Rais Ali Shein akikutana na serikali watendaji wa serikali yake. Je, watendaji hawa wanaifanya serikali iende mwendo wa mbwa-kachoka: hatua moja mbele, tisa nyuma?

Kwa kiasi kikubwa wengi tumekuwa na imani na kazi ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika kipindi chake cha mwaka mmoja na kidogo hivi. Kumekuwa na dalili kuwa kuna nia nzuri ya kuleta mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii na hata ya kiuchumi na kwa hilo pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu ndani ya Zanzibar iliyozoea vurugu, SUK imekuwa ikienda vizuri.

Kumejitokeza na kuwapo dalili za kuwa na uwazi ndani ya Serikali ingawa tunaona ulegelege katika masuala ya usimamizi na kuna baadhi ya mambo mtu usingetarajia kuwa yanatokea, lakini bado yapo wazi wazi kiasi ambacho baadhi ya wakati unaweza kujiuliza kama kuna Serikali makini.
Kuongezwa kwa bei ya karafuu, kuongezwa kwa mishahara ya wafanyakazi kumeonyesha dalili jinsi SUK inavyotizama pande zote za umma, yaani wakulima na wafanyakazi. Lakini, wakati wakulima wanafaidi moja kwa moja mauzo yao ya karafuu na kutia kibindoni mamilioni, mpaka leo kuna habari kuwa marekebisho ya mishahara yaliofanywa na Serikali bado hayajawafikia wafanyakazi waliolengwa.
Masikio yangu yamesikia malalamiko kadhaa kuwa kwa baadhi hayakuwa mabadiliko kitu na kwa kweli kuna watu ambao badala ya kuongezwa wamepunguziwa na mpaka leo hali inaendelea kuwa hivyo. Wakati wa chini wakilalamikia, “mkia wa mbuzi” inaeleweka jinsi ambavyo mambo yalivyogeuka kuwa “bambam” kwa wakurugenzi, wakurugenzi watendaji na makatibu wakuu, ambapo isingefaa kutaja kiwango wanachopata maana kitaleta sekeseke.
Jambo lingine katika hilo ni majigambo ya SUK kwamba nyongeza iliyotoa haijawahi kutolewa duniani kiasilimia, lakini ukweli ni kuwa haikulingana kabisa na kasi ya ukuaji wa uhalisi wa matumizi, na kwa hivyo pamoja na nyongeza hiyo mfanyakazi bado hana kikubwa anachokichukua nyumbani. Baya zaidi ni kuwa mfanyakazi huyu, kwa mazingira ya Zanzibar hana nafasi na kwa kweli hasa kuna uhaba wa kupata kazi za ziada kuweza kumuongezea kipato na kwa hivyo mara nyingi anakuwa mdokozi ndani ya mfumo wa kazi yake ili kujaliza kipato chake.
Mwanafunzi katika mwisho wa mwaka huu wa SUK, hapa nakusudia mwanafunzi wa kiwango cha elimu ya juu, ameachwa pabaya zaidi na utaratibu wa kudhamini wanafunzi ili waweze kumudu masomo yao katika vyuo vikuu. Pamoja na SUK kuchukua hatua ya kutafuna jongoo kwa meno, kwa kuanzisha Mfuko wake wa elimu ya juu, lakini haikuweza kutenga kiasi cha kutosha ili kiasi kikubwa cha wanafunzi waweze kupata mikopo, ambao kwa kiwango cha kipato cha Kizanzibari, ni wanafunzi wachache sana wanaoweza kulipiwa na wazazi, walezi na jamaa zao.
Na kwa kuwa hakuna utamaduni wa taasisi nyengine za nchi kama ZSSF, Bandari, Bima, ZRB na nyinginezo kurudisha sehemu ya faida yao katika sekta ya elimu japo kwa kudhamini wanafunzi kwa njia ya ushindani, basi kuja kwa Mfuko wa Elimu ya Juu hakujakuwa na manufaa makubwa.
Tumeona ari ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakijaribu kuishawishi SUK ifikiri nje ya boksi ( Think Out of the Box) kwa kutoa wazo la kupunguza fedha zilizotengwa kwa Mifuko ya Maendeleo ya Majimbo na kuzihaulisha katika sekta ya elimu, lakini sidhani kama hilo litafika mbali.
Athari ndio kama inayoonekana lakini pia isiyoonekana ambapo kwa mfano pamoja na fursa iliopo ni Wazanzibari wachache sana wanaosomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na madhara yake kuonekana baadae, yaani katika ujukuu.
Kwenye upande wa mabadiliko ya kisiasa mwaka umemalizika umma ukiwa na wasiwasi juu ya mjadala wa katiba unaokuja ambao kila uchao unasogezwa mbele na ambao hadi sasa hapaonekani dalili ya muelekeo wa SUK utakuwa ni upi.

Wakati Chama cha Wananchi (CUF) kimeanza kutoka wazi wazi kuelezea mtizamo na msimamo wake, hata kwamba ni Mshirika katika SUK, wananchi wangependa kusikia sauti kama hiyo kwa upande wa CCM, na sauti hiyo iwe ni moja.
Inaeleweka wazi kuwa kila Chama kina sera zake na manifesto iliyoiuza kwa umma, lakini umma unataka katika hili mitizamo ya kichama iwekwe mbali na iibuke mitizamo ya kizalendo ya Kizanzibari, la sivyo ikichukuliwa kuwa huu ni mjadala kama mengine, Zanzibar itajikuta imepwerewa jamvini.
Tatizo la vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi limebaki kama lilivyoanza. Maendeleo kidogo, lakini longolongo nyingi. Kelele nyingi zimepigwa lakini bado wananchi wananyimwa vitambulisho katika wakati ambapo kila mtu anajua kutakuwa na kura ya maoni 2014 ambayo ni muhimu kwa maslahi ya muda mrefu ya Zanzibar.
Juzi juzi iliibuka taarifa kuwa kuna kijana wa Kimasai ambaye kwa kuwa Mungu alitaka kudhihirisha kinachoendelea chini kwa chini, alidirik kupeleka barua kwa sheha mmoja Kaskazini ya Unguja na sheha akapeleka barua kituo cha Polisi na Kituo cha Polisi kupeleka barua Ofisi ya Vitambulisho kuwa kijana huyo amepoteza kitambulisho chake.
Huko nyuma iliwahi kutokea mzaliwa wa Msumbiji, ambaye bado ni mpigakura wa nchi hiyo kugundulika kuwa amepata ZAN ID ilhali kisheria Tanzania hairuhusu uraia wa nchi mbili, lakini hilo likaisha kimya kimya. Niliwahi kumwambia Dk Ali Muhammed Shein, Rais wa Zanzibar suala hilo na kushauri kuwa njia bora zaidi ya kuhakikisha kila mtu anapata haki yake ya ZAN ID ni kutumika sheria ya kila Mzanzibari kutembea na kitambulisho hicho.
Au kama nilivyowahi kushauri kabla hakuna njia bora kama kutoa vitambulisho kupitia maskuli na udhia huu ungekuwa umemalizwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu takriban kila Mzanzibari anapitia katika mfumo wa elimu. Kingine ambacho kimetia dosari katika kumalizia mwaka kwa SUK ni suala la kuongezewa mishahara wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kufikia zaidi ya shs millioni 4 kwa mwezi ilhali uchumi hauendani na maongezeko kama hayo.
Lakini, kwa sababu ya hali ilivyo Zanzibar kukosekana vyombo vya habari vikakamavu, kukosekana kwa jumuia zisizo za kiserikali zinazoweza kuchacharika na kuijuburi Serikali najua hili litapita kimya kimya. Nakumbuka wakati wa mkutano na waandishi wa habari kule Ikulu, mwandishi Munir Zakaria alimwambia Rais (Dk Shein) juu ya suala la uwiano wa matumizi ya kiserikali na uwezo. lakini pia haja ya maendeleo.
Mfano wa mwandishi huyo ulikuwa ni mtu aliyewekeza billioni moja katika mradi wa hoteli huko Pemba na ambaye ni mzalendo na Serikali kushindwa kuweka transfoma ya Shilingi millioni 100 na huku Serikali hiyo hiyo sio tu ikihimiza wazalendo wawekeze, lakini pia ikisema kuwa utalii ni sekta kiongozi.
Ningefurahi kujua, mbali ya mlolongo wa mafanikio ya SUK ambayo Dk. Shein amejinasibisha nayo, je, tatizo hilo la transoma kuelekea mradi huu ambayo pengine ni sawa na gari mbili tu za maafisa wa Serikali yake limetatuliwa?
Maana ni vitu kama hivi ndivyo vinavyoongeza haiba ya utendaji wa Serikali kwa sababu mtandao wa faida zake ni kubwa kwa jamii inayozunguka mradi huo na ujazo wa maana wa kodi kwa Serikali yenyewe.

Chanzo: Makala ya Ally Saleh katika gazeti la Mwananchi la 28 Disemba 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.