..‘TARATIBU ndiyo mwendo, siasa ya wazalendo’. Huo ulikuwa wito wa chama kimoja kikuu cha kisiasa huko Zanzibar katika zama za kuwania uhuru kutoka Uingereza.

Nakumbuka utotoni mwangu kuusikia sana wito huo na pia kuusoma kwenye kanga kwa vile ulikuwa jina kwenye kanga za sare walizokuwa wakijitanda wafuasi wa kike wa chama hicho.

Nimeukumbuka hivi sasa kwa vile wito huo unayasibu yanayojiri siku mbili hizi huko Visiwani. Inavyoonyesha ni kwamba baadhi ya wazalendo wa Zanzibar, wa itikadi na mirengo tofauti ya kisiasa, kama wameukumbatia wito huo kuwaongoza katika lengo lao la kuviokoa na kuvinusuru Visiwa hivyo vya Unguja na Pemba.

Wazalendo hao hawataki kufanya papara; hawataki pupa, hawataki vishindo. Wanafanya mambo asteaste wakitaka yende kwa utaratibu ilimradi waitunge shabaha yao vilivyo ili waweze kuidengua.

Ushahidi wa hayo umejianika kwenye kikao cha sasa cha Baraza la Wawakilishi chenye kuichambua na kuijadili Bajeti, kikao ambacho kimekuwa cha kihistoria kwa vile ni cha mwanzo aina yake kufanywa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Wananchi wa Zanzibar wanaisikiliza kwa raghba kubwa mijadala inayoendelea kwenye Baraza la Wawakilishi ambayo inarushwa na kuonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha serikali, TVZ.

Kwa kadiri nionavyo, kwa jumla wananchi hao wanaonyesha kuridhika na kazi inayofanywa na wawakilishi wao kwenye baraza hilo la kutunga sheria.

Pia nionavyo ni kwamba wananchi wanaufurahia umoja uliojidhihirisha wazi miongoni mwa wawakilishi wao kutoka vyama vya CCM na CUF, umoja unaoashiria kupevuka na kujiamini kwa wanasiasa wa mapande hayo mawili. Kwa hakika, umoja huo wa wawakilishi ni kama kioo cha umoja ulioshamiri siku hizi miongoni mwa watu wa Zanzibar.

Wengi wanauthamini na kuuenzi Umoja huo wakiamini kwamba ni chombo muhimu kitachoiwezesha Zanzibar iyafikie malengo yake ya kuvipatia Visiwa hivyo maendeleo na ufanisi.

Ni jambo la kutia moyo bila ya kiasi kuona jinsi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa vyama vyote viwili wanavyoikosoa Serikali. Lakini ukosaji huo si wa kuilaumu kwa nia ya kutaka kuibomoa bali ni ukosoaji wa kuisaidia katika upangaji na utekelezaji wa sera zake.

Kwa mfano, mjumbe mmoja wa Baraza hilo Hassan Hamad Omar akimhoji Waziri wa Viwanda na Masoko Nasor Ahmed Mazrui, alisikitika kwamba watu wengi wakitumai hali zao za maisha zitatengenea chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini bado gharama za maisha zinazidi kupanda.

Bei ya lita moja ya mafuta ya petroli imeruka kutoka shilingi 1,650 kufikia shilingi 2,055. Mafuta ya taa yamepanda kutoka shilingi 1,150 kufikia shilingi 1,650.

Kwa upande wa vyakula alitaja bei za mchele iliyopanda kutoka shilingi 700 hadi shilingi 1,200 kwa kilo moja na bei ya unga wa mahindi iliyopanda pia kutoka shilingi 700 kufikia shilingi 1,000 kwa kilo.

Akimjibu, waziri Mazrui alisema kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekwishakuanza kupanga mkakati wa kanuni zitazosaidia kuzuia upandaji wa kiholela wa bei za bidhaa humo Visiwani.

Jibu hilo ni la kutia moyo.

Hali kadhalika, inatia moyo kuiona Serikali ikiyaridhia na kuyakubali mapendekezo yanayotolewa na wajumbe wa vyama vyote. Mfano mzuri ni kuhusu suala la mafuta.

Wajumbe wa Baraza walidai patungwe mswada utakaowezesha kuundwa kwa Mamlaka ya Zanzibar ya Maendeleo ya Mafuta (Zanzibar Petroleum Development Authority). Shughuli za Mamlaka hayo zitakuwa kusimamia na kuharakisha uchimbaji wa mafuta katika eneo la Zanzibar, mafuta ambayo Waziri wa Zanzibar anayesimamia mambo ya nishati Ali Juma Shamhuna amelithibitishia Baraza kuwa yapo kwa viwango vitavyoweza kuleta faida ya kiuchumi endapo yatachimbwa.

Sidhani kama ninakosea nisemapo kwamba Baraza la Wawakilishi liliopo sasa limejaaliwa kuwa na dhima ya kimkakati si tu kuhusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Visiwani, bali pia kuhusu suala zima la Muungano. Tutaona jinsi mambo yatavyoibuka wakati wa mijadala ya sasa na ya vikao vijavyo vya Baraza hilo hadi kufikia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hadi sasa mijadala mingi kwenye kikao cha sasa cha Baraza la Wawakilishi imekuwa ikizichambua shughuli za Muungano huku Serikali ya Zanzibar ikiwa inajaribu, kwa dhamana ilizo nazo, kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi na ya kijamii ya Visiwa hivyo. Inafanya hivyo licha ya mipaka au vizingiti vilivyowekewa serikali ya Zanzibar na muundo wa sasa wa Muungano.

Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Omar Yusuf Mzee, hakuwa na haja ya kushikwa na kigugumizi alipomjibu Ismail Jussa Ladu, Mjumbe wa chama cha CUF, kwa kutamka kwamba lau Zanzibar itarejeshewa mamlaka yake yote kuhusu masuala ya kiuchumi na kijamii basi wizara yake itakuwa na uwezo thabiti wa kuusarif vilivyo uchumi wa Zanzibar.

Suala jingine alililoibua Ladu lilikuwa la hadhi ya Zanzibar. Alitaka Zanzibar izingatiwe kuwa ni dola huru panapohusika mambo yasiyo ya Muungano. Hivyo, kwa mfano, Ladu akitaka Zanzibar iwe mwanachama kamili na huru wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki badala ya kuwamo humo ikiwa chini ya kwapa za Muungano.

Kwa hilo lakini Makamu wa pili wa Rais, Seif Ali Iddi, Waziri wa Ushirikiano Mohamed Aboud na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Othman Masoud Othman walimzima Ladu kwa kusema kwamba ingawa hoja yake ilikuwa halali lakini aliileta katika wakati usio muafaka.

Bila ya shaka, kuna Wazanzibari wengi wanaoutia walakin msimamo huo wa kulizima suala hilo la uanachama wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Na kuna wengi pia wasioridhika na mkabala wa baadhi ya wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kutaka mashakil yenye kuhusika na Muungano yasijadiliwe kwa kina na kutanzuliwa hivi sasa.

Wenye hamasa ya kutaka masuala tata ya Muungano yatafutiwe ufumbuzi wa haraka wana sababu zao zinazowafanya wawe na msimamo huo. Hawaoni kuwa wanafanya papara kwani wanahoji kwamba kila miaka ikienda ndipo mambo yanapozidi kuchacha.

Jambo moja lisilo la kawaida kwenye vikao vya kujadili bajeti ni kutunga sheria mpya. Kikao cha sasa cha Baraza kimeuvunja mwiko huo na nnasikia miswada miwili muhimu itawasilishwa kwenye ukumbi wa Baraza hilo.

Fununu niliyopata ni kwamba mmoja utahusika na uundwaji wa Mamlaka ya Anga (Civil Aviation Authority), ambalo kwa kweli ni suala la Muungano. Wa pili utakuwa Mswada wa Kupinga Ufisadi na wa Maadili ya Umma (Anti-corruption and Public Ethics Bill).

Nnavyosikia ni kwamba uamuzi pia umekwishakatwa wa kuitisha Mkutano wa Mashauriano utaowahusisha washirika wote wa maendeleo ya Zanzibar yaani wafadhili wake.

Utapofanywa mkutano huo kwa mara ya mwanzo mahitaji ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano, na pengine hata ya Muungano, yatazungumzwa na kujadiliwa moja kwa moja baina ya Wazanzibari na wafadhili wao kutoka nje.

Kabla ya kikao hiki mambo hayo yamekuwa yakihodhiwa na Serikali ya Muungano au kama wasemavyo jamaa mitaani: ‘Bara imekuwa ikituamulia mambo hayo.’

Baada ya kuyatafakari yote hayo, ninaamini kuwa kikao cha sasa cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakumbukwa na vizazo vijavyo kuwa ni kikao cha mwanzo cha Baraza hilo kinachosisitiza na kuzitilia mkazo haki za Zanzibar ingawa Zanzibar ni mshirika wa Tanganyika katika Muungano.

Kitakumbukwa pia kwamba ni kikao cha awali kujadili masaala ya kitaifa bila ya kujali mjumbe gani anayetoa hoja au ni wa chama gani.

Yote hayo ni maendeleo — ni hatua kubwa katika kuulea umoja uliopo miongoni mwa Wazanzibari. Huenda ikawa kweli hakuna chapuchapu inayotakiwa na wale wenye kuibeza na kuikejeli Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini wengi wanahisi kuwa bora wakawie ilimradi wafike kuliko kuwa na pupa wakajikwaa na kuanguka.

________________________________________Makala ya Ahmed Rajab katika gazeti la Raia Mwema la 29 Juni 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.