Baadhi ya Wazanzibari waliojitokeza mapema mwaka huu kupinga Muungano hadharani. Kwa wao, chaguo la kwanza ni kutokuwa na Muungano, la pili ndio serikali tatu, hawataki kuuona wa serikali mbili wa sasa wala kuusikia wa serikali moja

Kwa vile Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba umepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, muswada huo utatekelezwa mara tu utapomalizika mchakato wa kuufanya uwe sheria kamili. Muswada huo ambao ni muhimu sana kwa watu wa Tanganyika na wa Zanzibar kwa vile utaamua mustakabali wa nchi zao mbili, utatekelezwa kwa mujibu wa ratiba au jedwali itayowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kati ya taasisi zote zitazoundwa katika utekelezwaji wa mchakato wa kuiandika upya Katiba mpya ya Muungano, iliyo na umuhimu mkubwa ni ile tume ya wajumbe 30 itakayokuwa na idadi sawa ya wawakilishi kutoka Tanganyika na Zanzibar.

Hii ndiyo taasisi itayoongoza kupanga na kusimamia huo mchakato mzima. Hali kadhalika itatoa mapendekezo itayokuwanayo juu ya misingi ya mizingo au vigezo na miongozo itayotangazwa na Rais wa Muungano baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar na pia kupata ridhaa yake.

Miongoni mwa majukumu muhimu sana ya tume au kamisheni hiyo itakuwa ni kazi ya kuuongoza mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi katika ngazi za chini kabisa za taifa hili. Huko Zanzibar kazi hiyo itafanyika katika ngazi ya shehia ambapo Wazanzibari watatakiwa watoe maoni yao kuhusu mwelekeo ujao wa nchi yao na pia kuhusu Muungano na Tanganyika.

Kwa mfano, wale watakaohudhuria mikutano itakayofanywa kwenye shehia zao huko Zanzibar au wataopeleka taarifa zao kwa maandishi kwenye kamisheni au kwa wao wenyewe kuhudhuria mbele ya kamisheni watakuwa na uwezo wa kutoa maoni yao kwa uhuru kabisa bila ya hofu.

Hali ya mambo haitokuwa tena kama zamani ambapo kaka mkubwa alikuwa akiongoza, akiangalia na hatimaye akijiamulia kuhusu ya sasa na yajayo ya Jamhuri ya Muungano. Kwa kufanya hivyo, kaka mkubwa alikuwa akiamua kuhusu mustakabali wa Tanganyika na ule wa Zanzibar, nchi huru zilizoungana mwaka 1964.

Vifungu vya muswada huu vinavyotaka pawepo na uwakilishi ulio sawa na ushiriki ulio sawa katika kufikia uamuzi katika mchakato huu vinaitambua ile kanuni ya kimsingi ya uhuru na mamlaka ya nchi hizo mbili pamoja na usawa wao. Utambuzi huo ni juu ya msingi wa kanuni za sheria za kimataifa pamoja na sheria za taifa hili.

Ninasema hivi kwa sababu Hati za Muungano ni mkataba wa kimataifa. Nathubutu pia kuongeza kwamba Hati hizo za Muungano ndizo nyaraka zilizo muhimu kushinda zote zilizotajwa kuhusika na historia ya utungwaji wa Katiba nchini Tanzania.

Tuwe wakweli pia na tukumbuke kwamba utungwaji wa Katiba nchini humu umeihusisha zaidi Tanganyika. Historia inakanushwa kwa kupuuzwa kama haipo ile Katiba ya Uhuru wa Zanzibar ya mwaka 1963, iliyopatikana baada ya mashauriano huko Lancaster House mjini London kati ya vyama; Zanzibar Nationalist Party na Afro-Shirazi Party.

Hali kadhalika, siku ya uhuru wa Zanzibar — Desemba 10, mwaka 1963 — baada ya miaka 70 ya ukoloni wa Uingereza haitambuliwi ingawa siku ya uhuru wa Tanganyika inaadhimishwa na kusherehekewa kuwa ni Sikukuu ya Kitaifa ya Tanzania.

Katika kuizingatia ripoti yake kamisheni inapaswa kuyatia maanani “maoni yanayolingana na yanayokinzana katika sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano” (yaani Tanganyika na Zanzibar) kuhusu mustakabali wa Muungano. Itapoangalia dhana nzima ya Muungano ama muundo wake itaona kwamba kuna ukinzani mkubwa kati ya wanachodai Wazanzibari na msimamo rasmi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Kwa bahati mbaya ni taabu kuutaja msimamo wa Watanganyika kuhusu Muungano, na iwapo wanapendelea waendelee nao au wauvunje. Ni taabu kwa sababu inavyoonyesha ni kwamba msimamo rasmi na wa wengi huko Bara katika muda wote huu wa miaka 47 ya Muungano ni kuwa Zanzibar ni mzigo kwa Tanganyika.

Tusisahau kwamba hali hiyo ilikuwa na ukweli katika kipindi kifupi sana cha historia ya Visiwani pale ilipokuwa kawaida kwa wanadamu kuwatesa wanadamu wenzao, pale wananchi walipokuwa wakinyimwa uhuru wao wa kimsingi na pale nchi hiyo ilipokuwa ikiongozwa na mtu mmoja. Kwa hakika, yaliyokuwa yakitokea Zanzibar kabla ya mwaka 1972 yameutia dosari uungwana na utu wa Mwalimu Julius Nyerere na pia yameitia dosari Tanzania.

Kamisheni yenye jukumu la kuichunguza na kuirekebisha Katiba imepewa mamlaka makubwa na lazima pachukuliwe hadhari wanapoteuliwa wajumbe wake na uongozi wake. Ni muhimu kwamba iwe huru na isifungamane na Serikali. Pia itambue kwamba itakabiliwa na changamoto nyingi kabla ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Atapoipata Rasimu hiyo, Rais ataunda Bunge la Katiba kwa masharti yaliyomo kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Katiba. Zanzibar itakuwa na asilimia 30 ya wajumbe kwenye Bunge hilo. Muhimu ni kwamba wajumbe wa Tanganyika na wale wa Zanzibar watapiga kura mbalimbali si kwa pamoja. Na kila upande utahitaji upate ridhaa ya wingi wa theluthi mbili ya wajumbe wake ili rasimu hiyo ya Katiba iweze kufikishwa kwa wananchi watoe uamuzi wao kwenye kura ya maoni.

Kwa Zanzibar hiyo kura ya maoni itasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na rasimu ya Katiba itapita endapo Wazanzibari wengi wataikubali.

Panaweza pakazuka mgogoro wa kisiasa ikiwa, kwa mfano, upande mmoja utaikataa hiyo rasimu ya Katiba mpya. Mgogoro huo utaweza kutanzuliwa kwa vile Katiba ya kale (yaani hii ya sasa) ya mwaka 1977, itaendelea kufanya kazi. Hatua hiyo itakuwa ni ya suluhisho la kisheria tu kwani matatizo ya kisiasa kuhusu mustakbali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatabidi yatanzuliwe kwa njia ya kirafiki kati ya Tanganyika na Zanzibar, tukikumbuka kwamba katika demokrasia ni matakwa ya watu yaliyo juu na yenye kutawala.

Inapaswa pia wakubwa wakumbuke ya kuwa kinyume cha miaka ya nyuma watu hawana tena hofu visiwani Zanzibar. Vilevile kinyume cha miaka ya nyuma vyama vya kisiasa vyenye matawi yao Zanzibar haviwezi tena kuwafukuza wenzao wa Visiwani au kuwatisha. Wala wale wenye kutokubaliana na msimamo rasmi wa kisiasa au wa kiitikadi hawafikiriwi tena kuwa ni wahaini wa Taifa la Tanzania.

Hivyo inatia moyo kuona kwamba Wazanzibari kwa mara ya kwanza katika historia yao ndani ya Muungano na Tanganyika, wamepewa haki yao ya kuwa washirika sawa. Pongezi ni kwa Wazanzibari wote na hasa viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na wale wenye kuhusika na mambo ya kikatiba na kisheria ambao kwa mara ya kwanza wametoa mapendekezo yanayolinda maslahi ya nchi yao.

Kuna hofu Zanzibar kuhusu namna kura ya maoni itavyoendeshwa na jinsi orodha ya kudumu ya wapigaji kura itavyotumiwa. Pia kuna manung’uniko mengi kuhusu kutolewa kwa vitambulisho vya ukaazi. Hofu iliyopo ni kwamba wasio Wazanzibari huenda pia wakashiriki kwenye kura ya maoni ijapokuwa sheria inasema wazi kwamba kutakuwa na kura mbili za maoni: moja kwa Watanganyika na nyingine kwa Wazanzibari.

Msimu wa kampeni umekwishaanza na kuna wengi Visiwani ambao wamekwishafikiria masharti magumu kuhusu Muungano na muundo wake wa baadaye na iwapo uendelee kama ulivyo sasa au la. Hili linapingwa na Wazanzibari wengi lakini inavyoonyesha ni kwamba viongozi wa Tanganyika wangependelea uendelee ulivyo, na pengine, hata baadaye, kuitimiza ndoto yao ya kuwa na serikali moja tu kwa sehemu zote mbili za Muungano, yaani Tanganyika na Zanzibar.

_________________________________________________________________________________________________________

Makala hii ya Ahmed Rajab kwa mara ya kwanza imechapishwa na gazeti la Raia Mwema la Dar es Salaam katika toleo la tarehe 30 Novemba 2011, chini ya kichwa cha habari “Upinzani mkubwa Zanzibar kwa wenye kutaka serikali moja…”.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.