Picha iliyochorwa mwaka 1886 kuonesha Zanzibar ya wakati huo

KUTELEZA si kuanguka na hivyo ingawa Zanzibar imekuwa ikiteleza kwa muda wa karibu nusu karne bado inaweza kuwa na nguvu za kusimama wima tena. Nguvu hizo itaweza kuzipata endapo tu itaubadili mfumo wa mahusiano yake ya kibiashara na mataifa mingine. Nadhani sikosei nisemapo kwamba maelezo ya mwanzo ya kina yanayoihusisha Zanzibar na uchumi wa kimataifa yaliandikwa na Wayunani, Wagiriki wa kale, kwenye kitabu kiitwacho ‘A Periplus Of The Erythraean Sea’. Labda tunaweza kulitafsiri jina la kitabu hicho kuwa na maana ya ‘Maelezo ya Bahari Kuu ya Hindi’.

Wayunani walikiandika kitabu hicho kama miaka 1,900 iliyopita wakitoa maelezo ya njia kuu za misafara ya kibiashara pamoja na bandari kuu za zama hizo.

Ukiyasoma maelezo hayo utatambua jinsi Zanzibar tangu zama za zama ilivyokuwa taifa la wafanya biashara na jinsi biashara ilivyokuwa ikiranda katika damu za watu wake.

Historia ya karne chache tu zilizopita inatukumbusha kuwa Visiwa hivyo vilisimama juu ya misingi ya biashara huru, ushuru mdogo wa forodha pamoja na kodi nyingine ndogo.

Visiwa hivyo pia vimesimama juu ya misingi ya mfumo thabiti na imara wa shughuli za fedha pamoja na hatua za kuwa na uchumi huru, hali ambayo ilistawisha biashara huru ya bidhaa na huduma.

Hivyo, kutokana na tajriba hiyo utaona kwamba uchumi wa maeneo huru si mgeni kwa Zanzibar. Si tukio jipya. Si shani wala si kioja.

Kwa hakika, bandari huru na sera za uchumi zitegemeazo maeneo huru ya kiuchumi na biashara huru si mizungu mipya kwingi kwingine duniani. Sera aina hizo zimekuwa zikitumika kwa miaka kama chombo cha kuvutia uwekezaji na rasilmali kutoka nje.

Sera hizo zimekuwa pia zikitumika kuwapatia watu ajira, kupatia mapato zaidi ya sarafu za kigeni na kuharakisha kupatikana kwa teknolojia na kuendeleza miundombinu.

Hoja kuu inayotumika kuitetea sera ya eneo huru la kiuchumi ni hii: kwamba kuifanya biashara iwe huru kunastawisha uzalishaji mali na kunalifanya soko liwe na uneemevu na ghanima kutokana na utendaji bora wa shughuli za kiuchumi.

Yote hayo yanazaa kupatikana kwa manufaa na bidhaa za ziada katika masoko ya dunia. Ziada hiyo nayo inamotisha ustawi wa kiuchumi na maendeleo.

Ili Zanzibar iweze kuwa na uchumi wa maeneo huru Serikali ya Umoja wa Kitaifa itabidi ikate uamuzi wa kuzibirua juu chini zile sera za kiuchumi zilizokuwa zikifuatwa na serikali za awamu zilizopita tangu Mapinduzi ya mwaka 1964.

Badala yake serikali hiyo itapaswa kuzikumbatia sera za kiuchumi zenye lengo la kutilia nguvu harakati za kiuchumi ndani ya Zanzibar na nje yake.

Dhamira iwe ni kuwavutia wafanyabiashara binafsi na taasisi za kibiashara zenye nia ya kufanya biashara katika Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kati na Kusini mwa Afrika ziifanye Zanzibar kuwa ni kituo cha shughuli na harakati zao za kibiashara.

Zanzibar itaweza tu kufanya hivyo pale itapowapa wafanya biashara hao na taasisi za kibiashara vivutio kama, kwa mfano, kulegezwa kwa vima vya riba, kuwapa wawekezaji vipindi virefu vya kusamehe ulipaji wa kodi, kulegeza masharti ya uwekezaji kutoka nje, kubinafsishisha mashirika ya serikali na kuwa na usimamizi madhubuti wa shughuli zinazohusika na mambo ya sarafu.

Ili wananchi wa kawaida waweze kunufaika itaijuzu serikali iwe macho kila saa na iwe na mikakati ya kupambana na mfumuko wa bei na mapato.

Sera ya kiuchumi ya serikali kuhusu masoko na sekta ya wafanyabiashara wa kibinafsi lazima itungwe kwa kuzingatia matilaba ya kimsingi ya kitaifa na si kwa kuzingatia mielekeo ya itikadi za kisiasa.

Hiyo si kazi ndogo. Nasema hivi kwa sababu kuna mambo yanayohitaji kutekelezwa ili sera hizo za kiuchumi zifanikiwe. Kwa mfano, patahitajika pawepo na mwambatano na uratibu wa sehemu zote za sera na mkakati wa kiuchumi.

Lengo lisiwe tu kuondosha ushuru na vizingiti vingine vya kibiashara, lakini pia liwe ni kuweka kanuni na taasisi za usimamizi za hali ya juu kimataifa.

Zanzibar itapojiunga na Uchumi wa Dunia si peke yake itayonufaika. Eneo zima la Afrika ya Mashariki na ya Kati, hasa Tanzania Bara, litachuma matunda ya ufanisi huo kwani kutaongezeka biashara na uwekezaji wa mashirika na taasisi za kimataifa zitazoweza kujipenyeza kwa urahisi katika masoko ya maeneo hayo kwa kuifanya Zanzibar iwe ni kituo chao cha kibiashara.

Uundwaji wa sekta ya kutoa huduma, muongezeko wa biashara na mfumo imara wa shughuli za benki na hazina ya serikali ni mambo ambayo yatawawezesha pia wateja kutoka Bara wapate huduma ambazo hadi sasa wanazipata wanaposafiri kwenda nchi za Magharibi, Mashariki ya Kati ama Singapore.

Mchakato wa kuigeuza Zanzibar na kuifanya iwe Singapore ya Afrika ya Mashariki utahitaji mashirikiano makubwa si tu baina ya sehemu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia utahitaji ushirikiano wa kiwango fulani wa eneo zima la Afrika ya Mashariki na ya Kati, na hasa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Taasisi na jumuiya za kimataifa pia zitahusika na mchakato huo.

Zanzibar inaweza kujifunza mengi kutokana na tajriba na uzoefu wa nchi nyingine zilizopata mafanikio kwa kufuata sera za uchumi wa maeneo huru. Mfano mzuri ni Mauritius.

Mauritius ilipopata uhuru mwaka 1968 ilikuwa ikitegemea zao moja tu, miwa, na mahuruji ya sukari. Sukari ikiipatia Mauritius zaidi ya asilimia 95 ya mapato ya mauzo ya bidhaa zake nje; vilevile zao hilo la miwa na viwanda vya sukari viliwapatia ajira zaidi ya nusu ya wafanya kazi wake.

Serikali ya Mauritius ikatanabahi harakaharaka kwamba uzalishaji wa sukari pekee hautoutosheleza uchumi wake. Hivyo, ikaamua kuugeuza uchumi wa kisiwa hicho na kuufanya uwe wa kusafirisha bidhaa za viwandani na kuvutia uwekezaji kutoka nje.

Mwaka 1971 ikatenga eneo maalumu la kutengenezea bidhaa za viwandani na ikatoa vichocheo mbalimbali vya kuvutia uwekezaji katika sekta ya utalii.

Hatua hizo ziliifanya Mauritius ipate ustawi wa haraka katika utalii na uzalishaji wa bidhaa viwandani.

Katika mwaka 1988, Sheria ya Benki ilifanyiwa marekebisho kuwaruhusu wateja walio wakaazi wa nje ya nchi hiyo waweze kuweka akiba zao katika benki zilizo Mauritius.

Mwaka mmoja baadaye serikali ya huko ikaanzisha Soko la Hisa na mwaka 1992 bandari huru ikaanzishwa rasmi Mauritius.

Kwa kuendelea kufuata sera ya kiuchumi inayozidi kuvutia uwekezaji, Mauritius imeweza kuyavutia makampuni ya nchi za kigeni yanayozidi 9,000. Mengi ya makampuni na mashirika hayo yanafanya biashara na India na Afrika ya Kusini.

Mauritius hali kadhalika ilipata rasilimali katika shughuli za benki pekee zinazozidi dola za Marekani bilioni moja.

Mauritius imeweza kupata yote hayo ikiwa ina utaratibu imara wa kusimamia shughuli za hazina ya serikali. Kwa kufuata sera hizo kila mwaka uchumi wake umekuwa ukikua kwa asilimia 5 na tangu mwaka 2001 kima cha kubadilishia sarafu za rupee za Mauritius kwa dola ya Marekani kimebakia kuwa kile kile cha baina ya rupee 29 na 31 kwa dola moja.

Tukiiangalia sarafu ya shilingi ya Tanzania tunaona mengine. Thamani ya sarafu hiyo imeanguka kutoka shilingi 950 kwa dola katika mwaka 2002 kufikia shilingi 1,550 kwa dola moja hii leo.

Hii leo Mauritius ni kituo muhimu cha kimataifa kinachotoa huduma za fedha na za kibiashara katika mambo ya benki, ya bima, ya teknolojia na utalii. Iko sawa na Singapore, Hong Kong, Bahamas, Visiwa vya Cayman, Visiwa vya Virgin na vinginevyo.

Nchi zote hizo nilizozitaja kama Zanzibar ni visiwa na Zanzibar inaweza kuwa mlango wa kuingilia nchi nyingine zenye uwezekano wa kuwa na utajiri mkubwa kama vile Tanzania Bara, Kenya, nchi za eneo la Maziwa Makuu na za Kusini mwa Afrika.

Ikiwa hapatochukuliwa hatua za haraka za kuleta mageuzi katika sera za kiuchumi basi kuna sekta fulani, kama vile ile ya biashara ya karafuu, ambazo zaweza kutoweka. Ikiwa patakosekana uwekezaji wa kibinafsi katika biashara hiyo basi biashara hiyo itaendelea kufifia na kutotoma.

Kama tulivyogusia katika sahafu hii kabla, tutaweza tu kuyapima mafanikio ya sera mpya za kiuchumi za Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Waziri wake wa Fedha kwa kuangalia namna zitavyomuathiri Mzanzibari wa kawaida.

Tutaiona serikali hiyo kuwa imeshindwa katika kazi zake ikiwa ukuaji wa uchumi tunaoutaraji hautokuwa na uwiano na upunguzwaji wa ufukara na ikiwa wananchi wa kawaida hawatopata ufanisi.

Kuifanya Zanzibar iwe na uchumi wa eneo huru kutachochea ukuaji haraka wa uchumi na kutairejesha Zanzibar kwenye ramani ya dunia. Hatua zote hizo lakini zitaangukia patupu endapo wananchi bado wataendelea kuwa na usumbufu wa maisha.

Sharti hizo sera mpya za kiuchumi ziifanye Zanzibar irejee kuwa nchi ya neema na ufanisi. La sivyo, basi hapatokuwa na la kufanya ila kuendelea nayo tuliyoyazoea kwa muda wa nusu karne na kuufanya ufukara uzidi kushtadi.


Makala ya Ahmed Rajab katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 25 Mei 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.