Waziri Mkuu wa Zanzibar baada ya uhuru wa 1963, Sheikh Hamad Shamte (kulia) akiiwakilisha nchi yake kwenye Umoja wa Mataifa

TENGE na tahanani iliyozuka majuzi Zanzibar wakati wa mijadala ya katiba ya Tanzania lazima iliwafanya wengi wasiozielewa hisia za Wazanzibari kuhusu Muungano waghumiwe. Samuel Sitta, waziri wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, aliingia kizaazaa alipozomewa alipokuwa akiizungumzia rasimu ya muswada wa sheria ya kuanzisha Tume ya Mapitio ya Katiba ya Tanzania na kuiona hiyo rasimu ikichanwa. Vishindo hivyo visistaajabishe. Jazba na hamasa zilizopandishwa na Wazanzibari waliokwenda kumsikiliza Sitta hazikuwa za bure. Wala hazikuwa za Wazanzibari wa mwelekeo fulani tu wa kisiasa. Zilikuwa hisia za Wazanzibari wote — wana CCM na wana CUF pamoja na wale wasio wafuasi wa chama cho chote cha kisiasa. Hii ni hali inayowashangaza wengi Bara wasiofahamu jinsi Muungano unavyowachoma Wazanzibari.

Wazanzibari hawakuviona hivyo vishindo vya katiba kuwa ni vigeni au kuwa viroja. Na ukiwauliza watakwambia kwamba wana historia ndefu ya michakato ya utungaji wa katiba. Watakutajia Lancaster House, lile jengo maarufu jijini London, ambako kulifanywa mkutano wa mwanzo wa kuizingatia katiba ya Zanzibar mwaka 1962.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa vyama vya Zanzibar Nationalist Party (Hizbu), Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) na Afro-Shirazi Party (ASP). Miongoni mwa wajumbe waliohudhuria walikuwa ni baadhi ya viongozi wa kihistoria wa Zanzibar. Nao ni Sheikh Ali Muhsin, Sheikh Muhammed Shamte, Sheikh Abeid Amani Karume na Sheikh Othman Shariff. Walihudhuria pia Abdallah Kassim Hanga, Hassan Nassor Moyo, Abdulrahman Babu na Salim Said Rashid, ingawa hawa wanne hawakushiriki kwenye mashauriano.

Ukiwachokorachokora tena Wazanzibari watakwambia kwamba katiba yao ya kwanza ilikuwa ile Katiba ya Uhuru ya mwaka 1963.

Baada ya Mapinduzi Januari 12 mwaka 1964, Baraza la Mapinduzi lilipitisha ile iitwayo Kanuni ya Serikali ya Kikatiba na Utawala wa Kisheria mnamo Februari 25 mwaka 1964.

Kanuni hiyo iliagiza ‘Baraza la Kikatiba la Watu wa Zanzibar’ liitishwe kabla ya Januari 11 mwaka 1965 ili kufanya maamuzi kuhusu katiba mpya ya Zanzibar.

Kwa bahati mbaya agizo hilo halikutimizwa kwa sababu muda si mrefu pakaundwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa hakika, Muungano huo uliundwa bila ya Hati za Muungano kuidhinishwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar kama ilivyotakiwa iwe kwa mujibu wa hizo Hati za Muungano na kama inavyohitajika kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria za Kimataifa na Utaratibu wa Mikataba.

Taksiri hiyo inaonekana wazi kwa vile ilani inayosema kwamba Baraza la Mapinduzi lilikutana na kuziidhinisha hizo Hati za Muungano ilichapishwa katika gazeti rasmi la serikali ya Tanganyika, the Tanganyika Gazette, na kutiwa saini na P.R. Ninnes Fifoot kwa vile alikuwa na wadhifa wa Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanganyika.

Ajabu ya mambo ni kwamba ilani hiyo haikuchapishwa katika gazeti rasmi la Serikali ya Zanzibar, the Zanzibar Gazette, na wala haikutiwa saini na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, ambaye wakati huo alikuwa Salim Said Rashid.

Kweli kulikuwa na Katiba ya Muda ya Muungano iliyotayarishwa kwa kuibadili kidogo Katiba ya Tanganyika na kuzifanya sheria husika za katiba hiyo ziwe zinatumika pia Zanzibar.

Hiyo lakini ilikuwa ni hatua ya muda na palikuwa na utaratibu uliowekwa wazi kwenye Hati za Muungano wa kuifikia katiba ya kudumu ambayo ilikuwa itungwe katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuundwa Muungano.

Kufikia Machi 24 mwaka 1965 Bunge la Muungano lilipitisha Hati ya Sheria ya Katiba yenye haki na uwezo wa kutunga au kubadilisha katiba. Hati hiyo ilivibadili vifungu vya Hati za Muungano na kukirefusha kipindi cha Katiba ya Muda ya Muungano mpaka utapofika ‘wakati muwafaka’.

Yote hayo yalitendeka licha ya kuwa Bunge la Muungano lenyewe halina mamlaka yo yote ya kisheria ya kuzibadili Hati na Sheria za Muungano bila ya mageuzi hayo pia kuridhiwa na baraza la utungaji sheria huko Zanzibar.

Mtindo huu ulifurutu ada na ulirejelewa mara kadha wa kadha kwa minajili ya kufanya mageuzi ya kisheria au kuongeza mambo katika ile orodha ya mambo yanayopaswa kuwa ya Muungano. Mwalimu Julius Nyerere alibabaishababaisha kwa kusema kwamba: ‘Mamlaka ni ridhaa ya watu. Si kipande tu cha karatasi.’

Kama mamlaka ni ridhaa ya watu basi mamlaka ya Muungano si ya halali kwani watu wa Zanzibar hawakushauriwa iwapo walitaka, walihitaji au walipendelea kuendelea kuwa katika Muungano. Wala baraza lenye kutunga sheria za Zanzibar halikushauriwa kama inavyopaswa.

Mwaka 1977 Nyerere aliiteua kamati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iupige mhuri na kuubariki muungano wa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na ASP. Halafu kamati hiyo ikakabidhiwa jukumu la kuandaa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo yalitendeka miaka 13 baada ya kuundwa Muungano licha ya kuwa kwa mujibu wa Hati za Muungano Baraza la Kutunga Katiba lilikuwa likutane kufikia Aprili mwaka 1965 kutunga muswada wa Katiba ya Muungano. Si hayo tu bali baraza hilo lilikuwa liwe na idadi sawa ya wajumbe wa Tanganyika na wa Zanzibar.

Mwaka 1979 Sheikh Aboud Jumbe, akiwa Rais wa Zanzibar, aliitoa ukumbini Katiba mpya ya Zanzibar miaka kumi na tano baada ya Mapinduzi ijapokuwa, kama tulivyokwishasema, Baraza la Mapinduzi liliamua Februari 1964 kwamba Zanzibar itakuwa na katiba mpya kufikia Januari 11 mwaka 1965. Katiba hiyo ya mwaka 1979 ikafanyiwa mabadiliko mwaka 1984.

Tukiiangaza basi historia ya Zanzibar kwa upande wa katiba na utungaji katiba tunaona kwamba Wazanzibari si wageni wa mchakato wa utungaji katiba. Wazanzibari wanatambua vyema athari za badiliko lo lote katika Katiba ya Muungano kwa vile marekebisho yaliyokwishafanywa kuhusu masuala ya Muungano yaliongezwa kiubabe na Bunge la Tanzania, bunge ambalo halina mamlaka au uwezo wa kisheria wa kufanya hivyo.

Akhasi ya mambo ni kwamba mageuzi hayo yaliifanya Zanzibar ipungukiwe na nguvu zake. Wengine wanahoji kwamba hali hiyo ndiyo iliyopelekea uchumi wa Zanzibar uzorote kwa muda wote huu wa karibu nusu karne.

Tukumbuke kwamba pamekuwako tume mbili — zikiongozwa na Majaji Francis Nyalali na Robert Kisanga — zilizoundwa na Serikali ya Muungano kuutalii mfumo wa Muungano na Katiba ya Muungano.

Mapendekezo makuu ya tume zote hizo mbili yalikataliwa na Marais wa Muungano. Hii rasimu ya sasa ya Muswada wa Sheria wa Mapitio ya katiba ya Muungano inatoa fursa ya tatu ya kuendelea na mchakato huo, kwa nia ya kutaka kuyajuwa maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo yatayopelekea kufanywa mageuzi.

Muda uliowekwa wa mchakato huo ni miaka mitano. Hayo yana maana kwamba kwa muda wa miaka mitano zaidi hali ya mambo itaselelea kuwa vivi hivi ilivyo na Zanzibar itaendelea kugubikwa na ufukara pamoja na uadimikaji wa neema za kiuchumi na kijamii.

Hivyo ni muhimu pachukuliwe hatua za dharura za kuiwezesha Zanzibar kisheria kuwa na mfumo wake wenyewe wa sera za kiuchumi na kijamii zitazoweza kuikwamua nchi hiyo.
Kwa vile huu muswada wa sasa umekataliwa na wananchi wa Zanzibar, wakiwemo miongoni mwao mawaziri kutoka vyama tofauti vya kisiasa, kuna umuhimu wa zoezi hili kuanzishwa upya. Tena liwe katika mfumo wa mashauriano kati ya serikali mbili, yaani Serikali ya Umoja wa Taifa ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Serikali hizo mbili ziwe wabia wenye haki sawa, yaani ziwe zinashauriana zikiwa washirika sawa katika Muungano, si upande mmoja kujifanya kaka na kuuona upande mwengine kuwa mdogo au usiostahiki haki sawa.

Hii leo ikiwa patafanywa kura ya maoni na Wazanzibari wataulizwa iwapo wanautaka Muungano uliopo na wajibu ama ‘ndio’ au ‘la’ sina shaka yo yote kwamba wengi wao wataukataa.

Hawatoukataa kwa sababu wanaamini ya kuwa kuna mapungufu katika mfumo wake. Wataukataa kimsingi kwani wanaamini ni Muungano ulioifanya hadhi ya Zanzibar ishuke kutoka kuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa ukubwa wa Jumla ya Pato la Kitaifa (GDP) na kutumbukia chubi katika shimo la ufukara na kuwa moja kati ya nchi zilizo na umasikini wa kutisha barani humo.

Kwa ufupi, wanaukataa Muungano kwa sababu wanaamini kwa dhati ya nafsi zao kwamba umewakandamiza. Kila wakipiga bongo wengi wa Wazanzibari wanaona kwamba mustakbali wa nchi yao utakuwa mzuri endapo tu patakuwako mfumo mpya wa mahusiano baina ya Zanzibar na ile nchi iliyokuwa ikiitwa Tanganyika.

Si hayo tu bali wanataka Zanzibar iwe na mahusiano hayo ikiwa ni mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Ili uweze kuhakikisha kwamba Zanzibar badala ya kuwa nchi yenye uhuru nusu inakuwa na uhuru kamili, mfumo huo mpya hautokuwa na budi ila kuirejeshea Zanzibar mamlaka yake yaliyoporwa kwa ghiliba na Tanganyika.

_______________________________________________________________________________________________

Makala hii ya Ahmed Rajab ilichapishwa kwa mara kwanza kwenye gazeti la RAIA MWEMA la Dar es Salaam, tarehe 13 Aprili 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.