Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd

SIAMINI kama Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi anataka mgogoro na wananchi wa Zanzibar. Bado ninaamini kuwa wana imani naye, wanampenda na wanamuunga mkono anapoonesha ujasiri na uthabiti katika kutekeleza majukumu mazito yanayoikabili serikali ya umoja wa kitaifa inayoundwa na vyama viwili vikuu vya CCM na CUF.

Gazeti la Zanzibar Leo, linalochapishwa kila siku na idara ya serikali, limemnukuu Balozi Iddi, akisema kuna wananchi wanaandaa upotoshaji wa makusudi wa fursa ya mjadala wa mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushawishi watu wauchukie muungano ili uvunjike.

Yeye anasema wenye mawazo kuwa ni bora muungano uvunjike ni wachochezi kwani anadai muungano huo ulioasisiwa rasmi tarehe 26 Aprili, 1964, una faida nyingi.

Moja ya faida hizo, anasema, ni ile fursa ya Wazanzibari wengi kuendesha maisha yao Tanzania Bara.

Wiki mbili tu zimepita tangu wananchi walalamike hadharani namna muungano unavyoendeshwa bila ya kuzingatia maslahi ya Zanzibar, na kueleza msimamo wao wa kutaka ije katiba ya Tanganyika kwanza ndipo wajadili mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Walitoa msimamo huo mbele ya viongozi wakuu wa serikali na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wakitoa maoni kuhusu muswada wa sheria ya marejeo/mapitio ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Walisikia kauli za kutoshirikishwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuandaa muswada huo, kama ilivyothibitishwa na mawaziri wawili wa SMZ, mwanasheria mkuu wa serikali na katibu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Kilio chao kikuu ni kutaka muungano endelevu na unaozingatia haki sawa kwa pande zote mbili zilizoungana; vinginevyo uvunjike maana wanaamini, Zanzibar inaburuzwa kwa kuletewa kila kitu kilichoandaliwa na wao kutakiwa tu kutoa maoni wakati ni haki kwao kushirikishwa kuandaa kitu chenyewe.

Sasa wapo tayari uvunjike kama ni lazima uendelee kwa mfumo wa serikali mbili, kwani unaendelea kuinyima Zanzibar mamlaka yake ya kujiamulia mambo yanayohusu maslahi ya wananchi wake na mustakbali wa nchi yao.

Walitaka serikali yao – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoendeshwa kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa– iitishe kura ya maoni kuuliza wananchi kama wanautaka muungano au la.

Pengine Balozi Iddi amekasirika. Ameumia kuhusu maoni hayo. Pengine maoni hayo yameudhi mtawala, ambaye ndiye mteuzi wake. Pengine maelezo yake ni ishara kwamba serikali ya umoja wa kitaifa inagongana kuhusu maoni ya wananchi juu ya muungano huo.

Vyovyote itakavyokuwa, Balozi Iddi ana uchaguzi mmoja tu: Amshauri Rais aliyemteua kwamba kusikiliza kilio na matakwa ya wananchi, hata kama kwa viongozi ni mabaya, ni jambo la muhimu sana katika dhana ya uongozi. Lazima wakubali kwamba haiwezekani rais awe ana akili kubwa zaidi kuliko wananchi anaowaongoza.

Wananchi wanasema muungano uvunjike kwa sababu hauwasaidii kiuchumi tofauti na ule wa Ulaya. Kwa miaka yote 47 muungano umeishi na matatizo. Kila upande una manung’uniko na hakuna ufumbuzi wa maana.

Hali imeendelea hivyo licha ya kamati mbalimbali kuundwa ili kushughulikia matatizo. Ripoti zimetolewa lakini mapendekezo yake yamebaki kwenye makaratasi badala ya kutolewa hadharani wananchi wakaelewa na serikali ikachukua hatua madhubuti kurekebisha.

Kwa mfano, hadi kikao cha Bunge kilichomalizika hivi karibuni, wizara ya fedha na uchumi ya serikali ya muungano ilishindwa kutoa majibu fasaha kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara kutozwa ushuru mara mbili wanapotoa bidhaa Zanzibar kuziingiza Tanzania Bara. Na hiki ni kilio cha zaidi ya miaka kumi
sasa.

Mfanyabiashara mmoja aliniambia wiki iliyopita kuwa alilazimishwa kulipa ushuru mara ya pili alipoingiza gari Dar es Salaam alilonunua Zanzibar na kuilipia ushuru.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010, Chama cha Wananchi (CUF) kililalamika kulazimishwa kulipa mara mbili ushuru wa gari walilotaka liingie Dar es Salaam kutoka Zanzibar ambako lilishalipiwa kodi.

Viongozi wa CUF walisema tayari kulikuwa na agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais, Dar es Salaam, kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotoza ushuru kwa bidhaa yoyote iliyokwishalipiwa ushuru ilipoingia Zanzibar kutoka nje ya Jamhuri ya Muungano. Ilitolewa taarifa kuwa TRA walisema hawawezi kuamrishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu masuala ya kodi.

Kuna malalamiko ya muda mrefu kwamba Zanzibar haiwezi kutekeleza sera zake mbalimbali za kuinua uchumi kwa sababu lazima zipate idhini wizara ya fedha na uchumi Dar es Salaam ambako ndiko sera za fedha na za sarafu ya Tanzania (Shilingi) zinakopangwa na kusimamiwa kutekelezwa.

Zanzibar wanadai kunyimwa haki ya kuanzisha uhusiano na mataifa au taasisi za kimataifa na hivyo kufungiwa milango ya fursa za kupata misaada ya kuimarisha uchumi wake na kustawisha watu wake; huku ikigawiwa sehemu ndogo mno ya misaada ambayo Tanzania inapata kutoka nje.

SMZ imethibitisha mara kadhaa kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) haisimamii uendeshaji/urekebishaji wa sera za kiuchumi za Zanzibar. Kwamba sera za BoT hazizingatii mipango ya SMZ. Ushahidi mzuri ni pale miaka ya kwanza ya 1990, SMZ ilipolazimika kufidiwa fedha ambazo ingekula hasara kutokana na bajeti yake kupanguka kwa vile serikali ya muungano ilipunguza thamani ya sarafu wakati SMZ ilishatangaza bajeti yake.

Kwa yote hayo, wananchi hawajaona ufumbuzi. Ukisikiliza kauli na matamshi ya viongozi hasa wa Jamhuri ya Muungano, na usipotafuta undani wa kinachoendelea, unaweza kuamini mambo yanakwenda vizuri baada ya tatizo fulani kutatuliwa. Umeliwa.

Uliza leo ilipo ripoti ya kamati ya wataalamu waliochunguza mfumo bora wa kugawana mapato ya nje yanayotokana na ruzuku/misaada na mikopo. Utashangaa usipopata jibu moja. Uchunguzi ulimalizika miaka minane iliyopita, ripoti iliwasilishwa serikalini zaidi ya miaka mitano sasa. Ripoti haijawekwa hadharani.

Kwa hiyo, mpaka leo, SMZ inaendelea kupewa asilimia 4.5 ya misaada inayopata Tanzania, kiwango ambacho kilikubaliwa kama majaribio wakati suala hilo linafanyiwa kazi.

Iwapo wananchi wa Zanzibar wanaamini muungano hauna maslahi kwao, zaidi ya hilo alolisema Balozi Iddi la Wazanzibari kuishi Bara, ambalo ni jambo la kiupuuzi sana kihalisia, ni muhimu kusikilizwa wanataka nini.

Ni wao wenye mamlaka ya haki ya kuamua wanataka kuishi vipi, kwa muungano upi. Na hakika, haya ndiyo miongoni mwa mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika utungaji wa katiba mpya ya jamhuri.

Makala ya Jabir Idrissa katika gazeti la MwanaHalisi la tarehe 27 Aprili 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.