Dkt. Shein, Dkt. Karume na Maalim Seif

Makala ya Tundu Lissu iliyochapishwa na gazeti la MwanaHalisi chini ya kichwa cha habari, Muungano wa Tanzania sasa umekuwa dhaifu zaidi, imenishawishi kutoa maoni kwa kuona inaelekeza watu sivyo.

Lissu, ambaye ni mwanasheria mwenzangu, anasema mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 yamedhoofisha muungano wa Tanzania kwa “kumong’onyoa misingi karibu yote ya muungano huo, kubadili sura ya muungano wenyewe, mipaka yake na muundo wake.” Ana khofu mabadiliko hayo “yanaweza kuwa chanzo kikuu cha kubomoka kwa Muungano na hata tishio kwa usalama wa mipaka ya Taifa.”

Anaamini mabadiliko hayo yaliitangaza Zanzibar ‘‘kuwa nchi yenye mipaka kamili” na kwamba “Rais anajua kuwa kabla ya mabadiliko hayo kufanyika, Zanzibar haikuwa nchi na wala mipaka yake haikutajwa.” Anaegemea kifungu cha kwanza cha Katiba ya Zanzibar kabla ya marekebisho, kinachosema, ‘‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Hapa kuna mambo mawili: Kwanza kuwa mabadiliko hayo ndio yaliyoitangaza Zanzibar nchi, na pili ndiyo yaliyobainisha mipaka ya Zanzibar ambayo mwanzo haikutajwa. Yote haya si kweli.

Zanzibar ilianza kuwa na katiba yake ya kwanza baada ya Mapinduzi ya 1964. Ilikuwa mwaka 1979. Baadaye ilifutwa na kuandikwa upya mwaka 1984 ilipoandikwa inayoendelea mpaka sasa. Ndiyo iliyofanyiwa marekebisho mara 10 yakiwemo haya yanayojadiliwa sasa. Je, Katiba hiyo haikutaja Zanzibar kama nchi hadi yalipokuja mabadiliko ya kumi? Ni kweli Katiba ya Zanzibar ya 1984 kabla ya marekebisho ya kumi ilieleza katika kifungu cha 1 kuwa “Zanzibar ni sehemu ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Lakini ukiwacha kifungu hicho, vifungu kadhaa au tuseme katiba yote inaitaja Zanzibar ni nchi.

(9)(i) Zanzibar itakuwa ni NCHI ya kidemokrasia na haki za kijamii.

(9)(2)(a) Mamlaka ya kuendesha NCHI ni ya wananchi wenyewe …

(10) Kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika NCHI itakuwa ni wajibu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar:

(10)(3) Itadhibiti uchumi wa NCHI kufuatana na misingi na madhumuni yaliyoelezwa na katiba hii.

(12)(3) Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu yatalindwa na kuamuliwa na mahkama pamoja na vyombo vya NCHI na vinginevyo vilivyowekwa na sheria.

(21)(i) Kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa NCHI…

(23)(2) Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasili ya Zanzibar, mali ya NCHI pamoja na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi…

Inaonyesha Lissu alitazama tu kifungu hicho cha kwanza, akapuuza vingine. Katiba ya Zanzibar imebaki na idadi ileile ya vifungu 135 hata baada ya marekebisho ya kumi.

Msingi mkuu wa katika kanuni za kutafsiri sheria, ni kuwa ili uweze kupata tafsiri sahihi kwa waraka wowote (iwe ni Katiba, Sheria, Mkataba n.k.) unapaswa kusoma waraka wote ndipo upate maana, tafsiri au dhamira inayopatikana katika waraka huo kuhusiana na jambo husika. Ni dhahiri huwezi kuchopoa kifungu kimoja tu ukapata usahihi.

Hebu tuangalie hichohicho kifungu cha kwanza kisemacho ‘‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.” Ni sawa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri Ya Muungano, lakini inasimama katika utambulisho upi? Ni sehemu kama Mkoa, Wilaya, Tarafa, Jimbo, Kata au kitongoji? Zanzibar ina katiba yake, ina Rais wake, ina Mahkama zake, ina mawaziri wake, ina Baraza lake la kutunga sheria (Baraza la Wawakilishi), ina watu wake (tena wana vitambulisho), ina bendera yake, ina wimbo wake wa Taifa, ina Mamlaka yake ya serikali za mitaa, ina magereza yake (Vyuo vya Mafunzo), ina vikosi vyake maalum vya ulinzi, ina mapato yake na bajeti yake n.k. Jee kuna Mkoa au Wilaya yenye yote hayo? Na yamekuwepo kabla ya mabadiliko yaliyofanywa.

Lissu anasema, “Rais anajua kuwa kabla ya mabadiliko hayo kufanyika, Zanzibar haikuwa nchi na wala mipaka yake haikutajwa.” Kabla ya mabadiliko ya kumi, Katiba ya Zanzibar 1984, kifungu cha 2(i) kinasema:

2(i) “Eneo la Zanzibar ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.” Baada ya mabadiliko ya kumi, kifungu hicho kinaendelea kuwepo kikisema: Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vidogo vilivyoizunguka bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar.”

Hoja ya pili ya Lissu ni mabadiliko haya yanadhoofisha Muungano kwa vile yameondoa mamlaka ya kuigawa Zanzibar katika mikoa kutoka mikononi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kuweka mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar. Hili ni kweli limefanyika katika mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar. Tujiulize sababu. Inaeleweka wazi kuwa ni Rais wa Zanzibar ambae kipindi chote tokea Muungano wa Tanzania uasisiwe 1964, ndie anayeigawa Zanzibar katika mikoa na wilaya.

Hakuna kumbukumbu inayoonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano amewahi kuigawa Zanzibar katika Mikoa au Wilaya. Sasa kwa takriban miaka 47 mamlaka hayo yalikuwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kikatiba lakini kiutendaji na kiutekelezaji Rais wa Zanzibar ndiye aliyekuwa anatekeleza mamlaka hayo. Mabadiliko yametambua hilo na kurekebisha. Haiwezekani tukadumisha vifungu ndani ya katiba ambavyo vinaonekana ni pambo tu. Bali hili litoshe kuonesha mkanganyiko unaozikumba katiba zetu mbili.

Hoja ya tatu ya Lissu ni kuwa mabadiliko ya kumi yamepunguza mamlaka ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Anasema: “Mabadiliko yamekiuka katiba kwa kuinyang’anya Mahakama ya Rufaa mamlaka ya kusikiliza rufaa zote zinazotoka katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.”

Hata mara moja tangu ianzishwe, haijawahi kutokea kwa Mahkama ya Rufaa kuwa na mamlaka ya kusikiliza rufaa zote zinazotoka katika Mahkama Kuu ya Zanzibar. Katiba ya Zanzibar iliipa mamlaka mahkama hiyo kwa baadhi ya kesi tu.

Kifungu cha 99 cha Katiba ya Zanzibar kinasema, Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania itakuwa na uwezo wa kusikiliza rufani toka Mahkama Kuu ya Zanzibar isipokuwa kesi zozote zinazohusika na:

Tafsiri ya katiba hii

Mambo ya kiislamu ambayo yameanza katika Mahkama za Kadhi.

Mambo mengine yoyote yaliyoainishwa katika katiba hii na sheria nyengine yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Ndio kusema mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar hayakuongeza kitu kwani pamoja na ukweli kwamba mahakama hiyo haitokuwa na uwezo wa kusikiliza rufani kutoka Mahkama Kuu ya Zanzibar iliyotokana na mambo kuhusiana na vifungu vya haki za binadamu, inajulikana mamlaka ya Mahkama ya Rufaa ya Tanzania kwa Zanzibar ni kwa baadhi ya kesi tu.

Ieleweke kuwa kifungu cha 99(b) cha Katiba ya Zanzibar kimetaja kwa ufupi tu “mambo yaliyoanzia Mahakama ya Kadhi” lakini kwa mujibu wa Sheria Na. 3 ya mwaka 1985 iliyounda Mahakama ya Kadhi, mambo yote yanayohusu ndoa, talaka, mirathi na haki stahiki za mtoto yanasikilizwa katika mahakama za kadhi endapo wahusika wote ni waumini wa dini ya Kiislamu.

Hivyo pamoja na ukweli wa kuwa mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar kwa kutumia kifungu cha 99(c) yameondoa uwezo wa Mahkama ya Rufaa kusikiliza masuala ya haki za binadamu, hakuna jipya. Lakini hata kama tukihoji busara iliyotumika katika kuliondoa suala la haki za Binadamu katika mamlaka ya Mahakama ya Rufaa bado si sahihi kujenga hoja kama kwamba hili la kuondoa baadhi ya mambo katika mamlaka ya Mahkama ya Rufaa ni jambo jipya lililokuja kwa mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.

Lissu anasema mabadikilo ya Katiba ya Zanzibar yamekiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano na kudhoofisha Muungano kwa vile sasa Zanzibar “imehalalisha uwepo wa vikosi vya Jeshi vya SMZ inavyoviita Idara Maalum.” Idara Maalum imekuwepo hata kabla ya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ikijumuisha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Chuo cha Mafunzo (cha wahalifu) na kifungu hichi hakikubadilishwa hata nukta wala namba za vifungu.

Lakini tujiulize hivi Zanzibar chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina uwezo wa kuunda majeshi? Tena tutumie hiyohiyo katiba ya Jamhuri ya Muungano aliyozungumzia Lissu.

Ni kweli, kama alivyosema kuwa ibara ya 147(i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema ‘‘ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania Jeshi la aina yoyote.”

Laitani mwandishi angeangalia kifungu cha 151 cha katiba hiyo akaona neno “Serikali” lilivyotafsiriwa angeondoa shaka yoyote juu ya uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweza kuunda na kuweka jeshi. Neno serikali linatafsiriwa kama:

“Serikali maana yake ni pamoja na serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Halmashauri ya Wilaya au Mji, na pia mtu yeyote anaetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali au Halmashauri.”

Tafsiri hii katika Katiba ya Muungano 1977 yenyewe inatoa fursa kwa serikali (ikiwemo SMZ) kama zilivyotafsiriwa na katiba hiyohiyo zilivyo na uwezo wa kuunda na kuweka jeshi.

Lissu amegusia vyeo vipya vya Zanzibar vya Makamo wa Kwanza wa Rais na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar vilivyoundwa na mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Anasema nayo yamekiuka katiba ya Muungano na hivyo ni ‘‘batili na hayana nguvu yoyote ya kisheria.” Ananukuu kifungu cha 64(3) cha Katiba ya Muungano 1977 kujenga hoja yake. Mbona amekinukuu nusu?

“Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka….”

Lakini kwa mshangao utagundua kuwa kifungu hicho kinaendelea kumalizia kama ifuatavyo (lakini mwandishi ameona hiyo sehemu ya mwisho ya kifungu hicho asiinukuu, kwa nini, haieleweki)

“… na pia endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka.”

Hivi muundo mzima wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na vyeo vya viongozi wa Serikali hiyo na watendaji wake ni jambo lililo chini ya mamlaka ya Bunge? Hamna popote katika katiba au sheria yoyote inayotoa mamlaka kwa Bunge juu ya kuunda vyeo au muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vyeo hivi vya makamo wawili wa Rais wa Zanzibar vimetokana na kundwa kwa Serikali yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa lakini kama vyeo hivi ni batili basi kwanza huo muundo wenyewe uliopelekea kuwepo kwa vyeo ungekuwa ni batili!

Muundo wa SMZ na vyeo katika Serikali tangu Aprili 1964 ni mambo yaliyo kwenye mamlaka ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na yanaongozwa na Katiba ya Zanzibar.

Lissu anaposema ilikuwa vema mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yakafuata misingi ya sheria anaonyesha kuwa sheria zimevunjwa. Hilo si kweli. Kwanza, yapasa atambuwe kuwa ni fikra potofu kuamini katiba ya Muungano ndio katiba mama na ile ya Zanzibar ni mtoto. Katiba zote hizi ni sawa kisheria. Katiba ya Zanzibar ina nguvu juu ya mambo yote ya Zanzibar (yasiyokuwa ya Muungano) wakati ya Muungano ina nguvu kwa mambo ya muungano na yale ya Tanganyika.

Hata kama baadhi ya taasisi, vyombo na vyeo vya Zanzibar vinatambuliwa katika katiba ya Muungano, hiyo haimaanishi kuwa katiba ya Muungano ndio inayosimamia mambo hayo. Juu ya yote haya, bado ninaamini mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano ni muhimu kwani iliyopo haitoshelezi wakati.


Makala hii ya Awadh A. Said ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika mtandao wa Mzalendo.Net na baadaye gazeti la MwanaHalisi la 23 Februari 2011. Mwandishi ni wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.

One thought on “Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar siyo yanayoudhoofisha Muungano”

  1. Wazanzibari tuzijue katiba zote mbili kwa ghaib hii ndio nusura pekee ya kujenga hoja zenye mashiko , sio tuwaache wana sheria tu siku wakiondoka tutakimbilia wapi??????

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.