SIKU moja, mwanzoni mwa mwaka 1971, tarehe hasa nimeisahau, nilikuwa nikipekuapekua vitabu katika duka la Collets lililokuwa kwenye barabara ya Charing Cross Road jijini London niliposikia mtu akiniita.

Duka la Collets lilikuwa maarufu duniani kote kwa vitabu lilivyokuwa likiviuza. Vingi vilikuwa vya mrengo wa kushoto na kulikuwa vingi vingine vilivyohusika na nchi za Ulimwengu wa Tatu.

Bibi Eva Collet aliyelianzisha duka hilo alikuwa na maingiliano makubwa na familia za Karl Marx na Friedrich Engels, waanzilishi wa nadharia ya Ukomunisti.

Collets likiuza zaidi ya vitabu. Pia likiuza beji za Kisovieti, mabiramu, na rekodi za muziki wa jazz. Ni mahali ambapo kama sikuwa na la kufanya nikipenda kwenda kuzubaazubaa nikiangalia magazeti ya kimaendeleo na vitabu.

Nilipomsikia mtu akiniita niligeuka na kumwona Oscar Kambona, waziri wa zamani wa Tanzania aliyefarakana na Mwalimu Julius Nyerere akatoroka nchini akikimbilia Uingereza alikokwenda kuishi uhamishoni.

Siku hizo Watanzania wengi waliokuwa nje walikuwa wakijitenga na Kambona kwani hata kuzungumza naye kukionekana kama kitendo cha kuisaliti Tanzania hasa kwa vile Kambona alikuwa akishirikiana na wakoloni Wakireno dhidi ya Tanzania. Watanzania wengi wakimkwepa na kumkimbia.

Hata hivyo, kwenye duka la Collets Kambona alikuwa amefuatana na Denis Phombeah, mmoja wa wanaharakati wa awali waliopigania uhuru wa Tanganyika na waasisi wa chama cha TANU na baba wa Grey Phombeah, mwandishi wa habari wa Kenya ambaye katika miaka ya karibuni alikuwa mtangazaji wa BBC.

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 Denis Phombeah aliteuliwa kuwa mwanabalozi katika Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar huko London. Phombeah alikuwa na mahusiano makubwa na baadhi ya jamaa wa chama cha Umma Party cha Zanzibar lakini kueleza vipi Mtanganyika huyo akawa mwanabalozi wa Zanzibar kabla ya Muungano kutanitoa katika maudhui niliyoyakusudia.

Nafikiri hata hatujawa na wakati wa kusalimiana kwa sababu Kambona moja kwa moja aliniambia: “Azizi katoroka jela jana lakini baadaye alikamatwa tena.” Nilishangaa na kumuuliza: “Azizi gani?” Akasema: “Twala.”

Habari alizokuwa akinipasha Kambona zilikuwa motomoto kwani alikuwa akimtaja Abdulaziz Ali Twala, aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na aliyewahi kuwa waziri wa fedha na wa afya katika Serikali ya Mapinduzi. Baadaye alikorofishana na Rais Sheikh Abeid Karume, akakamatwa na kufungwa bila ya kufikishwa mahakamani.

Sijui kwa uhakika nini kilichomchongea Twala. Lakini waliokuwa karibu naye wanasema kwamba alimuudhi Karume katika visa viwili alipokuwa waziri wa fedha.

Kiasi cha kwanza ambacho sikuweza bado kukithibitisha ni pale baada ya serikali kutumia fedha nyingi za sarafu za kigeni kuagiza ama peremende au chakleti kutoka nje. Inasemekana kwamba alipozisikia habari hizo Mwalimu Julius Nyerere alikasirika kiasi cha kumfanya afunge safari kwenda Zanzibar kueleza kwamba hatua hiyo haikuwa ya busara.

Karume akamtupia mpira Twala kwa kuidhinisha sarafu za kigeni zitumike hivyo na Twala naye, bila ya kufikiri sawasawa, akasema kwamba yeye alikuwa akitii tu amri yake Karume.

Sheikh Karume alikasirishwa sana na matamshi ya Twala. Nasikia kwamba baada ya Nyerere kuondoka Karume alimlaumu Twala akisema kwamba kwa mujibu wa mila za kikwetu mzee akijamba mbele za watu humsingizia mtoto na mtoto hutakiwa askut, akae kimya. Hivyo, Twala alikuwa mtovu wa adabu aliposema kwamba akifuata amri yake Karume.

Inasemekana kuwa kisa cha pili kilitokea pale Karume alipomuamrisha atoe fedha fulani naye Twala alidinda na kukataa katukatu akihoji kwamba kufanya hivyo ni kwenda kinyume na utaratibu wa serikali. Twala alitolewa wizara ya fedha na akapewa wizara ya afya aliyoishika kwa muda mfupi kabla ya kutolewa kwenye uwaziri na kufukuzwa kutoka Baraza la Mapinduzi.

Mambo yalizidi kumwendea kombo mwaka 1968 akiwa si tena waziri alipouomba ubalozi mdogo wa Marekani uliokuwa Zanzibar umpe msaada wa kwenda kusoma Marekani. Aliuomba huo msaada bila ya kuwa na hekima ya kumshauri au angalau kumueleza mapema Karume aliyekuja kuyajuwa hayo baada ya kuelezwa na Wamarekani waliotaka kujuwa fikra zake. Muda mfupi baada ya hapo Twala akatiwa mbaroni na kufungwa kwenye gereza la Langoni nje ya mji.

Alipotoroka kutoka Langoni Twala alikuwa pamoja na mfungwa mwenzake wa kisiasa Idris Abdalla Majura, aliyekuwa mzaliwa wa Bukoba. Inasemekana kwamba baada ya kutoroka walimwendea mtu waliyeamini kwamba atawasaidia kuwavusha hadi Bara lakini huyo bwana aliingiwa na hofu na akawaripoti kwa polisi. Hizo zilikuwa ni siku za vitisho vilivyowafanya Wazanzibari waogopane na hata wengine wajiogope wenyewe.

Nasikia kwamba baada ya kukamatwa tena Twala na Majura walipelekwa kwa ‘Ba Mkwe’, sehemu ya nyuma gerezani huko Kiinua Miguu ambako watu walikuwa wakiteswa. Inasemekana kwamba baadaye Twala na Majura waliuliwa kwa kupigwa risasi.

Twala na Majura hawakuwa wapinzani wa chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) kilichokuwa kikihodhi madaraka wakati huo. Walikuwa Wana-Afro ndi walioyaunga mkono kidhati mapinduzi ambayo baadaye yaliwameza. Hawakuwa peke yao. Wafuasi wengi wengine wa ASP walimezwa na Mapinduzi hayo.

Miongoni mwao walio maarufu ni akina Abdallah Kassim Hanga, Juma Maulidi (Jimmy Ringo), Mdungi Usi, Jaha Ubwa, Aboud Nadhif na Khamis Masoud. Jamaa zao na wa wengine waliofikwa na masaibu kama hayo, hadi leo hawakuarifiwa rasmi nini kilichowafika na kama wameuawa, waliuawa kwa sababu gani na walizikwa wapi.

Kuna wengi zaidi wasiokuwa wafuasi wa ASP ambao pia walifikwa na masaibu kama hayo ya kukamatwa, kufungwa gerezani na kupotea. Kuyaandika majina yao kutachukuwa sehemu kubwa ya sahafu hii na hivyo naitoshe tu nikisema kwamba waliopotea hawakuwa wafuasi wa chama kimoja tu cha kisiasa au wa kabila moja tu. Baadhi yao walikuwa hata hawahusiki na siasa.

Linalozidisha masikitiko ni kwamba jamaa wa hao waliopotea hawana uhakika wa majaaliwa yao. Hawajui kama watu wao wahai ama wamekufa na kama wamekufa hawajui wamezikwa wapi ili wende kuwapigia fatha na kuwaombea dua maiti wao.

Huu ni uonevu na si haki hata chembe. Waliopotea na waliopotelewa — wote wamedhulumiwa. Wanasononeka na wana dukuduku wanalovirithisha vizazi vyao.

Najua kwamba kuna watakaoona kwamba huu si wakati wa kuyakumbusha mambo haya hasa kwa vile Wazanzibari wameshughulika kuulea umoja wao mchanga uliopatikana baada ya miaka ya uhasama miongoni mwa jamii, uhasama ambao licha ya kurudisha nyuma maendeleo baadhi ya nyakati ulisababisha vifo vya raia.

Wenye kufikiri hivyo bila ya shaka wanaona bora Wazanzibari waachiwe waufaidi umoja wao mpya badala ya kuyafufua maovu ya kale ambayo ndiyo yaliyoigawa jamii na kuuzusha huo uhasama. Wanaona kwamba kuyafufua yaliyopita ni kuzusha fitna katika jamii na kwamba bora mambo hayo yafunikwe kombe mwanaharamu apite.

Hawa ndio wale wenye kusema kwamba ala kuli hali waliopotea ndo wamepotea hawawezi tena kurejeshwa.

Umuhimu wa historia, wa kujikumbusha yaliyopita ni kujua tulikotoka tukafika hapa tulipo na jinsi ya kujiepusha kurejelea kuyatenda makosa yaliopita.

Kwa nia hiyo, ninaamini kwamba serikali ina jukumu la kukiri kosa la mauaji ya kisiasa yaliyotokea chini ya serikali ya awamu ya kwanza na kwa kiwango fulani pia chini ya serikali ya awamu ya pili.

Serikali zilizopevuka na zenye kujiamini huwa zinayakiri makosa kama hayo. Huwataka radhi, na wakati mwingine huwalipa hata na fidia, jamaa wa waliopotea. Huona kuwa heri ije baa hiyo ili iondoke baa kubwa ya fitna itayoselelea katika nyoyo za waliopotezewa walio wao, fitna ambayo huenda ikaudhoufisha na kuusambaratisha Umoja wa Kitaifa ambao Wazanzibari wanauona kuwa ni adhimu.

Hivyo ninaamini kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ili kuuimarisha huo umoja, ina dhima na jukumu la kufikiria mkakati na utaratibu utakaolishughulikia suala hili nyeti na ambalo, ninakiri, kulifunga daftari lake kwa njia ambayo itawaridhisha waathirika wote huenda ikawa si kazi rahisi.

________________________________________Makala ya Ahmed Rajab katika gazeti la Raia Mwema la 6 Julai 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.