Mtalii katika fukwe za Nungwi, Kaskazini ya kisiwa cha Unguja

WATANZANIA kadhaa wanaotoka Bara wamepoteza makazi na biashara. Makazi na biashara zimeteketezwa moto na waharibifu. Wamerudishwa nyuma hatua nyingi. Wanahitaji kusaidiwa. Hakuna anayepata maumivu makubwa kama wao. Wapo wanaofurahia kilichowakumba. Naapa wapo. Tena wengi wakiwemo wenyeji wa maeneo yale.

Wapo watu wamechukia mwisho wa kuchukia. Kwa bahati mbaya, baadhi yao wamechukia kwa kuzugwa na hisia za kisiasa, ubaguzi na hususan, kwa kuhusianisha tukio na muungano kati ya Watanzania watokao Bara na Wazanzibari.

Waathirika wenyewe wamechukia sana na kwa bahati mbaya, napata picha kuwa nao wanaamini ni siasa na ubaguzi kwa kuwa wanatoka Bara.

Nina sababu nzuri ya kuazimia kusafisha hewa hii chafu kwani ninaelewa vizuri matatizo yaliyopo kwenye maeneo wanayoishi na kutafuta riziki.

Katika risala yao kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyefika haraka eneo la tukio ili kukagua uharibifu na kuonana na waathirika, walimpa salamu nzito.

Walimwambia wanawajua waliochoma mali zao ila wamesita tu kuwadhibiti kwa kuamini serikali itawadhibiti. Wakatisha, “tunataka serikali iwakamate wahusika wote na kuwapeleka mahakamani katika wiki moja, kabla hatujaamua kulipiza kisasi.”

Balozi Seif aliwatuliza hasira kwa kuwahakikishia kuwa serikali itafuatilia wahusika na kuwakamata kitaratibu ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Eneo lililoathirika lipo ndani ya Ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Unguja unaotambaa mwambao wa Bahari ya Hindi, hadi kusini mashariki mwa kisiwa.

Ni ukanda maarufu kwa shughuli za utalii zilizochipuka sana miaka ya 1990 baada ya serikali kutaka sekta ya utalii ikuzwe na kuchukua nafasi katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Serikali ilileta sera hiyo katika jitihada zake za kufufua uchumi uliokuwa umedhoofu kwa kiwango kikubwa baada ya karafuu, zao maarufu lililokuwa likitegemewa, kupoteza nafasi ya kuwa zao kiongozi la biashara. Hiyo ilitokana na kuanguka kwa bei yake katika soko la dunia.

Ukanda huu unajumuisha vijiji vya Kizimkazi, Mtende, Makunduchi, Jambiani, Paje, Bwejuu, Michamvi, Uroa, Pongwe (Kusini), Kiwengwa, Pwanimchangani, Matemwe na Nungwi (Kaskazini).

Kwenye vijiji hivi, vingine vikiwa vinafungamana na vijisiwa vinavyotumika kwa shughuli za uvuvi, kuna hoteli kubwa za mtindo wa vijiji zilizojengwa kwenye fukwe nyeupe na bikira katika mandhari tulivu yanayoleta picha mwanana inayovutia watalii.

Ukiangalia kwa mtizamo finyu, unaweza kusema ni kweli tukio hilo ni matokeo ya chuki za kisiasa au ubaguzi wa kimuungano.

Vizuri uchimbue. Jipe muda upite maeneo haya; uyaone yalivyo chini juu, nje ndani; jadili na wenyeji na viongozi wao. Uliza asasi binafsi. Waulize viongozi wa taasisi na idara za kiserikali. Kila upande una mengi ya kuyasema.

Naringa nilipita maeneo haya kati ya mwaka 2003 na 2005. Nikazungumza na wananchi ambao ni mazao ya mabibi na mababu walioishi kwa zama na dahari.

Shughuli zao kuu ni uvuvi, kwa kuwa ni maeneo ya kando na bahari, na kilimo cha juu kwa kujaaliwa ardhi nzuri – japo sehemu yingine ni mawe na uwanda – kwa mazao ya chakula na biashara.

Lipo tatizo kubwa la uhusiano mbaya wa wawekezaji wa sekta ya utalii na wenyeji. (Waathirika si wawekezaji bali wajasiriamali kwa lugha ya leo. Wamejichomeka humo. Nitaeleza kwa undani hili).

Kihistoria wenyeji katika maeneo haya ni waumini wakubwa wa dini ya Kiislam. Wapo waliotokana na familia zilizotajika tangu kale kushiba elimu ya dini hii. Wengine walipata malezi katika msingi huo zaidi kuliko elimu dunia.

Ndiyo kusema katika maeneo haya, watu wazima, vijana wa sasa ni waumini makini wa Uislam. Imani hizo wanazikomaza kwa watoto wao.

Maisha ya jamii hizi yanajulikana yalivyo ya kihafidhina hasa panapokuja watu wapya kutaka kupenyeza utamaduni mgeni ukiwemo wa dini nyingine.

Ukifika maeneo haya, wakati wa sala wote wanakimbilia misikitini kusali; asubuhi mapema na magharibi wote (wanaume) hukusanyika vijiwe vya kahawa kwa ajili ya kuamkiana na kusimuliana yahusuyo maisha yao. Huarifiana ya kupwa na ya kujaa kuhusu miji yao, nchi yao na dunia yote.

Watoto wasiokwenda shule asubuhi au mchana hushinda madrasa kusoma Kur’an na mafundisho mbalimbali ya Kiislam. Lakini nao wakati wa sala hujumuika misikitini na wakubwa zao kusali.

Katika maeneo haya, shughuli zinazokutanisha wakaazi na wakaazi wa vijiji vingine vya jirani au kutoka maeneo ya mbali ni maziko, harusi, maulid na dhikri. Hakuna muziki humu. Hakuna ulevi. Hakuna ngoma nje ya mikusanyiko hiyo.

Msiojua mjue katika maeneo haya, kiasili, huwezi kusikia harufu ya bangi wala ulevi. Kabla ya utalii kuvuta kila mtu, hukukuwa na mvuta bangi; mtu ambaye kidogo alivumiliwa ni mvuta sigara. Basi.

Wakati ule, huwezi kuona mwanamke amevaa katika namna ambayo unaona sehemu yoyote ya mwili wake zaidi ya vidole vya miguu, uso na viganja vya mikono.

Hata watalii waliotembea mitaani, waliheshimu mila na silka hizi. Walielekezwa na wenye hoteli na waongozaji wao mavazi muafaka wanapotaka kuzunguka mitaani.

Miaka ya 1960, ilikuwa ni marufuku mtalii mwanamme kuvaa pensi (suruali kipande). Wanawake wakilazimika kujitanda khanga juu na kuvaa gauni refu kupita magoti.

Ulevi haukutoka nje ya eneo la stoo. Wanywaji wakihesabika, tena kwa leseni ya serikali. Maduka ya ulevi yalikuwa ya kuhesabu katika mjimkongwe. Asiye leseni alipotamani ulevi, alilazimika kupanga na mwenye nayo.

Ilikuwa ni marufuku mtalii – na mtu yeyote – kukutwa amelewa mchana, hususan siku za mwezi wa Ramadhan. Au kukuta mtu anakula mchana ndani ya mwezi huu.

Mikahawa yote ilifungwa mchana mpaka ifike magharibi watu wanapoenda kusali na kufungua. Hayo ni katika mji, fikiria vijijini ilikuaje?

Hata utalii ulipoimarika miaka ya 1990, ukiheshimu mila za watu wa Zanzibar kwa miaka mingi ya historia ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Kuenea kwa watu waliojichomeka kwenye maeneo ya ukanda wa kaskazini na kusini mashariki kumebadilisha desturi hizi, mila hizi, imani hizi. Siku hizi kila kitu kinakwenda shaghalabaghala.

Leo, muziki unapigwa bila ya kusita tangu magharibi mpaka asubuhi kweupe. Mara kadhaa nishakuta muziki unanguruma mchana. Na muziki wa kizazi cha leo ulivyo mzito kutokana na teknolojia, usiombe kusikia.

Watalii wanatembea uchi – nasema uchi siyo nusu uchi. Watu waliojichomeka wanalewa mchana kweupe. Kutwa nzima ukipita maeneo ya ufukweni unakuta vikao vya walevi vipo kazini.

Tena watalii wanapita mitaani bukheri khamsa ishirini (bila ya hofu yoyote). Watalii wanadengua na wapenzi wao – wengine vijana wa ki Afrika – wakiwa wameshikana viuno na kunyonyana ndimi hadharani.

Huu ni utamaduni mpya kwa miji na uovu ifikiapo kwa wenyeji wa ukanda huu, niliokwishasema ni wahafidhina sana wa mila, desturi na imani zao.

Hata siku moja hawawezi kuvumilia kuona watoto wao wanajifunza mambo hayo. Ndio maana waliomba serikali idhibiti machafu haya.

Kuna suala la uhalali wa wajasiriamali hao kuwepo walipo. Ni tatizo la muda mrefu wananchi wamelalamika kuporwa ardhi waliyokuwa wakitumia kwa shughuli za kilimo. Serikali ni nzito kushughulikia haya.

Siyo tu nzito, ukweli imeendekeza siasa kulea desturi mbaya na gharama zinazidia wenyeji. Wanahasira. Sifurahii kilichotendeka, hapana. Najadili chimbuko. Kwamba wapi kulikosewa na haya ni madhara.

Itaendelea.

________________________________________________________________Makala ya Jabir Idrissa katika gazeti la MwanaHALISI la tarehe 18 Mei 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.