Mhariri wa Tanzania Daima akisindikizwa na askari polisi kuelekea kwenye chumba cha mahakama ya Kisutu. (Picha ya IPP Media)

Wapendwa watembeleaji wa Zanzibar Daima.

Hivi sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunaendelea kesi dhidi ya wahariri na waandishi wa gazeti la Tanzania Daima, kwa sababu ya makala ya Samson Mwigamba iliyotafsiriwa na watawala kuwa ni uchochezi. Kwa heshima ya mwandishi wa makala hiyo, kwa bodi ya uhariri ya Tanzania Daima na kwa uhuru wa habari, Zanzibar Daima inaichapisha tena makala hiyo hapa, kuonesha uungaji mkono wa wale wanaopaza sauti zao, na kupinga wale waozinyamazisha. Soma makala hiyo hapa chini:

Na Samson Mwigamba

MAKALA hii ilikuwa itoke Jumatano ya wiki iliyopita lakini kwa sababu za kiufundi ikashindikana. Imekuwa ni bahati nzuri kwamba inapotoka leo, ijibu swali la askari polisi dereva wa gari la maji ya kuwasha.

Askari huyo alimweleza Mwalimu Mkuu wa watu jinsi roho inavyomuuma pale anapowamwagia Watanzania wenzake maji hayo ya kuwasha wakati wakidai haki yao. Askari uliyeuliza na wenzako wote someni makala hii kwa utulivu. Huu ni waraka maalumu kwa askari wote wa majeshi yote vikosi vyote Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa lugha ya wazi zaidi nazungumza na askari wa Jeshi la Polisi Tanzania, Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa, askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), askari wa Jeshi la Magereza na wale wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Kuwa mwanajeshi lolote kati ya hayo niliyoyataja si dhambi na si kweli kwamba kuwa mwanajeshi kunakuondolea uwezo wa kufikiri na badala yake ukawa unafikiriwa na watu wengine.

Wala haimaanishi kuwa askari kuwa kama robot ndio nidhamu bora kuliko zote duniani. La hasha! Mimi nilikataa utumwa huo!

Mwaka 1999 nilihitimu elimu ya cheti cha ufundi mchundo, yaani Full Technician Certificate (FTC) katika uhandisi wa Elektroniki na Mawasiliano ya Anga, yaani Electronics & Telecommunications Engineering kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).

Nikiwa bado sijapata kazi ya maana, mwezi Aprili mwaka 2000 niliona tangazo la kazi ya Radio Technician katika Jeshi la Magereza. Nikatuma maombi na kuitwa kwenye usaili uliofanyika Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Magereza Ukonga, Dar es Salaam mwezi Juni 2000.

Wote tuliofaulu usaili tulipangiwa siku ya kuripoti Chuo cha Magereza Kiwira kule Tukuyu, Mbeya.

Kufika kule nilishuhudia mambo ya ajabu. Ingawa wao hufurahia na kusema eti wanakutoa uraiani na kuwa mwanajeshi lakini baadhi ya matendo yanayofanyika wakati wa mafunzo ya jeshi ni ya kuwapumbaza askari wetu ili baadaye wakiwa kazini, watawala wawatumie watakavyo.

Nilishindwa kuvumilia kaulimbiu ya wakufunzi wa jeshi pale walipoelekeza kwamba chochote kruta (askari mpya mafunzoni) unachoambiwa lazima uitikie “ndiyo afande”. Nilishindwa kuitikia kwa mfano pale mkufunzi mmoja mwenye cheo cha koplo alipotutamkia mfululizo wa sentensi zifuatazo:
Mkufunzi: Nyinyi makruta mbona wote hamkuja na majembe?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Hamkuambiwa makao makuu ya jeshi kwamba lazima mje na majembe?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Kwa hiyo kwa kuwa hamkuambiwa na nyinyi hamkuyabeba?
Makruta: Ndiyo afande!
Mkufunzi: Wote ni wapumbavu pamoja na mama zenu waliowazaa.
Makruta: Ndiyo afande!

Ni hayo pamoja na mambo mengine ya kulazimishwa kwenda kwenye kile kinachoitwa disko, ambapo pamoja na uchovu wa kutwa nzima wa kazi ngumu na nyingi bado ni lazima ukae hapo mpaka saa 4 usiku tena ukinyooshewa kidole tu na mwenzako lazima usimame na kuimbisha wimbo tena kwa tabasamu, wimbo mmoja wapo ukisema “Magereza ninavyokupenda nitakunywa sumu juu yako”, ndiyo yaliyonifanya nikakataa kazi ya jeshi baada ya wiki moja tu ya mafunzo.

Siku niliyokataa jeshi ilikuwa ni Jumatano asubuhi ambapo sikwenda mchakamchaka na wakati wenzako wanatawanyika kufanya usafi wa nje maeneo mbalimbali, mimi nilibeba begi langu na kuanza kuondoka chuoni majira ya saa moja na nusu hivi asubuhi.

Nilikamatwa na mkufunzi mmoja wa jeshi na kupelekwa pamoja na begi langu kwa Ofisa Mafunzo wa chuo. Aliponiuliza sababu nilimtajia mbili, kwanza kwamba sifurahii mambo ya jeshi na kubwa zaidi kwamba mimi ni Msabato na nimeambiwa na wenzangu kwamba hapa hakuna kwenda kusali, siku zote za juma ni kazi.

Kitu ambacho sitaweza maana Sabato takatifu lazima nipumzike! Bila kuuliza zaidi aliconclude kwa kuniambia kwamba, “Sijawahi kuona mtu anaacha kazi kwa ajili ya mambo ya dini.

”Ni dhahiri wewe ulikuja kutupeleleza na hivyo kazi yako imeisha sasa unataka kurudi. Tutakuweka rumande, tena ile ya polisi kwa wiki mbili wakati tunafanya upelelezi juu yako.”

Askari aliyenileta alianza kunivuta ili kunipeleka rumande lakini nilikataa huku nikiendelea kujieleza kwa ofisa mafunzo ili ajue kwamba sikuwa na mpango huo aliousema.

Baada ya kuelemewa na hoja zangu alinipeleka kwa makamu mkuu wa chuo ambaye yeye alitumia zaidi Biblia kunihubiri kwamba nakaidi amri ya mamlaka wakati hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.

Jibu langu lilikuwa fupi na lenye msimamo mzito kwamba ikiwa mamlaka ya wanadamu inafika mahali inanena tofauti na Mungu, Mtume Petro ametuandikia kwamba katika hali ya namna hiyo, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko mwanadamu”.

Na yeye alinishindwa akanipeleka kwa mkuu wa chuo na wao wote wakiwapo. Ushauri waliokuwa wakimpa mkuu wa chuo ni kwamba mimi niwekwe rumande kwanza ili wafanye upelelezi. Lakini sikuyumba katika msimamo wangu.

Nilimweleza mkuu wa chuo kwamba mimi ni raia na si mpelelezi. Nilizirudia rudia sababu zangu za kuacha jeshi tena kwa ujasiri mkubwa na kumhakikishia mkuu wa chuo kwamba akinipa hayo ninayoyataka niko tayari kubaki jeshini.
Hatimaye kauli ya mwisho ya mkuu wa chuo ilikuwa ni hii: “Jeshi ni wito. Tunaweza kumlazimisha huyu kijana kuwa mwanajeshi lakini baadaye ikatuletea madhara makubwa sana.” Akamalizia kwa kusema, “chukueni maelezo yake kwa maandishi kisha arudishe vifaa vya jeshi.”

Wakati naondoka nilimsikia ofisa mafunzo akitoa maelekezo kwa walio chini yake kwamba mwanafunzi mwingine wa jeshi akija kuripoti na kwenye daftari akajaza kwamba ni Msabato, msimsajili kwanza mpaka aje kwangu! Sijui kama Wasabato wameendelea kupokewa kwenye hicho chuo cha magereza lakini ninachotaka askari wote wa majeshi yetu yote na vikosi vyote, ni kwamba askari unaweza kusimama kwa miguu yako na kufikiri kwa akili yako mwenyewe!
Ndugu zangu askari, nchi imefika mahali ambapo Waingereza hupenda kupaita ‘critical point’. Ni mahali ambapo wananchi wako tayari kwa mabadiliko na watawala wako tayari kwa mapambano ili kubaki madarakani.

Katika point hii askari wetu wanakuwa na nafasi kubwa ya aidha kuwezesha mabadiliko hayo kutokea kwa wakati wanaoutaka wananchi, tena kwa amani ama kuyachelewesha (si kuyazuia) na kusababisha yatokee baadaye kidogo kuliko wananchi walivyotaka, tena baada ya kumwaga damu nyingi ya Watanzania wasio na hatia!

Napenda kurudia kwamba hakuna jeshi lolote duniani hata kama tungekusanya majeshi yote ya dunia hii na kuyaleta Tanzania hawataweza kuizuia nguvu ya umma pale inapokuwa imeamua kufanya mabadiliko.

Napenda tena kurudia kwamba si lazima askari mfanye kile ambacho wakubwa wenu wanataka na kuwaamuru kufanya. Tunaweza kusimama imara na kutetea haki za Watanzania tukiwamo na sisi askari. Niliwahi kugoma kutii amri ya kukamatwa na kuwekwa rumande.
Lakini pia mifano ni mingi na nisingependa kuchukua mifano kutoka nchi za Ulaya kama Uingereza ambako tulishuhudia wananchi wakiandamana mitaani na askari wao hawakuwahi hata kumpiga kofi tu mwandamanaji hata mmoja.
Walipohojiwa na vyombo vya habari walisema dhahiri kwamba waandamanaji ni raia halali wenye haki ya kufanya kile wanachokifanya kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yao. Katiba ya Tanzania na sheria za nchi hii zinatoa haki kama zile za Uingereza. Tofauti ni utekelezaji wa matakwa hayo ya kikatiba na kisheria. Watawala wa Uingereza wako tayari hata kung’oka madarakani ili kutekeleza matakwa ya nguvu ya umma.

Lakini wale wa Tanzania wako tayari kung’oa uhai wa raia wengi ili mradi kuzuia nguvu ya umma inayodai haki na wananya hivyo kwa sababu ya hofu ya kung’oka madarakani, jambo ambalo hawataki kabisa kulisikia. Na ndugu zangu askari napenda kuwaambia kwamba yote yanafanywa na watawala wetu kwa kuwategemea nyinyi.

Wanaminya haki zenu nyinyi wenyewe, haki za wazazi wenu, dada na ndugu zenu, marafiki zenu, jamaa zenu na majirani zenu. Chukulia mfano rafiki zangu Mtaki na Edwin. Tumesoma wote shule ya msingi pale Magu.

Nilichaguliwa kujiunga na Mazengo Sekondari, shule kubwa na ya muda mrefu ambayo sasa imegeuzwa kuwa chuo kikuu bila mabadiliko ya majengo.

Shule iliyokuwa na maabara nne kwa maana ya maabara ya baiolojia, kemia, fizikia na jiografia. Ilikuwa ni sekondari ya ufundi na hakuna karakana ambayo haikuwapo.

Shule iliyokuwa na walimu wa kutosha, vyumba vya kutosha vya madarasa na vya kulala mabwenini.
Katika bweni la Ujamaa kwa mfano, nilikokuwa naishi mimi, kuna vyumba kadhaa havikuwa na watu. Darasa la Form IVA ambalo nilikuwamo lilikuwa na wanafunzi 21 tu darasani.

Na mazingira mengine mengi ambayo sitaweza kuyataja hapa ambayo yanafanya wanafunzi wa leo wa Chuo Kikuu cha Mt. John wajiulize kama kweli ile ilikuwa ni shule ambayo haina maktaba wala vitabu vya kutosha, na mengineyo mengi mnayoyafahmu.

Nikafaulu kwa kiwango cha daraja la juu lililoniwezesha kuendelea mpaka chuo kikuu na kupata kazi nzuri kwenye Umoja wa Mataiifa.

Rafiki zangu nakumbuka mlivyoamua kujiunga na Jeshi la Polisi si kwa sababu mlipenda kazi hiyo ama kwamba mlikuwa na wito wa kuwa polisi kama mnavyodanganywa kwamba jeshi ni wito.

Nakumbuka mlijiunga huku mkilalamika kwamba mnalazimika kujiunga huko kwa sababu kiwango chenu cha ufaulu hakiwapi fursa ya kazi bora zaidi ya hiyo. Lakini mimi nawafahamu vizuri. Najua uwezo wenu wa darasani. Mliathiriwa na mazingira ya hovyo ya shule mlizosoma.

Rafiki zangu nyinyi wote leo ni wakuu wa vituo vikuu vya polisi vya wilaya katika wilaya za Mbozi na Igunga.
Leo hii mimi nimeacha kazi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kushiriki vema katika mapambano ya kutafuta ukombozi wa taifa hili.

Wadogo zenu na wadogo zangu mnawajua wako katika juhudi za kutafuta maisha lakini ni magumu. Wengine walikosa kabisa nafasi ya kujiunga hata na hiyo Magu Day.

Wakaishia Bulima na Kinango, ambako hali ilikuwa mbaya zaidi. Wakafeli kabisa na leo wanahangaika hapa na pale lakini watawala wanawawekea mazingira magumu mno ya kuendesha maisha.

Na sasa chukulia nao wametambua hali yao duni inasababishwa na watawala walafi na walaghai. Wamejaribu kutumia njia za kidiplomasia kudai haki zao wanakutana na watu wanaitwa wakuu wa wilaya na mikoa.

Wanaamua kuandamana, mnashiriki kuamrisha askari walio chini yenu kuwapiga na kuwaweka rumande na hatimaye kuwafungulia kesi za kubumba!

Askari wetu igeni mfano wa askari wa Misri! Pale wananchi walipoamua kuandamana kukomesha utawala wa kidhalimu wa miaka 30 chini ya Hosni Mubarak, askari waliwalinda badala ya kuwapiga.

Walikataa kwa sababu hata wao walikuwa wakiumizwa na Mubarak lakini zaidi ya hayo, waliokuwa wakiandamana walikuwa ni dada zao na ndugu zao na marafiki zao.

Hivi sasa nchi iko njia panda. Ugumu wa maisha umeongezeka mara nne na zaidi. Watawala hawalioni hilo wala hawajishughulishi kurekebisha hali ya mambo hususan hali ya uchumi.

Wako busy na kujiandaa kwa uchaguzi wa 2015. Mawaziri wako busy na kampeni za kuteuliwa kuwa wagombea wa urais kupitia chama tawala hapo 2015 na rais naye yuko busy kuandaa mtu wake ambaye anadhani akimrithisha jumba jeupe la pale Magogoni atasema mwacheni Ndugu Kikwete apumzike kwa amani.

Taifa limeamua kuandika katiba mpya, rais na serikali yake na chama chake wameamua kuuteka mchakato ingawa haikuwemo kwenye ilani yao ya uchaguzi ili tu waturudishie katiba ya mwaka 1977 na kuipa jina juu ya jalada KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA MWAKA 2014.

Natambua juhudi zinazoendelea hasa zikiongozwa na CHADEMA kujaribu kumkumbusha rais kwamba katiba iko juu yake na katiba ni mali ya wananchi na yeye anaajiriwa kwa katiba hiyo na si yeye kujiandalia katiba ili atawale kwa ulaini.

Lakini juhudi za kidiplomasia zikishindikana hapo ndipo itabidi haki ya watu idaiwe kwa maandamano na hapo askari wote tuungane na kuwa kama Misri, kwa kuwa Katiba mpya ni kwa masilahi yenu pia! Jaribuni kutafakari!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.