Rais Ali Mohammed Shein

KWA miezi miwili sasa kumekuwa kukishuhudia vikao vya serikali kujitathmini. Alianza kiongozi mkuu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. Alikutana na waandishi wa habari waandamizi na kuwaeleza tathmini yake ya utendaji tangu ashike usukani wa kuiongoza nchi hii ya visiwa.

Alitaja kile alichoamini ni hatua mbele. Akataja alivyoona ni vikwazo kwa serikali kupiga hatua nyingine zaidi mbele. Alitaja chimbuko la vikwazo hivyo. Alikemea wanaovileta – maana aliamini vingi vimetokana na tabia mbaya za watendaji aliowapa dhamana ndani ya serikali anayoiongoza.

Basi Dk. Shein alikiri zipo changamoto mbilitatu zinazohitaji kufanyiwa kazi ili kujenga msingi imara wa kuiwezesha serikali kufanikisha malengo yake kwa kipindi kilichoanza.

Sasa umemalizika mwaka mmoja wa SUK. Mwezi mmoja wa ziada, Disemba, umepita. Tulikuwa tunazungumzia yaliyohusu mwaka 2011. Umekwisha na umepita. Tunaingia mwaka mpya wa 2012. Miaka miwili tu kabla ya kuukuta mwaka wa uchaguzi mkuu, 2015.

Nataka sote kwa umoja wetu, Wazanzibari pamoja na rafiki zetu kutoka maeneo mengine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nje yake, tufikirie mambo mema, ambayo yataongeza nguvu ya kupiga hatua ya maendeleo kwa mwaka 2012.

Kwa hakika, kwa uhalisia wa mambo, mwaka huo wa uchaguzi tu ndio utaanzia Januari. Lakini, mipango ya serikali inayolenga katika kuratibu uchaguzi wenyewe itaanza mapema.

Inawezekana tayari serikali imeanza sasa kuchukua hatua muhimu za maandalizi na kutengeneza mazingira ili utakapofika mwaka ule, iwe imefika hatua nzuri ya kuja kuhakikishia wananchi na washirika wote wa masuala ya demokrasia kufanyika uchaguzi mkuu kwa amani na utengamano.

Akili na fikra zangu, zinalenga kushajiisha uongozi wa serikali kuwajibika kisawasawa katika kusimamia uchaguzi ulio huru, wa haki na utakaofuata vigezo vya kimataifa na kutaraji ukubalike ndani na katika jumuiya ya kimataifa.

Mwaka 2011 ilikuwa wa kuunda serikali. Mpaka sasa, wakuu wa mikoa na wilaya hawajatangazwa rasmi. Wanaotumika ni wale waliokuwepo kabla ya uchaguzi.

Dk. Shein aliteua viongozi wengi watendaji, wakiwemo wahafidhina wasiopenda mabadiliko, akiwarithi kutoka awamu ya rais mstaafu Amani Abeid Karume.

Hili limezorotesha ufanisi na kuchochea wananchi waichukie serikali. Rais alikemea watumishi wabaya. Makamu wake wa kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad, naye ametaja kasoro hii katika taarifa yake ya tathmini ya mwaka mmoja ya utendaji ya serikali ya umoja wa kitaifa (SUK), mbele ya waandishi wa habari 17 Desemba 2011.

Hata hivyo, hatukuona hatua hasa dhidi ya watendaji wakorofi. Ni watendaji hao walimtia rais katika mgogoro kwa kupendekeza wateule waliochoka kiumri na wasiokuwa na historia nzuri ya utendaji serikalini.

Dk. Shein anaonekana kama kiongozi mzito wa kudhibiti wakorofi aliowapa dhamana, kwa kuwa baadhi yao wamethibitika kuvuruga dhamira ya maridhiano.

Mfano mwingine ni wa ukorofi unaosababisha wananchi wengi kuendelea kuhenyea kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi licha ya kuwa kisheria, ni lazima kila mtu awe nacho. Ilitarajiwa wale masheha wanaolalamikiwa kukwamisha wananchi, wafukuzwe kazi.

Bado kuna tatizo la ufisadi serikalini. Wapo watendaji wamekithiri kwa uovu huu lakini bado wanaendelea kutesa kwa kujinufaisha kupitia ofisi za umma walizokabidhiwa kuziongoza.

Ipo simulizi ya baadhi yao kujimilikisha mitambo ya serikali na kuikodisha kwa wajenzi wa barabara. Hili linatajwa kuwagusa watendaji ndani ya Idara ya Ujenzi wa Barabara (UUB).

Kuna tatizo la baadhi ya wakuu wa taasisi za serikali kufanya kazi za wasaidizi wao kama kule Shirika la Bandari Zanzibar ambako kuna kigogo anaendesha mtambo wa kubebea makontena. Wafanyakazi wanamtuhumu kuwa anatumia mwanya huo kujinufaisha kwa kuwa wenye mizigo yao hulazimika kumfuata kuomba “msaada” unaotolewa kwa gharama.

Bado serikali ina mzigo mkubwa wa kupata mapato ya kutosheleza mahitaji yake. Kuna pengo kubwa la mapato kiasi cha serikali kulalamika kitendo cha wahisani kutotimiza ahadi ya kusaidia bajeti kwamba kinadhoofisha nguvu ya serikali kutekeleza mipango yake.

Serikali inakabiliwa na tatizo la kushindwa kuimarisha ipasavyo mitandao ya huduma za kijamii kama vile elimu, maji na tiba mahospitalini mwake.

Wanafunzi kadhaa waliofuzu kujiunga na vyuo vya elimu ya juu wamekwama kwa ukosefu wa fedha. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar imeshindwa kukidhi kiu ya vijana kusoma.

Makamu wa kwanza wa rais hivi karibuni aliwaambia waandishi wa habari kuwa kati ya vijana zaidi ya 1,200 waliofikia kiwango cha kujiunga na vyuo vikuu, ni 100 tu waliopatiwa fedha kutimiza ndoto zao.

Tatizo la maji safi kwa wananchi linaendelea. Kwa wakaazi wa mji wa Zanzibar, tatizo ni kubwa zaidi kutokana na mradi uliofadhiliwa na serikali ya China kukwama kabla ya kuyafikisha maji kwa watumiaji.

Mpaka sasa serikali inahangaika kupata wafadhili wa kuendeleza mradi huo mkubwa unaohusisha uchimbaji visima vikubwa eneo la Welezo na kutandaza mabomba makubwa maeneo ya mji.

Inatia moyo mradi wa kutengeneza vituo kadhaa vya afya vijijini kwa msaada wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), umefikia pazuri. Kiasi cha vituo 40 vimetengenezwa upya na kupatiwa vifaa tiba.

Lakini, bado Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, inayochukuliwa kuwa ndiyo hospitali ya rufaa Zanzibar, ina hali mbaya. Zana zimechakaa, na katika Kitengo cha Dharura (ICU) inasikitisha.

Zanzibar inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari bingwa. Wengi wamekimbilia nje kupata maslahi zaidi pamoja na mazingira bora ya kikazi. Baadhi ya madaktari wamekwenda nchini Botswana na wengine Tanzania Bara ambako imekuwa kimbilio kubwa kwa madaktari wanaohitimu katika miaka ya hivi karibuni.

Sekta hizi tatu – elimu, maji na afya – zinahitaji fedha nyingi kuzijenga na kuziimarisha. Kama serikali haitatilia mkazo kudhibiti wizi wa mapato au “kutafuna jongoo kwa meno,” ni dhahiri itajikuta ikitumia miaka yote minne iliyobaki kufikia uchaguzi wa 2015, ikiendelea kuahidi tu wananchi bali utekelezaji kaputi.

______________________________________________Makala ya Jabir Idrissa katika gazeti la MwanaHALISI linalochapishwa Dar es Salaam, 28 Disemba 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.