Kulikuwa na hoja gani ya kuitoa Zanzibar kwenye OIC, hata iwepo ya kuiweka Tanzania kwenye FIFA?

Zanzibar, ikiwa ni nchi yenye Waislamu wengi, ilishurutishwa enzi za utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi na Dk. Salmin Amour Juma katika miaka ya 1990, kujitoa kutoka Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) kwa kuwa mambo ya siasa za nje na uhusiano wa kimataifa ni ya Muungano. Mwaka huu, jaribio jengine la Zanzibar kujiunga na taasisi ya kimataifa, safari hii kupitia Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar (ZFA) kujiunga na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), lilikataliwa mwaka huu. Tena waliolikataa ni FIFA wenyewe kwa hoja kuwa eti “Zanzibar si nchi” na hivyo haina mamlaka kukubalika kuwa mwanachama wa Shirikisho hilo. Bila ya shaka haihitaji kukumbushwa kuwa England, Wales, Scotland na Ireland ya Kaskazini, ingawa itakimbilia kusema kwamba hadhi maalum iliyonayo England ni kwa kuwa ndiye mama wa dimba duniani.

Lakini, ikiwa kujiunga Zanzibar katika Jumuiya ya Kiislamu ni mwiko kwa sababu nchi hiyo haina mamlaka hayo na imejiingiza OIC kwa mlango wa nyuma, basi wakati sasa umewadia kwa waziri anayehusika na michezo wa Zanzibar, Abdullahi Jihad, Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar na uongozi wa ZFA, kuvaa njuga na kuanza kuhoji uhalali wa Tanzania Bara kujiunga na FIFA, kujiunga na Halmashauri Kuu ya Olimpiki Ulimwenguni (IOC), kujiunga na Shirika la Mabondia Ulimwenguni (World Boxing Federation – WBF) na mashirika mengine ya michezo mbalimbali ya kimataifa, wakati michezo si suala la Muungano. Ikiwa haikuwa sawa kwa Zanzibar kujiunga na OIC , itakuwaje sawa kwa Tanzania Bara kujiunga kwenye jumuiya hizo za kimataifa kwa jambo ambalo si la Muungano, ikitumia jina la Muungano wa Tanzania? Je, mashirikisho ya michezo ya pande hizi mbili za Muungano yaliwahi kukaa pamoja kuomba uanchama kwa ubia? Hata kama yalifanya hivyo, yalitumia sharia ipi?

Waziri anayehusika na Michezo Zanzibar, Abdillahi Jihadi Hassan

Hivyo sivyo hali inavyoonekana katika FIFA. Laiti ingelikuwa hivyo, ZFA isingelikuwa ikihanikiza kupiga hodi mlangoni mwa FIFA kuomba uwanachama wake pekee. Mabaraza mawili ya taifa ya michezo ya pande hizo mbili sasa yanapaswa kuitisha kikao kujadili nani mwenye mamlaka hasa ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kihalali katika mashirika ya michezo ya kimataifa, yakiwemo FIFA, IOC na WBF.
Katika wakati huo inapojadiliwa katiba mpya, ni muda muwafaka wa kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika medani ya spoti kwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dimba linapaswa kwanza kuchezwa nyumbani Dar es Salaam na Zanzibar kabla kukimbilia Zurich -Makao Makuu ya FIFA, Cairo – Makao Makuu ya Shirikisho la Kabumbu la Afrika (CAF) au Lausane, Uswisi, kwenye Makao Makuu ya Kamati ya Olimpiki Ulimwenguni. Zanzibar na Tanzania Bara lazima zikae sasa kutatua kero hii nyengine ya Muungano.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili kupitia serikali na mabaraza ya michezo, yafumbuwe kitandawili hiki kikuu: Ilikuwaje Tanganyika, kwa kutumia kawa la Tanzania, inaendelea kubeba bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania medani za kimataifa za michezo, ilihali michezo si suala la Muungano?
Hapa Zanzibar kupitia Serikali ya Mapinduzi (SMZ), ZFA na BMZ ndiyo yenye turufu nzito ya kuwafanya ndugu zao wa damu wa Tanzania Bara kuridhia kukaa pamoja nao tena kwa nia safi ya kuchanganya upya karata na kuamua moja kati ya mawili: ama kuacha spoti kuendelea kuwa si suala la Muungano na kila upande usake uwanachama wake ulimwenguni au kuibadili Katiba na Hati ya Muungano na kulijumuisha katika Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa na timu moja. Lolote kati ya hilo, Zanzibar itakuwa ndiyo iliyovuna, ingawa Tanganyika pia haitapoteza kitu.

Zanzibar ishikilie msimamo kwamba Tanzania Bara haipaswi kupepea bendera ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika medani za kimataifa ilhali spoti si suala la Muungano. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wa nchi mbili na hakuna upande wenye haki kulitumia jina hilo kwa masilahi ya upande mmoja tu katika masuala yasiyo ya Muungano.

Rais wa Shirikisho la Mpira la Tanzania Bara, Leonard Tenga

Ni hapa inapostahiki kuhoji Tanzania katika FIFA, IOC, WBF na mwenginemo, inamuakilisha nani: Tanganyika au Zanzibar? Nani aliyetoa mamlaka au idhini ya uwaklilishi huo? Je mashirika hayo ya kimataifa yalifichwa kuwa michezo si suala la Muungano au mashirika yenyewe yalijuwa lakini yakajifanya kuziba macho na masikio kwa makusudi, kama ulivyofanya Umoja wa Mataifa kukiondoa kiti cha Zanzibar bila ya idhini ya kimaandishi kutoka Zanzibar? Kwa nini FIFA ilipokataa ombi la uwanachama la ZFA, haikuhoji uwanachama wa Shirikisho la Michezo la Tanzania Bara (TFF) kwa misingi ya kuwa michezo si jambo la Muungano? Lakini kwa nini uongozi wa ZFA nao wenyewe haukuhoji uwanachama wa TFF? Au kwa kuwa isingelikuwa picha njema kidiplomasia? Ikiwa ni hivyo, mbona Tanzania Bara ilihoji uwanachama wa Zanzibar katika Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) na kuivua nguo hadharani Zanzibar itoke? Kwa nini Rais Mwinyi na Komando Salmin walifedheheshwa? Waliofanya hivyo walikuwa hawajui diplomasia, au ukweli kwamba 99% ya Wazanzibari ni Waislamu, ambao wangelifaidika na OIC?

Ikija ikadhihirika kuwa mashirika ya michezo ya Tanzania Bara yameingia katika vyama na jumuiya za kimataifa kinyemela kama ilivyoingia Zanzibar katika OIC miaka ya 1990 kwa mlango wa nyuma na kulazimishwa itoke, Tanzania Bara inabidi kusimamishwa uwanachama wake kwanza, hadi suala la uhalali wa uwakilishi wake lipatiwe ufumbuzi, baada ya pande zote mbili kuamua hadhi ya michezo katika Muungano.

Kwa hivyo, mlango ule ule iliotolewa Zanzibar kwenye OIC, ndio uwe ule ule wa ZFA kuingilia FIFA. Ama sivyo Tanzania Bara nayo ifunge virago vyake na ikae nje ya FIFA, IOC, WBF na mashirika mengine ya kimataifa kama ilivyokaa nje ya OIC Zanzibar. Kwa hili pande zote mbili zitakuwa nje – nje ya FIFA na mashirika mengine ya kimataifa ya michezo na nje ya OIC, kama ambavyo hadi leo hii hakuna upande uliorudi huko tangu Zanzibar ilipolazimishwa kutoka tangu enzi za utawala wa Rais Mwinyi na Dk. Salmin pale kibiriti cha Komando kilipotikiswa Dodoma.

Wakati kukaa nje ya Jumuiya ya Kiislamu hakujawakera baadhi ya Watanzania Bara wasio Waislamu hadi sasa, kukaa nje ya FIFA, CAF na IOC kutawakereketa wote bila ya kuchagua dini au madhehebu na, hivyo, watatafuta haraka ufumbuzi wa kukitegua kitandawili hiki .Ufumbuzi huo uje kabla ya Kombe la Dunia la FIFA 2014 na Michezo ya Olimpiki ya Brazil 2016. Mpira sasa uko langoni mwenu Wazanzibari muucheze. Wenzetu wameshatia goli langoni mwa FIFA, IOC, WBF na Mashirika mengine ya Kimataifa.


Makala ya Ramadhan Ali, mwandishi wa michezo wa siku nyingi. Miongoni mwa vitabu vyake ni “Africa at the Olympics, “The Rise of African Football (1984)” na “African Football Stars in the Bundesliga (2002)”. Alikuwa pia mtangazaji wa muda mrefu wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, Ujerumani.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.