Maridhiao ya Wazanzibari yaliyozaa serikali ya umoja wa kitaifa yalikusudiwa sio tu kuwa na Zanzibar isiyo na mpasuko wa kisiasa, bali pia Zanzibar isiyo na mianya ya ufisadi. SUKZ sasa yapaswa kuiziba yote kwa nguvu zote.

UKICHUNGUZA kwa undani mwenendo wa mambo kiutendaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, utagundua rushwa ni tatizo kubwa kuliko linavyotizamwa. Kama si mapenzi kwa rushwa kuwaganda baadhi ya watendaji waandamizi, tusingeona mchele wa kiwango duni ‘mapembe’ unaingizwa ilhali viongozi hao na wanaowashibisha matumbo kwa rushwa, wanajua kiafya mchele huo ni hatari.

Kwanini kama si wakubwa kupakata rushwa serikali haikushitaki wafanyabiashara waliolazimisha kufuli za ghala ulipohifadhiwa mchele mbovu zivunjwe ili shehena ipakiwe kwenye malori na hatimaye kutoroshwa nje ya Zanzibar na kuuzwa.

Bila ya mapenzi kwa rushwa, tusingeshuhudia wafanyabiashara wa mafuta ya petroli wakiyaficha kwa kutaraji bei kupanda; wala tusingeona injini za gari zinaharibika kwa mafuta yaliyochakachuliwa.

Ni utamaduni wa kuamini katika rushwa unabadili akili za watendaji na viongozi serikalini na kuidhinisha ugawaji holela wa viwanja au nyumba za zikiwemo zilizojengwa kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini pale Mombasa Kwa Mchina.

Isitoshe, katika eneo hili la ardhi, ufisadi umejikita mno mpaka kuchochea migogoro ya ardhi maeneo ya vijijini, hasahasa kwenye fukwe huku makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakijitwalia maeneo kwa kisingizio cha kamati za maendeleo za majimbo, na kuyauza kwa mamilioni ya shilingi.

Utamaduni wa watendaji kukumbatia rushwa, ndio unasababisha gari za serikali zitengenezwe kwenye gereji bubu wakati wahisani walifadhili ujenzi wa karakana ya kisasa eneo la Chumbuni.

Kuipenda rushwa ndio sababu ya manunuzi mengi ya serikali na taasisi zake kufanywa pasina kufuata utaratibu unaohusisha pia utangazaji wa zabuni unaoelekezwa na Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2003.

Ni ajabu kubaini kuwa miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010, viongozi wachache wa juu walifanikisha uuzaji au ukodishaji wa majengo tunu ya serikali – Mambomsiige na lililokuwa makao makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Ni ufisadi tu uliosababisha mpaka leo serikali ifunge mdomo badala ya kuufungua na kueleza nini hasa kiliusibu mradi wa Star City , uliopangwa kujengwa eneo huru la kiuchumi la Fumba.

Nini kama si ufisadi maeneo huru ya kiuchumi kama la Amani Industrial Park na Micheweni kukosa wawekezaji leo?

Hata ushenzi unaotamalaki wa watawala kula njama na wakuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kuvuruga taratibu ili kusaidia chama chao kuendelea kukalia Ikulu ni matokeo ya kulea ufisadi tu.

Hata siku moja haitarajiwi matokeo ya uchaguzi yaitwe halali iwapo yalitangazwa baada ya matokeo ya majimbo kadhaa kufutwa; au wanajeshi kupora masanduku ya kura na kwenda kuziharibu kura halali au polisi kuua wananchi wanaosubiri kutangaziwa viongozi waliowapigia kura.

Eti uendeshe uchaguzi, halafu baada ya wiki tume itangaze washindi huku mitaa ikiwa inanuka damu za wananchi wema wanaoamini kuwa ni haki yao ya kuzaliwa, si zawadi kama watawala wanavyoamini, kupewa nafasi ya kuchagua kiongozi wamtakae.

Nini kama si ufisadi watendaji wa wizara ya elimu kuidhinisha wasichana tisa kwenda India kwa ajili ya kozi za kitaalamu kwa ufadhili lakini wakarudishwa kwa sababu hawakutimiza vigezo kule. Na wazazi au walezi wao walikamuliwa fedha kusaidia gharama.

Ni kitu gani hasa kama si rushwa kinachosababisha Ali Ferej Tamim kuendelea kubebwa katika Chama cha Soka (ZFA) wakati hawezi hata kuandaa na kusimamia hafla moja ya kuchangisha fedha za kuihudumia timu ya taifa ndio maana inashiriki mashindano ya CECAFA wachezaji wakiwa hoi bin taabani kwa njaa.

Zipo simulizi kuwa ajira serikalini hazipatikani kiutaratibu kwa vijana wa kike na wa kiume mpaka wanawake wajitolee kuwaridhisha watoa ajira na mpaka wanaume wawe wametokana na vizazi vya ASP na baadaye CCM.

Hiyo nayo ni rushwa kama ilivyo nyingine – mtumishi wa umma kulazimisha malipo ndipo atoe huduma kwa mwananchi.

Hata pale polisi wanapoamua kumaliza kesi za udhalilishaji watoto, hasa wa kike, kwenye vituo vidogo, wanafanya hivyo kwa sababu waliobambwa na matendo hayo, wamewalisha fedha haramu.

Polisi gani anakubali mtoto wake aharibiwe halafu kesi hiyo iishie kituo kidogo ambako rafiki yake au adui yake ndiye mkuu? Hakuna, ila anapotezea kesi inayohusu mtoto wa mwenzake. Rushwa tu.

Aibu kubwa kwamba hata kwa taasisi inayotegemea kwa utoaji wa haki, mahakama, nako mahakimu fulani wanapokea, wengine wanaomba rushwa kupitia kwa makarani wao, ili kuua kesi au kudhulumu mtuhumiwa asiye kosa afungwe.

Wapo mahakimu wanadhani hawajulikani wanapodai rushwa. Wanajulikana maana wanaotoa ili mambo yao yafanikiwe, wanatenda hayo kwa ari, nguvu na kasi mpya zaidi. Mahakimu waovu lazima watajwe kwa njia yoyote iliyopo – mnaweza kunitajia niwataje humu – ikiwemo ya watuhumiwa kuwakataa au kuwalalamikia kwa kiongozi wao – jaji mkuu.

Kumbe sasa mazingira yanaonyesha kabisa kuwa hata wale wafanyabiashara wa chakula wanaopewa misamaha ya kodi, hurudisha ile faida wanayoipata kuwagawia wakubwa waliofanikisha msamaha kupatikana. Rushwa tupu.

Ni rushwa kwa sababu ni upuuzi viongozi kulalamika tu “oh wafanyabiashara wanapewa misamaha ya kodi wanapoingiza mchele, sukari ua unga wa ngano lakini wanaendelea kuuza kwa bei kubwa bidhaa.”

Kwanini wasikamatwe na kushitakiwa mahakamani kama wamevunja sheria? Ni kwa kuwa wanajua hawaguswi maana kabla ya msamaha, au wakati msamaha unatolewa, walishawalisha mapato haramu viongozi waliowasaidia.

Na leo, nathubutu kusema wazi hapa kwamba ni utamaduni huohuo wa watendaji serikalini kupenda mapato haramu (rushwa) uliochangia ajali ya mv Spice Islander 1.

Juu ya matendo maovu ya watendaji wa serikali, nasema siamini kama rushwa hizi zinaingia kwenye mikono ya viongozi wakuu watatu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Siamini kama kiongozi mkuu, Dk. Ali Mohamed Shein anapokea rushwa hizi; wala siamini kama makamu wake wa kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad anapokea; na siamini kama makamu wa pili, Balozi Seif Ali Idi anaweza kupokea rushwa hizi.

Nina maana sijatia imani sana kwa mawaziri wengi kama hawali rushwa. Kuna mambo ya ovyo mengi yanatendeka katika sekta zao za utawala; ni vigumu kuamini yanatendeka bila ya wanaonufaika nayo, kutoa milungula.

Nitaendelea kuamini hivyo mpaka nitapokoma kusikia wapo mawaziri wanakumbatia rushwa. Mengi tunayafuatilia na ipo siku tutayaanika.

Matumaini ya wananchi ni kuona sheria mpya ya kupambana na ufisadi, ile iliyokuja miaka 20 baada ya kuzimwa kifisadi, inatumika kubana mafisadi wa uchumi. Kuipitisha na kuisaini haitoshi. Itumike kikamilifu tena bila hofu.

_________________________________________________________________
Makala ya Jabir Idrissa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.