Maalim Seif Sharif Hamad

Wanaotamani kuivunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUKZ) ni sawa na wale wenye kutaka kuendesha gari kwa kutumia kioo cha kutizamia nyuma kila wakati. Watu wa namna hii hata ifanyike miujiza gani Zanzibar basi wataendelea kuponda na kulalamika na wakikipata kifursa basi watalirukia gari na watasema wao ndio waliokuwa madereva waliofikisha Zanzibar kunako amani na neema.

Hili la amani na utulivu tumeliona juzi ilipopewa nishani “Kamati ya Ali Mzee” na Balozi wa Kimarekani. Nikitamani angalau atokee mjumbe mmoja tu kati ya hao wajumbe sita angalau akasema “nimeipokea nishani hii kwa niaba ya Wazanzibari wote, kwa niaba yetu, na zaidi kwa niaba ya waasisi halisi walioifanya kazi kubwa ya kuiweka misingi ya Maridhiano.” Inawezekana kuwa yote au baadhi ya haya yalitajwa lakini jee, hili la waasisi halisi wa Maridhiano lilitajwa au ndo penye nishani kuna shani?

Waasisi wa Maridhiano yalioirudishia Zanzibar amani na utulivu baada ya miaka 50 ni hawa wafuatao: Rais Amani Karume, Maalim Seif, Mzee Hassan Nassor Moyo, Ismail Jussa, Mohammed Ahmed Al Mugheiry (Eddy Riamy), Mansour Yussuf Himid, Abubakar Khamis, na Salim Bimani. Kawaulizeni hawa na kawaulizeni waliopewa nishani na Ubalozi wa Mrekani mupate kuujua ukweli kwani wote hawa wahai na wana nguvu zao – alhamdulillah.

Ukimtoa Rais Mstaafu Karume na Maalim Seif, katika hao sita kuna makada wawili ambao wako karibu sana na viongozi wa juu kabisa wa pande mbili, mmoja wa CUF na wa pili wa CCM. Makada hao walikuwa vinara vya mwanzo waliouanzisha mchakato wa Maridhiano yaliofaulu Zanzibar mwaka 2010 na kupigiwa kura ya maoni na wananchi wa Zanzibar.

Tayari historia changa ya Maridhiano imeshaanza kupotoshwa kwa kutowataja waasisi wa Maridhiano hayo ambayo ndio yalioweza kuyaleta mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar. Tusistaajabu kuuona upotoshaji huu ambao unafanywa chini ya macho yetu, kutungiwa vitabu vya kuwasomeshea wanafunzi wetu maskulini. Wasomi na waandishi wa habari nao wameshaanza kuubeba huu upotoshaji na kuanza kuueneza na kujijengea sifa za kichambuzi na za “kisomi” kuhusu Maridhiano yaliofanyika Zanzibar mwaka 2010.

“Kamati ya Ali Mzee” isingeliweza kufanya lolote lile bila ya mambo yote kuasisiwa na kuwekwa tayari na waasisi wa Maridhiyano na huu ukweli ni muhimu kamati ya utendaji ya Maridhiano iliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kuukubali hadharani ili kuweka mizani sawa juu ya hili suala muhimu la ki Nchi na la Kitaifa la Zanzibar. Tukidharau itabidi tusubiri miaka 50 mengine ili vizazi vijavyo vije kuiweka sawa rikodi ya historia na kuufunua ukweli. Athari ya kulificha hili ni kuondoa hisia ya utamaduni wa ukweli na kuwatambua wazalendo wote walioshiriki katika kuiokoa Zanzibar. Mmefikiria leo ingelikuwaje kama Zanzibar hakuna SUK na hili vuguvugu lenye kuvuma kutoka Mashariki ya Kati?

Kiasi wajitokeze watu kutaka kuibomowa SUK Zanzibar kwa sababu hawawajui ni akina nani khasa na kwa malengo gani waliisimamia kazi tukufu ya kuirejeshea Zanzibar amani na utulivu baada ya miaka 50 ya kuranda jangwani. Na kuna wanaotamani SUK isingelikuwepo ili yanayotokea Mashariki ya Kati yatokee na Zanzibar na katika fujo wapate nafasi ya kujijenga kisiasa na kiubinafsi.

Kuna watakaosema si muhimu nani kafanya au kasababishwa na Allah kuyaunga mkono Maridhiano kwa kujua au kwa kutokujua, kwa kutaka au kutotaka. Muhimu Maridhiano yamefanyika. Kila mmmoja wao alifanya kwa nia yake na atalipwa na Allah kwa nia yake. Na iwe hivyo lakini ukweli utabakia kuwa Maridhiano yalikuwa na waasisi wake na yalioombewa dua na wananchi na SUK inawakilisha umoja wa wananchi wa Zanzibar ambao dua zao zilitakabaliwa na Allah, na kukaribishwa na wengi duniani.
Kwa hiyo wenye ndoto za kutaka kuibomowa SUKZ wasisahau kurudi kwa wananchi kwanza. Hakuna kurudi nyuma baada ya kukitia mkononi kile ambacho Zanzibar ikikililia kwa nusu karne – miaka 50 – nacho ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hakuna ambaye anafurahikiwa na hali ya kiilimu na ya kimaisha Zanzibar, lakini dawa ni:

Kwanza, kuirudisha Nchi ya Zanzibar kunako ramani ya dunia kupitia Katiba ya Zanzibar.

Kuilinda Nchi ya Zanzibar.

Na hii ya tatu ndio kazi kubwa zaidi: kuziinua hali za kimaisha za Wazanzibari walio wengi kwa kuuinua uchumi, ilimu na afya, kupitia wajuzi na wataalamu wa Kizanzibari wenye fani mbali mbali, wa ndani na wa nje, kwa kuungwa mkono na wanasiasa, na si kwa wanasiasa kuifanya kazi ya wajuzi na wataalamu.

Wakati tunayafanyia kazi mambo matatu hayo, tusiyasahau mambo mawili:
Kuwapinga wahafidhina wa pande zote mbili kwa sababu kwa Zanzibar Mpya uhafidhina ni kensa, tena ile kensa mbaya yenye kuuwa haraka.
Wasiotutakia kheri wameshawasha vibatari wanapanga wakipangua kwa kuona kuwa wakati ndio huu wa kututenda tena.

Wahafidhina na wanaotupangia maovu wanapanga, na Allah anapanga, na Allah ndiye mkubwa wa wapangaji.
Tuamke na tujipange.

Hakuna ambaye anafurahikiwa na hali ya kiilimu na ya kiuchumi namna ilivyo mbaya Zanzibar lakini dawa ni kuijenga Zanzibar mpya na si kuibomowa SUKZ. Wallahi shetani adui wa binaadamu. Zanzibar kuwa shwari imekuwa jambo la kulinunia?


Makala ya Dkt. Harith Ghassany

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.