Na Ally Saleh

Pengine kuna ukweli kuwa suala la mjadala wa Sheria ya Kupitia Katiba uliofanywa katika vituo vitatu ulitawaliwa na jazba na hamasa za kisiasa kwa kiasi fulani lakini kuna ukweli kuwa hasira za wananchi zilistahiki kabisa. Kwangu ni ishara kuwa taasisi iliyoaminiwa kutunga sheria yaani kitengo cha kutunga sheria cha Afisi ya Mwansheria Mkuu kuwa kimeoza lakini pia nina wasi wasi na vikao vya makatibu wakuu na ushauri wao kwa Serikali na nina wasiwasi zaidi na Baraza la Mawaziri juu ya nafasi yao ya kupitia miswada inayopelekwa huko.

Lakini nina shaka zaidi juu ya nia ya Serikali katika suala la kuleta mabadilkko ya Katiba au kuunda upya Katiba ya nchi hii kwa kutizama jinsi mswada huo ulivyotengezewa rasimu yake, ambapo hivi sasa kama ningekuwa mimi Mwanasheria Mkuu basi ningejizika chini kwa aibu.

Nasema hivyo kwa sababu nyingi. Kwanza kwa sababu ya makosa ambayo yametolewa na wanasheria na watu wengine wa Tanzania Bara lakini zaidi kwa makosa ambavyo yametolewa na wanasheria na watu wengine wa Zanzibar jambo ambalo ndio msingi wa makala yangu hii.

Hii fursa ya kuupelekea mswada kupata maoni ya umma ni tukio ambalo limeweza kufunua juu ya udhaifu na ukosefu wa uelewa wa watalamu wetu katika mambo ya msingi. Hii imenipa fikra kuwa kumbe kuna haja ya kwamba taasisi zenye kusimamia mambo ya Muungano ulazima wa kuajiriwa Wazanzibari kama vile kitengo cha kutunga sheria cha Mwanasheria wa Muungano na Tanzania Bara.

Kakika muswada huo kwenye kifungu chenye kutaja watu wasioweza kuwa Wajumbe wa Kamisheni ya Kuratibu Maoni kukosa uelewa wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaoitwaje kwa jina lao rasmi kulionekana dhahiri na kwa kweli ni jambo la kutisha.

Muswada wenyewe kwa ujumla wake umedhirisha ni namna gani “wenzetu” wasiovyojua na hata kuamini kabisa kuwa Muungano ni suala la nchi mbili na kwamba katika hali zote usawa katika hilo lazima uonekane na pia kujengeka kwa mazoea mabaya, nje ya utaratibu wa Katiba.

Mazoea mabaya ni kama vile kuamini kuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania (T) ni mkubwa zaidi kuliko wa Zanzibar hata kama mwanasheria huyo husimamia mambo mengine ambayo si ya Muungano, na hata kwamba suala la sheria si la Muungano, kama ambavyo imezoeleka kuwa Waziri wa Sheria wa Tanzania ni mkubwa kuliko yule wa Zanzibar.

Kwa hivyo inatosha kabisa kwa Mwanasheria Mkuu wa (T) kufanya lolote lile kwa kumshauri au bila ya kumshauri au hata kuwepo au kusiwepo na makubaliano kama ilivyotokezea katika kadhia hii.

Pia tumekuwa na mazoea yalioelekea kuwa “fikra tukufu” zote za kutunga sheria za Muungano lazima zianzie kwenye Serikali ya Muungano na Katiba imeshindwa kuweka utaratibu ambao pia chanzo cha sheria za Muungano pia kinaweza kuanzia kutoka Zanzibar.

Tumeambiwa ni kweli palikuwa na mawasiliano ya awali, lakini kilichofanyika ni Zanzibar kupelekewa kopi ya kwanza ya Muswda na sio pande hizo mbili kukaa pamoja kutengeneza hiyo kopi ya kwanza. Zanzibar iliupitia Muswada huo na kupeleka mapendekezo yake kadhaa.

Kimya kikapita hadi kuibuka kwa kopi ya pili ya Muswada uliopelekwa kwa umma hivi sasa bila ya Mwanasheria Mkuu (T) kwanza kurudisha kopi hiyo mpya kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na kupuuza mambo kadhaa yaliopendekezwa na Zanzibar.

Kwa hakika mambo ya Zanzibar yanasemwa na Wazanzibari wenyewe na ndipo ikawa wachangiaji wengi wa Tanzania Bara, iwe ni Dodoma au Dar es salaam wamekosoa katika maeneo ambayo ya kidemorasia na kiutendaji, ilhali wakosoaji wa Zanzibar wameonyesha jinsi Zanzibar ilivyodharauliwa na kukosemwa haki zake.

Kwa mazoea tuliotoka nayo huko nyuma Zanzibar ni “kuukeni” na Bara ni “kuumeni” na kama tulivyo Waafrika wanaume ndio wenye kauli na wanawake ni watu wa kushauriwa na kuarifiwa tu. Na ndivyo watunzi wa Muswada huo walivyofanya kwa kuona Zanzibar ilikuwa Zanzibar kabla ya Muungano na sasa si Zanzibar ni sehemu tu ya Jamhuri ya Muungano.

Muswada huo ambao unajadili khatma kubwa ya Muungano unampa Rais Zanzibar nafasi ya kushauriwa Rais wa Muungano anapounda Kamisheni ya Kukusanya Maoni, nafasi ya kupewa kopi baada ya kukusanya maoni, si inamtosha bwana, itakuwa mtunzi wa Muswada huo alikuwa akifikiri.

Kwa hivyo Rais wa Muungano, atunda Tume kwa kumshauri tu, atampa kopi bila kutaka mawazo yake kama mshirika wake kamili (full partner) wa Muungano, mambo ambayo katika mjadala wa Muswada Wazanzibari wameonyesha wazi kuwa wameshindwa kuyameza mambo hayo.

Rais wa Zanzibar hatashiriki kutengeza hadidu rejea katika jambo linalomhusu sawa kwa sawa na mwenziwe wa Muungano, hata kuwa na sauti katika kuundwa Sekretariati ambayo haikutajwa itakuwa na wajumbe wa ngapi au kama itakuwa sawa kwa sawa; Rais wa Zanzibar hatashiriki kuteua wajumbe wa Tume ya Kuratibu Maoni ila kushauriwa tu, Rais wa Zanzibar hatashiriki kutoa maoni juu ya ripoti ya Kamisheni na Rais wa Zanzibar hatakuwa na nafasi yoyote katika suala la kuunda Bunge la Katiba kama litakuwepo.

Mtanzania mwenzangu unaesoma makala hii usishangae ila hivyo ndivyo ilivyo katika sheria hiyo ambayo Mzanzibari mmoja Sheikh Farid Hadi aliamua kuichana kuonyesha hasira zake kwa jinsi nafasi ya Zanzibar ilivyofanywa kuwa nduchu ndani ya Muungano ambao mwezi huu tutauadhimisha kuundwa kwake.

Mambo mengine ambayo yalishangaza Wazanzibari kuhusu wataalamu wetu wa kutunga sheria na kwa kiasi kuzusha hasira ni yale ya Muswada kusema kuwa taratibu wa kupitisha Katiba zitatumia utaratibu wa kawaida wa Bunge ambao huhitaji thuluthi mbili ya Bunge zima ilhali ikieleweka idadi ya Wabunge wa Zanzibar ni kidogo.

Hilo linapingwa na Wazanzibari kwamba lisifanyike pamoja na kuwa Bunge la kawadia la ssa halina mamlaka ya kutengeza Katiba mpya na mamlaka yake yanaishia kurekebisha katiba jambo ambalo nalo kwenye sheria Muswada limejichanganya hapa na pale, na iwapo Serikali inalenga Katiba mpya au kongwe kurekebishwa haliko wazi.

Wazanzibari pia wanahoji suala la kura ya maoni, ambalo limepenyezwa katika sheria hiyo ilhali kulikuwa na umuhimu wa Serikali ya Muungano kutunga sheria kamili ya Kura ya Maoni ambayo inaweza kufanya kazi katika mambo mengine kadhaa wa kadhaa.

Lakini la muhimu zaidi kwa Wazanzibari ni kuwa Kura hiyo ya maoni lazima ielezwe wazi jee ina masharti gani kama vile idadi ya chini ya wapiga kura, idadi ya kupitisha mshindi, jee ni ya ushauri au ni ya kuibana serikali juu ya maamuzi ya wananchi.

Lakini pia muhimu Wazanzibari wanasema kwao ni lazima wapige kura kama wao na wenzao wa Bara wapige kura peke yao. Kisha wanasema sheria lazima iwe wazi juu ya maamuzi ya umma kwa mfano ikitokea Wazanzibari wakikataa kuipitisha Katiba hiyo athari yake ni nini katika hali ambayo wenzao wa Bara wameikubali.

Kwa fikra zangu ni kwamba kuja kwa Muswada huo kumedhihirisha mambo mengi lakini kubwa kabisa ni kwamba kuna uteterekaji mkubwa wa nia ya kisiasa katika suala zima la Muungano. Pili kuna mawazo mpaya nay a kizazi kipya ambayo yanataka yapewe nafasi sio ya kusikilizwa tu, lakini ya kuzaa fikra mpya za Muungano.

Ni wazi kuwa Muungano hautabaki katika hali yake ya sasa kwa sababu umuhimu wa kurudi katika Mkataba wa Muungano ni jambo la msingi. Kwa fikra zangu Muungano ni vunge lenye madudu mengi na kwa hivyo haja ya kuyapunguza ndio jambo muhimu kabisa.

Muungano ninao uona ukija ni ule ambao utakuwa na mambo yasiozidi 10 ya Muungano, maana kwa hali hiyo ndio itakuwa rahisi kuwa na uhusiano baina ya nchi hizi mbili na sio nchi moja na moja ikiitwa sehemu ya nchi hiyo hiyo ilhali ni mshirika kamili. Hili ndio ambalo nimeliona kwenye mjadala wa Muswada wa kuunda Tume ya Kuratibu Maoni, nikiamini kuwa macho yangu hayana kengeza.

________________________________________________________________________________________________

Makala hii ya Ally Saleh ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 13 Aprili 2011 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.