Rais Jakaya Kikwete

Zanzibar Daima imepokea barua ifuatayo kupitia njia ya e-mail kutoka kwa anwani iliyojitambilisha kama Uhuru Wetu. Barua hii inaelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, kutoka kwa kundi la watu wanaojiita wawakilishi wa mikoa mitano ya Zanzibar. Ambapo Zanzibar Daima haiwezi kuthibitisha uhalali wa kuwepo kwa kundi hilo, inatambua kwamba hisia zinazoelezwa kwenye barua yenyewe ni za msingi na ni maarufu miongoni mwa jamii ya Kizanzibari. Hapa tunaichapisha kama ilivyo kwa lengo la kuwapa wengine fursa ya kujua kilichomo.

BARUA YA WAZI KWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ikulu – Magogoni,
Dar es Salaam
Tanzaania.

Kwako Mheshimiwa Rais,
YAH: MUUNGANO WA MIAKA 47 WA JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR NA JAMHURI YA TANGANYIKA
Mheshimiwa Rais wetu kipenzi, sisi tulioandika barua hii ni kwa makubaliano na ushirikiano wa dhati na wananchi wenzetu wa mikoa mitano ya Zanzibar, ili kukufikishia wewe mlezi na kiongozi mwenye dhamana ya taifa letu.
Kwa masikitiko makubwa hatuna budi kufikisha kilio chetu kwako wewe Rais wetu ambaye upo katika kipindi chako cha pili na cha lala-salama kikatiba katika kuliongoza taifa hili bila ya mafanikio juu ya ahadi zako ulizozitoa za kuzimaliza kero za muungano baina ya watu wa Zanzibar na Watanganyika.
Mheshimiwa Rais, tunajua wazi kwamba wakati bado unao; lakini kila jua linapozama ndivyo kadiri siku za mamlaka yako kama rais zinavyozidi kupotea. Hivyo fahamu unaondoka ukiwa na deni kubwa kwetu Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla. Deni hili ni lile uliloanza kulibebea ahadi ya utekelezaji ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya uwongozi wako.
Utakumbuka kabla ya kuingia katika uchaguzi wa mwaka 2005, wakati Chama Cha Mapinduzi – CCM kilipokua na wagombea wengi wenye sifa zinazoshabihiana, ulikuja kwetu Zanzibar kwa watoto wetu ambao baadhi yao ni viongozi wetu; ili kuomba kuungwa mkono na kupewa ushirikiano huku ukiwaahidi kwamba ungezipatia ufumbuzi kero zote za Muungano, lakini kumbe tulitia mkono kizani.
Mheshimiwa Rais, ahadi zako juu ya kuziondoa kero za Muungano ulizibainisha hadharani wakati ulipolizindua Bunge la tisa (9) Disemba 30, 2005 pale ulipobainisha majukumu matatu (3) ya msingi ambayo wewe na serekali yako mungeyatekeleza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha pande zote mbili zilizounda Muungano zinafaidika na kuridhishwa na Muungano wao huo. Aidha katika kipengele cha tatu (3) ulituahidi kuwa demokrasia yetu itazidi kustawi na serekali yako itaendeshwa kwa misingi ya utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu.
Licha wewe na serekali yako kushindwa kuyatekeleza yale mambo makuu matatu uliyoyapa kipaumbele katika awamu yako ya 2005 – 2010, lakini hukujisikia aibu kuwaeleza watanzania kupitia Bunge jipya la kumi (10) kwamba mambo yale uliyoyaahidi katika Bunge lililopita (la tisa) bado yataendelea kuwa ndiyo majukumu yako ya msingi katika kipindi chako hiki cha pili (2010 – 1015).
Mheshimiwa rais, utakumbuka wakati unalihutubia Bunge hili la kumi (10) tulilonalo hivi sasa ulitoa vipaumbele kumi na tatu (13) licha ya kushindwa na vile vitatu vya mwanzo (vya Bunge la tisa); na ulituahidi watanzania kwamba utavitekeleza kwa ARI ZAIDI, NGUVU ZAIDI NA KASI ZAIDI. Mheshimiwa nadhani haitakua vibaya kama tutakukukumbusha walau kidogo baadhi ya ahadi ulizotuahidi katika hutuba yako ya Bunge la kumi:
Kwanza kabisa uliahidi kwamba utahakikisha nchi yetu inaendelea kuwa yenye umoja, amani, na usalama; na muungano wetu utaendelea kudumu na kuimarika.
Pia kwa mara nyengine tena uliahidi kuimarisha utawala bora, demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu, wakati ukijua wazi kwamba katika miaka mitano yako ya mwanzo vipengele vyote hivi viwili ulishindwa kuvitekeleza.
Jee Mheshimiwa Rais, hii rasimu kuhusu mpya uliyotuandalia kwa ushirikiano wa makusudi na serekali yako bila hata kufuata kanuni na sheria za muungano wetu; ndio kutaka kuimarisha umoja, amani na usalama wa kweli?
Jee huu ndio utawala bora, utawala wa sheria wa demokrasia yenye kujali haki za binadamu?
Au huu ndio mkakati maalum wa kuhakikisha kuwa muungano wetu unaendelea kudumu na kuimarika?
Mheshimiwa Rais, sisi wazee tunaowakilisha wenzetu wa mikoa mitano ya Zanzibar tunaunga mkono kwa nguvu zetu zote wale wote waliokataa na kuupinga mswada huo (rasimu ya mswada ya utaratibu wa kutunga katiba). Sambamba na hili, tunachukua nafasi hii kutoa pongezi kwa wazanzibari wote walioacha tofauti zao zote na kuweza kusimama kidete na kwa pamoja kwa hoja za wazi na madhubuti katika kupinga mswada huu unaoonekana wazi kuandaliwa kwa makusudi mazima ili kuiteketeza na kuimaliza Zanzibar. Hii ni haki ya kikatiba kwao kwa sababu Zanzibar ni nchi yao halali na hivyo hawana budi kuonyesha uzalendo na kuchokeshwa kwao na dharau, kebehi za serekali ya muungano kwa nchi yao.
Mheshimiwa Rais, tunakuomba kwa heshima zote wewe na serekali yetu ya muungano; tafadhalini sana sana msikie kilio cha wazanzibari. Tunajua asili na tabia yako wewe si mtu wa pupa, jazba na hamaki. Bali tabia yako imepambwa na busara, hekima, usikivu na utaratibu, sifa ambazo ni sawa na lulu na ndizo zinazokutofautisha sana wewe na baadhi ya viongozi waliotangulia. Jambo hili limewiyana sana kwa wewe kuwa rais, kwani Ikulu ya Rais inatarajiwa wakati wote ionekane ni yenye kutumia busara, hekima na taadhima katika kuongoza kwa kujali maslahi ya wananchi wa maeneo yote kwa kuzingatia misingi sahihi ya utu na ubinadamu.
Kwa kuwa tunataka ziendelee sifa njema hizi kwako, tunakuomba sana usikizibie masikio kilio chetu wazanzibari. Kisikilize kwa kuzingatia uhalali na sheria, na wala hatudai kupendelewa kama wengine wanavyoweza kudhania.
Mheshimiwa Rais, wazanzibari si wenda-wazimu, si mataahira, na wala si wajinga wa kudiriki kupinga kitu bila ya kujua dhara na athari zake. Wazanzibari wanataka mabadiliko makubwa ndani ya muungano tulionao, kwani tunaamini na ndivyo ukweli ulivyo kwamba makubaliano ya muungano wetu huu (the articles of union) yamekiukwa na hivyo kuweka kasoro kubwa katika uhalali wake.
Sisi tunaamini kwamba huu ni wakati muafaka na mnasaba wa kuujadili muungano upya. Na baadae watu wa Zanzibar na watu wa Tanganyika (Tanzania bara) wapewe fursa ya peee ya kuulizwa juu ya muungano upi wanaoutaka. Hivyo majibu yatakayotoka pande zote mbili ndiyo yapewe tume ili yafanyiwe kazi inayostahiki,ijapokuwa tume itakua inayafanyia kazi maoni ambayo yalishafanyiwa kazi katika repoti ya Jaji Nyalali ya mwaka 1992, na ripoti ya Jaji Robert Kisanga, katika maoni yote yalipendekeza kuundwa kwa serekali tatu (3).
Haikuishia hapo, lakini pia katika serekali ya Rais Ali Hassan Mwinyi; waziri mkuu wake wakati ule John Samuel Malecela alikwishakamilisha na kulieleza Bunge juu ya nia ya kuwepo mswaada wa kuanzishwa kwa serekali ya Tanganyika; wakati wewe Mheshimiwa Rais ulikua ni mbunge. Lakini muasisi wa taifa la Tanganyika Mwalimu Nyerere akatumia uwezo wa chama na kulilazimisha bunge lisiujadili, na hatimaye baadae kufukuzwa kwa Malecela kwa nafasi ya uwaziri mkuu. Ukiyaangalia haya yote yanaonesha maoni ya watanzania ni kuundwa kwa serekali tatu. Pamoja na maoni yote hayo, serekali ya muungano ikayapuuza na yamebakia katika kumbukumbu na maandiko tu.
Ikiwa yote haya yalipuuzwa; jee hiyo tume itakayoundwa itakuja kufanya nini? Au maoni yanayotakiwa yatolewe ni ya kuundwa kwa serekali moja? Kwani tokea zamani ilishaonekana serekali mbili hazitakiwi, moja haikubaliki, na serekali tatu ni kinyume na sera ya chama tawala (C.C.M).
Januari 12, 1964 sisi wazanzibari tulifanya mapinduzi, haya hayakua mapinduzi ya kuondosha kilemba bali yalikua mapinduzi ya wakulima na wafanya kazi yenye dhamira na lengo la kuimarisha dola ya Zanzibar na ustawi wa wa jamii na maisha ya vizazi vyake ya kuondosha aina zote za madhila, matabaka na kuimarisha heshima ya ndani na ya nje ya nchi, sio kugeuzwa mkoa, na wala sio Rais wetu wa Zanzibar kuwa waziri katika serekali ya muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Rais, haitakua ajabu kama itafikia pahala ama wazanzibari, watanganyika, au wote kwa pamoja kama watakataa muungano. Maamuzi yao yaheshimiwe na tuachane na muungano kwa salama na amani.
Hii haitakua aibu kwetu kwani ni jambo la kawaida kwa mataifa yaliyoungana na hatamae kugawanyika ili kila mmoja ashike ubao wake na aendelee na safari katika jahazi lake. Zipo nchi nyingi zilizowahi kupita katika mkondo kama huu wa Muungano na leo hii wameshasahau kama walikua wamoja.
Tukiachilia mifano ya zamani ya kama taifa la USSR – Union of Soviet Socialist Republics ambao uliundwa na mataifa kama vile Armenia, Azerbaijan, Belarus, Estonia, Georgia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Latvia, Lithuania, Moldova, Russia, Tajikistan, Turkmenistan, Ukraine, na Uzbekistan. Muungano huu ulidumu takriban kwa miaka 67,na hivyo una historia kubwa zaidi kwani ni tangu mwaka 1924 na uliweza kuvunjika mwaka1991.
Sasa tuuchukue mfano wa karibu sana wa taifa la SUDAN; nchi iliyokua moja tangu enzi lakini leo imegawika na kuwa mataifa mawili huru baada ya watu waishio Sudan ya kusini walipopiga kura ya maoni (Sudan referendum) tarehe 9 hadi 15 Januari 2011 na kuona kuna haja ya kujitenga na wenzao wa kaskazini. Haya yalikuwa ni utekelezaji wa makubaliano ya 2005 ya Naivasha (Naivasha Agreement) baina ya serekali kuu ya Khartoum (Sudan) na mrengo uliojulikana kwa jina la Sudan People’s Liberation Army/Movement (SPLA/M)
Je katika mungano wetu wa Tanzania hapakua na makubaliano yoyote juu ya pande hizi mbili? Yalikuwepo (the articles of union) yenye mambo kumi na moja (11) tu. Basi kwa nini makubalino hayo yavunjwe? Na ni nani alikua na mamlaka ya kufanya hivyo; kama si dharau na kebehi kwa Zanzibar?
Mheshimiwa Rais, tarehe 26/04/2011 ni siku ya kusherehekea muungano huu tunaoulilia hapa, na tuna imani kubwa wewe ndiye mgeni rasmi wa hafla hiyo itakayofanyika uwanja wa Amaan – Zanzibar. Sisi wenyeji wako wa Zanzibar tunakwambia “karibu sana”. Tunakukaribisha lakini ujuwe kuwa wazanzibari wote utakaowaona hapo, na hata wale watakaokuzunguka katika jukwaa kubwa; hawana furaha kabisa na muungano. Bali wana dukuduku, machungu na masononeko juu ya muungano.
Tafadhali sana Mheshimiwa Rais; tunakuomba usikie mawazo yetu, ili uyachukue na kuyapa nafasi kubwa katika maamuzi yako. Wazanzibari wanataka nchi yao yenye mamlaka kamili ya kuendesha dola yao.kati sisi na nyie tutabakia na udugu na ujirani mwema.
Sisi wazee tunasema “mficha maradhi kifo humuumbua”.
“Pasaka njema”
Imetumwa na wazee wanaowakilisha mikoa mitano ya Zanzibar leo tarehe 21/04/2011 na:
Mwakilishi wa mkoa wa kaskazini Pemba,
Mbwana Ali Faki
Mwakilishi wa mkoa wa kusini Pemba,
Bikhole Sheha Khatoro
Mwakilishi wa mkoa wa kusini Unguja,
Ussi Ameri Nahoda
Mwakilishi wa mkoa wa kaskazini Unguja,
Haji Mbaruku Bakari
Mwakilishi wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,
Mpatani Mussa Sariboko

Nakla:
Vyombo vya habari.

3 thoughts on “Wazanzibari wamwandikia barua ya wazi Rais Kikwete”

 1. Kwa mujibu wa tafsiri ya Qurani Takatifu ya marehemu Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy Suratul Hujurat 26 Aya ya 6 :

  “Enyi mlioamini! Kama fasiki (asiyekuwa wa kutegemewa) akikujieni na habari (yoyote ile msimkubalie tu) bali pelelezeni (kwanza), msije mkawadhuru watu kwa ujahili na mkawa wenye kujuta juu ya yale mliyoyatenda”

  Pelelezeni kwanza kama majina ya wawakilishi waliotajwa kwenye hii “barua ya wazi” ya hapa chini inayojitaja kuwa “Imetumwa na wazee wanaowakilisha mikoa mitano ya Zanzibar” ni ya kubuni au hujui kama habari unazozieneza zinatoka kwa mtu faasik au taasisi faasik?

  Suala la ukombozi wa Zanzibar tayari linafuata mkondo maalumu wa kisheria kwa hiyo nawatahadharisha msitumbukie ndani ya mtego wa mafaasik wa kutaka kutuletea chokochoko na fujo ambazo tayari zimeshapokelewa kwa furaha kubwa na maadui wa Wazanzibari na wa mustakbal mwema na wa amani wa Zanzibar Mpya.

 2. mimi nikiangalia kwa umakini zaidi ni kua muungano hautufai kwa sababu ndani ya karibu nusu karne haukua na manufaa na sisi zaidi ya kutukandamiza.lakini kubwa zaidi ni hawa wenzetu tulioungana kua yote hayo waliyotufanyia bado hawajaridhikka sasa wanaona bora watupige sindano ya kututoa akili.mimi nadhani kama walikua na lengo zuri wasingefikia kusema kua suala la muungano lijadiliwe kwa baadhi ya mambo na lisizungumzwe kuvunjika.mwisho tungelipendelea wananchi tupewe fursa ya kupiga kura ya maoni kua tunautaka au hatuutaki na sio kukaa watu watano sita tena wa upande mmoja wakaamua kua muungano usijadiliwe kuhusu kuvunjika hili suala la kuwepo na kutokuwepo muungano ni la wananchi wote katika pande zote mbili na si la watu wachache wa DODOMA.

 3. Zanzibar Daima ilipokea barua hii kupitia e-mail. Inawezekana sana watu waliotajwa kwenye barua yenyewe hawapo kabisa. Na kwa hivyo haitoki kwa watu wanaojuilikana hasa kama nafsi moja moja. Lakini ni wazi kwamba kilichoelezwa kwenye barua kinawakilisha, kwa kiasi kikubwa, mtazamo na msimamo wa Wazanzibari walio wengi, kama ilivyodhihirika majuzi kwenye mikutano ya kukusanya maoni ya utaratibu wa utafutaji wa maoni ya katiba mpya, mjini Unguja.

  Kuchapishwa kwa barua hii hapa hakutokani na usahihi wa majina ya hao waliojiita wawakilishi wa mikoa mitano ya Zanzibar, bali maudhui ya barua yenyewe. Kwa maana nyengine, ni ujumbe na sio mjumbe kilichozingatiwa na Zanzibar Daima kama hoja ya kuipokea na kukubalia kuichapisha barua hii tena.

Leave a Reply to zanzibardaima Cancel reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.