Na Mohammed Ghassany

Hata baada ya karibuni nusu karne ya Muungano, bado masuala ya uhalali, usahihi na ulazima wa Muungano wenyewe ni mambo yanayopata ufuasi mkubwa Zanzibar. Hali ni tafauti kabisa na upande wa pili wa Muungano huu, Tanganyika, ambako si watu wengi ambao hata wanauhisi Muungano wenyewe.

Hoja yangu ni kuwa, Wazanzibari na Watanganyika wana malezi tafauti kuhusiana na sura na dhati ya Muungano huu. Ambapo Watanganyika wanauangalia huu kuwa ni wa serikali moja, Wazanzibari wanauangalia kuwa ni wa shirikisho la serikali tatu (au, angalau, ulitakiwa uwe hivyo). Ambapo Watanganyika hawashughuliki sana kuuwazia, maana si sehemu ya maisha yao, Wazanzibari wanalala wakiamka nao mawazoni, maana wanaamini una athari kubwa kwa maisha yao. Unaweza kufahamu kwa nini Watanganyika hawashughuliki nao sana, kwa kuwa tayari ‘wametengenezwa’ kuuamini, kinyume na Wazanzibari ambao ‘wametengenezwa’ kuushuku.

Unaweza usiambiwe haya moja kwa moja au neno kwa neno, lakini tabia, matendo na maono ya watu ndiyo yanayosomeka hivyo. Kwa mfano, si rahisi kumkuta Mtanganyika anajiita kwa jina hilo, maana kwa wengi wao Tanganyika imeshapotea. Hata wewe ukimuita hivyo katika muktadha wa Muungano, atakuchukulia kuwa u mbaguzi tu.

Lakini kila mara utamkuta Mzanzibari akijiita na akijinasibisha kwa Uzanzibari wake; na kama kuna orodha ya mambo kumi yanayowagusa Wazanzibari wote kwa pamoja, la hisia zao kwa Uzanzibari na dhidi ya Muungano litakuwa namba moja, kabla ya dini, vyama, na au uzawa wao.

Huu ni uamuzi wa kimapinduzi kwa pande zote mbili za Muungano. Kwa Tanganyika ni wa kimapinduzi kwa kuwa umeweza kupindua fikra za karibuni vichwa milioni 40 na kuvifanya viamini kitu kimoja tu. Utanzania.

Kwa Zanzibar ni wa kimapinduzi kwa kuwa vichwa milioni moja tu, ambavyo vinafanya chini ya asilimia 3 tu ya Watanzania wote na vinakaa chini ya asilimia moja tu ya ardhi yote ya Jamhuri ya Muungano, vimeweza kuhimili kubakia na ‘hisia za kutokuridhika’ kwa miaka 47 ya Muungano huu. Lazima tukiri kwamba ni ujasiri tu ndio unaomuwezesha mwanaadamu kuweza kukaa na fundo la moyo kwa miaka mingi kama hii, akiendelea ‘kuridhika na kutokuridhika’ kwake!

Hili la Wazanzibari kuendelea kuishi ndani ya Muungano ‘wakiridhika na kutokuridhika’ kwao, ndilo wengine wanalolichukulia kimakosa kwamba linamaanisha kuwa Muungano huu ni halali na unatakiwa! Kwa maoni yangu, hiyo ni tafsiri potofu, lakini inaakisi ukweli unaoufanya Muungano uendelee kuwapo kwa karibuni nusu karne sasa.

Vyenginevyo, tunapaswa kukiri kuwa kuna kutokuridhika kwa upande wa Zanzibar; na kwa kuwa Zanzibar ni sehemu moja kuu ya Muungano huu, basi hisia zake hazipaswi kupuuzwa tena. Kukiri ukweli huu ndiko kutakakotusaidia kuyageuza mateso yetu kuwa faraja. Kwa nini na kwa vipi?

Kwanza, kutayaendeleza mapinduzi ya kweli ya Zanzibar kwa kuyapa maana katika maisha ya kila siku na ya kila mmoja wetu. Kwa dhati yake, mapinduzi ni matokeo ya kutokuridhika, ambako huletwa na “mgogoro kati ya njia ambazo watu wanaouona ukweli na njia ambazo wangelipenda ukweli huo uwe”.

Pili, Zanzibar inauona ukweli kuwa Muungano huu, katika hali uliyo, ni tatizo kwake na, sasa, ni moja kati ya mawili: ama uwe sehemu ya utatuzi wa tatizo lenyewe au usiwepo kabisa. Kwa kutumia maneno ya mwanasiasa mmoja kijana wa Zanzibar, “ni ama Muungano wa kuhishimiana au basi.”

Huko hakuwezekani ila kwa mapinduzi; na hayo si mapinduzi ya mapanga na marungu, wala bunduki na mizinga, bali ni ya fikra na ya mkakati, ambayo yanatakiwa yapitie hatua tano zifuatazo:

i. Kujitayarisha kwa ajili ya mapinduzi
ii. Kuporomoka kwa mfumo mkongwe
iii. Kuharibika kwa mahusiano makongwe
iv. Kujenga mahusiano mapya
v. Kuuimarisha mfumo mpya

Ama kwa kujijua au kutojijua, tayari tumeshapita kipindi cha kwanza cha matayarisho kwa ajili ya mapinduzi, ambacho kilitawaliwa na woga wa wananchi na mateso kutoka kwa watawala. Hicho kilikuwa ni kipindi ambacho, ingawa palikuwa na kiwango kikubwa cha kutokuridhika na jinsi Muungano huu unavyoikandamiza Zanzibar, si Wazanzibari wengi waliokuwa na uthubutu wa kusema kutokuridhika huko. Bali hata wale wachache waliothubutu, walisemea vibuyuni, ambako ama walichokisema kilimalizwa huko huko au wenyewe walimalizwa kwa njia zao za kumalizana. Silazimiki kuwataja kwa majina wala kuitaja mikasa ya aina hiyo kwenye historia ya miongo miwili ya kwanza ya Muungano (1964 – 1984) kuhalalisha hoja hii.

Sasa tulipo, kwa maoni yangu, ni katika hatua ya pili ya mapinduzi, ambapo mfumo mkongwe wa Muungano usio na maslahi kwa Zanzibar unaelekea kuporomoka. Kawaida kipindi hichi ni matokeo ya kupotea kwa uongozi ndani ya kundi la watawala, ambapo mgawanyiko wa makundi humfanya kila mmoja kutenda kivyake.

Mara nyingi hatua hii haifikiwi mpaka ajitokeze kiongozi anayejiona kuwa mwanamageuzi kutaka kuunusuru mfumo mkongwe; na akafeli. Turgot na Necker walijaribu kuunusuru ufalme wa Ufaransa kabla ya mwaka 1798 na Stolpyin akafanya jaribio kama hilo nchini Urusi kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini wote walishindwa.

Huwa ni wakati ambapo, kutokana na mtikisiko wake, mfumo mkongwe huwa kama tayari umeshakufa kitambo, lakini kwa kuwa watu wanaothubutu kuyathibitisha mauti yake hawajatokea, basi mfumo huo huendelea kuwepo tu ukiishi kwa upepo. Kikwetu tunaiita hali hii ya kuwa maiti-kwenenda. Muungano huu sasa ni maiti-kwenenda!

Huu ni mfano wa kile kisa cha mauti ya Nabii Suleiman (A.S), ambaye hata baada ya kuwa alifariki siku nyingi akiwa amekaa kwenye kiti chake cha ufalme, lakini raia wake, wakiwamo wanyama, wanaadamu na majini, waliendelea kuamini kuwa mfalme wao amekaa kitini akiwasimamia. Ni hadi mchwa walipokuja kuila fimbo yake, ambayo alikuwa ameegemea, ndipo wakatanabahi kuwa kitambo kirefu Suleiman hawakuwa naye tena.

Historia ya Ufaransa inathibitisha hivyo pia. Kuna watu waliojuwa kuwa awamu ya tatu ya serikali ya nchi hiyo ilishakufa tangu mwaka 1934, lakini maziko yake yalikuja kufanywa mwaka 1940. Miaka sita baadaye!

Wazo ninalojaribu kuliwasilisha hapa ni kuwa: kuna siku yale yale matakwa ya Wazanzibari, kama yalivyoelezwa kupitia Ripoti za Tume za Jaji Nyalali na Jaji Kisanga, ndiyo yatakayoongoza mahusiano baina ya Tanganyika na Zanzibar (yawe na jina lolote lile: Muungano, Shirikisho, Umoja, Ushirikiano, n.k) na wala sio Katiba ya Muungano iliyopo sasa wala hiyo inayoambiwa kuwa itaandikwa upya baada ya uchaguzi wa 2015. Na viashiria vya utabiri huo vimeanza kujengeka kitambo.

Leo tunazungumzia Muungano ambapo Zanzibar ina bendera yake, ina wimbo wake wa taifa, ina vikosi vyake vya ulinzi mbali ya katiba, bunge na rais wake mwenye madaraka zaidi kuliko miaka kumi nyuma. Tunazungumzia Muungano ambapo utambulisho wa Uzanzibari umeshindwa kuuliwa na kuzikwa hata baada ya nusu karne nzima. Huu, hapana shaka, si Muungano ambao mmoja wa waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika, aliuwazia.

Kwa mujibu wa maneno na matendo yake, Nyerere alipendelea sana kuona kuwa, haraka iwezekanavyo, raia wa pande zote mbili wanajitambulisha kwa Utanzania wao tu, kiumbe chake. Hii ni kwa kuwa, Nyerere, kama walivyo Watanganyika wengine wengi, alipuuzia sana hisia za uzalendo wa Kizanzibari. Hata hivyo, kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa muasisi mwengine, Mzee Abeid Karume wa Zanzibar, aliiwazia Zanzibar yake vyengine na vikubwa zaidi ya haya.

Changamoto iliyo mbele yetu kwa sasa ni ukweli kwamba hatua za tatu, nne na tano zinakuja kwa kasi na, yumkini, hatuna matayarisho mazuri kuzikabili. Kwa mfano, hatua ya tatu, ambayo ni ya kuharibika kwa mahusiano makongwe, kwa mintarafu ya kuharibika kwa muundo wa sasa wa Muungano, ina matatizo yake.

Mojawapo ni kwamba, wenye maslahi na mahusiano haya hivi sasa, wanajitahidi kutumia nguvu zao za ziada kuzuia yasiharibike. Na ingawa, kutokana na matakwa ya kiwakati hawataweza kuzuia chochote, lakini, kama tusemavyo kikwetu ‘buyu likigwa, hugwa na vishindovye’. Maana yake ni kuwa, mti mkubwa kama mbuyu unapoanguka, unakuwa na vishindo vikubwa pia: husababisha maafa kwa pale unapong’okea, ambapo huweza kuchimbika shimo kubwa litakalochukua muda kufukilika, na kule unakoangukia, ambako nako huweza kuelemea nyumba au wapita njia na kuwajeruhi, kama si kuwatoa roho zao kabisa! Muungano huu ni mbuyu mkubwa, lakini mkongwe na, hivyo, dhaifu kwenye mizizi yake!

Ulimwengu una mifano mingi kama hii. Kuna wa Indonesia na Timori ya Mashariki, wa Morocco na Sahara ya Magharibi, wa China na Macao au na Hong Kong. Mwengine mumekuwa na mafanikio, na mwengine bado mapambano yanaendelea. Muongo uliopita ulianza kushuhudia mahusiano makongwe baina ya Syria na Lebanon yakianza kuharibika. Na Lebanon ndiyo iliyoonekana kulipia gharama za kipindi hiki, pale wanaharakati walio mstari wa mbele kusaidia maharibiko hayo, walipoanza kukabiliwa na vitendo vya kigaidi vinavyoaminika kusimamiwa na kuongozwa na Syria ndani ya ardhi ya Lebanon. Haitakuwa ajabu hata kidogo kwa Zanzibar kukumbwa na hayo hayo, japo kwa staili na matukio mengine.

Lakini hakuna sababu ya kutishika wala kuvunjika moyo kwa sababu mbili: kwanza, lolote litakalotokea kwa mwanaharakati wa Kizanzibari, ikiwa ni kwa ajili ya imani ya nchi yake, basi halina majuto. Pili, kipindi hiki kinapoanza tu, hutanguliwa haraka sana na kipindi cha ujenzi wa mahusiano mapya, ambacho nitakifananisha na ujenzi wa nyumba mpya juu ya kongwe, ambao ni maarufu kwa jamii za watu masikini kama Zanzibar.

Katika mazingira haya, mwenye nyumba huendelea kujenga nyumba mpya, huku yeye akiwemo ndani. Anachofanya ni kuvunja kiambaza kimoja kwanza na kusimamisha kipya mahala pa kilichovunjwa, kabla hajakwenda katika kiambaza chengine.

Ingawa huweza kuchukua muda mrefu kwa nyumba kukamilika, kutegemea na uwezo wa kifedha, kiufundi na mazingira ya ujenzi; lakini ni staili ya ujenzi ambayo ina faida moja kubwa: hakuna wakati ambapo mwenye nyumba analazimika kulala nje, hata kama katika kipindi cha ujenzi wake, huwa hakai katika makaazi mazuri sana.

Hapo ndipo, kwa maoni yangu, Muungano huu unapoelekea. Unaingia kwenye kuvunjika na kuundika kwa wakati mmoja. Tunakwenda katika kipindi ambacho hatutasema kuwa hatuna Muungano moja kwa moja, lakini pia hatutakuwa na Muungano huu uliopo sasa.

Mwisho tutaingia kwenye kuimarisha mahusiano mapya tutakayoyajenga; maana ukweli ni kwamba Zanzibar, Tanganyika na mataifa mengine ya jirani, yataendelea kuwa katika mahusiano ya ukaribu, udugu na ujirani mwema daima na dawamu. Huu ni uhusiano wa zaidi ya milenia mbili na hauwezi kupuuzwa wala kuvunjwa. Lakini tafauti na sasa, mahusiano yajayo kwa sababu ya mapinduzi haya, yatakuwa na sura nyengine na matakwa mengine. Kuna ambao tunataka mahusiano hayo yawe kama yale ya mataifa yaliyo kwenye Umoja wa Ulaya (EU) au Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba (GCC).

Hata hivyo, lazima tuzinduke Wazanzibari. Kwamba jambo pekee linaloweza kutufikisha hapo ni moja tu, nalo ni mkono mmoja kuyashikilia mapinduzi yetu na mwengine kuishikilia Zanzibar yetu, ambayo imeelezewa vyema kwenye Mabadiliko ya Kumi ya Katiba yaliyofanywa na Baraza la Wawakilishi mwaka jana. Tuiamini, tuitetee, tuilinde na tuisimamie Katiba yetu hii, maana ndani yake muna kila aina ya fursa na silaha ya kufanikisha mapinduzi yetu.

One thought on “Miaka 47 ya Muungano, Zanzibar na Mapinduzi mapya”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.