Nachukulia kuwa gazeti la leo (8 Januari 2012) na Nipashe, kupitia habari iliyotumwa na mwandishi wake wa Zanzibar (Mwinyi Sadalla), halijamzulia uwongo Mohammed Aboud, kwa kumnukuu akisema “Ni hatari kuwa na mfumo wa kutoa urais wa Muungano kwa zamu kwa sababu ni mwanzo wa kuligawa taifa vipande.”

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Muhamed akizungumza na ujumbe wa Kampuni inayo shuhulikia Ujenzi na Uchumi wa nje(ANHU)Group co,LTD ya China kulia yake ni Makamo wa Rais wa Kampuni hiyo Wang Hao,huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar.
Waziri wa Nchi ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Muhamed.

Na ikiwa hivyo ndivyo, basi tuna haki ya kuijadili kauli yake na ikibidi hata kumjadili yeye mwenyewe mtoa kauli, maana mwisho wa habari hiyo amenukuliwa tena akisema yeye kama yeye, anaona mfumo wa Muungano wa Serikali Mbili ndio unaofaa.

Mazingira iliyotolewa kauli hii yanaonesha kuwa ni kwa ajili ya kujibu ile ya Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ya mwishoni mwa mwaka uliopita, ambapo alisema kwamba ni jambo muhimu kwa Katiba Mpya inayokuja kuweka uwiano (mpokezano) wa nafasi ya uraisi wa Muungano baina ya pande zinazouunda Muungano huu, akipigia mfano wa Katiba ya Muungano wa Visiwa vya Comoro.

Mambo matatu ni ya kuyakumbushia hapa: kwanza, Aboud ni waziri katika serikali ya Zanzibar, ambayo inaogozwa na vyama viwili (CUF na CCM), ingawa matakwa ya kikatiba kwa sasa, sera ya CCM ndiyo inayopewa haki ya kuongoza serikali, kwani ndicho chama kilichotoa rais. Aboud ni waziri kutoka CCM. Pili, Aboud ni waziri kwenye ofisi ya makamo wa pili wa rais (kutoka CCM). Tatu, Aboud ni mtu aliyetumikia sehemu kubwa ya uwanasiasa wake akiwa kwenye serikali ya Muungano, sehemu kubwa ya hiyo hiyo sehemu kubwa akiwa amenyanyuliwa kutoka chini kwenda juu bila ya yeye mwenyewe kujituma kwenye umma (hapa nakusudia umma wa Kizanzibari).

Tuko wengi tunaowachukulia wanasiasa wa aina yake kuwa ni Tanganyika-oriented, kwa maana ya kuwa wamejengwa na kukuzwa kuyatumikia matakwa ya Tanganyika, haidhuru matakwa hayo yawe yako dhidi ya Zanzibar. Na mifano iko tele, chungu nzima!

Uhusiano wa mambo hayo matatu na kauli yake hii uko wazi. Kwanza, kimsingi CCM yenyewe (CCM yenyewe ni ya Dodoma) haiipi nafasi Zanzibar kama nchi huru ndani ya Muungano, bali kinyume chake. Miaka 48 ya Muungano huu kuwa kama ulivyo, ambapo Zanzibar imeminywa na kuminywa hadi kubakia majeruhi asiye matumaini, ni matokeo ya CCM Dodoma.

Kwa msingi huo, akiwa kama mwana-CCM wa aina hiyo, kauli hii si ya ajabu wala ya kutulazimisha kuijadili sana. Tunaijadili sasa kwa kuwa kuna mengine ndani yake. Nalo ni hili la pili: ofisi anayoiwakilisha, yaani Makamo wa Pili wa Rais. Kwa kusema hivi, ofisi hiyo inamjibu Makamo wa Kwanza wa Rais, ambaye ndiye aliyetoa hoja hii ya uwiano (mpokezano).

Na kwa hili, Makamo wa Kwanza aliwakilisha maoni ya Wazanzibari walio wengi na, hivyo, ofisi ya makamo wa pili imefanya kinyume chake. Mimi nasimama upande wa Makamo wa Kwanza, nikiamini alikuwa na ni sahihi na naipinga kauli ya ofisi ya Makamo wa Pili, nikiamini haikuwa na si sahihi kwetu Wazanzibari.

Aboud anasema utaratibu wa kupokezana uraisi wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar utaigawa Tanzania, kwa kuwa kuna siku mikoa mingine ya Tanzania itataka uraisi uwe wa kubadilishana kutoka kila mkoa. Nachelea kuuita ujinga, lakini najikusuru kusema kwamba haingii akilini ikiwa waziri kwenye serikali ya Zanzibar, naye anaamini kuwa Zanzibar ni kama mkoa tu mwengine wa Tanzania! Kwamba hoja inayotumiwa na Zanzibar kudai haki yake kwenye Muungano inaweza pia kutumiwa na mikoa mingine, na hivyo bora kuinyamazisha maana mwisho wake utakuwa mchafu-koge!

Mohammed Aboud Mohammed, Zanzibar si mkoa wa Tanzania. Zanzibar, hata kwa katiba uliyoapa, ni moja kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwanza, Dodoma na Singida hazikuungana pamoja kuunda Tanzania. Kwa ujumla wake, hizo zinaunda sehemu moja tu ya Tanzania, (Tanganyika). Na hili siamini kama ni somo ambalo nilipaswa hapa kulitoa kwako!

Nachelea kusema kwamba kwa viongozi wa serikali wa aina hii waliopo kwenye ofisi ya makamo wa pili wa rais, Zanzibar ina safari refu ya kuienda kabla haki yake haijaheshimiwa ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano.

Hakuna siku nyengine yoyote huko mbele Zanzibar itatoa rais wa Jamhuri ya Muungano, maana kwa hakika wanaofanya maamuzi ya nani awe raisi wa Tanzania si Wazanzibari. Unaposema kwamba ulinganishe vigezo vya uwezo tu peke yake, Tanganyika kama ilivyo Zanzibar haina upungufu wa raia wenye uwezo wa kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kigezo hicho pekee kikitumika, mwisho wa siku wanaofanya maamuzi watapiga kura, na walio wengi (ama katika kuwapitisha wagombea kwenye vyama au katika uchaguzi mkuu) watamchagua yule mwenye sifa ya ziada kwao, yaani ukuruba. Huo ndio ukweli!

Lakini kwa nini kauli hii ikaja sas? Sababu moja ni hiyo niliyoitaja, kwamba anajibiwa Makamo wa Kwanza, Maalim Seif. Na kama nilivyoonesha, kwa kuwa kwa hili Maalim Seif aliwakilisha mtazamo wa Wazanzibari tulio wengi, maana yake ni kuwa ofisi ya makamo wa pili inatujibu sisi Wazanzibari kwa wingi na umoja wetu. Inatujibu kwamba kutokea upande wao, tusitarajie chochote katika Katiba Mpya inayokuja zaidi ya kuzishadidia shemere za Muungano zilizopo na hata ikibidi kuziongeza nyengine.

Sababu nyengine ni uwezekano kwamba Waziri Aboud na wengine katika ofisi wanayoiwakilisha, wanatupa macho yao mwaka 2015, maana ndipo pua zao zinapofikia. Wanaangalia uwezekano wa ama uraisi wa Zanzibar, uraisi wa Muungano au hata umakamo rais wa Muungano?

Yale yale yaliyoizamisha Zanzibar kwa miaka 50 kabla ya Maridhiano yaliyopo sasa, ndiyo haya haya ninayoyazungumzia sasa. safari tunayo, Wazanzibari wenzangu. Lakini tusivunjike moyo. Tutafika.

Wallahi tutafika, walaukarihalmunaafiqun!

3 thoughts on “Zanzibar tutafika, walaukarihalmunafiqun!”

  1. huyu bwana tunaijua vyema historia yake na maisha yake. asikuumishe kichwa. alipata ngekewa ya kuongoza Wizara Tanganyika na Zanzibar lkn c kwa sifa. c mwanasiasa, c mtaalamu wala c msomi. ni zari la mentali tu wala rafiki yangu ackuumishe kichwa kumjadili. ila inauma km mzanzibari kutamka vitu pumba km hivyo. tunaona haya ila tutafanyaje! cha mcngi tuwe na mcmamo ktk mambo ya mcngi hasa Taifa/Dola huru la Zanzibar. hakuna Serikali 1,2 wala 3. hapa ni Uhuru wetu kutoka kwa mkoloni Tanganyiaka.

  2. wewe ni mpemba au mzanzibari? sasa tuambie maringo mulionao ni utajiri au elimu muruke na kusambaratika duniani kote .MIMI NAONA NI UMASIKINI WA KUTAFUTA RIZIKI NDIO UMEWAFANYA KUPIGA KELELE.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.