Watalii 'wakioga' jua kwenye fukwe za Zanzibar

PWANIMCHANGANI imegeuka gharika. Tangu pale wanakijiji walipoteketeza mabanda ya biashara ya wajasiriamali kutoka Tanzania Bara, polisi wamepiga kambi na kukamatakamata watu. Hakuna kiongozi wa polisi anayekubali kusema watu wangapi wameshakamatwa, lakini taarifa zilizonifikia kutoka kijijini na kwa walinzi wa mazingira na haki za binadamu, zinasema “ni wengi.”

Wanasema askari anagonga mlango wa nyumba yako, wanachukua anayetoka. Bali wanaotakiwa hasa ni wanaume.

Zinakuja taarifa kumbe siku moja kabla, wanakijiji kupitia mkutano na viongozi wao, walijadili kwa kina mashakil (matatizo makubwa) yanayoletwa na wajasiriamali na kupitisha azimio la kuteketeza mabanda.

Wanakijiji wa Pwanimchangani wamekuwa wakilalamika muda mrefu kuhusu vitendo viovu vinavyofanywa na wahamiaji wanaofurika maeneo ambayo moja ya biashara yao kubwa, ni ulevi – baba wa maasi.

Wanywaji wakishautwika, kinachofuata ni muziki wa sauti kubwa, kelele na vituko ambavyo ni kero kijijini. Athari za vitendo hivyo zinatua kwa watoto na jamii kwa jumla.

Yote hayo ni mambo mageni kwa kijiji hiki na vile vya jirani. Ni kero kwa ukanda mzima wa kaskazini mashariki kama ilivyo kwa kusini mashariki mwa kisiwa cha Unguja.

Ulevi, kelele na vituko si katika utamaduni wao. Katika nchi inayoheshimu maadili na silka za wananchi wenyeji, vitendo kama hivi vingekwishadhibitiwa zamani.

Hakuna wa kuvidhibiti isipokuwa wananchi wenyewe kwa utaratibu; lakini viongozi wa kiserikali ndio wenye dhamana ya kulinda mila na desturi za watu.

Kwani Zanzibar haina viongozi? Mbona wapo wengi na katika kila ngazi. Yupo rais, yupo waziri anayehusika na ulinzi wa haki za kiraia, wapo mawaziri wanaosimamia ustawi wa jamii, mazingira, biashara na utalii.

Wapo wakuu wa mikoa/wilaya. Wapo masheha.

Nilipozuru vijiji vya mwambao wa bahari ya Hindi – (2003 na 2005) – nilielezwa tatizo kubwa la kutowajibika kwa viongozi wa serikali katika kutatua matatizo ya wananchi tangu sekta ya utalii ilipoanza kushamiri.

Nilielezwa suala la wajasiriamali kuvamia maeneo ya ardhi na kuyashikilia. Kelele za wananchi kutaka waachiwe maeneo yao zimepuuzwa kwa majibu mepesi.

“Kila mtu ana haki ya kuishi atakapo katika Jamhuri ya Muungano.” Kama anaishi kisheria haihusu.

Uporaji wa ardhi katika ukanda huu ni tatizo kubwa. Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamehodhi maeneo yanayotumiwa na wananchi kwa kilimo. Baadhi yao waliuza maeneo hayo kwa fedha nyingi – Nungwi na Kidoti ni mfano tu.

Ni pamoja na maeneo haya kumejengwa holela. Hata miundombinu ya huduma nyinginezo ilijengwa kinyemela. Hapana shaka hakuna ulipaji kodi. Wajasiriamali wanafanya kazi kama vile wapo msituni.

Zanzibar imekuwa na tatizo la siku nyingi la siasa kutawala kila nyanja. Tangu uchaguzi wa 1995, viongozi wa CCM walibuni mpango wa kuvuruga uchaguzi kwa kushirikisha wasiokuwa Wazanzibari. Wameutekeleza vizuri.

Kupitia mgongo wa serikali walifadhili vijana walalahoi katika wilaya za Dar es Salaam pamoja na Bagamoyo na Mkuranga na kuwapeleka Zanzibar wakati wa uandikishaji wapiga kura na wakati wa upigaji kura.

Mpigapicha mmoja aliyestaafu aliwahi kutamka hadharani aliponyimwa ajira ya mkataba, kuwa viongozi wa CCM wamesahau alisaidia kufanikisha ushindi 1995 na 2000. Alidai kupelekwa Mkuranga akifuatana na mpigapicha kijana kupiga picha vijana waliokuja kuingizwa kwenye daftari la wapiga kura.

Baadhi ya wale waliorudi – maana wapo waliogoma kwa kuhofia kupigwa na wenyeji – na kupiga kura wakati wa uchaguzi, waligoma kuondoka kwa kusema: “Ni zamu yetu kutafuta maisha kama wao wameshapata walichotaka.”
Wengi wa waliobaki, walipelekwa vijijini ya mkoa wa Kaskazini Unguja.

Watu wanakumbuka namna wanawake waliotoka mkoa wa Tanga walivyohanikiza kijini cha Nungwi hata kusababisha wanawake wenyeji kuandamana hadi kwa mkuu wa wilaya wakitaka lazima wanawake hao wageni wafukuzwe kwani “walikuwa wanachochea zinaa kwa kuwalaghai waume zao.”

Walilalamika kuwa waume zao, hasa vijana, waliokuwa wakivua, wamekuwa wakitoroka familia zao na kutumia fedha zote kufuga vimada waliofungua makazi yao maeneo ya ufukweni.

Katika kujibu malalamiko, wanawake wa Kitanga walisema: “Sisi tunaishi hapahapa na kama wanaume wanajiachia kwetu hatuwezi kuwanyima. Tunawapa huduma ambazo wanazikosa kwa wake zao.”

Ni hapa kuliibuka misamiati ya kuonyesha namna gani mapenzi ya wanawake hao yalivyowazingua wanaume wa Nungwi hata kusahau familia zao. Leo ukienda masoko ya Mkokotoni na Kinyasini, utakuta wachuuzi wengi wa bidhaa ni wanawake waliotoka nje ya Zanzibar.

Nataka ieleweke kwamba wanaoitwa wajasiriamali waliingia kinyemela. Walitwaa ardhi. Walijenga mabanda. Wanaishi bila ya kufuata taratibu.

Viongozi wa serikali, zilizopita na iliyopo, pamoja na CCM, wanalijua hili chini juu.

Kwa mfano, Samia Suluhu Hassan, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania (Muungano), alipokuwa anasimamia wizara ya biashara, utalii na uwekezaji, aliwahi kuendesha operesheni ya kuvunja makazi holela.

Alilaumu viongozi wa maeneo hasa mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kukaribisha wahamiaji kinymela. Mbele ya wananchi katika moja ya mikutano yake, alisema: “Nyinyi ndio mliwakaribisha, mkaidhinisha wapatiwe kitambulisho cha Mzanzibari…. mnalalamika nini.”

Bali inajulikana dhahiri masheha hawakuwa na ubavu. Mara nyingi wakisema wanatekeleza amri za wakubwa.

Samia alifanya ziara maalum kufuatilia malalamiko ya wenye hoteli za kitalii kwamba makazi holela pembeni mwa hoteli, yanaharibu mandhari. Watalii waliyalalamikia na kutishia kutotembelea Zanzibar.

Uliokuwa mtaji wa kisiasa, umekuwa kero ya kisiasa. Hii ni changamoto mojawapo ya waziri mpya, Nassor Ahmed Mazrui, anayetoka Chama cha Wananchi (CUF), chama mlalamikaji mkuu wa ufisadi katika siasa.

Hakuna ubaya kwa Mtanzania kutafuta maisha popote anapotaka, lakini je aweza kufanya hivyo kinyemela? Atoke Makunduchi, Bambi au Nungwi, akavamie eneo Kigamboni na kujenga? Ataachiwa?

Wazanzibari wengi wamelewea Bara. Wamevamia ardhi? Wameanzisha maduka bila leseni? Hawalipi kodi? Niulize haya kwa sababu wapo wanaoamini unyama ule umefanywa kwa sababu wahusika ni watu kutoka Bara.

Nasema njia iliyotumika kudhibiti kero ni mbaya na ni uvunjaji sheria. Utaratibu ni kitu muhimu kufuatwa.

Sasa Pwanimchangani kumejaa hofu. Mwandishi mwandamizi Ally Saleh aliyefika kijijini wiki iliyopita, alielezwa na familia za wanaoshikiliwa na dola kwa kesi ya tukio hilo, kuwa wanaumia.

Ni wanaume saba tu walioshikwa. Nyumbani wameacha wanawake kadhaa na watoto 24, wakiwemo wanaosoma, hawana msaada. Vijiji hivi vya pwani vina umasikini mkubwa licha ya kuzungukwa na maliasili nono.

Hawana msaada tofauti na wale walioathirika ambao wanasaidiwa na taasisi na hata serikali.

Wenyeji wanajiona kama “wanaharamu” kwa wanavyofanyiwa ndani ya eneo lao. Wanasikitika kutengwa na mbunge wao, Kheri Khatib, na Mwakilishi wao, Abdi Mossi, ambao hawajaonekana kijijini tangu tukio ingwa wamesaidia gharama za wakili.


Makala ya Jabir Idrissa katika gazeti la MwanaHALISI la tarehe 25 Mei 2011

3 thoughts on “Ya Pwani Mchangani ni matokeo tu – 2”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.