WACHINA wanashikilia kuwa ni usemi wao wa kale lakini nadhani ni Heraclitus (Herakleitos ), mwanafalsafa wa Kiyunani wa karne ya 500 kabla ya kuzaliwa Yesu, aliyekuwa wa mwanzo kusema: ‘Mtu hawezi kutia miguu mara mbili katika mto huo huo.’ Heraclitus alikusudia kusema kwamba haiyumkiniki kwa mtu kutumbukiza mguu wake mara mbili katika maji hayo hayo ya mto. Ukishatia mguu na kuutoa maji mengine hupita, hayawi tena yale yale ya awali. Kiini cha falsafa yake ni kwamba mageuzi ndiyo yanayousukuma ulimwengu na kuufanya uwe bora. Na mageuzi ndiyo yanayowashughulisha Wazanzibari siku mbili hizi. Wanataka mageuzi ya kimsingi yafanywe katika mahusiano baina ya nchi yao na ile nchi iliyokuwa ikiitwa Tanganyika.

Jumatatu ya juzi gazeti moja la hapa nchini lilimnukuu mwanasiasa mkongwe Hassan Nassor Moyo, mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, akisema : ‘Naunga mkono vijana wanaohoji Muungano, Muungano ni wao, sisi muda wetu umekwisha, wananchi wana haki ya kuhoji uhalali wa Muungano.’

Kwa mujibu wa gazeti hilo Moyo alisema kwamba wakati wa mchakato wa kurekebisha Katiba, Muungano pia utaangaliwa lakini mambo muhimu yamezuiwa yasizungumziwe.

‘Kwanini uwazuie watu kujadili Muungano…? Nyerere hakuwa Askofu wala Karume hakuwa Mufti, wote walikuwa wanasiasa na ndio waliounda Muungano, kwanini wanasiasa wa leo wasiruhusiwe?’

Mzee Moyo pia aliligusia suala nyeti la rasilimali ya mafuta. Alisema mkataba wa awali haukuzungumzia suala la mafuta kuwa chini ya Muungano, bali ni Bunge lililoliingiza kuwa moja ya mambo ya Muungano.

Swali la iwapo kuna mafuta na gasi asilia Zanzibar liliibuka katika miaka ya 1950 pale kampuni ya Shell ilipoanza kuchimba visima vya mafuta huko Kama, Unguja. Haikuchukuwa muda kampuni hiyo ikavifukia visima hivyo na kuondoka kwenda zake.

Nakumbuka siku hizo jinsi hatua hiyo ilivyozusha fadhaa na kuwafanya wananchi wa Zanzibar wapigwe na mshangao. Wakiamini kwamba serikali ya Kikoloni ya wakati huo haikuitakia kheri Zanzibar, kwamba haikutaka iwe na rasilimali hiyo ya mafuta.

Fadhaa na mshangao huo umezagaa tena hii leo. Lakini siku hizi wanaamini kwamba ni Serikali ya Muungano isiyotaka Zanzibar iwe na udhibiti wa hiyo maliasili ya mafuta ambayo, kama yapo, yatawafaidia Wazanzibari.

Wamekuwa na msimamo huo kwa sababu wanasema kwamba kwa muda wa zaidi ya miaka 15 Serikali ya Muungano imekuwa ikikataa kutambua kwamba Zanzibar ndiyo iwe na mamlaka ya mafuta hayo kama yatapatikana.

Serikali ya Muungano imekuwa na msimamo huo licha ya kuwa Baraza la Wawakilishi liliirejeshea Serikali ya Zanzibar kutoka Serikali ya Muungano mamlaka juu ya suala la mafuta na gasi asilia.

Bwana Mkubwa kabisa nchini humu anayaelewa vyema hayo kwani alielezwa wazi, tena kadamnasi, na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume, wakati wa sherehe za miaka 46 ya Mapinduzi kule Gombani, Pemba. Karume alisema hadharani kwamba uamuzi huo wa Wazanzibari umeshafikiwa na unapaswa uheshimiwe.

Isitoshe. Nimeambiwa kwamba baada ya hapo Serikali ya Zanzibar iliiandikia rasmi Serikali ya Muungano kupitia Waziri Kuu kuiarifu kuhusu uamuzi huo. Barua hiyo iliitaka Serikali ya Muungano ichukuwe hatua za kupeleka marekebisho ya Katiba ya Muungano bungeni ili kuliondoa suala la mafuta na gesi asilia kutoka orodha ya mambo ya Muungano.

Hadi leo lakini jibu la Serikali ya Muungano limekuwa jii. Ndiyo Wazanzibari wakawa wanauliza kwa hili Serikali ya Muungano ifahamike vipi? Serikali ya Muungano inaipa ujumbe gani Serikali ya Zanzibar?

Wanaendelea kusaili kwa nini suala hili linaendelea kung’ang’aniwa kuwa ni la Muungano ilhali moja ya nchi mbili katika Muungano imekwishaamua kupitia chombo kinachowawakilisha wananchi wake kwamba haitaki suala hilo liendelee kuwa la Muungano?

Maswali hayo yanatufikisha kwenye swali mama. Nalo ni kwamba, jee Tanzania-Bara, kwa kujitia chini ya kwapa za Serikali ya Muungano, inatumia mabavu kulazimisha suala la mafuta na gesi asilia kuwa la Muungano kinyume na matakwa ya Wazanzibari? Kama ni hivyo, inafanya hivyo kwa manufaa na maslahi ya nani?

Uamuzi wa Baraza la Wawakilishi kwa hakika umeifanya Zanzibar iondowe rasmi ridhaa yake ya suala hilo kuendelea kuwemo katika orodha ya mambo ya Muungano.

Wakati Tanzania-Bara ikiwa inaendeleza utafiti wa mafuta na gesi katika maeneo yake kuendelea kukataa kulimaliza suala hili kwa njia ya marekebisho ya Katiba yanayotakiwa na Zanzibar kunakwamisha na kuhujumu azma ya Zanzibar ya kuruhusu utafutaji na uchimbaji wa mafuta uendelee.

Wazanzibari wanahoji kwamba Serikali ya Zanzibar imeshatoa muda wa kutosha katika kulitanzua suala hili na uamuzi wake imekwishaufanya. Wanasema kwamba wakati umefika ikiwa Serikali ya Muungano bado inakataa kuliondoa suala hili katika mambo ya Muungano, basi Serikali ya Zanzibar ichukue uamuzi wa kimapinduzi zaidi wa kuendelea na hatua nyingine zilizoamuliwa na Baraza la Wawakilishi.

Moja kati ya hatua hizo ni kuitaka Serikali ya Zanzibar iunde Mamlaka yake ya kusimamia utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia (Zanzibar Petroleum Development Authority) na itoe leseni kwa kampuni zitakazoonyesha utayari wa kufikia mikataba na Zanzibar na kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta ianze.

Hali ya mambo ilivyo sasa ni kwamba kuna baadhi ya makampuni kama vile ile ya Shell ya Uingereza na Antrim Energy ya Canada (ambayo inasemekana inakusudia kuuza haki zake kwa kampuni inayomilikiwa na Serikali ya Ras Al-Khaimah, mojawapo ya Falme za Kiarabu katika Ghuba) ambazo zimepewa leseni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na Shirika la Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC).

Tatizo ni kwamba TPDC si Shirika la Muungano na wala halina mamlaka Zanzibar. Na serikali ya Zanzibar imekataa kuzitambua leseni hizo zilizotolewa na shirika lisilo na mamlaka halali Visiwani.

Inasemekana kuwa baadhi ya kampuni hizo zimo mbioni kutaka ziruhusiwe kuendelea na utafiti na ikibidi kuanza uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar kwa kutumia leseni walizopewa na TPDC.

Kampuni hizo zinasema kuwa masuala ya wapi faida iende au vipi uwe mgawanyo wa mapato yaendelee kujadiliwa. Hoja ni kuwa hata yakifika masuala hayo kuamuliwa na kupatiwa ufumbuzi, basi utafutaji na pengine uchimbaji wa mafuta utakuwa umeshapiga hatua kubwa.

Ninavyofahamu ni kuwa Serikali ya Zanzibar haiko tayari kwa hilo kwani inaona ni ujanja wa kutaka kuihalalisha TPDC kuwa na mamlaka Zanzibar na baadaye Zanzibar itakuja kuambiwa kuwa ilishatambua uhalali wa TPDC ndani ya Visiwa hivyo.

Suala la uchimbaji mafuta Zanzibar lina umuhimu mkubwa sana hasa kwa vile kuna mahitaji makubwa ya mafuta duniani na bei ya rasilimali hiyo imepanda kwa asilimia 23 mwaka huu kufikia zaidi ya dola za Kimarekani 110 kwa pipa moja la mafuta.

Bei hiyo imeruka hivyo kutokana na machafuko ya kisiasa katika Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini yaliyowang’oa kwenye madaraka viongozi wa Misri na Tunisia na kusambaa hadi Libya, Algeria, Bahrain, Oman, Syria na Yemen.

Tukiangalia Libya tu tunaona jinsi mapigano nchini humo yalivyopunguza uzalishaji wa mafuta. Kwa mujibu wa Shirika la habari la Bloomberg mwaka jana kwa wastani Libya ikichimba mafuta ya kujaza mapipa milioni moja na laki sita kwa siku lakini mwezi huu uliopita, wa Machi, idadi hiyo ilishuka hadi mapipa 390,000 kwa siku.

Ikiwa kweli kuna kiasi kikubwa cha mafuta yatakayogunduliwa Zanzibar, na kuna ushahidi kwamba kuna akiba tosha ya mafuta kusababisha uchimbaji wa mali hiyo asili, basi Zanzibar itaingia katika medani inayohusika na siasa za mafuta na nishati duniani.

Itapojikuta katika hali hiyo Zanzibar itabidi ikae macho wazi ili ijiepushe kufanya makosa yaliyofanywa na nchi zinazotoa mafuta, hasa zile zilizo barani Afrika.

Tumeona kwa mfano jinsi ufisadi ulivyozivunja Nigeria na Angola na kuzifanya zisiweze kuitumia rasilimali hiyo kwa manufaa ya wengi wa wananchi wake.

Hivyo, inapoendelea na mipango yake ya kutafuta na kuchimba mafuta Serikali ya Umoja wa Kitaifa lazima iwe na uwazi na ihakikishe kwamba mchakato wote wa mashaurino na washirika wa nje yanafanywa bila ya kuingizwa ufisadi.

Mafuta yatapogunduliwa na kuchimbwa, itachukuwa takriban muda usiopungua miaka mitano kabla ya Zanzibar kuanza kupata mapato kutokana na mauzo ya hiyo maliasili. Hivyo, patahitajika ubusara wa kuzisarifu fedha zitazopatikana kutokana na mauzo hayo.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa itabidi ianzishe Mfuko Maalum wa Mafuta ya Zanzibar (Zanzibar Oil Fund) ambao utawekeza fedha zitazopatikana kutokana na mauzo ya mafuta kwenye taasisi na miradi ya ndani na nje ya nchi.


Makala ya Ahmed Raajab iliyochapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Raia Mwema la tarehe 27 Aprili, 2011, Dar es Salaam. Mwandishi anapatikana kwa kupitia: ahmed@ahmedrajab.com

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.