Kwa mara nyengine tena, Wazanzibari wakikukwa katika mchakato wa Katiba mpya. Pana nia njema hapa?

Katika makala hii, mwandishi Ally Saleh anahoji: “(Hata) wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walilalamika kuwa muswada huo unajadiliwa na wao katika semina na sio kikao cha Baraza, lakini pia katika dakika za majeruhi. Walisema wazi wazi kuwa hawaamini kuwa fikra zao zitaweza kuchukuliwa na kuingizwa na watungaji muswada, kwa kuwa semina hiyo ilikuwa ikifanyika Jumamosi na Serikali ya Muungano ilikuwa na mpango wa kuupeleka Muswada huko Bungeni Jumatatu inayofuata. Mtu ambaye amekuwa akifuatilia kadhia hii, ataona wazi wazi kuwa kumekuwa na “tabia” fulani katika serikali zote mbili za Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika suala hili, nayo ni ile ya kuwa imepania kuwa Muswada huu usonge mbele vyovyote iwavyo.”

Kwa mara nyengine tena, mbele ya umma Serikali ya Tanzania imepeleka Muswada wa Marekebisho ya Katiba, ili utayarishe mazingira ya wananchi kuifanya kazi hiyo baada ya miaka karibu 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Haya yanatokea kutokana na yale yanayoonekana ni madai ya umma ya kutaka mabadiliko ya Katiba kama alivyosema profesa wangu, Josephat Kanywanyi, kwamba kilio hiki ni cha wananchi kutaka kujua haki za kiuchumi, ugawaji wa rasilmali, namna ya kudhibiti watu wanaowachagua na jinsi serikali yao inavyotumia fedha za umma.

Ila inavyoonekana ni kana kwamba Serikali imeuleta muswaada huo kama kwamba ni kwa hisani tu, na kwa hivyo namna ambavyo umekuwa ukiletwa inaonekana kama kwamba ni ile ya kusukumiziwa na kwamba wananchi wapokee kama ulivyo na wasiuhoji kabisa.

Kama si hivyo, mtu atajiuliza, basi mbona Serikali ilipoleta muswada kwa mara ya kwanza sio tu ulikuwa na makosa ambayo usingeyatarajia, lakini pia ulikuwa na upungufu mkubwa ambao haukubaliki kwa sababu ya kukosa mantiki na kutojali, kwa mfano, maslahi ya Zanzibar?

Serikali inabeza nguvu ya raia

Wakati ule lawama kubwa ilizuka pale ilipotokea muswada kuchanwa Zanzibar, lakini pia kuwepo na vurugu kubwa Dar es Salaam na Dodoma. Angalau basi Dar es Salaam na Dodoma vilikuwa ni vituo vilivyopangwa kuwa na mjadala, lakini Zanzibar ilikumbukwa dakika ya mwisho, tena baada ya kushituliwa na Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammed Ibrahim Sanya.

Serikali hiyo hiyo ya Tanzania ilijitia hamnazo (kwa lugha ya mjini) na kuchapisha Muswada wa Kiingereza tu, kama kwamba haijui au imesahau kuwa umma mkubwa wa Watanzania ni wanaosema na kusoma Kiswahili. Hilo nalo likapigiwa kelele kubwa.

Labda kutokana na utamaduni usiozoeleka, serikali haijioni katika hali ya kawaida muswada wake kujadiliwa katika upana wa umma na, kwa hivyo, inaelekea haikujiandaa kabisa katika hilo. Hatuna jengine la kusema zaidi ya hivyo kwa dalili tunazoziona.

Inawezekana makala hii ikisomwa, muswada utakuwa umeshapitishwa – na mwandishi anajua uwezekano huo upo. Lakini kinachofanywa ni kuweka rikodi kuwa makala hii inatoa sauti za Wazanzibari kutoridhika na yale yanayoitwa marekebisho yaliyofanywa katika muswada ulioletwa tena mbele ya umma.

Hata SMZ nayo haitaki ushauri wa umma

Kama mara ya kwanza wananchi wa Zanzibar walipata fursa ya kuujadili muswada huo, basi mara hii hilo halikuwepo kabisa. Sababu ni nyingi; na mbili zake ni hizi ambazo ndizo ninazozihisi mie:

Kwanza ni kwa sababu kwetu Zanzibar kuna “taasisi” moja tu iitwayo Baraza la Katiba, ambayo imekuwa ikijushughulisha na uhamasishaji wa masuala haya ya Mabadiliko ya Katiba, ilhali ikiwa na bajeti duni. Pili, Serikali ya Zanzibar yenyewe – ikiwa inahitaji kuungwa mkono kupambana – haionekani kutaka ushiriki wa wananchi katika hili.

Ikumbukwe kuwa serikali hiyo hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, ilipotaka msaada wa ushauri, iliwaita na kuwashirikisha watalaamu kadhaa wa sheria na watu wenye ushawishi katika jamii, lakini baada ya hapo ikawatenga kama vile hawapo kabisa.

Mwishoni mwa wiki, ikawa kama ilivyokuwa mara ya mwanzo, fikra ya kuishirikisha Zanzibar ikaja dakika ya mwisho. Hii ni pale ilipoandaliwa semina ya dakika ya mwisho kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambao nao nilipenda waliposema ukweli wao kuwa wengine waliupata muswada usiku uliotangulia, kuonyesha udhaifu na uharakishaji wa maandalizi.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pia walilalamika kuwa muswada huo unajadiliwa na wao katika semina na sio kikao cha Baraza, lakini pia katika dakika za majeruhi. Walisema wazi wazi kuwa hawaamini kuwa fikra zao zitaweza kuchukuliwa na kuingizwa na watungaji muswada, kwa kuwa semina hiyo ilikuwa ikifanyika Jumamosi na Serikali ya Muungano ilikuwa na mpango wa kuupeleka Muswada huko Bungeni Jumatatu inayofuata.

Mtu ambaye amekuwa akifuatilia kadhia hii, ataona wazi wazi kuwa kumekuwa na “tabia” fulani katika serikali zote mbili za Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika suala hili, nayo ni ile ya kuwa imepania kuwa Muswada huu usonge mbele vyovyote iwavyo.

Hoja kubwa ya serikali hizo ni kukimbilia wakati. Kwamba imepaniwa kuwa Katiba itumike kwa kusadifu na maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanzania na, kwa hivyo, hazionekani kujali kukanyagwakanyagwa kwa taratibu, ilimradi tu lengo hilo la April 26, 2014 linafikiwa.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walikuwa na hoja nyingi, tokea za muundo wa muswada huo hadi ujazo wake, ambao waliona kuna upungufu mkubwa na ambao ungefaa urekebishwe kabla ya kupelekwa Bungeni kwa faida kubwa zaidi ya umma.

Historia itawahukumu watawala, SMZ na SMT

Serikali zote mbili zimekuwa zikianzia na hoja hasi, ambayo sasa inaonekana kwa makusudi ikikuzwa, yaani kuwa hakuna uelewa wa matakwa ya sheria hiyo. Yaani kuwa watu wanachoelewa hayo ndio marekebisho yenyewe ya Katiba; na sio kama ilivyo kuwa huo ni muswada wa kuelekeza kuunda Tume itayoratibu Ukusanyaji wa Maoni juu ya Mabadiliko ya Katiba.

Kwa mantiki hiyo hiyo ya watu kutojua kanuni za Bunge, basi kumezuka hoja ambayo upande wa serikali unailinda kwa nguvu zote, nayo ni ile ya muswada kusomwa kwa mara ya pili katika kikao cha Bunge kinachoendelea hivi sasa huko Dodoma.

Walio upande usiowafiki hoja hiyo, walisema ni muhimu sana muswada huo ungesomwa kwa mara ya kwanza ili kutoa fursa ya kwenda kwa wananchi, kwa sababu kubwa ya kwamba tafsiri ya Kiswahili ambayo awali haikuwepo, ni maalumati kwenda kwa wananchi wachangie.

Katika hili, serikali ilishikilia kani zake kuwa umeshasomwa mara ya kwanza na kusomwa kwake mara ya pili hapo Jumatatu, basi ilikuwa ni kwa mujibu wa kanuni za Bunge.

Kwa kauli hiyo, hoja inayojengwa hapa ni kuwa iwapo wasemaji dhidi ya hoja hii hawaelewi madhumuni ya muswada huo, basi hawana haki ya kuusemea na, kwa hivyo, maoni yao ni ya kupuuzwa. Kila linalosemwa jawabu ni kuwa hawa hawaelewi taratibu za Bunge.

Kwa ufupi ni kuwa muswada ulipangiwa usomwe, liwalo na liwe. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walitaka busara itumike muswada huo usipelekwe Bungeni, ili kutoa muda wa kuingiza marekebisho kutokana na mapungufu waliyoyaonyesha kuwamo katika muswada huo – kama ambavyo makundi kadhaa ya kijamii ya huko Tanzania Bara, kama Jukwaa la Katiba na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika walivyopendekeza.

Makundi mengine yamefika mbali zaidi, hata kusema kuwa wataitisha maandamano ya nchi nzima iwapo Muswada huo ungelisomwa kwa mara ya pili. Jambo ambalo lisingewezwa kutamkwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, lakini ilitosha kuwasikia hata mawaziri kama Mansour Yussuf Himid na Omar Yussuf Mzee wakiukosoa pamoja na kwamba pia ulipita Baraza la Mapinduzi.

Lakini kilichonishangaza ni maoni ya mwanasheria Ibrahim Mzee, ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi. Nikisema kushangaa si kwa maana hasi, bali chanya. Wengi tunamjua Ibrahim kuwa ni mmoja wa wanasheria makini hapa Zanzibar na haogopi kusema maoni yake.

Kilichonishangaza ni kule kutanabahi kwangu kumbe inavyoelekea Wizara ya Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar bado hawajatumia vya kutosha utaalamu mkubwa uliopo serikalini katika mambo ya Katiba kama kutoka kwa watu wenye hadhi ya taaluma kama ya Ibrahim Mzee.

Naamini kama wangekuwa wanafanya hivyo, na sio kujifungia wao kwa wao, haki za Zanzibar zingelindwa zaidi. Lakini Wizara ya Katiba na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wajue kuwa hili ni jukumu kubwa na wasione kuwa wanaweza kulibeba kwa kifua na migongo yao peke yao.

Ikija ikitokezea kutota wajue kuwa watakuwa ’masuul’ kwa umma. Kwanza kwa kushindwa kwao kutengeza mazingira ili mchango wa umma uwe mkubwa zaidi, lakini pili kwa kutotafuta hata utaalamu ulioko serikalini kama wanaogopa ulioko nje.

Na tukipata nafasi ya kuwanyooshea kidole, tutafanya hivyo, kama ambavyo leo tunamfanyia Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume, kwa kuiingiza nchi hii katika Muungano bila ya ushauri wa wanasheria na ndio maana leo tuko hapa.

Moja ya jambo ambalo Karume hatasamehewa na Wazanzibari ni kuingiza Zanzibar katika Muungano, ambao haiwezi tena kujitoa. Na Serikali ya sasa ya Zanzibar ijue kuwa ina jukumu kubwa kuzuia Zanzibar isimezwe kabisa ndani ya mabadiliko haya yajayo, maana kila Mzanzibari anaamini kuwa mara zote watu wetu huzidiwa kwa kete. Japo wengine wataona si hofu ya msingi, lakini ushahidi wa hayo ni hii hali iliyopo sasa.

Ndio maana wananchi wa Zanzibar na hata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wana hoja kuwa kabla ya mjadala huo, ingepaswa kwanza watu waulizwe je, wanautaka au hawautaki Muungano?

Na wanataka pia kujua kuwa kutakuwa na kipengele wakati wa Kura ya Maoni kinachoonesha kuwa athari za kura za HAPANA zitakuwa na maana ya Muungano kujadiliwa upya? Lakini hilo halina jawabu mpaka sasa, zaidi ya kuwa kura ikikataliwa ni kurudi Katiba ya sasa, jambo ambalo najua litazua sekeseke kubwa hapa Zanzibar, hata kama tutajaribu kwa sasa kulifumbia macho!


Makala ya Ally Saleh, 16 Novemba 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.