Prof. Palamagamba Kabudi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Miongoni mwa mada kubwa kwenye mitandao ya Kizanzibari hivi sasa ni kauli ya ya Profesa Palamagamba Kabudi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyetaka mjadala wa katiba mpya usiguse suala la Muungano, kama alivyonukuliwa na gazeti moja la Dar es Salaam. Hoja ya Prof. Kabudi ni kwamba kuujadili Muungano kutapelekea hatimaye kuuvunja. Hoja ya Wazanzibari ni kwamba kujadiliwa Muungano ni haki ya msingi ya wananchi, ambayo haiwezi kuzuiliwa kwa namna yoyote ile, bila ya kujali matokeo ya mjadala huo. Kwa nini pana tafauti hii baina ya Watanganyika na Wazanzibari kuhusiana na Muungano? Kwa maoni yangu, kuna sababu tatu.

Moja, bila ya kuzingatia maandiko yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Wazanzibari wanatambua kwamba Tanganyika na serikali yake ni vitu hai, vipo na vinaishi. Wanaamini kuwa ile iitwayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo hiyo hiyo Tanganyika yenye mipaka na jina jipya, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ndiyo hiyo hiyo Serikali ya Tanganyika.

Pili, kuna ushahidi wa kimazingira na kivitendo unaonesha kuwa serikali hiyo ya Tanganyika kwa jina la Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina sera maalum kuelekea Zanzibar ambayo inasema: “Kuwa na Jamhuri ya Muungano imara, ni kuwa na Zanzibar dhaifu; na kuwa na Zanzibar imara ni kuwa na Jamhuri ya Muungano dhaifu.” Kwa hivyo, linapokuja suala la kuujadili Muungano huu, khofu ya Tanganyika ni kuwa kutapelekea kuvunjika kwa Muungano na hivyo kupoteza himaya yake; na matarajio ya Zanzibar ni kuwa kutapelekea kupatikana suluhisho la Muungano huu, haidhuru kama suluhisho litakuwa ni huko kuvunjika kwake.

Tatu, kihistoria, Wazanzibari wameandaliwa kuuangalia Muungano huu katika sura ya Shirikisho, ambalo lilichukuwa baadhi tu ya mamlaka kutoka kila upande, yaani Tanganyika na Zanzibar, na kubakisha sehemu nyengine ya mamlaka hayo kwa serikali za nchi husika. Hiyo ndiyo dhana inayoakisika katika Katiba ya Zanzibar. Lakini Watanganyika wameandaliwa kuuangalia Muungano huu kama ni wa serikali moja tu, ambapo hawaoni mipaka ya kimamlaka baina ya Zanzibar na Tanganyika. Hiyo ndiyo dhana inayoakisika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.