Muasisi wa Muungano, Julius Kambarage Nyerere

Hakuna woga katika kulizungumza suala la kuvunja Muungano. Liliopo ni kulizungumza kwa kutumia hikma kwa maana ya kila kitu tukiweke mahala pake. Ni muhimu kufikiria na kuyapanga mambo kwa kutumia busara na kuona mbali. Nakubali kuwa neno ”Muungano” kwa Wazanzibari wengi limeshakuwa na dosari kubwa kutokana na historia ya ukandamizaji na mabavu yaliofanywa kwanza na utawala wa Tanganyika, na baadae Tanzania Bara, juu ya Zanzibar.

Kwa maana hiyo ipo haja ya Zanzibar na Tanganyika kurudi kama zilivokuwa kabla ya tarehe 26 Aprili 1964. Hiyo nini maana yake? Hapo ndipo penye dhana ya nchi mbili na Serikali mbili zilizoungana. Mbili. Moja, nchi ya Zanzibar, ya pili, Tanganyika. Mimi huko sikuoni ni kuvunja Muungano. Huko ni kuzirejesha nchi mbili katika hali ya usawa ili ziweze kuhishimiana.

Fikra ya kuzaliwa tena Tanganyika haikhusiani hata kidogo na kutatua kero za Muungano, au kuyapunguza mambo yalioingizwa kisheria au kinyemela ndani ya Khati za Muungano au Katiba ya Muungano. Ni kuanza upya alifu na ujiti.

Kuzaliwa tena kwa Tanganyika hakuna maana ya kuwarudisha tena Watanganyika wawe na ”domination” ndani ya Serikali ya Muungano. Muungano wa miaka 47 iliopita ni dalili tosha kuwa haufai kwa sababu moja tu: utawala wa Tanganyika na wa Tanzania Bara kwa takriban nusu karne iliopita, wametumia nguvu zao za Kidola, kukimbilia Umoja, au kile walichokiona wao kuwa ni Muungano, kwa kutumia ujanja, uwongo, unafik, uonevu, unyanyasaji, ubaguzi, fitina, dhidi ya Zanzibar na baina ya Wazanzibari.

Ikiwa kuirudisha Tanganyika ni kuendeleza sifa za mifarakano kwa kutumia neno la ”Muungano” basi itakuwa ni kubadilisha majina tu na kuendeleza unyanyasaji wa Zanzibar. Zanzibar irudi na iwe na sifa zake zote za Kitaifa na za Kimatiafa, na Tanganyika pia irudi iwe na sifa zake zote za Kitaifa na za Kimataifa, na zitizamane kama ni nchi mbili zilizo sawasawa.

Narudia. Sifa ya kwanza ni nchi mbili zilizo huru zirudi katika sifa zake kama ni nchi mbili zilizo sawa sawa. Hakuna mdogo, hakuna mkubwa. Hakuna jogoo, hakuna kuku mke. Hakuna chura, hakuna tembo.

Kwa mantiki hiyo ule ”Muungano” wa miaka 47 iliopita haufai na usiwepo tena. Kama huko ni kuuvunja na uvunjwe kwa sababu Muungano huo haurekebishiki kwa sababu misingi yake ni mibovu kwa kuwa imetokana na khadaa, ujanja, na udhalilishaji mwingi. Muungano wenye kuendeshwa na sifa mbaya ni Muungano wa Kiibilisi na si wa viumbe wenye nia nzuri na kuwatakia jirani yao na kizazi chao kheri.

Zanzibar nje ya Muungano inawezekana lakini Zanzibar nje ya mashirikiano ya ujirani mwema na Tanganyika ni khasama na vita visivokwisha. Kwanza, bila ya kuwepo mfumo mpya wa mashirikiano baina ya nchi mbili zilizo huru, basi daima kutakuwepo na uongozi Tanganyika ambao utajilaumu na utalaumu ”kwanini tumewaachia Wazanzibari watoke ndani ya Muungano?”

Na hilo litakuja kwa nguvu kubwa zaidi khasa pale Zanzibar itakapoenyesha kasi kubwa ya maendeleo na Tanganyika itakapoendelea kudorora, kutofahamiana wenyewe kwa wenyewe, na kukosa dira ya wapi wanataka kwenda na kwenye faida kwa wananchi walio wengi.

Na ndio maana nikasema, na nitaendelea kusema, kuwa lazima uwepo mfumo mpya wa ”Muungano” au tuyaite ”Mashirikiano” baina ya Zanzibar na Tanganyika ili kupunguza majadiliano makubwa ambayo yanaweza kugeuka na kuwa ugomvi mkubwa baina nchi mbili jirani na baina ya wananchi wake. Lazima tujilinde na hilo.

Nchi za Ulaya zimeishi kwenye ukhasama na vita vya inafika miaka elfu moja na mamilioni ya roho za watu wao na mali kupotea. Hivi sasa wamesikilizana na hakuna matatizo ya mipaka au kurushiana risasi baina yao.

Lakini Wazungu hao hao mpaka hii leo wanaamini kuwa historia ya jana ya Europe ndio historia ya kesho ya nchi za Kiafrika na nyenginezo zenye kuendelea. Wanataka lazima tuuwane kwanza kabla ya kupatana na kuungana. Wasomi na viongozi wetu wamebebwa na mtazamo huo kwa hishma tulionayo kwa Mzungu hata akiwa wa karata.

Nchi za Ulaya zilianza kuheshimiana baada ya vita vya pili vya dunia na walipoanza na msingi na mtazamo wa kuheshimiana, ndipo walipoweza kuvuna matunda makubwa ya utulivu na neema ndani ya miaka 50 iliopita, tena khatua kwa khatua, na walisaidiwa sana na Marekani.

Hivi sasa kila nchi inataka kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa sababu zimeshaona kuwa kuna faida kubwa kuwemo ndani ya Jumuiya ya Ulaya. Hata Morocco na Israel wanataka kuwa wanachama! Hakuna hata nchi moja iliotaka kuungana na Muungano wa Tanzania. Hata Rais Kenneth Kaunda wa Zambia ambaye alikuwa karibu sana na Mwalimu Nyerere hakutamani!

Na Wazungu hawakuanza kwa kutaka Shrikisho (Federation). Walianza na ”Confederation”. Na hiyo ndio ilikuwa fikra ya “architect” wa Jumuiya ya Ulaya, Jean Monnet. Na bado mpaka hii leo hawana kiti kimoja cha EU katika Umoja wa Mataifa, lakini Umoja wao unazidi kuwa mkubwa.

Kuhusu ”demokrasia” mimi binafsi si muumini mkubwa wa falsafa hiyo yenye kutoka nchi za Magharibi na khasa Marekani. Muhimu zaidi kwangu mimi ni Uhuru wa kiuchumi unaomuwezesha binaadamu kuchagua mambo muhimu yanayomtatulia matatizo ya maisha yake ya kila siku.

Chakula, maji, malazi, nguo, ilimu, afya, nk. Kuna faida gani kupiga kura kama siwezi kuwalisha na kuwapa ilimu nzuri watoto wangu na jamaa zangu? Kawaulize Wachina na Warusi watakupa jibu. Ipi ina faida zaidi, demokrasia ya Kimarekani au maendeleo ya kiuchumi?

Zanzibar inao Uhuru wa kuzungumza na hata wa kuandika na khasa huu wa karibuni wa kuzitetea haki za Zanzibar. Tatizo linakuja pale uhuru wa kujieleza, kwa kuzungumza au kuandika unapokuwa umesimama juu ya dhana au upotoshaji. Singapore ina sheria za kuwafungulia mashtaka wanahabari na mashirika yao wenye kusema ovyo bila ya ushahidi wa wanayoyaandika.

Sheria kama hizo zinawafanya hata waandishi wa habari wanaoishi nje ya Singapore kuchukuwa tahadhari kubwa kwa sababu Serikali ya Singapore ikiamua kukushitaki basi huna budi kuyatolea ushahidi ulioyaandika.

Akishindwa kuthibitisha, shirika au mwandishi binafsi alipe gharama tena kubwa. Leo Zanzibar kila siku inapakwa na kupakaziwa kila aina ya uchafu duniani kwenye vijitabu vya kutangaza utalii, ndani ya magaazeti, nk.

Lakini juu ya yote hayo, leo Wazanzibari wamekuwa kitu kimoja. Na ukipeleleza utaona maadui wa Zanzibari, wa ndani, wa jirani, na wa nje, wanakuja na kila uwongo ili waendelee kuwafitinisha Wazanzibari.

Na ndio maana Zanzibar inahitajia kuzidi kuiongezea zege misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Viongozi wachache sana wahafidhina wenye ushawishi mkubwa ndani ya vyama vya siasa wako tayari kuzitumia hali ngumu za maisha ya wananchi kuivuruga SUK ili wajijengee umaarufu wa kisiasa. Haya yatazidi kila tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu tuliorithishwa na Wazungu vikiwemo vyama vya siasa.

Wanasahau, au labda niseme hawajali, kuwa bila ya SUK hakuna muungano baina ya Wazanzibari ndani na nje ya Zanzibar, na bila ya muungano wa Wazanzibari, ni rahisi kuuendeleza Muungano wa Tanzania Bara ambao Wazanzibari hawautaki.

Zanzibar imeshaweka msimamo wake hadharani na bila ya woga wala kiwewe. Muungano uliopo hautakiwi na ukipigiwa Kura ya Maoni leo kabla ua kesho basi Wazanzibari walio wengi wataukataa tena kwa kishindo.

Sasa kazi iko upande wa pili – Tanzania Bara. Utaweza kuchomoza uongozi wenye fikra mpya Tanzania Bara na kukubali kuwa tatizo la Muungano ni lao wao na la upande wao, au wataendelea kuifanya Zanzibar na Wazanzibari ndio tatizo?

Kubwa kuliko lote, ni tatizo la uongozi na viongozi wa Tanzania Bara kutojiona kuwa ndio tatizo au wana tatizo katika suala zima la Muungano. Watakapofika na kujiona kuwa wao ndio tatizo basi tatizo sugu baina ya Zanzibar na Tanganyika litaweza kuondoka mara moja.

Ndio nikasema bila ya Wazanzibari kuwa na mtazamo wa kiujumla wa pamoja basi safari yetu itazidi kuwa refu na wababaishaji watazidi kujipa uhai. Kikombe kikiwa ni cha rangi ya buluu basi ukiyatia maji meupe ndani yake huonekana ni yenye rangi ya buluu.

Wakikataa kujiona kama wao (na vibaraka vyao vilioko Zanzibar ndani ya CCM na CUF) ndio tatizo sugu basi Muungano ambao Wazanzibari hawautaki utavunjika na utawaangukia wenye kuulinda kwa mabavu.

Juu ya yote hayo, Wazanzibari wamezikataa kero za Muungano lakini bado hatuna sauti moja ya muelekeo wa kiujumla wa wapi tunataka kwenda na kwa kuifuata njia ya mfumo upi.

Binafsi naamini ndani ya moyo wangu kuwa njia iliopo na yenye faida kwa Zanzibar na Tanzania Bara, ni moja tu, na hakuna ya pili.

Muungano bora ni ule ambao utakubali kuwa Zanzibar na Tanganyika ni nchi mbili huru zilizo sawa na zenye sifa kamili za Kitaifa na za Kimataifa. Hapo ina maana Muungano huu tulionao haufai. Na ndio maana kuna haja ya kurudi tulikotoka kabla ya tarehe 26 Aprili, 1964.

Kwa kiasi kikubwa, Zanzibar ya leo inajuwa nini inataka na wapi inataka kwenda lakini bado Wazanzibari hawajakubaliana kwa sauti moja juu ya mfumo wa nchi mbili (2) zilizo sawa na zenye Seikali zake mbili (2) kama ilivokuwa kabla ya tarehe 26 Aprili, 1964.

Tatizo litakuja pale Tanzania Bara inapoamua au itakapoamua kubakia ndani ya mfumo ambao umeshapitwa na wakati na dahari.

Na ndipo nilipolinganisha ”approach” ya nchi za Ulaya na Zanzibar na Tanganyika kurudi kama ni nchi mbili huru zilizo sawa na zenye kuhishimiana.

Tusirudishwe kama alivotutahadharisha Profesa Ibrahim Noor, kwenye Zanzibar na Tanganyika itakayokuwa Mikoa.

Sasa hapo ndipo penye hatari mama na tusisahau kuwa tayari rasimu ya Katiba iko tayari ya kuifanya Zanzibar na Tanganyika iwe Mikoa itakayotawaliwa na Magavana!

Tunataka Tanganyika izaliwe ili Zanzibar na Tanganyika ziwe nchi mbili huru zilizo sawa. Na hilo halitofanyika bila ya kuliondoa hili pazia la Serikali ya Muungano lililolivua guo Tanganyika na kuisitiri kwa koti la Muungano.

Ni muhimu tukiondowe hichi kiini macho ili tunapojadiliana isiwe wengine tumekaa upande mmoja wa meza na wengine upande wa pili.

Sote tukae upande mmoja na tuliweke tatizo mbele yetu sote.

Makala ya Dr. Harith Ghassany

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.