Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein

SIAMINI kama kutokuwepo kwangu katika mkutano wa waandishi wa habari na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kulipunguza mvuto wa mkutano. Ni kweli sikuwepo, na baadhi ya waliogundua kwa kutoniona televisheni zilipoonesha baadaye, wameuliza sababu. Ila waandishi walikuwepo, tena wengine wakubwa tu kiumri na uzoefu kazini kunizidi. Waliuliza maswali muhimu. Wanasema mengine yalipata maelezo badala majibu. Pamoja na hayo, faida iliyotakikana kiuandishi ilipatikana.

Ninasikitika, MwanaHALISI, taasisi ninayofanyia kazi tangu Julai 2006, ilinyimwa mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo uliofanyika Ikulu tarehe 3 Novemba. Sikualikwa mimi kama mwandishi binafsi wala kama mhariri wa gazeti hili kama walivyoalikwa wahariri wengine.

Wala siyo kwamba hatukualikwa kwa kuwa wasaidizi wa rais walisahau. Hawakusahau. Walikusudia kutotualika. Walitia nia tangu pale walipojadili vyombo gani viandikiwe mwaliko. Ikulu ya Zanzibar, ninaamini kwa kutafakari hasa, ilipanga MwanaHALISI tusishuhudie mkutano huo. Hawakutaka sisi tumsikilize rais kwa karibu.

Ninajua wasaidizi hao, wakiwemo Kurugenzi ya Mawasiliano, walipiga simu kwa baadhi ya waandishi kuulizia anuani au/na simu za wahariri wa magazeti yaliyosajiliwa Dar es Salaam. Walitajiwa MwanaHALISI. Walitajiwa hata jina langu, mhariri wa MwanaHALISI ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar kindakindaki nisiye na pengine pa kutafutiwa kama asili yangu. Sitambi hapa lakini najichukulia kuwa mtu mwenye maslahi makubwa na siasa za Zanzibar ingawa si mwanasiasa.

Siwalaumu watendaji wa Ikulu wala wenzao Idara ya Habari Zanzibar (MAELEZO) waliosaidiana kualika wahariri. Wote wanajua kilichowasukuma kutotualika. Nami naweza kuagua kwanini hawakutualika. Kimaskhara naweza kusema labda kwa fikra zao waliamini nikiwepo, nitamaliza sambusa na keki pamoja na cha/soda. Ndio maana nasema siwalaumu.

Inatokea hii baadhi ya watendaji wakafikiria vitu vidogo mno mahali ambapo panahitaji mtu kufikiri kwa upana zaidi. Lakini kwa uzito, najua utendaji wa staili hii, ni dalili za watu kutotaka kubadilika na kukataa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Labda ni kwa kuona hata wakitenda vema na kwa viwango, hakuna kuzawadiwa. Hilo linatosha kwao kutenda kama vile Zanzibar na watu wake wangali katika zama za ujima.

Bado watumishi wengi hawaamini fikra hasi zimechangia kudumaza maendeleo katika sekta ya umma – serikalini. Wao wanadhani nchi ingali katika wakati wa kuiachia serikali kutenda kwa utashi wa viongozi bila kujali kama utashi huo unafanana na matakwa ya wananchi. Wanabaki palepale pa kutaka serikali isihojiwe na kiongozi wake asihojiwe na mtu yeyote kama vile alivyowahi kutamka Dk. Shein aliposikia malalamiko ya wananchi kuhoji mantiki ya serikali kukodisha majengo ya kihistoria ya Mambomsiige kwa mwekezaji ili ajenge hoteli.

Kwa kuamini kuwa serikali ni dude lenye maguvu makubwa yasiyomithilika, Rais Dk. Shein akaamini ni halali kwake kuzuia watu – wale alioapa kuwatumikia kwa uadilifu, bila ya kuwabagua kwa namna yoyote ile, na kwa kuzingatia katiba na sheria – kuuliza na kuhoji namna serikali inavyoendesha shughuli zake. Kwa sababu ndivyo rais alivyoamini, inadhihirika wazi sasa imani hiyo ninayoiona kama muendelezo wa utendaji uliokuwepo Ikulu kabla, imezidi kuganda mawazoni mwa watendaji hao.

Waendelee kuamini hivyo lakini najua iko siku watauona ukweli wa mambo. Watatahayari na kutahayuri. Hawajui siku zote “maandishi yapo ukutani.” Hapa namkumbuka mzee gwiji katika uandishi wa habari, marehemu Ali Mohamed Ali (Nabwa) – Allah amghufirie madhambi yake mbele ya haki aliko. Watendaji wa Ikulu wanaendeleza imani kwamba kuikosoa serikali au viongozi wa serikali na taasisi zake bado ni jambo lisilokubalika; ni dhambi – haramu mut’laki.

Hili ni tatizo kubwa bado katika serikali yetu. Mabadiliko makubwa ya mitizamo ya watumishi yanahitajika. Katika serikali ya karne tuliyopo, unahitaji viongozi wenye mawazo ya kuona mbali na kufikiri na kutenda ukilenga tija. Watumishi au watendaji wanaoendelea kutenda huku wakiwa wamelala, si lazima iwe usingizi tunaoujua, bali wakiyafunikiza mawazo yao kwenye zulia, hawawezi kuleta mabadiliko yanayotakiwa.

Wananchi leo wanataka mabadiliko yanayochochea ufanisi katika utoaji wa huduma na ujenzi wa uchumi wa nchi yao. Hebu tafakari, kwamba mara tu baada ya Rais Dk. Shein kuelekeza wasaidizi wake waandae mkutano wa waandishi wa habari/wahariri Ikulu ili kumsikiliza rais akieleza hatua iliyofikiwa tangu aingie madarakani na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba 2010, wasaidizi wakaanza kufikiria “nani na nani tusiwaalike.”

Hapo unatarajia jema gani wasaidizi hao wenye mawazo mgando (wahafidhina) wanaweza kufikiria kulitenda kwa maslahi ya umma wakiwa Ikulu au popote panapohusika na masuala yanayomhusu rais? Wanafikiria majina ya watu badala ya faida itakayopatikana kwa kualika waandishi wanaoijua nchi, viongozi wake, watu wake pamoja na matumaini yao. Utatarajia utendaji wa tija hapo?

Ni fikra hizo za watendaji serikalini zinaelezea dhahir-shahir sababu za waandishi kumkosa kwa mwaka mzima kiongozi ambaye wakati akichukua fomu ya kutafuta uteuzi, aliahidi akichaguliwa, atakuwa akikutana mara kwa mara na waandishi ili kuelezea maendeleo ya shughuli za serikali. Inawezekana hakuna msaidizi aliyeshawishi haja ya rais kukutana na waandishi ilipofika miezi mitatu ya uongozi. Hapo, tayari kulikuwa na matatizo mengi na kelele nyingi za wananchi wakihoji mambo kadhaa.

Ni wakati ambao rais alikuwa akilaumiwa na makada, wakongwe na chipukizi, kwa kuhisiwa anazidiwa kete (kimaamuzi) na viongozi kutoka chama cha upinzani aliowateua ili kumsaidia kazi katika hatua ya kutekeleza matakwa ya kikatiba ambayo wananchi waliyaidhinisha kupitia kura ya maoni 31 Julai. Hakuna aliyejali. Badala yake, wasaidizi wakabaki kufurahia mtindo wa kiongozi kujibu lawama majukwaani na kwenye mikutano ya ndani kati yake na viongozi wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni hapo rais alisikika akirudisha makombora kwa kauli kama “Mimi ndiye mwamuzi wa kila kitu katika serikali, ninae makamu wa kwanza wa rais, na yupo makamu wa pili, lakini hawa ni washauri wangu tu si waamuzi. Mimi ndiye ninayeamua.” Mkutano wa rais na waandishi/wahariri ni historia. Si umekwisha? Rais alijieleza vya kutosha maana mwenyewe alijua aliwachosha waliokuwa wakimsikiliza.

Hakuna kilichobadilika. Watendaji walewale, staili ya utendaji ni ileile. Siku nne baada ya mkutano, Rais analalamika kuwa aliowapa dhamana wamejisahau, hawajali wananchi na hivyo kuichonganisha serikali na wananchi. Kweli, wananchi wanalalamika. Rushwa inaendelea. Uzembe na uvivu, kejeli na kiburi vinaendelea. Matendo ya wizi, ubadhirifu na ufisadi yanaendelea serikalini. Na kwa kuwa hakuna usimamizi mzuri, najua ari itakuwa zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi.


Makala ya Jabir Idrissa, MwanaHALISI, 16 Novemba 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.