Mjumbe wa kamati ya Maridhiano ya Wazanzibari, Mzee Nassor Moyo (kulia), akimkabidhi mmoja wa waasisi wa Maridhiano hayo, Rais Mstaafu Amani Karume, nishani ya mashujaa wa Zanzibar kwa kutambua mchango wa kiongozi huyo. Ni bahati mbaya sana kwamba sasa watendaji kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ambalo ni zao la Maridhiano hayo, wanataka kuyazika na roho yake!

Hakuna cha kuficha sasa. Utumishi wa umma ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) unaumwa na unatumiwa vibaya na baadhi ya watu kwa maslahi binafsi. Watendaji wakorofi ndio wagonjwa wenyewe. Kwa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakipata simulizi mara kwa mara za misuguano ya kiutendaji inayotokea katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambayo kwa mwaka mmoja sasa imeanza kuendeshwa kwa muundo wa serikali ya ushirikiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Mara utasikia mtendaji fulani amekwaruzana au haelewani na waziri wake; au mtendaji wa wizara fulani anadharau wananchi anaokutana nao ili kuhudumiwa, au utasikia fedha hazijatolewa kwasababu katibu mkuu au mkurugenzi wa mipango na uendeshaji amezuia kasma husika.

Nami nimekuwa nikiamini na kusema wazi na kwa lugha isiyo na ukakasi, kwamba watendaji wengi serikalini hawataki kubadilika kiutendaji – wameendekeza uhafidhina na kuuendeleza. Wapo watendaji wameamua kwa makusudi, kuzorotesha maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kwa harubu kubwa, baada ya waasisi wa maridhiano hayo kuweka nguvu nyingi za hali na mali pamoja na muda wao mwingi ili kuyafanikisha.

Watendaji hao wamekataa kutambua mchango muhimu wa viongozi walioheshimika na kujitolea kubuni mpango wa kukutanisha viongozi wakuu wa vyama hivyo ili kujadili hali ya mambo ilivyo na namna inavyohitaji kudhibitiwa. Wakawahimiza kufikia makubaliano ili kujenga mwelekeo au mustakabali mpya wa nchi.

Tangu mapema sana, waliamua kuyakebehi makubaliano yaliyofikiwa baada ya msingi uliowekwa hadharani tarehe 5 Novemba mwaka 2009, pale Amani Abeid Karume, aliyekuwa rais, na Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, walipokutana Ikulu na kutoa taarifa ya kujenga dhamira ya maridhiano ya kisiasa.

Inasikitisha na kustaajabisha sana kuona watendaji, baadhi wakiwa walioelimika vema kufikia kubeba digrii mbili mifukoni, wameendelea kuwa hayawani. Wanatumikia utashi wao badala ya wananchi waliowapa dhamana. Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni, mjini Zanzibar, Jumamosi iliyopita, tarehe 17 Desemba, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif alisema dhamira ya maridhiano bado haijaganda akilini au nyoyoni mwa watendaji.

Alikuwa akitoa tathmini ya mwaka mmoja ya utendaji kazi wa serikali ya umoja, aliposema malengo ya kuanzishwa kwa mfumo wa serikali shirikishi wa kuchukua nafasi ya mfumo tenganishi, hayajazama kwa watendaji wengi. “Wanaendesha shughuli za umma kwa taratibu zilezile ambazo hazisaidii sana kuimarisha umoja wetu.

Mheshimiwa Rais (Dk. Shein) amekuwa akieleza kwa mkazo mkubwa haja ya watendaji wa serikali kubadilika. Amefanya hivyo kila alipopata nafasi. Nataasafu (nathubutu) kusema baadhi ya watendaji wanafanya kazi kwa mazoea. Hawajabadilika. Ile kasi ya kuwahudumia wananchi ambayo Mheshimiwa Rais aliitarajia bado haijaridhisha.” Nini maana ya matamshi haya? Ina maana kuwa baadhi ya watendaji ambao ni watumishi wa umma si wanasiasa, wamebaki wakorofi.
Hawataki kufuata kanuni, taratibu wala sheria za utumishi ambazo zinahimiza kila mtumishi kujitahidi kuleta ufanisi ili kuiwezesha serikali kufikia malengo ilojiwekea.

Leo, ni aibu ilioje kwa rais na wasaidizi wake wakuu kutumia muda adhimu uliopaswa kutumika kwa ajili ya kazi za kujenga uchumi na ustawi wa wananchi, kuendelea kukemea watendaji aliowateua na kuwaapisha kubeba dhamana ya kusaidia serikali kutimiza malengo yake.

Dk. Shein alishawasema hadharani katika hotuba yake ya Baraza la Idd el Haji alipoonyesha kuguswa na mwenendo mbaya wa watendaji wakorofi. Kwamba kuna viongozi aliowapa dhamana ya kutumikia watu wanadharau na kukejeli wananchi.

Akatahadharisha kuwa mtindo huo unasababisha kuichonganisha serikali na wananchi na hivyo waanze kuichukia serikali yao waliyoipa ridhaa na kuitarajia kuimarisha ustawi wao. Akataka waache. Hawajasikia, na kama wamesikia hawajatii agizo la rais, agizo la serikali anayoiongoza. Wameamua kuziba masikio wasisikie kilio cha wananchi na agizo hilo la rais aliyewateua, na wanafumba macho wasione madhila wanayowapatisha wananchi kinyume na matarajio yao na ya rais aliyewateua.

Ukweli ni kwamba wapo watendaji wamejihusisha kwa mazingira ya siri na wengine kwa dhahiri na harakati za kisiasa zilizoegemea CCM, chama wanachoamini kuwa kitadumu daima na kuendelea kuwadekeza kufanya watakavyo na wasidhibitiwe kwa namna yoyote ile.

Hawa ndio watendaji ambao wanatumia magari ya serikali kuhudhuria mikutano ya siasa ya chama chao hicho; wanaoyatoa magari kwa ndugu zao kufanikisha shughuli za kisiasa au za nyumbani wakati wa kazi na baada ya kazi.

Tumeambiwa namna baadhi yao wanavyokiuka taratibu za manunuzi ya umma; wanavyolazimisha matumizi mabaya ya fedha kwa maslahi binafsi; wanavyochagua waajiriwa wapya kwa kuzingatia misingi ya hisia za kisiasa na uhusiano wa kindugu; na wanavyotamba kuwa wao “hawagusiki” maana ni “wateuliwa na rais.” Bila ya aibu, ni watendaji hawa wanamfikisha kiongozi mkuu wa upinzani kisiasa, Maalim Seif, kulaumu kidiplomasia umangimeza unaofanywa na serikali kutokana na uhuni wa masheha kukataa kuidhinisha barua za wananchi wanaotaka kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Wanaohusika wanajua fika kwamba kisheria ni kosa kwa mtu kutokuwa na kitambulisho hicho, na akishitakiwa na kupatikana na hatia ya kutokuwa na ID bila ya sababu ya msingi, anahukumiwa kifungo cha jela au faini au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Hawajali kitu. Wanaendelea kuhalifu misingi ya utawala bora bila la kuhofia kudhibitiwa. Kama vile wana uhakika wa mia kwa mia kuwa hakuna kiongozi aliye juu yao atakayewachukulia hatua. Sasa ni kitu mbaya kuendeleza utamaduni wa impunity ndani ya maridhiano. Kwamba mtu unatenda kosa kwa kujua lakini unatenda kwa sababu una uhakika hutaulizwa na yeyote.

Tuseme watendaji wengi wa SUK wameitia mfukoni serikali. Balaa kubwa hili! Hawa ni watendaji wa kuwaonea huruma kwa kuwa hawajielewi kwamba wanajiendekeza mno isivyotakiwa. Kwamba wanazidi kupitwa na wakati na watakuja kujuta baadaye kamba waliyoishikilia itakapokatika. Siku zote hakuna uovu unaodumu maisha. Lazima tu utafika mwisho.

Chanzo: Makala ya Jabir Idrissa katika safu ya Kalamu ya Jabir kwenye gazeti la MwanaHALISI, 28 Disemba 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.