Mzee Hassan Nassor Moyo

HATUNA budi tushukuru kwamba mwaka jana visiwa vya Zanzibar viliweza kukwepa machafuko, migawanyiko na migogoro ya kisiasa iliyozikumba nchi kadhaa barani Afrika na ulimwenguni kwa jumla. Kinyume na kawaida, mwaka ulipita bila ya kuzuka vituko vyovyote au mapambano yoyote ya kisiasa baina ya wafuasi wa vyama vikuu viwili vya CCM na CUF Visiwani humo au kama ilivyokuwa zamani baina ya vyama vya ZNP na ASP.

Hilo ni jambo kubwa hasa kwa vile mwaka huo ulizaliwa miezi isiyotimu hata mitatu baada ya Uchaguzi Mkuu uliokuwa na matokeo ambayo wengi wa wafuasi wa chama cha CUF waliyapinga. Na hapa hekima iliyotumiwa na uongozi wa CUF inastahili pongezi.

Kulikuwa na hatari kwamba matokeo hayo yangesababisha vurugu nyingine za kisiasa visiwani humo. Vurugu aina hizo ndizo zilizokuwa zamani zikizusha mifarakano miongoni mwa Wazanzibari na kuleta mpasuko katika jamii, mpasuko ambao wengi wakidhani hauna dawa.

Ukweli ni kwamba mpasuko huo ulikuwa na dawa. Waliokuwa na dawa hiyo walikuwa wenyewe Wazanzibari. Watu wa nje na taasisi zao walipojaribu kuleta suluhu hawakufanikiwa. Lakini wenyeji walipong’amua kuwa kila wakiuendekeza uhasama wao ndipo wanapozidi kuathirika, wakajizatiti kuukomesha kwa maslahi yao wenyewe.

Rais mstaafu, Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamadi walionyesha ustadi mkubwa wa kisiasa kwa kufikia Maridhiano. Kuna Wazanzibari wenzao kadhaa ambao waliwatia moyo na kuwasaidia kuyafikia hayo Maridhiano. Ninaamini kwamba iko siku wanahistoria watapokuwa wanakipitia na kukitalii kipindi hiki watawatambua kuwa ni mashujaa wa amani.

Miongoni mwao ni Hassan Nassor Moyo aliyekuwa mshenga mkuu katika ndoa hii ya kisiasa. Mzee Moyo ni mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya mwaka 1964, aliyewahi kuwa waziri katika serikali za Zanzibar na Tanzania na ambaye sasa ameziweka upande siasa za kichama na kuwahimiza Wazanzibari na viongozi wao wa kisiasa waungane kwa maslahi ya taifa lao.

Msimamo wake huo na wa wengine kama yeye wenye itikadi tofauti unaashiria kuwa yale mapambano ya kisiasa ya baina ya mwaka 1957 na mwaka 2010 hayatoendelezwa tena. Badala yake yatakuwa ni mambo ya kukumbukwa.

Kwa hakika, kwa muda mrefu Wazanzibari wamekuwa wakitambua kwamba siasa za vyama na historia ndefu ya siasa hizo, ndizo zilizokuwa zikiwagawa na kuzusha ukinzani miongoni mwao. Wakati ule utiifu kwa vyama na sera za vyama ulionekana kuwa ni muhimu zaidi kushinda maslahi ya nchi.

Hizo tofauti za kisiasa zilikuwa na athari mbaya kwa maendeleo ya Zanzibar kwa upande wa kiuchumi na hata wa kijamii. Maridhiano yaliyopatikana na yaliyoleta umoja katika nchi yameleta vile vile hali ya matumaini makubwa kwa mustakbali wa Zanzibar.

Matokeo ya yote hayo ni kwamba hivi sasa kuna uwezekano wa Zanzibar kuweza kunusurika isiporomoke kabisa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hali kadhalika kuna tumaini kubwa kwamba visiwa hivyo murua vinaweza kuokolewa na kupatiwa maendeleo kwa manufaa ya vizazi vyake vya sasa na vijavyo.

Wazanzibari walifanya busara kubwa walipoamua kuyasahau yaliyopita na kuganga yajayo, hususan kuhusu mustakbali wa nchi yao na wapi wanakotaka ielekee baada ya miaka 47 ya Muungano.

Mwaka 2011 ulishuhudia kuimarishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo nayo iliustawisha umoja wa Wazanzibari bila ya kujali utiifu wao wa kichama. Serikali hiyo pia ilionekana ikichukuwa hatua kwa kuzingatia manufaa ya nchi badala ya maslahi ya chama chochote cha kisiasa.

Huu ni mwanzo mwema. Hatukutaraji kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja serikali hiyo itaweza kuyatatua matatizo yote ya visiwa hivyo. Matatizo yanayoikabili ni makubwa mno. Kila sekta unayoiangalia na kuitathmini unaona ina mashakil yasiyosemeka.

Jitihada zinafanywa lakini kila uchao jitihada hizo zinapambana na uzembe, ubadhirifu wa fedha za umma, urasimu usiohitajika, ulaji rushwa na ufisadi kwa jumla. Huo ndio uzoefu wa muda mrefu wa watumishi wa serikali.

Pia ingawa viongozi wamenuia kuujenga umoja wa Wazanzibari bado kuna kubaguana-baguana katika uteuzi wa watendaji wa ngazi za juu serikalini. Hiyo ndiyo hali halisi.

Pamoja na hayo serikali haikufanikiwa kuwapatia wananchi huduma za umeme na maji bila ya kuwakatiakatia. Hizo ni miongoni mwa kasoro zilizopo. Katika sekta hii ya huduma hizo pia Zanzibar inaweza kujifunza kutoka visiwa vingine vya Bahari ya Hindi, hasa Mauritius na Ushelisheli, visiwa vyenye mengi yanayofanana na Zanzibar.

Kwa upande wa uchumi, serikali imejaribu kupandisha bei za karafuu na inaonyesha ina nia ya kupunguza bei za baadhi ya bidhaa za maisha ya kila siku. Safari lakini ni ndefu na kuna mengi ya kufanywa na kusawazishwa, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali ili angalau waweze kukidhi mahitaji yao muhimu ya kila siku.

La kutia moyo, hata hivyo, ni kuona kwamba serikali imeazimia kwamba inahakikisha itakuwa na mamlaka au madaraka ya kusimamia shughuli zote zinazohusu uchumi wa Zanzibar.

La awali katika orodha ya masuala ya kiuchumi ambayo Zanzibar inataka iwe na madaraka kamili juu yake ni suala la mafuta na gesi asilia ya Zanzibar. Kwa muda wa zaidi ya miaka 10, suala hili lilizifanya serikali za Zanzibar na Muungano zisuguane ‘roho’ na mpaka sasa hapajapatikana ufumbuzi ulio wazi.

Wengi Visiwani wanaendelea kujiuliza iweje mali za asili za Tanzania Bara kama gesi asilia na maadini zisiwe za Muungano bali za Bara tu na mafuta na gesi asilia ya Zanzibar yawe ya Muungano?

Kuhusu suala hili msimamo wa serikali ya Zanzibar ni wazi na si wa kutetereka: inataka iwe na mamlaka kamili ya kusimamia shughuli zote zinazohusu mafuta yake na gesi asilia kuanzia uchimbaji hadi mauzo na kwamba, mapato yatayopatikana yataingia katika hazina ya Zanzibar.

Jingine la kutia moyo ni kuona kwamba kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1964 hivi sasa Zanzibar ina ajenda yake ambayo ni tofauti na ile ya mwenzake ndani ya Muungano.

Ajenda hii, kama tulivyoieleza katika makala zilizopita,imepiga hatua kubwa tangu ianze kupigiwa debe na inavyoonyesha Wazanzibari wengi hawana wasiwasi nayo. Msingi wake ni kutaka usawa baina ya Zanzibar na Tanganyika.

Wanaamini kwamba ni sera hii tu itakayoweza kuwakomboa wao na wale wanaopigania usawa huo kwa upande wa Tanganyika pia. Wanaamini vilevile kwamba watapata hasara kubwa pindi watapoiacha hiyo Ajenda yao au watapojiachia wagawike tena kivyama.

Bila ya shaka kusema haya hakumaanishi kwamba Wazanzibari hawautaki mfumo wa vyama vingi vya kisiasa au kwamba wameuzika upinzani wa kisiasa, la hasha.

Katika kila jamii lazima kuna watu au mtu mwenye mitizamo na misimamo tofauti ya kisiasa. Lakini katika jamii za kidemokrasia watu wenye misimamo tofauti huvumiliana na kuridhiana panapohusika maslahi ya kitaifa.

Zaidi panapokuja masuala nyeti yenye kuhusu uhuru au uhai wa taifa lao basi pande zenye kukinzana huzika tofauti zao na huwa na msimamo mmoja. Huzitupilia mbali ilani za vyama vyao zisije ilani hizo zikageuka na kuwa laana kwa taifa.

Huo ndio wenye kuitwa umoja wa kitaifa. Ilani za vyama huwa haziruhusiwi kuwa chachu ya watu kukimbilia mapanga kila wanapozozana kisiasa.

Ni matumaini ya wengi wa Wazanzibari kwamba mwaka huu wa 2012, mshikamano huu uliopo sasa utafungua ukurasa mwingine wa malengo yaliyokusudiwa ya kuijenga Zanzibar mpya na kunyanyua hali za maisha za watu wake.

Kazi hiyo ni ngumu. Lakini katika karata hizi za kisiasa turufu haimo mikononi mwa Rais Ali Mohamed Shein na serikali yake tu, bali pia imo mikononi mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, chombo kikuu cha utungaji wa sheria visiwani.

Wazanzibari ndio waliowapa turufu hiyo tokea walipopiga ile kura ya kihistoria ya maoni kuunga mkono Maridhiano katikati mwa mwaka 2010. Mzee Moyo na wenzake wamekwishatoa mchango wao. Ni mchango wa kihistoria na wenye kuonyesha uzalendo wa hali ya juu.

Sasa taasisi hizo tatu — Rais, serikali na Baraza — zina changamoto ya kuicheza vizuri turufu hiyo kwani taasisi hizo ndizo zenye dhima ya kuisarifu hiyo turufu. Wazanzibari wanaukaribisha 2012 huku wakiwa na matumaini makubwa kwamba hawatovunjwa moyo.

______________________________________________
Makala ya Ahmed Rajab katika gazeti la Raia Mwema linalochapishwa Dar es Salaam, 4 Januari 2012

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.