Mwinyi Haji Makame, kiongozi wa karibuni kabisa wa Serikali ya Zanzibar kutoa kauli zinazoashiria ubaguzi wa wazi kwa misingi ya historia za kisiasa. Lazima kauli kama hizo zipigwe vita.

Leo nataka nizungumzie kuhusu suala la ubaguzi ambalo limekuwa tatizo sugu hapa Zanzibar na zaidi ubaguzi huo ni ule wa kumtizama mtu kwa dhana za kisiasa, jambo ambalo linaviza maendeleo ya visiwa hivi.

Tokea mabadiliko makubwa ya kisiasa ya 1964 kufuatia Mapinduzi nimekuwa nikisema mara nyingi Zanzibar kama nchi ilishindwa kuandaa mikakaati ambayo ingesaidia kuondosha tatizo la chuki za kisiasa zilizojengeka kabla ya Mapinduzi hayo.

Chuki za Zanzibar Nationalist Party ZNP, Zanzibar and Pemba Peoples Party ZPPP kwa upande mmoja na upande mwengine ikiwa ni chama cha ASP, nja ambazo zilifikia kilele pale vyama hivyo vilipouungana na kuchanganya kura zao na kwa hivyo kuchukua Serikali ya kwanza ya Uhuru hapo 1963.

Ubaya ni kuwa chuki hizo zimeachwa zikuwe na zimee, pengine wengine wamekuwa wakifaidika nazo na ndipo pia zikajitokeza wakati siasa za vyama vingi 1992 ziliporudi na kuzagaa kwa hatari sana hata katika kizazi kipya ambacho hakikuwa kikijua ZNP, ZPPP wala Afro Shirazi zaidi ya ngano walizokuwa wakisikia.

Chuki hizo zilipelekea maovu mengi kutokea katika jamii na familia kutengana. Mizizi yake iliingia katika uendeshaji wa Serikali ambapo mtu yoyote ambaye angedhaniwa asie wa chama kilicho madaraka imemuia vigumu kupata ajira au kupata cheo.

Baada ya muda mrefu na jamii na nchi kutanabahi kuwa tumekuwa tukienda kusiko na hilo si jambo la tija kwetu, viongozi wawili wakuu wa vyama kinzani, Dk Amani Karume na Maalim Seif Shariff ambavyo kwa sababu zisizo za msingi vilikuwa vikiendelea kuhusisha na siasa za kabla Mapinduzi vilipoamua kuwa imechosha na imetosha.

Wakasema chuki na ubaguzi iwe basi. Wakasema ni hatari kwa maslahi na mustakbali wa nchi ambapo athari yake ilionekana pia katika kila msimu wa uchaguzi kwa kukosekana mshindi aliyepata imani ya nchi na kwa hivyo kuwa vigumu kushika hatamu za uongozi.

Wakachoka kuonekana kila siku kuna magomvi katika nchi na kuona nchi inaendelea kugawika nusu kwa nusu na kuwa wanaofaidi fursa za nchi ni upande mmoja tu wa siasa na mwengine ukiula huu, chembilecho msemo maarufu wa Mombasa hapo zamani.

Lakini wiki tatu nyuma nilibahatika kuwasilisha makala katika semina ya REDET ambapo nilitakiwa nitizame suala la ushirikishi tokea kuundwa kwa Serikaliya Umoja wa Kitaifa (SUK) , ambayo moja ya jukumu lake lilikuwa au lingekuwa kujaribu kumaliza suala la ubaguzi ndani ya jamii kutokana na siasa.

Ilikuwa ni fikra yangu kuwa hapana juhudi maalum iliyochokuliwa kuhakikisha chuki kama hizo zinazikwa na ndio maana hakuna kikubwa kilichobadilika kwa sababu ushiriki wa kujenga nchi bado una masharti na unalalia upande mmoja na hilo linaiweka SUK njia panda.

Katika mkutano huo ilitokana kauli ambayo mpaka leo inanitetemesha pale nilipotoa hoja ya kukata mizizi ya ubaguzi kwa kuondosha kipingamizi cha Wazanzibari wasio na asili ya Kiafrika kuweza kujiunga na vikosi vya ulinzi kama watapenda, lakini kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mustafa Muhammd kusema, “Haiwezekani kwa bunduki na risasi kupewa kwa mpinzani.”

Ilibidi nifungue darasa kuelezea tofauti ya mpinzani na raia. Kwamba raia wote katika nchi wanatakiwa wawe na haki sawa bila ya kujali asili zao, na nikatoa mfano wa Marekani ambapo hata raia wenye asili Iran wana haki kamili ya kuingia jeshini.

Kumbe kauli ya kiongozi huyo bado inaashiria kuwa hali haijabadilika ndani ya jamii na kuwa bado chuki za kisiasa zipo na mara hii zikijitokeza kupitia kiongozi ambaye ni Waziri tena katika Ofisi ya Rais, Dk. Mwinyihaji Makame.

Katika sehemu kubwa mno ya maisha yangu nimekuwa nikibaguliwa hapa Zanzibar. Nimefukuzwa kazi, nimezuiliwa kuingia sehemu kadhaa, nimetishiwa maisha hadharani hata mbele ya Rais Mkapa, nimebandikwa majina mengi, lakini hili alilonifanyia Waziri Dk Mwinyihaji nimeshindwa kulistahamilia kwa sababu nilikuwa najaribu kujenga imani kwamba ubaguzi unaondoka, ingawa najua bado upo.

Nilisikitishwa kauli ya ubaguzi kutoka kwa Waziri ambaye ni msaidizi muhimu wa Rais na bila kisisi, aibu wala majuto yoyote akatoa kauli kama jambo la kawaida tu, kitendo ambacho kimedhihirisha labda pengine yeye si muumini mzuri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo msingi wake mmoja ni kuondosha ubaguzi wa kisiasa.

Tulikuwa katika mkutano wa waandishi wa habari ambapo Dk. Mwinyihaji alikuwa akikaimu nafasi ya Waziri wa Fedha na kuitishwa kueleza hali ya nishati ndani ya nchi ambapo kulikuwa na uhaba mkubwa wa petroli.

Nilimbana Waziri katika hoja mbili. Kwanza kitendo cha Serikali kukaa wiki mbili bila taarifa ya si uhaba bali ukosefu wa nishati hiyo na nikasema hilo haliwezi kukubalika. Pili nilijaribu kujenga hoja kuwa uchumi wa nchi ulisimama nikimtaka Waziri atoe takwimu Serikali imekosa mapato kiasi gani na uchumi umeathirika kiasi gani nikitaka takwimu.

Kwa kiasi kikubwa mkutano huo ulikuwa mkali na mimi na mwandishi Salma Said tukawa hatumpi Waziri nafasi ya kuvuta pumzi, na kwa kiasi aliona huo ni utovu wa nidhamu kwa kuwa pengine amezoea mikutano ya waandishi wa habari ambapo anasema mpaka anakwisha bila ya kukatishwa au kutupiwa suala la kumkinza. Katika hili nafikiri anapaswa kupata mafunzo upya.

Basi Waziri hakuweza kuchukua na usthamilivu ukamshinda na hapo akajivua gamba na kujionyesha rangi zake halisi, Ah…utanambia nini bwana…nyie kama baba mmoja mama mmoja mna yenu mengine twambieni….sio haya bwana. Sote Wazanzibari bwana msitudanganye bwana…Wewe Buto (albarto yaani ally saleh) nakufahamu toka uko wapi mpaka leo…na huyu (mwandishi salma said) nakufahamu toka zamani mpaka leo”Sote Wazanzibari bwana msitudanganye. Wewe Albarto nakufahamu toka uko wapi huko mpaka leo…na wewe Salma nakujua uzuri…”

Kwa hakika nilimuonea huruma sana Waziri Dk. Mwinyihaji kwa kuwa mpaka leo ana fikra kuwatizama watu kwa kuamini anawatia kwenye dema la kisiasa. Kwa wageni wa siasa za Zanzibar alichokusudia kusema Dk Mwinyihaji kuwa anatua kwamba mimi na mwenzangu anatuhusisha na chama cha CUF na kwa hivyo ni wapinzani hata sasa ambapo CUF imo ndani ya Serikali.

Upande mwengine niliumia kuona kuwa bado kunaweza kuwa na mawazo kama hayo miongoni mwa watu ambao Dk. Ali Muhammed Shein amewapa vyeo vya uwaziri na unajiuliza kwa mtizamo huu nchi inakwenda wapi na kweli ubaguzi nchi hii utaondoka?

Wiki chache nyuma niliandika makala katika safu hii ya kuwataka Watanzania waache kulalamika na wachukue hatua kadri watavyoweza na mimi nikafanya hivyo kwa kuamini kiasi changu kilitosha lakini muhimu zaidi ni kufikisha ujumbe.

Nilitangaza kususia shughuli za Serikali ya Zanzibar kwa wiki moja na mgomo wangu unaisha leo nikiamini roho yangu imekuwa safi ijapo mgomo wangu haukuitikisa Serikali lakini angalau na mimi nimesimama kupinga ubaguzi ambao nimefanyiwa sana lakini sitokubali kuustahamilia tena.
Ningependa pia kutoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kukataa kubaguliwa na kuwapinga akina Dk Mwinyihaji wengine iwe ni mawaziri, watendaji au hata Wazanzibari wenzao wa kawaida. Kwamba ubaguzi hauna nafasi tena na kuwa Zanzibar bila ya ubaguzi inawezekana, uwe ndio wito wetu kwa kila ngazi.
_________________________________________________________________
Makala ya Ally Saleh

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.