Na Ahmed Rajab

ZANZIBAR ya leo si Zanzibar ya jana. Kuna siku ambapo Zanzibar ilikuwa na machafuko ya kisiasa lakini uchumi wake ulikuwa imara, ulistakimu. Na pale palipokuwa na udhaifu hapakuwa na aliyekuwa akilia kwa njaa.

Siku hizi Zanzibar ina utulivu wa kisiasa lakini uchumi wake umesambaratika na kuvurugika. Vilio vya njaa vimehanikiza Unguja na Pemba, mijini na mashambani.

Kwa muda wa miaka kama sita kabla ya Uingereza kuipa Zanzibar uhuru mwezi Desemba mwaka 1963, Visiwa hivyo vilidamirika vikitumbukia katika shimo la migogoro ya kisiasa. Jamii ilipasuka pande mbili — nusu ya wananchi wakikiunga mkono chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP), au Hizbu, na nusu wakikiunga mkono chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).

Tunaweza kuwalaumu viongozi wa kisiasa wa pande zote mbili kwa ushindani wao mkali wa kisiasa wa kupigania madaraka uliosababisha kuzuka kwa hali hiyo. Kampeni zao za kuwania madaraka zilijaa fataki za kisiasa ambazo mara kwa mara zikifyetuka na hatimaye kusababisha moto wa Mapinduzi ya Januari 1964.

Mkesha wa kupandisha bendera yake ya Uhuru na kuwa Taifa huru la 37 barani Afrika, Zanzibar ilikuwa na uchumi uliokua kwa ghafla.

Sekta yake ya biashara za watu binafsi ilikuwa ikizalisha mali vya kutosha na karafuu zake, nyingi na nzuri zaidi zikitoka Pemba, zikivuma duniani kwa sifa zake. Umaarufu wa karafuu za Zanzibar ulitapakaa kila pembe ya dunia.

Siku hizo idara ya utumishi wa serikali Visiwani ilikuwa na ustadi wa utendaji bora wa kazi. Watumishi wake wakichapa kazi bila ya kutarajia bakhshishi au vivutio vingine vya kifisadi.

Wakati huo Zanzibar ilikuwa kituo muhimu cha kibiashara katika eneo zima la Afrika ya Mashariki na ya Kati kama ilivyokuwa tangu zama za kale.

Linalosahauliwa ni kwamba Zanzibar haikuwa tu kituo cha biashara bali ilikuwa vilevile kituo muhimu cha ilmu ya dini ya Kiislamu. Wanachuoni kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ya Mashariki na ya Kati wakimiminika Unguja kwenda kuchota ilmu kutoka kisima cha masheikh na maulamaa wa huko.

Majina ya maulamaa hao yataselelea katika historia ya Uislamu katika Afrika ya Mashariki. Walikuwa ni watu wa makabila tofauti waliotukuka kwa ilmu waliyokuwa nayo.

Miongoni mwao walikuwa Sayyid Ahmed bin Sumeyt na mwanawe Sayyid Omar bin Sumeyt, Sheikh Suleiman al Alawy, Sheikh Abdallah Saleh Farsy, Sheikh Hafidh bin Ameir, Sheikh Fatawi bin Issa, Sheikh Muhyiddin bin Ali, Sheikh Shauri wa Donge, Sheikh Abubakar Bakathir, Sheikh Ahmed Mohamed Mlomri, Sheikh Muhammed Omar (Bwana wa Shangani) na Sheikh Muhsin bin Ali Barwani (babake Ali Muhsin Barwani, aliyekuwa kiongozi wa Hizbu). Kila mmoja wao anahitaji kitabu au vitabu kuelezea wasifu wake.

Wengine kama wao ni Sheikh Muhammed bin Waziri, Sayyid Mansab bin Ali, mwanawe Sayyid Hamid na mjukuu wake Sayyid Ahmed Hamid Mansab, Sheikh Burhan Mkelle, Sheikh Suleiman Hayati, aliyekuwa na asili ya Kihindi, Sayyid Omar Abdallah (Mwinyi Baraka) na Sheikh Ameir Tajo, ambaye pia alikuwa mwanasiasa.

Wote hao wakiweka darsa zilizokuwa zikiwavutia wengi kutoka sehemu mbalimbali za Afrika. Hivi sasa tumebakiwa na Sheikh Habib Ali Kombo, anayekaribia umri wa miaka 90.

Baadhi ya maulamaa hao walikuwa watunzi waliotunga vitabu kwa lugha ya Kiarabu vilivyochapishwa ama Beirut au Cairo. Vingine, vya Kiarabu na Kiswahili, vikichapishwa humu humu Afrika ya Mashariki, ama Zanzibar kwenyewe au Mombasa, Kenya.

Sifa za wanachuoni hao wa kale wa Zanzibar zikitambulika kwingi toka Cairo kwenye Chuo Kikuu cha Al Azhar hadi Makkah.

Ajabu ni kwamba wengi wao walipata ilmu yao hapo hapo Zanzibar. Lakini ilikuwa ilmu ya hali ya juu, iliyomplelekea, kwa mfano, Sayyid Ahmed bin Abu Bakr bin Sumeyt, atunukiwe nishani na Sultan Abdul Hamid wa Uturuki mwaka 1886. Sayyid Ahmed bin Sumeyt alibobea katika fani mbalimbali.

Hadi mkesha wa Uhuru waliokuwa wakiisaka ilmu kutoka sehemu nyingine za Afrika ya Mashariki walielekea Zanzibar. Hali hiyo iliendelea hadi kabla tu ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Hata hivyo, kisiasa Zanzibar ilikuwa na mpasuko mkubwa ulioigawa jamii na kuvifanya Visiwa hivyo viangukie pabaya. Katika miaka yote hiyo na bila ya pingamizi zo zote mapande ya kisiasa yaliyokuwa yakishindana yaliigeuza Zanzibar kuwa ni medani ya mapigano.

Migogoro ya kisiasa ilikuwa haiishi na uhasama wa kisiasa ukijipenyeza na kuathiri mahusiano ya kijamii. Wakati wote huo wa vita ya kisiasa Zanzibar haikumudu kufanya lolote la maana ela ikijikokota tu.

Hii leo, kwa upande mwingine, hali ya kiuchumi na ya kijamii ya Zanzibar ni tofauti kabisa, kama mbingu na ardhi, na ile iliyokuwa imeshtadi mkesha wa Uhuru. Siku hizi Wazanzibari wanayafaidi matunda ya umoja wa kisiasa na inavyoonyesha ni kwamba Wazanzibari, kwa jumla, wana ajenda moja kuhusu mustakbali wa nchi yao.

Hitilafu kubwa inaonekana katika hali ya uchumi ikilinganishwa na ilivyokuwa nusu karne iliyopita. Hii leo uchumi wa Visiwani umeshuka sana na ushahidi wa hali hiyo uko bayana kwa kila anayetaka kuuona Unguja na Pemba.

Huduma za kijamii zimemegwa, ufisadi unakodoa macho na umasikini na ufukara umezagaa na kuenea kwa wengi wa wananchi. Wengi miongoni mwao hawawezi hata kujipatia dola moja ya Marekani kwa siku.

Jambo la kutia moyo, juu ya mashakil yote hayo, ni kuwaona Wazanzibari, wakiwa wanajiamini na wamesimama imara wakitambua nini wanachotaka kifanywe ili nchi yao ipate maendeleo ya kiuchumi baada ya kuwa na utulivu wa kisiasa.

Hamna shaka yoyote kwamba fanikio kubwa la serikali ya mwanzo ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar ni kupatikana umoja wa wananchi wake. Muhimu zaidi ni jinsi Wazanzibari hii leo walivyo na imani na viongozi wao.

Hata hivyo, serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa inakabiliwa, na bado itakabiliwa, na changamoto kubwa zaidi.

Changamoto hiyo ni kushinda ile ya kuondosha uhasama Visiwani humo. Hii ni changamoto ya kunyanyua maisha ya watu wa kawaida. Na jana Jumatano ya Juni 15, masikio ya Wazanzibari yaliitega hotuba ya Bajeti ya mwanzo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyotolewa na waziri wa fedha katika Baraza la Wawakilishi.

Bajeti hiyo ilitolewa kama wiki hivi baada ya zile za Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Walipokuwa wakizipanga bajeti hizo mawaziri wa fedha wa serikali za nchi hizo nne walizingatia sana yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika nchi za Kiarabu.

Mawaziri hao wamekuwa wakitambua kwamba umati wa vijana wasio na ajira katika nchi zao wanaweza kumiminika barabarani na kuanza kuwaigiza wenzao wa Tunisia na Misri.

Na Wazanzibari watajua ikiwa serikali yao ina mipango kabambe ya kuukwamua uchumi au ikiwa itaziigiza serikali zilizopita kuwanyerereza wananchi na kuwalaghai kwa ahadi za mapovu.

Siku mbili hizi kuna minong’ononong’ono mitaani kwamba serikali ya Umoja wa Kitaifa haikutenda cha maana tangu iundwe. Miongoni mwa lawama nyingi zilizopo ni kwamba uchumi bado unazorota, wananchi wanaendelea kuishi katika mazingira ya uchafu, ufisadi haukupungua na upinzani rasmi umezimwa.

Yote hayo yanaweza kuwa kweli lakini ni pupa za kitoto kuitarajia serikali isiyotimu mwaka kurekibisha yaliyoharibiwa kwa muda wa nusu karne. Muhimu ni kwamba pawepo na utawala ulio na uwazi na wenye kuendesha mambo kwa kufuata sheria za nchi na za kimataifa.

Umoja walio nao sasa Wazanzibari unawapa fursa adhimu ya kuwawezesha kukaa kitako na kupanga namna ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa faida ya vizazi vya leo na vijavyo. Muafaka na ushirikiano aina hiyo usiojali tofauti za kisiasa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Serikali nayo inawajibika kutambua umuhimu wa kuwapa nafasi wananchi katika utungaji wa sera zitazoleta maendeleo.

________________________________________Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 15 Juni 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.