Picha maarufu ya kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar kumaanisha Muungano mwaka 1964. Vijana wa Umoja wa Kitaifa wa Zanzibar wanataka Zanzibar irudi kuwa jamhuri kwanza, kisha ndipo izungumzie uhusiano wake na Tanganyika.

Bado tuna kazi kubwa ya kuuelimisha umma wa Kizanzibari na kutafautisha baina ya njia na mitazamo miwili tafauti yenye kuitoa Zanzibar kutoka makucha ya Muungano na papo hapo kuirudisha katika kiganja cha Muungano kupitia Mkataba wa Muungano. Ikiwa hoja zetu hazikusimama juu ya misingi madhubuti basi sehemu kubwa ya elimu ya uraia tunayoitoa itakuwa haifahamiki kama ni ya kuitoa Zanzibar makuchani au kuirudisha kiganjani. Kwa ufupi tunapenda kuzizungumzia nguzo tatu na zote za msingi zenye kutoa mwanga kwenye suala zima la Zanzibar nje ya makucha na nje ya kiganja.

Nguzo ya kwanza ni nguzo ya wakati. Baada ya nusu karne tumeipata fursa adhimu ya sisi wananchi wa Zanzibar kutoa mawazo yetu juu ya mfumo na muelekeo wa Nchi yetu ya Zanzibar kwa mujibu wa maamuzi ya ndani ya Zanzibar yanayotokana na Katiba ya Zanzibar na maamuzi ya Wazanzibari kwa UJUMLA na si kutoka Tanzania Bara/Tanganyika iliojificha, kama ilivyozoweleka kwa muda wa miaka 48.

Nguzo ya pili ni kwamba Wazanzibari WENGI tunahitaji kujitawala, na tunataka nchi yetu ijifungue kabisa kutokana na pingu za Muungano na za Tanganyika iliojificha nyuma ya Muungano.

Tukisema hivyo hatuna maana ya kufuta uwezekano wa ushirikiano baina ya pande mbili hizo na nyenginezo, almuradi tu mambo hayo yakubaliwe BAADA ya kuwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar (JWZ) itakayokuwa na uhuru na mamlaka KAMILI yenye kujitegemea kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na sheria za kimataifa.

Ni LAZIMA kuwepo na mashirikiano na ujirani mwema (zero-conflict) na Tanzania Bara. Hilo halina mjadala hata kidogo na wala Zanzibar haiwezi hata kidogo kukaa kwa uadui na Tanzania Bara. Lakini ni kujidanganya na ni kucheza na shilingi chooni kufikiria kuwa tunaweza kuwa waasisi wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kwa kuitoa Zanzibar katika makucha ya Muungano na kuirejesha kwenye kiganja kipya cha Muungano kupitia Mkataba wa Muungano.

Wenye kuufikiria mfumo wa Nchi za Ulaya (European Union) wakumbuke kuwa nchi 27 wanachama zote zina uhuru wake kamili lakini Ujerumani (na Ufaransa) kutokana na nguvu zake za kiuchumi na mengineyo, ina uwezo wa kuzibana Kikatiba (Treaties) nchi wanachama katika masuala ya sera ya nje  na mengineyo.
Kubwa ambalo Zanzibar inaweza kupewa katika mfumo wa Mkataba wa Muungano ni mzunguko wa Kikatiba wa Urais (rotational presidency) baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) (au Jamhuri ya Watu wa Zanzibar (JWZ)), na Serikali ya Jamhuri ya Muungano (au Jamhuri ya Tanganyika), na kupunguzwa baadhi ya mambo ya Muungano ambayo si ya uti wa mgongo wa nchi yenye mamlaka yake kamili (full sovereignty).

Sasa wanaosimama juu ya hoja ya Muungano wa Mkataba, bila ya KWANZA au hata BAADA ya kuwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, wana nia ya kuyapunguza mambo ya Muungano kwa manufaa ya Zanzibar na Wazanzibari. Wanaweza kuamua kuyapunguza “Mambo 11 ya Muungano ya asili”, au ”Mambo 22 ya Muungano kwa mujibu wa Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kama ilivyo tajwa katika Ibara ya 4 ya Katiba ya 1977”, au ”Mambo 31 ya Muungano yalivyo baada ya kunyumbuliwa.”

Sisi Vijana wa Umoja wa Kitaifa (SUK) tunahoji hivi. Zanzibar haihitajii kuyapunguza mambo 11, 22, au 31, ya Muungano. Ikiwa ni kuchukuwa au kupewa, Zanzibar inahitajia mambo mawili tu (2), na si zaidi ya mawili (2):

1. Jamhuri ya Watu wa Zanzibar juu ya meza.

2. Zanzibar yenye MAMLAKA KAMILI (FULL SOVEREIGNTY) ya kujiamulia Kikatiba mambo yake ya NDANI na ya NJE.

Tunawauliza ndugu zetu wa Mkataba wa Muungano. Je, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, au Tanzania Bara (Tanganyika iliojificha), kweli ipo tayari kutupa mambo hayo mawili (2); au wako tayari kuyapunguza mambo 11, 22 au 31 kwa sababu hayatowapunguzia mazowea yao ya kuiamulia Zanzibar kama walivyokwisha zowea? Au kutupa hayo mambo mawili (2) kwao wao ni sawa na kunywa sumu, ilhali kwa Zanzibar hayo mambo mawili ni mambo pekee yenye kuirejeshea uhai Zanzibar kama vile hewa ya Oxygen (O2) inavyompa uhai binaadamu!

Sisi Vijana wa Umoja wa Kitaifa (SUK) tunaamini kwa dhati yetu na kwa kuungwa mkono na ushahidi wa miaka 48 iliopita ya Mkataba/Katiba, kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haipo tayari kuipa Zanzibar Oxygen (O2):

1. Jamhuri ya Watu wa Zanzibar juu ya Meza.

2. JWZ yenye Mamlaka Kamili ya Kitaifa na ya Kimataifa.

Kama kuna jambo ambalo litakuwa na faida kubwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali kwa kutumia ushujaa wa hali ya juu, na kwa maslaha ya Umoja wa Afrika, kuwaachia Wazanzibari wafanye maamuzi ya mustakbal wa nchi yao kwa hiari, na kutowaona kuwa ni wasaliti wenye nia mbaya ya kuuvunja Muungano ambao hauwawakilishi wala hauna maslaha na wao.

Sisi kama Vijana wa Umoja wa Kitaifa (SUK) tutawaunga mkono mia juu ya mia ndugu zetu wa Mkataba wa Muungano iwapo wataamua kuwapa Wazanzibari elimu ya uraia itakayowawezesha kufikia maazimio ya Mkataba wa Amani na Tanzania Bara wa kuachana kwa njia ya salama na amani (amicable relationship) badala ya kuachana kwa ukhasama (hostile relationship).

Tutibu ugonjwa KWANZA kwa kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kutoka makucha ya Muungano badala ya kuungangania Mkataba wa Muungano ambao utaturudisha kwenye kiganja kisafi na kucha mpya za Muungano. Wala hatukubaliani na mawazo ya kusema na kudai kuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar haitawezekana; jambo hilo halijathibitishwa. Lakini hata hivyo, ni watu wachache sana wanaoweza kukataa na kuamini kuwa kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ni jambo lisilowezekana.

Kuna khofu inayotokana na ukweli kuwa vyama vikubwa vya kisiasa Zanzibar vinapata ruzuku kutoka Serikali ya Muungano, na kuirudisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar bila ya dhamana ya kuulinda Muungano kupitia Mkataba wa Muungano, ni kuzikosa ruzuku na tunza za kisiasa kutoka Tanzania Bara. Suala, nini bora? Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na mustakbal wa vizazi vya Kizanzibari au maslaha ya kivyama? Kwani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar itakuwa haina uwezo au itashindwa kupiva ruzuku vyama vya kisiasa vya Kizanzibari? Maslahi ya Zanzibar ni makubwa zaidi kuliko vyama vya siasa.

Mwisho ni kwamba, juhudi zetu za kuirudisha hadhi ya Zanzibar kitaifa na kimataifa kwa kukirudisha kiti cha Zanzibar cha Umoja wa Mataifa (UN), ni lazima ziwe ni juhudi za taifa zima la Zanzibar inayojumlisha haki za Wazanzibari WOTE.

Muhimu kuliko yote: UZANZIBARI utuunganishe. Kupitia nyenzo ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Zanzibar itajirejeshea Mamlaka yake kamili ya Kitaifa na ya Kimataifa.

Wazanzibari mtakapojiona mko kwenye njia panda na hamna hakika mwende kushoto au kulia, basi kumbukeni kama mnataka kuwa waasisi wa kuitoa Zanzibar kwenya makucha ya Muungano na kuirudisha kwenye kiganja cha Muungano kwa:

1. Kuyapunguza mambo 11, 22, au 31 ya Muungano na kuirudisha tena Zanzibar isiyo na Mamlaka Kamili ya Kitaifa na Kimataifa juu ya kiganja cha Muungano, au mnataka muwe waasisi wa:

2. Kuirudisha Kikatiba Jamhuri ya Watu wa Zanzibar juu ya meza yenye Mamlaka yake Kamili ya Kitaifa na Kimataifa na yenye ujirani mwema na Tanzania Bara, baada ya kupigiwa Kura ya Maoni na Wazanzibari.

Mkataba wa Amani (zero-conflict) baina ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Tanzania Bara/Tanganyika KWANZA.

Jamhuri ya Watu wa Zanzibar KWANZA!

_____________________________________________________________________________

Makala hii imeandikwa na Khalid Gwiji wa Jumuiya ya Vijana wa Umoja wa Kitaifa Zanzibar

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.