Uumini wangu kwa Maridhiano ya Wazanzibari hautetereki au hauporomoki. Niliyaamini yalipozaliwa miaka miwili nyuma, nayaamini leo yakiwa yamefanikisha Serikali ya Umoja wa Mataifa ya Zanzibar (SUKZ), nitayaamini kesho, keshokutwa na milele. Hata hivyo, kwangu Maridhiano hayo ni njia ya kufikia lengo, ambayo ni Ajenda ya Zanzibar, na sio lengo lenyewe. Nakusudia kuwa tuliporidhiana hatukuridhiana kwa sababu tupate kuridhiana. Tuliridhiana ili tuikomboe Zanzibar. Hapa tunaweza kutafautiana kuhusu maana ya ‘ukombozi wa Zanzibar‘, lakini juu ya kilele cha tafauti yetu, tutakubaliana kuwa, kwa ilivyo sasa, Zanzibar haiko huru; inahitaji ukombozi – na Maridhiano ni njia ya kufikia huko.

Kwa hivyo, tunalazimika kuisafisha njia tunayopita ili kurahisisha safari yetu kuelekea kwenye lengo letu. Nakusudia kuwa ni lazima (wala si hiyari) kwetu kuyasafisha Maridhiano haya na uchafu wowote, maana kama njia ni chafu, safari itakuwa ngumu kufikia mwisho, na huenda hata isikamilike. Wengine tumeanza kuiona njia hii ikianza kuchafuliwa, ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Siku Maridhiano yalipozaliwa, Ikulu ya Zanzibar. MIaka miwili baadaye, kama hayakulindwa, hatari ni kufa yangali machanga
Siku Maridhiano yalipozaliwa, Ikulu ya Zanzibar. MIaka miwili baadaye, kama hayakulindwa, hatari ni kufa yangali machanga

Tumeuona uundwaji na utendaji kazi wa SUKZ. Hapana. Tumeiona tabia ya uundwaji na ufanyaji kazi huo. Katikati yake tunamuona Rais Ali Mohammed Shein, ambaye ukiwacha Baraza lake la mawaziri kuwa na sura ya Umoja wa Kitaifa, hivyo sivyo ilivyo baki ya serikali yake, kuanzia makatibu wakuu wa mawizara hadi masheha shehia. Na mwenyewe, anajiona kuwa ana hoja. Kwamba, muongozo wa Katiba ya Zanzibar unamtaka kuweka sura ya Umoja wa Kitaifa katika ngazi ya mawaziri tu, na sio nje ya hapo.

Lakini hoja hiyo inasahau ukweli wa kimantiki. Kwamba serikali ya Umoja wa Kitaifa ni matokeo ya Maridhiano. Ni kweli kuwa Maridhiano haya baadaye yalipelekwa kwenye Baraza la Wawakilishi kuundiwa sheria, yakawa sehemu ya Katiba, lakini msingi wa chochote kinachokuja juu ya hapa, ni hayo hayo Maridhiano.

Kimantiki na katika kiwango ambacho Umoja wa Kitaifa unahusika, utekelezaji wa Maridhiano haupaswi kukiukwa kwa kisingizio cha Katiba. Juu ya yote, Katiba haikumzuia Rais Shein kuteua makatibu wakuu, manaibu wao, wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya na hata masheha, kwa kutumia moyo wa Maridhiano.

Moyo wa Maridhiano pia unamtaka Rais Shein kuwa karibu sana (tena sana kabisa) na Makamo wake wa Kwanza, kuhakikisha kuwa njia ya Maridhiano inasafishwa dhidi ya uchafu wowote ule, hata kama halazimishwi hivyo na Katiba. Maana, kwa uhakika hasa, Dk. Shein si raisi wa kikatiba. Dk. Shein ni rais wa Maridhiano. Huo ndio ukweli, tukitaka kuwa wakweli.

Hivi sasa Zanzibar imo kwenye kipindi muhimu sana katika historia yake. Baada ya miaka karibuni 50 ya kuwekwa chini ya Muungano, ambao kwa wengi ni aina nyengine ya ukoloni dhidi ya nchi hiyo, vuguvugu la mageuzi liko juu. Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar yamechochea mchakato wa Katiba Mpya kwa Jamhuri ya Muungano.

Matokeo ya mchakato huo, sasa itakuwa ni wananchi wa pande zote mbili – Tanganyika na Zanzibar – kuulizwa maoni yao kuhusiana na hatima ya Jamhuri ya Muungano. Maoni hayo yatapatikana kwa kura, na kura itapigwa na wenye sifa. Kwa Zanzibar, ukiacha kutimia umri wa miaka 18, sifa nyengine kubwa ni kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan-ID). Mamia kwa maelfu ya Wazanzibari hadi sasa hawajapatiwa vitambulisho hivyo. Kura ikija, hawa hawatashiriki.

Kwa jambo lisilo la bahati mbaya, wengi wa hao (kama si wote) ni wale wanaoonekana kukiunga mkono Chama cha Wananchi (CUF), mmoja wa mwenza muhimu katika SUKZ na Maridhiano. Makusudi inaonekana kwa kila sura yake kwenye hili. Makusudi ya kuichafua njia ya Maridhiano. Makusudi ya kuturudisha tulikotoka, bali mbali zaidi ya hapo.

Rais Shein ana nguvu kamili za kuizuia Zanzibar isirudi ilikotoka. Anaweza kuendesha gari hii ya SUKZ kwenye njia ya Maridhiano kuelekea kwenye lengo letu – ukombozi wa kweli wa Zanzibar. Lakini hilo litafanyika ikiwa yeye mwenyewe ni muumini wa kweli wa Maridhiano, ikiwa ni mfuasi wa umoja wa kweli, na ana ndoto ile ile waliyonayo waumini wengine wa Maridhiano – Ajenda ya Zanzibar.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.