Rais Jakaya Kikwete ameiapisha Tume ya Katiba, kama inavyojuilikana, ambayo jukumu lake ni kukusanya maoni ya Watanzania juu ya katiba wanayoitaka. Katika uapishaji huo uliofanyika Ikulu ya Magogoni, Ijumaa ya 13 Aprili 2012, Rais Kikwete aliwakumbusha ’ambao’ hawautaki Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wajuwe kuwa si Tume yake aliyoiunda ya kuwasaidia kupata muradi wao.

Mimi ninampa changamoto Rais Kikwete, akiwa kama kiongozi wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba iwe kwa kupitia Tume yake aliyoiapisha au njia nyengine, sio tu kwamba wasioutaka Muungano watauvunja, bali tayari ’wameshauvunja’. Kilichobakia ni kuusomea Arubaini yake, kwa mila za kwetu.

Dalili moja kwamba Muungano huu umeshavunjika tayari, ni yeye kulazimika kutumia muda wake kuwazungumzia watu wa kundi hilo, ambao miaka 20 nyuma wasingekuwa sehemu ya hotuba ya Rais, bali watu waliokwishanyamazishwa chini kwa chini. Ndiyo, Mheshimiwa Rais, wanaotaka kuuvunja Muungano, wanauvunja vipande vipande!

Wala sisemi hivyo kwa sababu ya mihadhara ya Jumuiya za Kiislamu na Baraza la Katiba na wimbi la maoni kwenye mitandao ya kijamii inayotumiwa na Wazanzibari. Najua na nathamini sana mchango wa kipekee wa kazi hizo, lakini najua pia kwamba kazi kubwa kabisa inahitajika kufanywa kutimiza azma ya wasioutaka Muungano.

Nje ya sababu na hoja za kisheria na kisomi ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu na wanaharakati kadhaa, mimi nataka nizungumzie hizi za akina miye pangu-pakavu, ambao hatujui mengi sana kuhusu sheria na utaalamu wa siasa.

La msingi kuliko yote, ni kuweka wazi kwamba Muungano wowote wenye nguvu unalazimika kujengwa na washirika wenye nguvu pia, walio huru na wenye uchaguzi wa uhuru huo. Kinachoipa maana hoja ya kuuvunja, kwa hivyo, ni hadithi nzima ya Muungano wenyewe. Nakusudia si kwa sababu tu Zanzibar imepoteza nguvu ndani ya miaka hii ikaribiayo 50 ya Muungano, bali kwa kuwa mshirika mwenzake naye amepoteza mengi sana. Zanzibar haitoki nje ya Muungano, kwa hivyo, kwa maslahi tu ya Zanzibar, bali pia kwa maslahi ya Tanganyika.

Tanganyika ambayo imeshindwa kujisimamia yenyewe ndani ya miaka yake 50 ya uhuru haina uwezo wa kuwa na umoja na Zanzibar. Taifa ambalo limekumbatia udini, ukabila na ueneo, kwa hakika, si mwenza anayeweza kuwa na maslahi. Zanzibar inaonekana kuwa imeshaamua kwenda mbele kama taifa moja, likiwacha migawanyiko nyuma yake. Tanganyika ndiyo sasa inazidi kuzama kwenye utengano.

Wala isije ikahojiwa kwamba Zanzibar iliihitaji Tanganyika siku hizo ilipokuwa na mpasuko, ikasaidiwa nayo kufika hapa ilipo na sasa inataka kuiacha mkono baada ya kufikia hatua ya umoja wake. Isisemwe hivyo kwa kuwa huo sio ukweli. Ndani ya miaka ikaribiayo 50 ya Muungano, Zanzibar ilijikuta ikigawanyika zaidi kuliko kuungana, na tupo wengi tunaohoji kwa mifano ya wazi kwamba Muungano ulisimama kama nyenzo ya kuwagawa na sio kuwaunganisha Wazanzibari. Kwa hivyo, kifo cha Muungano hakitakwenda na roho ya umoja wa Wazanzibari, maana uhai wa Muungano haukusaidia katika maisha ya umoja wa Wazanzibari. Uache Muungano uende, Zanzibar na Tanganyika zibakie kila mmoja na kwake. Baina yo mataifa hayo mawili, pawe na heshima ya udugu na ujirani mwema.

Tanganyika ambayo imejaaliwa sufufu za mali na muluku, rasilimali za kila aina na majina, lakini ambayo kwa miaka yote 50 ya uhuru wake imezidi kuzama kwenye lindi la ufukara na kugeuka kuwa taifa ombaomba, si mwenza mzuri kwa Zanzibar ambayo ina uhaba wa rasilimali, eneo na hata watu. Yaliyopo Tanganyika yangelikuwa na maana kwa Zanzibar, lau Tanganyika isingalijiwachia yenyewe kuliwa na ufisadi, ubadhirifu na wizi wa mali ya umma. Lakini hivyo sivyo ambavyo imekuwa. Badala yake pande zote mbili zinazama pamoja kwenye umasikini uliotitia.

Wala isije ikahojiwa kwamba Wazanzibari wametumia fursa zilizopo Tanganyika kujiimarisha kiuchumi kupitia Muungano huu, maana ukweli ni tafauti. Uwepo wa wafanyabiashara wa Zanzibar (na kwa hakika wengi wao ni wabangaizaji tu) ndani ya ardhi ya Tanganyika, hakuwezi kuwa na maana tafauti ya kuwapo kwa wawekezaji wa nchi nyengine ndani ya ardhi hiyo. Ni bahati mbaya sana, kwamba holela waliyoikuta wafanyabiashara wa Zanzibar, wameitumia kwa kiwango kile kile ambacho wafanyabiashara wengine wote wanaitumia. Na hilo si jambo la kujisifu hata kidogo.

Sasa nini kinachotokea? Watanganyika hucheka na kujipongeza waangaliapo namna walivyoidhibiti Zanzibar wakiamini haifurukuti na kamwe haitafurukuta. Huipuruzia na kuwapuruzia Wazanzibari mshipi, lakini kwa mawanda yasiyokwenda mbali. Kisha wenyewe hulia wazitazamapo hali za maisha yao wenyewe, changamoto nyingi na matatizo yanayowakabili. Na ndio hapo hugundua kwamba hata haya mabavu yao dhidi ya Zanzibar hayawafalii jambo. Nguvu ya Muungano inapungua na Zanzibar inaelekea kwenye uhuru wake.

Kwa hivyo, kwa Rais Kikwete na wenye mtazamo kama wake, ukweli uliopo ukutani ni kwamba, Muungano huu unavunjika si kwa sababu tu Wazanzibari wanataka iwe hivyo, bali kwa kuwa Tanganyika haiihimili tena Zanzibar. Si leo tena!

2 thoughts on “Zanzibar yaelekea kwenye uhuru wake”

  1. watanganyika walikuwa hawafikirii kabisa kwamba iko siku wazanzibari watadai nchi yao. walidhani siku zote tingelikuwa makapi yao. Lakini sasa The time has come hakuna kurudi nyuma tudai uhuru wetu upwa

  2. Mnadai uhuru wenu kutoka kwa nani, kwa sababu Tanganyika mnayoisema haipo, kuna Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Zanzibar iliyomo ndani ya hiyo Tanzania basi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.