi wa kiafrika kutoka sehemu mbali mbali barani humo. Vipindi vya “Learning by Ear“ vimetayarishwa kwa lugha sita: Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamharik. Tafadhali tutembelee kupitia tovuti yetu: http://www.dw.de/lbe/kiswahili.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Deutsche Welle inatangaza mara tatu kila siku; saa 12:00 asubuhi, saa 7:00 mchana na saa 12:00 jioni, saa za Afrika Mashariki, kupitia masafa mafupi. Matangazo yetu pia yanapatikana moja kwa moja kupitia mtandao wetu: http://www.dw.de/kiswahili katika nyakati hizo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.