Siingii kwenye kundi la wanaoajiaminisha kuwa kuikosoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUKZ), au viongozi wa serikali hiyo ni sawa sawa na kuihujumu serikali yetu au kuongozwa na chuki dhidi ya viongozi wetu. Na nina sababu mbili za kuepuka kuingia kwenye kundi hilo: moja ni kwamba, miezi saba iliyopita, nilikuwa sehemu ya harakati za kupigania kuja kwa serikali hii, kwa kuendesha kampeni ya Kura ya Ndio karibuni katika kila wilaya, ikiwa si kila jimbo la Zanzibar.

Sikuwahi kuwa na wasiwasi wa kushindwa kwenye kura ile. Bila ya shaka, sikuwa na sababu ya kuwa na imani ya moja kwa moja na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na taasisi nyengine zinazohusiana kwa namna moja ama nyengine na mfumo wa uchaguzi. Uzoefu ulinifundisha kuiamini kikamilifu ile kanuni ya Kiingereza: hope for the best, prepare for the worst (tarajia kheri, jitayarishe kwa shari).

Siku Maalim Seif alipoinusuru Zanzibar na umwagikaji damu uliokuwa karibuni kutokea, alipoyabeba Maridhiano kifuani pake na kukubali matokeo ya uchaguzi wa 2010, kwenye ukumbi wa Bwanani. Na katika picha hii ya kihistoria akimpongeza Dkt. Ali Mohammed Shein kwa 'ushindi wa Wazanzibari.' Je, Dkt. Shein ameyageuka Maridhiano?
Matokeo ya uchaguzi wa 2010: Mwanzo wa kuyajenga au kuyavunja Maridhiano?

Ila, mimi na swahibu yangu na ndugu yangu, Issa Hussein, tulikuwa na wasiwasi zaidi kwenye namna ambavyo serikali tunayoihubiri itakavyokuja kukabiliana na changamoto ya kuyatimiza matarajio makubwa ya umma kwa muundo wa serikali tuliokuwa tukiwashawishi wauunge mkono.

Wala sikumbuki kwamba viongozi wetu (nakusudia viongozi waliokuwa wakiendehsa kampeni za waziwazi za Ndio), walikuwa wanaahidi makubwa kama milima. Ahadi ya kudumu ninayoikumbuka, ni amani na masikizano. Ni kweli kuwa, kwa mujibu wa Maslow’s Hierrachy of Needs, watu hawali amani wala masikizano. Wanakula wali na samaki!

Lakini, kama kuna jambo la ajabu kwa siasa za Zanzibar ni hili. Kabla ya kampeni hizi, nilikuwa nimekuja hapa hapa Ujerumani kuhudhuria mafunzo ya Mkakati wa Mawasiliano, na niliwashangaza washiriki nilipowaambia kuwa, angalau kwa wakati ule nilipoondoka Zanzibar, Wazanzibari walikuwa wamemthibitishia Maslow kwamba alikosea alipotoa nadharia yake ya piramidi ya mahitaji.

Kwa mujibu wa Maslow, mahitaji ya kila siku ya maisha: chakula, maji, makaazi na hata umeme, ndio ya msingi kwa watu, na yale mengine kama demokrasia, haki za binaadamu, uhuru na amani, ni ya baadaye. Nilipoondoka Zanzibar, umeme ulikuwa haupo kwa zaidi ya mwezi, hivyo maisha yalipindukia kuwa magumu. Hata hayo mahitaji muhimu kwa maisha yalihatarishwa.

Lakini nyuma kidogo, ikawa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Hamad, amekutana na Rais Amani Karume, kuanzisha msingi wa Maridhiano. Wazanzibari wakasahau kwamba wana shida ya maisha, hawana umeme, maji hayapatikani, hata matibabu ya watoto wao yanashindikana hospitali, wakajiunga nyuma ya viongozi wao, kuyaengaenga Maridhiano ya Kisiasa. Kipindi kikapita salama usalimini!

Kwa hivyo, kwenye kampeni za Ndio, ilisemwa kuwa, Zanzibar ikiwa na amani na maridhiano, basi itakuwa rahisi zaidi kuvuna imani ya wawekezaji wa ndani na nje na pia inawezekana kuwashawishi Wazanzibari wenyewe kushiriki kwenye ujenzi wa nchi yao, maana serikali iliyopo, ni yao wote. Sote tunajua kuwa uwekezaji na uwajibikaji ni mambo ya msingi sana kwa maendeleo.

Hata hivyo, taaluma ya mawasiliano inathibitisha kuwa, kwenye mkufu wa mawasiliano, ujumbe husafiri; na katika safari yake, hubadilika kituo hadi kituo na hata unapofikia kituo chake cha mwisho, ile maana yake ya mwanzo huwa imeshabeba vingi vya njiani. Ndio maana Waswahili husema “hadithi ni ncha saba!”.

Kwa hivyo, kwamba leo kuna wakosoaji wa SUKZ si jambo la ajabu. Kila aliyeunga mkono ujio wa serikali hii, alijua kitambo kwamba ni suala litakalokuja. Labda nikiri kwamba, kosa kwa sisi tuliokuwa kwenye kiwango cha kampeni, ni vile kutokujiandaa kwa kile kiitwacho Expectation Management, yaani uwezo wa kuyamudu matarajio ya umma mara baada ya mabadiliko ya mfumo wa uongozi. Lakini hili, kama ni kosa, si la wakosoaji. Ni la waungaji mkono wa SUKZ.

Nimesema nina sababu mbili za kutokuchukulia wakosoaji wa SUKZ kuwa wana njama ya kuihujumu serikali na viongozi wake. Ya pili ni kuwa, naepuka hukumu hii, kwani binafsi ni miongoni mwa waliohukumiwa hivyo kimakosa na watetezi wa mfumo wa serikali uliopita, wa mshindi kuchukua yote.

Tulionekana kwamba, sababu ya kutaka mfumo wa uendeshaji nchi ubadilishwe ni kwa kuwa hatukuipenda Serikali ya Mapinduzi, kwamba tuliwachukia watu waliokuwa na vyeo kwenye serikali hiyo, kwamba tulikuwa na ajenda nyengine nje ya ile tuliyokuwa tukiibainisha. Na bila ya shaka, kila majina tukaitwa.

Nafurahi kwamba, hivi sasa miongoni mwa waliokuwa wakituhukumu hivyo, ndio waliomo kwenye serikali hiyo hiyo, na sisi tukiwa nje yake. Angalau tumethibitisha hoja kwamba, hatukutaka sisi kwenda pale na kuwafukuza wao, bali tuliwataka wao wenyewe wabadilishe mfumo wa kutuongoza. Wazungu wangeliita hii paradigm shift, na ndicho kilichotokezea Zanzibar!

Kwa hivyo, wakosoaji nawaikosoe SUKZ. Wayakosoe maamuzi au utendaji wa viongozi wa SUKZ. Wakosoe kwa hoja. Na sisi waungaji mkono wake tupo. Tutaitetea. Na tutaitetea kama mfumo tulioupigania, ambao tuliuamini na bado tunauamini, kwamba ndio bora zaidi kwa Zanzibar yetu.

Sipendi kuwaelekeza wakosoaji nini waseme na nini wasiseme katika ukosoaji wao, lakini kama ningekuwa na nafasi ya kushauri, basi ningelisema tuweke hoja moja baada ya nyengine mezani. Halafu tuzijadili kwa pamoja.

Kwa mfano, je mfumo huu wa kuiongoza Zanzibar yetu una mapungufu au makosa gani? Je, tumeweka vigezo gani vya kuhukumu kufaulu na kufeli kwa mfumo wenyewe, kwa upande mmoja, na kwa watendaji wanaousimamia mfumo huu hivi sasa, kwa upande mwengine?

Binafsi naona fakhari kwamba, nchi yangu ya Zanzibar imeweza kukipata kwa njia ya amani kile ambacho wengine wanakipata kwa kumwaga damu. Kilichofanyika Misri, Tunisia na kinachoendelea sasa Libya, Yemen, Bahrain na Algeria, ambacho kinamwaga damu za mamia ya watu, sisi tulikifanya kwenye meza.

Bila ya shaka, ni kutia chumvi mno kusema kwamba tayari tumefanikiwa. Hapana, bado safari ni ndefu, lakini ni lazima tuiende. Ninachoweza kusema ni kuwa, tumefika hapa tulipo, baada ya kujifunza kwa makosa yetu ya huko nyuma. Tuliposimama sasa ndipo, na busara ni kusonga mbele, si kurudi nyuma. SUKZ ni ya kujengwa, si ya kubomolewa!

One thought on “SUKZ ni ya kujengwa si ya kubomolewa”

  1. Ulilolisema ni lamsingi sana, binafsi kwa uoni wangu sina cha kukubishia katika hilo. Tulikuwa waathirika wa mfumo wa chukuwa chote kwa karne kabla na baada ya mapinduzi. Chambilecho wa bongo KAJIKHOFU changu kidogo ni jinsi wakuu wa idara mbali mbali wanavyoendele kuteuliwa na wengi wao wamechoka au walengwa hawaridhiki nao jambo ambalo linaweza kuturejesha tena nyuma ijapokuwa kwa kirobo hatua. Changa moto hazikwepeki ila ufundi ni jinsi ya kuzikabili.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.